Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Virusi Vya Corona COVID19 na Ujauzito

 

Je, wajawazito na kina mama wanaonyonyesha wanahitaji kujua nini kuhusu virusi vya corona?

Kuna mengi yasiyofahamika kuhusu madhara ya virusi vya corona kwa wajawazito na kina mama wanaonyonyesha. Lakini uelewa wa madhara ya virusi hivi utaongezeka kadiri muda unavyoenda.

Kuwa mjamzito huleta wasiwasi na hali ya sintofahamu kwa wamama wengi watarajiwa, hata kama kila kitu kinaenda sawa.

Wanahitaji kuepuka aina fulani ya vyakula mfano samaki wasiopikwa vizuri na jibini laini. Hii ni kwasababu miili yao inabadilika kwa kiasi kikubwa kila siku na utaratibu wake wa kawaida unaweza kuvurugika.

Taifa la Uingereza ni moja ya nchi ambazo hivi karibuni zimewahusisha wanawake wajawazito katika kundi la watu walio katika hatari za kupata maambukizi haya. Inashauriwa wanawake wajawazito kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ili kupunguza nafasi za kushika virusi vya Corona. Inaeleweka, wajawazito wengi na familia zao wana wasiwasi na wamechaganyikiwa kwasababu ya ujio huu wa Virusi vya Corona.

Pamoja yote hayo, ukweli unabaki kuwa hatuna ufahamu wa kutosha kuhusu madhara ya virusi hivi vya Corona COVID-19 kwa wajauzito. Kuwepo kwa ufahamu wa kutosha husaidia kuchukua hatua za uhakika. Uwepo mdogo wa wanawake wajawazito waliopata maambukizi haya pamoja na ufahamu wa kutosha wa Virusi hivi vya Corona kwa ujumla utatusaidia kutoa ushauri wa ziada kwa wanawake wajawazito kuchukua tahadhari mapema.

Mfumo Dhaifu wa Kinga ya Mwili

Mwanzoni ilidhaniwa kipindi cha ujauzito kinga ya mwili ya mwanamke inadhoofika na kumfanya kuwa katika hatari ya kupata maambukizo. Hata hivyo, kama ilivyo vitu vingi vinavyohusiana na mwili wa binadamu ushahidi mpya unaonesha kuwa kinga mwili ya mjamzito hupanda kipindi cha ujauzito, na wakati mwingine huwa ni ya kubadilika badilika.

Mabadiliko haya ya kinga ya mwili kipindi cha ujauzito ni muhimu kwa ajili ya kumpa nafasi mtoto anayeendelea kukua katika hatua tofauti za ujauzito. Kwa mfano katika hatua za kwanza za ujauzito kinga ya mwili inabadilika ili kuruhusu upandikizaji katika mwili. Wakati mwingine mfumo wa kinga unahitaji kujirekebisha katika njia tofauti, mfano mzuri ni wakati mwili wa mwanamke unajiandaa kupata uchungu wa kujifungua.

Jambo la muhimu katika maelezo yote haya ni kwamba kuwa na mfumo wa kinga wenye kubadilika badilika inakuweka katika hatari kubwa ya matatizo ya Virusi vya Corona kama vile shida katika upumuaji na hata homa ya mapafu (pneumonia).

Kitu cha kwanza cha kutiliwa mkazo ni wanawake wajawazito waendelee kuhudhuria miadi yao ya kliniki katika hospitali isipokuwa kama wameambiwa vinginevyo na mkunga au daktari wao.

Kwa sasa hakuna sababu ya kubadilisha mpango wako wa kujifungua, kama uliandaa hapo awali. Mpango wa kujifungua unahusisha mahali unapotarajia kujifungulia (hospitali, zahanati, kituo cha afya, au nyumbani) na aina gani ya dawa za maumivu unatarajia kupata.

Walakini, ikiwa umeonekana na dalili zinazoashiria maambukizi ya Virusi vya Corona, kama kikohozi kikavu au joto kubwa la mwili, kubanwa kifua na kupumua kwa shida,  ni lazima ujitenge (self-isolation) na wasiliana na daktari au mkunga wako haraka.

Vilevile, kwa wanawake wajawazito wenye matatizo mengine ya kiafya wanahitaji kuwa makini zaidi na kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ikiwezekana kufikiria kujitenga (self-isolation) kipindi cha ujauzito. Wanawake waliopata ugonjwa wa kisukari, aina ya ugonjwa wa kisukari ambayo ni matokeo ya ujauzito ijulikanayo “Ugonjwa wa Kisukari kipindi cha Ujauzito” (gestational diabetes), wanatakiwa kuchukua tahadhari na kupunguza migusano na watu.

Kuwa mgonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito ni kundi la hatari hata bila kupata Virusi vya Corona, kwasababu ugonjwa huu wa kisukari unaongeza ugumu wakati wa ujauzito na kujifungua. Zaidi ya hapo, viwango vikubwa vya sukari katika damu kwa mda mrefu bila kutibiwa na kuangaliwa vizuri vinaweza kudhoofisha mfumo wa kinga zaidi.

Kutokana na mfumo wa kinga unaobadilika kila hatua wakati wa ujauzito ni vizuri wanawake wasio na matatizo ya kiafya kuchukua tahadhari na kukaa mbali na watu pale inapobidi.

Kama ilivyo wajawazito wengi wanaishi na wenzi wao au mara nyingine mtoto/watoto wao wengine, ushauri huu ni vizuri kufuatwa ili kupunguza nafasi ya kuweka afya ya mama mjamzito katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Corona.

Tahadhari hizo ni pamoja na kufanya kazi ukiwa nyumbani kwa wale wanaoweza, kataa mgusano wa aina yeyote na watu na epuka sehemu za mikusanyiko.

Mwisho kabisa, ili kuwasaidia wajawazito kuwa na ujauzito wenye afya na kinga ya mwili nzuri katika kipindi hiki, ni vizuri kuzingatia mlo bora wenye madini chuma kwa wingi (kama mboga za majani zenye kijani kilichokolea, samaki na mayai) na madini ya foliki ambayo yanapatikana kwenye maharage, kunde, maharage ya kijani n.k. Bila kusahau vidonge vya vitamini vya kila siku ulivyoandikiwa na daktari wako vinasaidia pia.

Je, ninaweza kumpatia mtoto wangu Virusi vya Corona?

Je, kuna uwezekano wa mama mjamzito aliyepata maambukizi ya Virusi vya Corona kumpatia mtoto anayeendelea kukua ndani ya mwili wake?  Hili ni moja ya swali linalowaumiza wajawazito wengi na familia zao.

Ukweli ni kwamba kuna maambukizi mengi ya virusi, bakteria na fangasi ambayo yanaweza kupatiwa mtoto kipindi cha ujauzito, kama vile Virusi vya Ukimwi, Homa ya Manjano, Tetekuwanga, Rubela na Toxoplasmosis (maambukizi yanayosababishwa kwa kula nyama isiyopikwa vizuri na iliyogusana na kinyesi cha paka).

Hakuna ushahidi unaoonyesha Virusi vya Corona vinaweza kumpata mtoto aliye tumboni kama mama mjamzito anayo maambukizi. Ila kwa sababu virusi hivi ni vipya wanasayansi wanaendelea kuusoma ugonjwa huu taratibu na tutegemee taarifa zaidi hapo mbeleni.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la kujitegemea la Kidaktari liitwalo “The Lancet” ambalo liliwafuatilia wanawake 9 waliopatikana na maambukizi ya virusi hivi baada ya kufanyiwa vipimo nchini China, waligundua hakuna mtoto hata mmoja aliyezaliwa na maambukizi haya (ikumbukwe wanawake hawa wote walijifungua kwa njia ya upasuaji). Ijapokuwa idadi ni ndogo ila inatia matumaini.

Pia hakuna ushahidi ulioonyesha kulikuwa na virusi ndani ya kimiminika cha amnion “Amniotic fluid” hichi ni kimiminika kinachomzunguka na kumlinda mtoto wakati wa ujauzito. Pia hakuna ushaidi uliopatikana ndani ya sampuli za damu zilizochukuliwa kutoka katika kitovu cha kila mtoto. Hali hii inaweza kupendekeza kujifungua kwa njia ya kawaida kwa mjamzito aliye na maambukizi ni njia salama, lakini hatuna majibu ya uhakika kuhusu hili kwasababu idadi ya tafiti zilizofanywa ni ndogo sana.

Kwa tafiti zote hizi inaonyesha kuna ushahidi kidogo kuwa watoto wanaweza kupata maambukizi ya virusi hivi kutoka kwa mama zao wakati wa ujauzito.

Je, ninaweza kumpatia mtoto wangu maambukizi kwa njia ya kunyonyesha?

Hakuna uwazi wa kutosha katika suala la maziwa ya mama, hata hivyo hatuwezi fanya hitimisho kama maziwa ya mama yanabeba virusi au la!

Baadhi ya virusi, kama virusi vya UKIMWI vinajulikana kuenezwa kwa njia ya maziwa ya mama, lakini mpaka tulipofikia hakuna ushahidi kuwa Virusi vya Corona COVID-19 vinaweza kuenezwa kwa njia hii pia.

Ushauri uliopo ni kuwa wamama ambao hawana maambukizi haya waendelee kuwanyonyesha watoto wao ila wakumbuke kunawa mikono yao vizuri kabla na baada ya kuwanyonyesha.

Ikiwa mama ataonekana na dalili za kukohoa au joto kubwa la mwili, ni vizuri atumie njia mbadala ya kunyonyesha (mf: vifaa maalumu vya kukamua maziwa) na kumpatia mtu mwingine asiye na maambukizi kumlisha mtoto mpaka atakapo pona.

Kuna ushahidi wa kutosha kuwa maziwa ya mama ni mazuri kwa kuongeza kinga mwili ya mtoto, hivyo kusitisha moja kwa moja kumnyonyesha mtoto wako kunaweza kumuweka katika  hatari ya kupata maambukizi kwa urahisi.

Kadiri muda unavyokwenda, haitaepukika na tutarajie kushuhudia wanawake wengi wajawazito wakipata virusi vya corona COVID-19, hii itapelekea wanasayansi kuweza kutambua zaidi jinsi kirusi hiki kinafanya kazi na ni kwa namna gani kinamuathiri mjamzito. Kwa sasa kuchukua hatua za kujikinga ni muhimu – kuosha mikono kwa maji tiririka, kuepuka kukaa karibu karibu sana ikiwemo kuepuka maeneo yenye mikusanyiko ya watoto, kukaa nyumbani, kuepuka wageni ni njia zinazohitaji kufuatwa kuweza kuwa salama.

 

IMEPITIWA: 19 MARCH 2020

 

 

Ulaji Bora Kipindi cha Ujauzito

Kuna msemo wa zamani wa ujauzito usemao, “ukiwa mjamzito, unakula chakula cha watu wawili”. Wanawake wengi wanaamini wanaweza kuongeza chakula wanachokula na uzito wa ziada wanaopata utapungua baada ya ujauzito. Hata hivyo, hii sio kweli. Kabla ya ujauzito unatakiwa kula takribani kalori 2000 kwa siku kutegemea na uzito na aina ya kazi yako. Kipindi cha ujauzito kalori unayochukua ndani ya mwili lazima iongezeke kwa karibu kalori 200 kwa siku kuanzia kipindi cha tatu cha miezi mitatu ya ujauzito (Third trimester).

Kalori za ziada zinampatia mtoto nguvu na virutubisho. Zinahitajika pia kwa ukuaji wa plasenta, kuongeza ujazo wa damu, na kujenga maji maji ya ukuta wa uzazi. Pia zinahitajika kusambaza nguvu ya ziada kwenye mwili wako inayohitajika kufanya mambo yote ya ziada ya ujauzito katika mwili wako.

Mwanamke aliye na uzito wa kuzidi mwanzoni mwa mimba yake aendelee kula kalori ya ziada isipokuwa daktari akimshauri vinginevyo. Ujauzito sio mda wa kupunguza uzito au kama moja ya njia ya kuyeyusha mafuta, hii ni hatari kwa mtoto wako. Hata hivyo wanawake walioanza na uzito mkubwa mwanzoni mwa ujauzito, hupungua wakiaanza kufuata maisha yenye afya, ikiwemo vyakula vyenye nyuzinyuzi zitokanazo na mbogamboga, matunda na mbogamboga na protini pungufu na punguzo la fati mbaya. Hawa wanawake watajikuta wanapungua uzito baada ya mtoto kuzaliwa kiurahisi kama wametumia miezi tisa kuwa wenye afya na kuwa katika umbo zuri.

Mwanamke aliye na uzito pungufu inawezekana kuhamasishwa kuongeza uzito wa ziada, ambapo atashauriwa kula zaidi ya kalori 200 zilizopendekezwa, na atashauriwa kuongeza kalori zake anazochukua kwenye vyakula kabla ya kipindi cha tatu cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito. Hii itakua lazima kumruhusu kuwa na ujauzito wa afya na kuwa na uwezo wa kuunga mkono ukuaji mzuri wa mtoto.

Ukiwa umezoea kula milo mitatu kwa siku kabla ya ujauzito, utajikuta ukila milo sita midogo ndani ya siku. Hii haimaanishi kuwa unakula milo mingi, ila ni milo midogo mitatu na vitafunwa vitatu vyenye afya. Hii haisaidi tu kudhibiti kiwango cha sukari ndani ya mwili, lakini pia hurahisisha mmeng’enyo wa chakula.

Milo midogo pia inamsaidia mwanamke anayesumbuliwa na magonjwa ya asubuhi yanayosababisha matatizo machache katika mfumo wa chakula. Wanawake wanosumbuliwa na kukosa choo wanaweza kupata faida na milo midogo midogo kila baada ya masaa machache badala ya kula milo miwili au mitatu mikubwa.

Kama magonjwa ya asubuhi ni makali (kichefuchefu cha asubuhi na kutapika), na hauna chakula cha kutosha mwilini ni hatari kwa afya ya mtoto wako, ni muhimu kuongea na daktari wako kuepuka matatizo wakati wa ujauzito. Kutapika kwa kupitiliza ni vema kuripotiwa kwa daktari mara moja.

Vidokezo vya Urembo Kipindi cha Ujauzito

Ni vipi nitaonekana mrembo kipindi cha ujauzito ni swali wanalokuja nalo wakina mama wengi. Kuna njia kumi sahihi za kukusaidia kufurahia urembo wako hasa katika kipindi maalumu maishani mwako.

 1. Kunywa maji

Kipindi cha ujauzito unahitajika kupata maji mengi kwa siku. Yatakusaidia kusafisha na kutoa taka na sumu mwilini mwako. Zaidi maji yanasaidia kutunza kiasi cha kimiminika kinachotakiwa mwilini mwako. Maji ni muhimu zaidi kwa afya yako na mwanao. Kunywa angalau lita 2 za maji kwa siku.

 1. Mlo sahihi

Unahitaji uangalizi na umakini wa ziada katika chakula unachokula wakati wa ujauzito na afya yako. Inashauriwa kumuhusisha daktari wako kukuandalia ratiba ya aina ya chakula unachotakiwa kula. Fuatilia ratiba hii kwa umakini, kula kwa afya, ikiwa pia ni muhimu kwa ajili ya mtoto wako.

 1. Pata muda wa kulala

Uchovu ni dalili moja wapo anazopata mama mjamzito hasa katika kipindi cha mwanzo. Kupumzika vizuri ni muhimu kwa ajili ya mwili na akili yako mwenyewe. Hakikisha unapata muda mzuri na wa kutosha kupumzika kiasi kwamba mwili wako uwe unahisi uchovu kidogo. Jiweke huru wakati wa kulala. Pumzika kwa usahihi, unaweza kutaka kutumia mito au kitu kingine cha kukuweka huru unapolala.

 1. Uzito sahihi

Unahitajika kuangalia uzito wako kipindi cha ujauzito. Baadhi ya wakina mama wanakula chochote na kila kitu pasipo kuhofia kuhusu uzito. Ikiwa ni kawaida kuongezeka uzito wakati wa ujauzito, si vema kiafya kuongezeka katika njia tofauti. Uzito unaongezeka kwa kula vyakula ambavyo havina msaada mwilini, mara kwa mara kula mlo sahihi, unaweza kumuhusisha daktari wako kwa machaguo bora.

 1. Mazoezi

Ndio, ni muhimu! Kuna mazoezi maalumu kwa ajili ya wajawazito. Hudhuria darasa la mazoezi ya yoga yaliyoandaliwa kwa ajili ya wajawazito, pata muda wa kukutana na wajawazito wengine na kujifunza na kupata uzoefu. Unaweza pia kumuomba ushauri daktari ni michezo gani unaweza kushiriki.

 1. Epuka michirizi

Wakina mama wengi wanalalamika kupata michirizi baada ya kujifungua. Unahitaji kuchukulia uangalizi hili wakati wa ujauzito.  Tumia cream uliyoshauriwa au zinazouzwa kwa ajili ya kuondoa michirizi. Tumia kila siku kuukanda mwili wako. Unaweza pia kutaka kuepuka kukimbia, kuruka au kugonga kama njia ya kuepuka michirizi.

 1. Thamini umbo lako

Pindi unatoka katika matembezi vaa nguo ya kuonyesha umbo lako, umbo la mwanamke ni zuri wakati wa ujauzito, ujauzito unamuongezea hipsi mwanamke. Tumia nafasi hii kuvaa nguo za kushika mwili wako vizuri ili kuonyesha vema hipsi zako.

 1. Uangalizi wa ngozi

Pamoja na yote wakati wa ujauzito, usisahau ngozi yako. Urembo katika kipindi cha ujauzito ikiwemo urembo wa ngozi, kwa kupendelea mimea tiba katika kipindi sahihi. Kutokana na mabadiliko ya homoni kunaweza kuwa na athari kidogo katika ngozi yako. Unaeza kutumia bidhaa za kulinda ngozi kwa kuzingatia aina ya ngozi yako lakini hakikisha hutumii kemikali hatarishi.

 1. Make-Up

Mwanamke hachukizwi na make up! kutokana na mabadiliko ya homoni unaweza kupata madoa usoni hivyo poda ni mkombozi. Make up ndio mkombozi, tena angalia zile ambazo hazitumii kemikali kali.

 1. Pumzika

Mwisho na muhimu zaidi ni kukumbuka kupumzika, weka mapumziko katika ratiba yako. Lala chini kwa muda unapopata nafasi. Pumzisha mwili wako. Ujauzito unaweza kuja na stress sana lakini hakikisha hazikushindi, jinsi unavozidi kupumzika ndivo jinsi unaonekana mrembo.

IMEPITIWA: JUNI 2020

Zifahamu chanjo sahihi. Je, Mtoto wako anazipata kwa wakati?

Chanjo ni nini?

Chanjo huokoa maisha ya hadi watoto milioni 3 kila mwaka. Chanjo hukinga maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.
Kisayansi chanjo ni kitendo cha kupewa kinga mwili kwa njia ya kuamsha vitoa kinga viwe tayari kupambana na adui ambaye wanamjua tayari.

Umuhimu wa chanjo

Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo. Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii. Kinga ya utotoni ni muhimu sana hasa kwa ukuaji wa baadae. Hivyo basi, chanjo kwa mtoto katika mwaka wake wa kwanza na katika mwaka wa pili ni muhimu sana.
Ni muhimu pia, kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa. Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto.
Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu kuwa kutoa chanjo kwa mtoto mgonjwa kidogo au mwenye ulemavu au mwenye upungufu wa lishe ni salama.

Ukweli kwa ajili ya familia na jamii kuhusu chanjo

1. Chanjo ni jambo la lazima. Kila mtoto ni lazima apate chanjo zote zilizopendekezwa. Kinga ya utotoni ni muhimu sana; chanjo katika mwaka wa kwanza na wa pili zina umuhimu wa pekee. Wazazi wote au walezi wengine wanapaswa kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu muda wa kukamilisha chanjo zinazohitajika.

2. Chanjo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mengi hatarishi. Mtoto ambaye hajapata chanjo yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi, ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha.

3. Mama wote wajawazito pamoja na watoto wao wanapaswa kukingwa dhidi ya pepopunda. Hata kama mama aliwahi kupata chanjo kabla , anapaswa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu kama bado anahitaji kupewa chanjo ya pepopunda.

4. Sindano mpya hazina budi kutumika kwa kila mtu anayepata chanjo. Kila mtu anapaswa kudai sindano mpya kwa kila chanjo anayopewa.

5. Ugonjwa huweza kuenea haraka watu wengi wanapokuwa wamekusanyika pamoja. Watoto wote wanaoishi katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa , hasa katika mazingira ya wakimbizi au ya watu waliojikusanya kutokana na janga fulani, wanapaswa kupewa chanjo haraka.

6. Kadi ya chanjo ya mtoto (au ya mtu mzima) haina budi kuwasilishwa kwa mtoa chanjo kabla ya kutolewa kwa chanjo.

Aina za chanjo

BCG (Bacile Calmette-Guérin)
Watoto wote wanastahili kupokea chanjo itwayo BCG (Bacile Calmette-Guérin) vaccine. Hii huumpa mtoto kinga dhidi ya aina zingine za kifua kikuu na ukoma.

DTP au DPT (Dondakoo, Pepopunda na Kifaduro)
Watoto wote wanastahili chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro kupitia aina ya chanjo iitwayo DTP au DPT vaccine. Viini vya dondakoo husababisha maambukizi ya njia ya kuingizia hewa na huenda ikasababisha shida za kupumua na hata kifo. Pepopunda nayo husababisha kukauka kwa misuli na maumivu makali yanayo sababishwa na mkazo wa misuli. Mkazo huo wa misuli unaweza sababisha kifo. Kifaduro huathiri njia ya kuigizia hewa na kusababisha kikohozi kinachoweza dumu wiki nne hadi nane na ni hatari sana kwa watoto wachanga.

Wanawake wote waja wazito na watoto wachanga wanahitaji chanjo ya pepopunda.

Surua
Watoto wote wanastahili kupokea chanjo dhidi ya surua. Maradhi ya surua husababisha utapiamlo, udhaifu wa maendeleo ya ubongo na huweza kufanya mtoto kiziwi au kipofu. Ishara zinazoelekeza kuwa mtoto anaweza kuwa anaugua surua ni pamoja na kuongezeka kwa joto mwilini, upele, kikohozi, kumwaga kamasi na macho kubadilika na kuwa mekundu. Tahadhari, mtoto anaweza kufa kutokana na surua.

Polio
Watoto wote wanastahili chanjo dhidi ya polio. Dalili za polio ni utepe kwenye mguu au mkono na udhaifu wa kukitumia kiungo kilicho athirika. Kwa kila watoto mia mbili wanaoambukizwa maradhi ya polio, mmoja atapata ulemavu wa maisha.

Ratiba za chanjo hutofautiana kulingana na nchi au sehemu ya nchi unayoishi. Ni muhimu kufuatilia ratiba ya chanjo kwa mujibu wa mwongozo wa taifa. Watoto wanastahili kupokea chanjo kwa umri unaostahili na kwa muda unaostahili.
Pamoja na kutofautiana huku kwa ratiba za chanjo kati ya nchi na nchi, unaweza kufuatilia utaratibu uliopendekezwa na CDC (Centre for Disease Control) hapa chini.

Ufuatao ni mtiririko wa chanjo husika na wakati muafaka ambao mtoto wako anatakiwa awe ameshapatiwa.

UMRIAINA YA CHANJOINATOLEWAJEMUHIMU KUJUA
0 – AnapozaliwaKifua Kikuu (BCG)  Sindano bega la kulia  Ni lazima kovu lotokee kwenye bega la kulia baada ya muda  
 Polio (OPV 0)Matone mdomoniChanjo ya ugonjwa wa kupooza ya kuanzia
    
Wiki ya 6Polio (OPV 1)Matone mdomoniChanjo ya kwanza ya ugonjwa wa kupooza
 DTB-HepB-Hib1 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B)Sindano paja la kushotoChanjo ya kwanza ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja.
 PCV 1Sindano paja la kuliaChanjo ya Nimonia ya kwanza
 Rota 1Matone mdomoniChanjo ya Kuhara ya kwanza
    
Wiki ya 10Polio (OPV 2)Matone mdomoniChanjo ya pili ya ugonjwa wa kupooza
 DTB-HepB-Hib2 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B)Sindano paja la kushotoChanjo ya pili ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja.
 PCV 2Sindano paja la kuliaChanjo ya Nimonia ya pili
 Rota 2Matone mdomoniChanjo ya kuhara ya pili
    
Wiki ya 14Polio (OPV 3)Matone mdomoniChanjo ya mwisho ya ugonjwa wa kupooza
 DTB-HepB-Hib3 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B)Sindano paja la kushotoChanjo ya tatu ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja.
 PCV 3Sindano paja la kuliaChanjo ya Nimonia ya tatu
    
Miezi 9Measles (MR 1)Sindano bega la kushotoChanjo ya kwanza ya surua
    
Miezi 15Measles (MR 2)Sindano bega la kushotoChanjo ya pili ya surua

IMEPITIWA: 26 MAY 2020

Kipimo cha Ultrasound Kipindi cha Ujauzito

Kipimo cha Ultrasound ni Nini?

Kipimo cha ultrasound ni uchunguzi unaotolewa kwa wajawazito wengi kabla ya kujifungua. Kinatumia mawimbi ya sauti kuonyesha picha ya mtoto aliyeko tumboni. Kipimo hichi kinamsaidia mtoa huduma kuangalia afya na ukuaji wa mtoto aliye tumboni.

Kipimo cha ultrasound kinamsaidia daktari kuona kama kuna tatizo katika ogani, mishipa na tishu bila kufanya upasuaji. Tofauti na tekinolojia nyingine, ultrasound haitumi mionzi, ndio maana ni njia inayopendekezwa kwaajili ya kuangalia ukuaji wa kijusi kipindi cha ujauzito. Wakati wa kufanya kipimo cha ultrasound ni muhimu sana kwa wajawazito wengi- ni mara ya kwanza unapoweza kumuona mtoto wako. Unaweza kuona mikono, miguu na sehemu nyingine za mwili kulingana na lini kipimo kitachukuliwa na mkao wa mtoto wako tumboni. Utaweza pia kujua jinsia ya mtoto wako.

Wanawake wemgi wanafanya kipimo cha ultrasound katika kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito (second trimester) wiki 18-20 ya ujauzito. Baadhi wanafanya katika kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya ujauzito (kabla ya wiki ya 14 ya ujauzito). Idadi ya vipimo vya utrasound na muda unaweza tofautiana kwa wanawake wenye aina fulani ya matatizo ya kiafya kama asthma na kisukari.

Kuna Tofauti Gani Kati ya Kipimo cha Ultrasound na X-ray?

Ultrasound inatumia mawimbi ya sauti na mwangwi kutoa picha hai, kama video.

X-rays ni njia rahisi na haraka kwa mtaalamu wa afya kutumia kuona viungo vya ndani ya mwili na hali ya mifupa. X-rays zinatumia mionzi kupiga picha ya ogani za ndani ya mwili, na mionzi hiyo ina madhara makubwa kwa afya ya binadamu. Picha zinazopigwa zinafanana na kivuli cha mwili wa ndani wa binadamu.

Kwanini kipimo cha Ultrsound Kinafanyika?

Vipimo hivi vitampatia mama mtarajiwa nafasi ya kumuona mtoto wake ambaye hajazaliwa. Lakini pia kipimo hichi kina kazi nyingine.

Daktari wako atakutaka ufanye kipimo hich kama utakua na maumivu, kuvimba au dalili nyingine itakayo hitaji uchunguzi wa ogani za ndani ya mwili. Ultrasound inaweza kuangalia sehemu za mwili kama vile: kibofu cha mkojo, ubongo (wa mtoto), macho, figo, ini, ovari, bandama, uterasi, korodani, na mishipa ya damu.

Je, Kuna Aina Tofauti za Vipimo vya Ultrasound?

Ndio. Aina ya kipimo inategemea na uchunguzi anaoufanya daktari na ujauzito wako una umri gani. Ultrasound zote zinatumia kifaa kinachoitwa ‘transducer’ kinachotumia mawimbi ya sauti kutengeneza picha ya mtoto wako kwenye kompyuta. Aina kuu mbili za ultrasound ni:

‘Transabdominal ultrasound’: aina hii inafanyika sana kipindi cha ujauzito, mama mjamzito hulala juu ya kitanda kwa mgongo kisha mhudumu wa afya atapaka kimiminika maalumu ‘gel’ juu ya tumbo lako kusaidia mawimbi ya sauti kutembea kwa urahisi na kupata picha nzuri. Baada ya kukupa ‘gel’ atatumia ‘transducer’ kupapasa juu ya tumbo lako. Masaa mawili kabla ya kufanya kipimo hichi ni vizuri kunywa maji glasi kadhaa ili kibofu kiwe kimejaa wakati wa zoezi hili. Kibofu kilichojaa kinasaidia mawimbi ya sauti kutembea kwa urahisi zaidi na kupata picha nzuri. Aina hii ya ultrasound itachukua dakika 20.

‘Trasvaginal ultrasound’: aina hii inafanyika kupitia ukeni (njia ya uzazi). Utalala juu ya kitanda kwa mgongo na kupanua miguu yako. Mtoa huduma ataingiza kwenye uke wako ‘transduce’ nyembemba yenye muonekano kama kijifimbo cha kiongozi wa muziki. Utasikia msuguano kutoka kwenye ‘transducer’ bila maumivu. Katika aina hii ya ultrasound kibofu chako si lazima kijae, itachukua dakika 20.

Mtoa huduma anaweza kutumia aina nyingine za ultrasound kupata taarifa zaidi lakini mara nyingi ni kwa jambo muhimu:

‘Doppler ultrasound’: aina hii inatumika kuangalia usambazaji wa damu kwa mtoto wako ikiwa sio mzuri. ‘Transducer’ itatumika kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto wako na kupima usambaaji wa damu kwenye kitovu cha kichanga na baadhi ya mishipa ya damu ya mtoto wako. Matumizi ya aina hii ya ultrasound yanatumika kuangalia kama una aina fulani ya ugonjwa wa damu (Rh disease) ambao unaleta matatizo makubwa kwa mtoto kama hautatibiwa. Kipimo hichi kinaweza kufanyika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, lakini kinaweza kufanyika mapema zaidi.

‘3-D ultrasound’: kinachukua picha elfu moja kwa wakati mmoja, inaweza chukua picha ya kuonekana vizuri kama picha za kawaida. Kipimo hichi kinatumika kuhakikisha ogani za mtoto zinakua na kuendelea vizuri. Kinaangalia kasoro katika uso wa mtoto na matatizo katika mfuko wa uzazi.

‘4-D ultasound’: ni sawa na 3-D, ila hiki kinaonyesha mwondoko wa mtoto wako katika video.

Maandalizi ya Kufanya Kipimo cha Ultrasound Kipindi cha Ujauzito

Kabla ya kufanya kipimo hichi, utaambiwa unywe maji mengi na kubana mkojo wako kwa kipindi fulani ili kibofu chako kiwe kimejaa mda wa uchunguzi. Hii ni muhimu kwa vipimo vya ujauzito mchanga, kibofu kilichojaa kinasukuma mfuko wa uzazi juu ili picha za mtoto zipatikane kwa urahisi zaidi.

Mtoa huduma au daktari atakayeshughulikia suala zima la kufanya kipimo cha ultrasound atakupa maelekezo ya mda gani kabla ya kipimo unywe maji na kiasi gani cha maji unywe.

Kwa kawaida ultrasound hazina maumivu. Unaweza kuona usumbufu wakati kibofu chako kimejaa au wakati wanafanya ‘transvaginal ultrasound’.

Nini Kinatokea Wakati wa Ultrasound?

Wakati wa ultrasound utapakwa kimiminika maalumu ‘gel’ kwenye tumbo lako na kifaa maalumu kinachotoa na kupokea mawimbi ya sauti ‘transducer’ kitapitishwa juu ya Ngozi yako. Mawimbi ya sauti yanatua juu yam too na maeneo mengine ndani ya mwili, kutengeneza picha kwenye skrini ya TV.

Ultrasound zinazofanyika mimba ikiwa change zinatakiwa kufanyika kwa njia ya uke ‘transvaginally’. Hii ina maanisha badala ya kutumia ‘transducer’ juu ya ngozi ya tumbo la chini, kifaa chembamba kitaingizwa taratibu ukeni na kuchuka picha za mtoto.

Mtaalamu wa huduma hii anaweza kukuonyesha baadhi ya picha za mtoto wako kwenye skrini na kutoa kopi baadhi kwaajili yako. Picha hizi zitaangaliwa pia na mkunga wako.

Je, Unahitaji Kufanya Kipimo cha Ultrasound Mara Ngapi Kipindi cha Ujauzito?

Ikumbukwe kuwa itakuwa ngumu kuona chochote katika wiki chache za kwanza za ujauzito, ila kijusi kitaanza kuonekana zaidi wiki ya 13.

Wanawake wengi wanajiuliza mara ngapi anatakiwa kufanya kipimo cha ultrasound? Inatofautiana kulingana na mama na ujauzito wake, zifuatazo ni baadhi ya vipimo vya ultrasound unavyoweza kutarajia:

Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

Kipimo cha kwanza kinaweza kufanyika kati ya wiki ya 6 mpaka ya 8. Lakini baadhi ya madaktari wanafanya kipimo hichi kama uko katika hali hatari ya ujauzito. Hali hizi ni pamoja na maumivu ya tumbo la chini, kutoka damu na historia yoyote ya kasoro baada ya kuzaliwa mtoto au mimba kuharibika.

Kipimo kingine (dating scan) kinashauriwa kufanyika kwa wanawake wajawazito wasio na uhakika wa umri wa ujauzito wao na lini wanatarajiwa kujifungua, hii inasababishwa na uwepo wa mzunguko wa hedhi usio wa kawaida. Majibu ya kipimo cha ultrasound yatasaidia kuthibitisha umri wa ujauzito na kumpatia mama rekodi za uhakika. Vilevile matokeo ya kipimo hichi yanaweza kumuonyesha kama mama ana ujauzito wa mtoto mmoja au mapacha. Kipimo hichi kinaweza kufanyika kuanzia wiki ya 10-13 ya ujauzito.

Ndani ya kipindi hichi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito kipimo kingine cha ultrasound (nuchal translucency scan) kinafanyika kwa wajawazito kati ya wiki 14-20 ya ujauzito. Kipimo hiki kinafanyika pamoja na kipimo cha damu kwa nia ya kutambua kama mtoto yuko na hatari ya kuwa kasoro za maumbile (down syndrome). Kama majibu yataonyesha kuna hatari zaidi vipimo vingine vitafanyika zaidi.

Miezi mitatu ya pili ya ujauzito

Wiki ya 18 mpaka 20 kipimo cha ultrasound kinashauriwa kufanyika ili kuangalia ukuaji wa mtoto. Vipimo tofauti vitafanyika kuangalia ukuaji na maendeleo yam toto. Kijusi kitatathminiwa kama kina aina yeyote ya kasoro katika kichwa, miguu, moyo na ogani nyingine ndani ya mwili.

Katika hatua hii ya ujauzito jinsia ya mtoto inaweza kugunduliwa. Inaweza kuwa vigumu kuona sehemu za siri za mtoto ikiwa mtoto amekaa vibaya tumboni.

Uchunguzi wa mlango wa uzazi, kiasi cha uoevu wa amnion (amniotic fluid) na nafasi ya placenta katika mfuko wa uzazi utafanyika .

Miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito

Kipimo cha ultrasound baada ya wiki ya 35 ni salama zaidi na cha uhakika zaidi kukuhakikishia kuwa mtoto wako anakua kawaida.

Lakini pia, ikiwa ujauzito wako uko katika hatari kubwa kwa mfano kama una shinikizo kubwa la damu, kisukari, unatoka damu, kiasi kidogo cha uoevu wa amnion, una dalili za kujifungua kabla ya wakati, umri zaidi ya miaka 35, daktari anaweza kufanya kipimo cha ultrasound ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto ni nzuri. Kipimo cha ultrasound wakati huu kitasaidia kutathmini kama mtoto amekaa mkao unaotakiwa tumboni au amegeuka. Na njia gani ya kujifungua itumike kama mtoto amegeuka.

Licha ya hayo, kipimo cha ultrasound katika kipindi hiki hakiwezi onyesha siku ya uhakika ya kujifungua na uzito wa mtoto.

Kumbuka:

Inapendekezwa kwa wanawake wenye ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja au wanapatwa na kutoka damu ukeni mara kadhaa kufanya kipimo cha ultrasound mara kwa mara.

Sababu / Faida za Kufanya vipimo vya Ultrasound Kipindi cha Ujauzito

 • Kuthibitisha ujauzito.
 • Kuangalia kama una mtoto zaidi ya mmoja.
 • Kuweka tarehe ya kujifungua kwa kuangalia umri na ukuaji wa mtoto.
 • Kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto, hali ya misuli, mwondoko na ukuaji kwa ujumla.
 • Kupima ovari na mfuko wa ujauzito.
 • Kufuatilia ujauzito uliotungika nje ya mfuko wa uzazi.
 • Kutathmini hatari za mtoto aliyepatikana na kasoro za maumbile kama ugonjwa wa ‘down sydrome’
 • Kuangalia ukuaji wa kimwili wa mtoto na kuangalia kama anakua ipasavyo.
 • Kuangalia kiasi cha uoevu wa amioni (amniotic fluid) kinachomzunguka mtoto katika mfuko wa uzazi.
 • Kutambua nafasi ya plasenta.
 • Kuangalia mkao wa mtoto kabla ya kujifungua.

Hasara za kufanya kipimo cha ultrasound

Ultrasound ni salama kwako na kwa mtoto ikiwa itafanywa vizuri na mtoa huduma mwenye ujuzi nayo. Ultrasound ni kipimo salama zaidi kuliko X-rays kwasababu kinatumia mawimbi ya sauti badala ya mionzi.

Kama ilivyo kama vipimo vingine, kipimo cha ultrasound hakiwezi kuona kila tatizo. Wakati mwingine kinakosea kugundua baadhi ya kasoro.

IMEPITIWA: 28 APRILI 2020.

Vidokezo Vitakavyomsaidia Mama Kupona Haraka Baada ya Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji.

Kujifungua salama ni muda wa furaha sana. Ni wakati unaofanikiwa kukutana na mtoto aliyekuwa anakua ndani yako kwa kipindi cha miezi tisa. Lakini pia kujifungua inaweza kukugharimu, hususa kama umejifungua kwa njia ya upasuaji. Itakuchukua mda mrefu kupona kuliko aliyejifungua kwa njia ya kawaida.

Ufuatao ni ushauri utakao kumsaidia mama aliyejifungua kwa njia ya upasuaji kupona haraka, ili upate muda wa kutosha kumjua na kumlea mtoto wako mchanga.

Pata Mapumziko ya Kutosha.

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni upasuaji mkubwa. Kama ilivyo upasuaji mwingine, mwili wako unahitaji mda wa kupona baada ya hapo. Tegemea kubaki hospitali kwa siku tatu mpaka nne baada ya kujifungua (au zaidi ya hapo kama kulitokea tatizo lingine la kiafya), kisha upe mwili wako wiki sita kupona kabisa.

Ni rahisi kusema zaidi ya kutenda. Ni vigumu kwenda kulala kwa masaa kadhaa huku una mtoto anayehitaji uangalifu mwingi kutoka kwako.

Huenda umesikia ushauri huu wa “lala kila mtoto wako akilala” kwa marafiki na ndugu zako wa karibu. Wako sahihi. Jaribu kulala kila mtoto anapolala. Omba msaada wa kubadilisha nepi na kazi mbalimbali za nyumbani kwa rafiki na ndugu zako wa karibu ili upate muda wa kupumzika kidogo pale inapowezekana. Dakika chache za kupumzika hapa na pale katikati ya siku zinasaidia.

Uangalie Mwili Wako

Kuwa makini zaidi kila unachofanya huku ukiendelea kupona. Epuka kupanda na kushuka ngazi kadiri uwezavyo. Weka mahitaji muhimu ya mtoto na wewe (chakula, nepi, kanga,nguo zako na mtoto) karibu na wewe ili usiamke kila mara.

Usinyanyue kitu chochote kizito zaidi ya mtoto wako. Omba msaada kwa mpenzi/mme wako au rafiki au ndugu yako.

Ni vizuri ukashika sehemu ya kidonda kila unapokohoa au kupiga chafya.

Inaweza kukuchukua mpaka wiki nane kurudia ratiba zako za kwaida. Ni vizuri kumuuliza daktarin wako lini inafaa wewe kufanya mazoezi tena, kurudi kazini na kuendesha gari. Pia subiria mpaka daktari atakapo kuruhusu kujamiana tena.

Epuka mazoezi mazito, ila unaweza kufanya mazoezi mepesi kama kutembea taratibu kila unapoweza. Mzunguko huu utasaidia mwili wako kupona na kuzuia tatizo la kukosa choo na damu kuganda. Pia kutembea ni moja ya njia ya kumtambulisha mtoto katika ulimwengu.

Kama unavyoangalia afya yako ya mwili usisahau hali ya hisia zako. Kuwa na mtoto inaleta hisia ambazo hujawahi kutarajia. Kama ukisikia kuchoka,huzuni au kuvunjika moyo usizipuuzie hisia hizo. Ongea na rafiki yako wa karibu,mwenzi wako, daktari yako au hata mshauri nasaa.

Punguza Maumivu Yako ya Mwili

Katika wakati huu unaonyonyesha, ni vema kumuuliza daktari au mkunga wako dawa gani ya maumivu unaweza tumia.

Kulingana na kiwango cha maumivu, daktari atakuandikia dawa ya kupunguza maumivu au kukushauri utumie dawa za kutuliza maumivu kama ibuprofen (Advil,Motrin)

Unaweza kutumia mpira wa maji ya moto kupunguza maumivu katika eneo la mshono na tumbo la chini kwa ujumla, hakikisha unatumia maji ya uvuguvugu.

Lenga katika Ulaji wa Lishe Bora.

Lishe bora ni muhimu katika miezi baada ya kujifungua kama ilivyokuwa kipindi ukiwa mjamzito. Bado wewe ni chanzo kikuu cha virutubisho kwa mwanao kama unanyonyesha. Kula vyakula vya kila aina itasaidia mtoto kukua katika afya na nguvu.

Utafiti unaonyesha ulaji wa mbogamboga za majani wakati unanyonyesha unasaidia kuyapa maziwa ladha ambayo inaongeza kasi ya mtoto kunyonya na kufurahia maziwa ya mama kadiri anavyokua.

Pia kunywa vimiminika vingi, hususani maji. Unahitaji vimiminika vya ziada kuongeza upatikanaji wa maziwa na kuzuia kukosa choo.

Wasiliana na Daktari Endapo:

Bado utapata maumivu katika eneo la mshono, unaweza kutoka damu au kutoka usaha mpaka wiki ya sita baada ya upasuaji. Hii ni kawaida.

Lakini dalili zifuatazo zinakupa  haki ya kuwasiliana na daktari wako, kwasababu zinaweza kuwa ishara za maambukizo:

 • Kuvimba, uwekundu, au usaha kutungika katika mshono
 • Maumivu kuzunguka mshono
 • Homa kali zaidi ya 38⁰C (100.4⁰F)
 • Usaha wenye harufu mbaya kutoka ukeni
 • Kutoka damu nyingi ukeni
 • Kuvimba au uwekundu katika ngozi ya miguuni
 • Kupumua kwa shida
 • Maumivu ya kifua
 • Maumivu ya matiti

Pia wasiliana na daktari wako kama unasikia huzuni na unyonge.

Mwisho kabisa, kama una rafiki au ndugu ambaye alipitia hali hii ya kujifungua kwa njia ya upasuaji, usijilinganishe nao. Kila mwanamke ana uzoefu wa tofauti katika njia hii ya kujifungua. Lenga katika kupona na upatie muda mwili wako kurudia hali yake ya awali.

IMEPITIWA:02 APRIL 2020

Begi la Hospitali Unapokwenda Kujifungua

Nini cha kufungasha kwenye begi la hospitali?

Sasa ni wakati wa kukusanya vitu muhimu utakavyohitaji wakati wa uchungu na kujifungua na baada ya mtoto kuzaliwa, hivyo andaa begi lako wakati unakaribia wiki ya 36 ya ujauzito. Hospitali zinaweza kutofautiana kanuni na sheria za kipi unapaswa kubeba na kipi hakiruhusiwi,wasiliana na mkunga wako kufahamu mambo muhimu ya kuongeza kwenye orodha ya mahitaji ya begi la hospitali.

Ni nini nifungashe kwaajili ya uchungu?

Mpango wa kujifungua na kumbukumbu za uzazi ulizoandika pembeni. Mfuko wenye vifaa vya kujifungulia mama unaopatikana kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya serikalini nchini kwa bei ya shilingi 21000/=. Mfuko huo una:

 • Mipira ya mikono (surgical gloves 4 pairs)
 • Taulo ya kike ya uzazi (maternanity pad)
 • Pamba kubwa (cotton wool gm.500)
 • Nguo ya mtoto (cloth material for new born)
 • Vibana kitovu (2 umbilical cord clamp)
 • Mpira wa kuzuia uchafu
 • Nyembe za kupasulia(surgical blades0
 • Nyuzi za kushonea
 • Bomba la sindano
 • Dawa ya kuongeza uchungu (Misoprostol)

 

Pia ni vyema kufungasha vitu vifuatavyo: 

 • Gauni (dera) ambalo litakusaidia wakati unaugulia uchungu ukiwa unazunguka korido za hospitali. Pia utahitaji lingine baada ya kujifungua, na vema likawa lepesi.
 • Kandambili au malapa rahisi kuvaa na kuvua.
 • Soksi, amini usiamini unaweza hisi baridi miguuni wakati wa uchungu.
 • Gauni lililochakaa kidogo(kuukuu) ya kuvaa wakati wa kujifungua. Haina haja ya kununua gauni jipya wakati wa kujifungua maana unaweza kuchafuka sana wakati uko chumba cha kujifungulia.
 • Mafuta laini(mafuta ya nazi au nyonyo) ya kupaka mwilini ikiwa utapendelea kukandwa wakati wa uchungu.
 • Mafuta maalum(lip balm) ya kupaka midomo, midomo yako inaweza kukauka haraka wakati uko chumba cha kujifungulia.
 • Vinywaji au vitafunio kwaajili yako wakati uko kwenye uchungu. Vinywaji vya kuongeza nguvu ni vizuri au unaweza kutumia glukosi kukusaidia kuendelea.
 • Vitu kama jarida, kitabu au kompyuta ndogo vya kukusaidia kujiburudisha au kukusaidia muda kwenda.
 • Kama una nywele ndefu, vibanio maalumu vya kubana nywele ni muhimu.
 • Mito,ikiwa hospitali inaruhusu, ni vyema kubeba mito ya ziada kutoka nyumbani itakayokusiadia kusikia nafuu.
 • Kama muziki ni moja ya kiburudisho chako ni vyema kubeba simu yenye chaji ya kutosha au “MP3 player”.

 

Mwenza wangu wakati wa kujifungua afungashe nini?

 • Kimiminika cha kupunguza joto (water spray) au feni ya mkononi ya kupunguza joto wakati ukiwa kwenye chumba cha kujifungulia.
 • Viatu salama na vyepesi vya kuvaa wakati mnazunguka kwenye korido.
 • Nguo za kubadilisha.
 • Mirija ya kusaidia kukunywesha maji au kinywaji chochote wakati wa uchungu.
 • Simu na chaja. Simu yenye “stopwatch” au “timer” inaweza kusaidia kujua baada ya muda gani mibano ya misuli ya uterasi (contractions) itaatokea. Mibano ya misuli ya uterasi (contractions) hutokea kwa muda na kurudia tena baada ya muda wakati wa kujifungua. Au kama simu ni ya kupapasa kuna “app” maalumu za kuweza kufanya kazi hii.
 • Kamera ya kidigitali au kamera ya simu, kwaajili ya kuchukua picha au video fupi kama utapendelea wakati wa kujifungua au mda mchache baada ya mtoto kuzaliwa.
 • Vitafunwa na vinywaji. Hutapendezwa msaidizi wako wa kujifungua akiwa na njaa au kiu mbele yako. Akifungasha kinywaji na kitu cha kula ataweza kukaa na wewe zidi kuliko kutoka na kutafuta chakula

Ni nini nifungashe kwaajili ya baada ya kujifungua?

 • Nguo ya kwenda nyumbani. Utahitaji nguo nyepesi na isiyobana kuvaa wakati ukiwa hospitalini na safari ya kwenda nyumbani. Itachukua mda tumbo lako kurudi kama awali, hivyo utahitaji kuvaa nguo za uzazi kwa muda.
 • Muongozo jinsi ya kuanza kunyonyesha,ambayo utaupata wakati wa kliniki za awali na mkunga wako.
 • Sidiria za kunyonyeshea, fungasha mbili au tatu.
 • Vitambaa malumu vya kukinga maziwa yasimwagike.
 • Pedi za uzazi au vitambaa maalumu ambavyo vinaweza kusaidia.
 • Gauni la kulala ambalo linafunguka mbele,litakusaidia siku za kwanza wakati wa kunyonyesha.
 • Mahitaji ya kuoga na usafi wa mwili kama sabuni, mafuta, mswaki na dawa ya mswaki, manukato mapole ya makwapani(deodorant).
 • Taulo na chanuo.
 • Chupi za zamani au chupi za kutupwa baada ya kutumika. Chupi mpya na nzuri zinaweza kuchafuka sana wakati wa kujifungua. Chupi kubwa za pamba ni nzuri hasa kama utafanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, hazitasugua na kutonesha kidonda.

Nifungashe nini kwaajili ya mtoto?

 • Nguo tatu au nne za kulala na vesti.
 • Blanketi la mtoto, jaokua hospitali inaweza kuwa na joto, mtoto wako atahitaji blanketi kama kutakua na baridi wakati wa kuondoka.
 • Vitambaa vya kumfuta mtoto akicheuwa.
 • Jozi moja ya soksi.
 • Nguo moja kwaajili ya kusafiria kurudi nyumbani.

Manunuzi Muhimu Kipindi cha Ujauzito Unapokaribia Kujifungua

Manunuzi kwa ajili ya mtoto mchanga

Mahitaji muhimu kwa ajili ya mtoto mchanga katika tarehe za mwanzo katika mwezi aliozaliwa tangu siku ya kwanza.

 1. Mahitaji ya mlo

Ni wazo zuri kama utamnyonyesha mwanao. Lakini kutokana na maisha ya sasa akina mama wengi wanapendelea  kumtengenezea mlo  tofauti  utahitaji kufuata kanuni, mahitaji hayo ni kama:

 • Maziwa ya unga
 • Chupa 6 za maziwa
 • Kiosha chupa na begi la kuhifadhia
 • Brashi ya kusafisha chupa pamoja na maji ya uvuguvugu
 • Eproni
 • Mto
 • Kitambaa cha kumkinga mtoto akicheua

Kama utaamua kumlisha maziwa yako kwa chupa utahitaji kitu cha kukamulia maziwa na vifaa vingine kama kiosha chupa na begi la kuhifadhia. Kusafisha chupa kwa majimoto ni muhimu sana hasa katika chupa anazotumia mtoto. Unapaswa kusafisha vema hizo chupa ili kuepuka kubeba uchafu  na maambukizo mengine yanayotokana na uchafu wa muda mrefu.

 1. Mavazi ya msingi

Kwa siku za mwanzo mtoto atahitaji mavazi mengi, hivyo hakikisha umenunua mavazi ya kutosha. Zingatia yafuatayo unaponunua mavazi kwa ajili ya mtoto;

 • Nguo za kipimo chake ingawa anakua kwa haraka
 • Ovaroli zenye mikono mirefu na mifupi ambazo zina vifungo katikati
 • Gloves 2 za mikono ili kumlinda mtoto asijikwaruze
 • Jozi 6 za viatu na soksi pamoja na nguo za kulalia
 • Jozi 6 za nguo za kutokea unapokwenda kuwaona ndugu na marafiki.
 • Kofia 2 za pamba kumlinda mtoto masikio na kichwa kipindi cha baridi.
 • Kwa kutegemea hali ya hewa, nunua jozi 2 za sweta au jaketi.

Nguo za mtoto zisafishwe na kuhifadhiwa sehemu salama kuzilinda kutokana na uchafu.

 1. Malazi

Pindi tuu unaporudi nyumbani mtoto wako atahitaji sehemu ya kupumzikia , unaweza kuchagua sehemu kwa ajili yake pembeni ya kitanda chako. Hakikisha umepata mpangilio wa kitanda kabla ya kichanga  kufika nyumbani. Uangalizi uchukuliwe kabla ya kununua neti,  hakikisha unapata bora na salama. Mahitaji sahihi katika kitanda cha mtoto ni;

 • Kitanda chenye ubora
 • Shuka2 hadi 3 za kufiti
 • Shuka3 hadi 4 zisizopitisha maji
 • Blanketi 3 za pamba

Kama utaenda kuazima au kununua kwa mtumba ni vema kuangalia zilizo bora.

 1. Mahitaji muhimu ya usafi wa mwili

Vifaa kwa ajili ya kumfanya kichanga awe salama na huru wakati wa kuoga. Utalazimika kuwa na vitu vifuatavyo;

 • Kuandaa sehemu salama kwa ajili ya kuoga, utatakiwa kununua beseni.
 • Taulo 2 za kuogea na pakiti 2 za sabuni ya kufulia nguo za mtoto
 • Shampuu ya mtoto na sabuni ya kumuogeshea mtoto wako
 • Losheni na mafuta ya kumpaka mtoto baada ya kuoga
 • Brashi ya kuchania nywele au seti ya vitana na vikatia kucha
 • Usimpulizie manukato mtoto mwilini.

Manunuzi Muhimu ya Mama Baada ya Kujifungua

Mahitaji ya mama baada ya kujifungua.

 • Nguo zenye kukuweka huru: kama dera, gauni kubwa na taiti za wazazi.
 • Taulo za mama wazazi: baada ya kujifungua unaweza ukatoka damu ukeni kwasababu ya kuvunjika ukuta wa mji wa mimba na inaweza dumu wiki mbili au mpaka wiki sita.
 • Maji na vinywaji vya kutosha: mama anahitaji kuwa na maji mengi mwilini.
 • Taulo za kutumia wakati wa kunyonyesha: mara baada ya kujifungua maziwa yanaweza jaa na kuvuja, uwepo wa taulo utakusaidia kukinga chuchu maziwa yasivuje.
 • Brazia za kunyonyeshea: chombo cha kujisaidia mara baada ya kutoka hospitali,kujisaidia inaweza kuwa ngumu. Chombo maalumu kitafanya urahisi wakati wa kukojoa.
 • Dawa za kulainisha choo: baada ya kujifungua kupata choo ni ngumu hivyo ongea na mkunga wako au daktari kupata matibabu mapema.

Manunuzi Muhimu ya Mtoto Baada ya Kujifungua

Mahitaji Muhimu ya Mtoto

 • Diapers (Nepi)

 

 • Wipes (taulo zenye maji): kwaajili ya kumfuta mtoto akijisaidia haja kubwa na haja ndogo.

 

 • Sabuni nzuri kwaajili ya kufulia nguo za mtoto: watoto wanazaliwa na ngozi nyeti, ni vyema kuchagua sabuni nzuri na yenye harufu nzuri katika ufuaji wa nguo za mwanao.

 

 • Mto wa kumbebea mtoto: mto huu utasaidia kuleta ahueni kwa mama hasa mgongoni, uti wa mgongo na mikono. Pia kwa wamama waliofanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua unasaidia kupunguza mgandamizo kwenye kidonda. Dhumuni la kwanza la mto ni kumleta mtoto karibu na wewe na karibu na maziwa hasa wakati wa kumnyonyesha. Ni muhimu kuwa na mto ili kumsaidia mtoto kunyonya vizuri bila usumbufu.

 

 • Vitambaa vya kumfuta mtoto: watoto wanacheuwa kila wakati, ni vizuri kuandaa vitambaa maalumu kwaaji;o ya kumfuta kila saa anapocheuwa au kutema mate.

 

 • Bebeo la mtoto: sio kila mda utambeba mwanao akikuhitaji. Kuna mda utahitaji kutumia mikono yako, hivyo ni vizuri kutafuta bebeo la kumbebea.

 

 • Chupa za mtoto: kama bado hujanunua chupa kwaajili ya kulishia mtoto maziwa na maji miezi sita ikifika, ni wakati mzuri wa kununua sasa.

 

 • Pampu ya titi: kama utawahi kurudi kazini na mtoto hajafika wakati wa kuanza kula vyakula vingine, pampu ya titi itakusaidia kukamua maziwa kwaajili ya baadae ukienda kazini. Kumbuka maziwa hayo yaliokamuliwa ni vema yakahifadhiwa katika hali ya joto na kupewa mtoto katika hali ya uvuguvugu. Unaweza tumia maji ya moto kuhifadhi.

 

 • Sabuni ya mtoto: ni vizuri kutumia sabuni maalumu za watoto kama family for baby au nyingineyo.ikiwa sabuni hizi zimemkataa mtoto jaribu kutumia sabuni ya kipande kama jamaa. Epuka sabuni zenye marashi makali kwa mtoto.