Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Umuhimu wa Mazoezi Kabla na Baada ya Kujifungua

Afya yako baada ya kujifungua inabainishwa na mwili wako kabla ya kujifungua. Hivyo basi, inashauriwa mwanamke kufuata utaratibu mzuri wa mazoezi mara kwa mara kabla ya kushika ujauzito ili kuanda mwili wake kukabiliana na kazi nzito itakayokuja wakati wa uchungu na kujifungua. Mwanamke ambaye alikua imara katika mazoezi atakuwa na uchungu wa mda mfupi kuliko mwanamke ambaye hakuwa imara katika mazoezi. Habari nzuri ni kwamba unaweza kuanza aina yeyeote ya mazoezi, hata kama haujawahi kufanya mazoezi.

Faida za Mazoezi

 • Yanapunguza kubana kwa misuli na msongo wa mawazo.
 • Yanapunguza maumivu ya mgongo.
 • Yananyoosha misuli na kuandaa mwili kwaajili ya siku ya kujifungua
 • Yanaimarisha mzunguko wa damu
 • Yanaimarisha uzazi (uwezo wa kupata ujauzito)
 • Yanaimarisha muonekano na mkao wa mwili.
 • Yanaimarisha ustahimili, wepesi na stamina ya mwili.

Fanya mazoezi mara 4 mpaka 5 kwa wiki ukizingatia mazoezi ya kuimarisha pumzi badala ya mazoezi ya kupunguza mwili. Kujinyoosha, kuogelea, kukimbia na kutembea yajumuishwe katika mpango wa mazoezi.

Muongozo wa Mazoezi Kabla ya Kujifungua

 • Epuka aina yeyote ya mazoezi yayohusisha kuruka na kusababisha majeraha/ kuumia katika tumbo.
 • Epuka mazoezi yanayofanya moyo kwenda kasi sana au kutoka jasho sana.
 • Epuka mazoezi ya kukata tumbo (sit-up & crunches).
 • Epuka kujinyoosha kupitiliza. Inaweza kusababisha jeraha linalotokana na kuachia kwa kiungo cha mwili.
 • Usibane pumzi wakati wa aina yeyote ya mazoezi.
 • Ujauzito unapoendelea kukua, mazoezi yote yapunguzwe na kuweka kikomo mazoezi yote yanayosababisha kupumua kwa nguvu miezi ya mwisho.

Muongozo wa Mazoezi Baada ya Kujifungua

Baada ya kujifungua sio mda wa kuutesa mwili, uruhusu mwili upone kabla ya kuanza mazoezi. Baada ya kupata kibali kutoka kwa daktari au mkunga, unaweza kuanza na mazoezi mepesi ndani ya nyumba yanayozingatia kunyoosha sehemu ya tumbo. Unaweza kujumuisha matembezi mepesi. Mazoezi yatakusaidia kurudia mwili wako wa awali kabla ya ujauzito.

 • Anza mazoezi ya kunyoosha tumbo lako ukiwa bado ndani ya nyumba yako.
 • Jumuisha matembezi mepesi
 • Baada ya miezi mitatu baada ya kujifungua, anza kujumuisha mazoezi ya kuimarisha pumzi na kutoa jasho kama kuogelea. Kama unapendelea kutumia vifaa wakati wa mazoezi unaweza kuanza kutumia pia, kumbuka isiwe vyuma vya kunyanyua.
 • Yoga inaweza kujumuishwa kwenye mpango wako wa mazoezi baada ya miezi mitatu.
 • Epuka mazoezi makali kama kukimbia na kuruka.
 • Epuka kunyanyua vyuma vizito na kujinyoosha sana.

Lishe

 • Hakikisha mwili una maji ya kutosha wakati wote.
 • Mama anatakiwa kula kawaida bila kuruka milo. Anatakiwa kujumuisha vyakula vinavyosaidia utengenezaji wa maziwa ya kutosha katika mlo wake.
 • Kula vyakula vyenye protini, mbogamboga za kijani za majani, vyakula jamii ya mikunde na matunda kwa wingi.
 • Kunywa angalau glasi moja ya maji kabla ya kunyonyesha.

Mazoezi na Vidokezo vya Kupunguza Tumbo Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji

Ingawa kuwa mama ni jambo zuri na la kujivunia, wamama wengi wapya wanajaribu kurudia mwonekano wao kabla ya kujifungua. Walakini, baada ya kujifungua kwa upasuaji mwili wako unahitaji muda kupona kwanza. Kujilazimisha kupungua uzito ni hatari, kunaweza kusababisha matatizo yasiyo hitajika. Katika Makala hii, tutakupatia baadhi ya njia salama na madhubuti za kupunguza tumbo baada ya kujifungua kwa upasuaji.

Unatakiwa kusubiri mda gani mpaka kuanza mazoezi?

Kwanini?

Madaktari wanashauri kusubiria wiki 6 mpaka 8 kabla ya kuanza mazoezi yeyote. Usiposubiria mwili wako kupona vizuri unaweza kupata matatizo hatari kama vile:

 • Kutoka damu kwa wingi
 • Majeraha ya viungo na misuli
 • Mshono kufunguka

Hivyo, pata maoni ya daktari kwanza kabla ya kuanza kufanya mazoezi.

Vidokezo vya Kupunguza Tumbo Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Kazi ya kuhakikisha tumbo lako linapungua inaweza kuonekana ngumu na isiyo na matumaini, lakini tunakuhakikishia, ni rahisi kufanikishwa kwa vidokezo hivi:

Pata “massage”

Wiki mbili baada ya kujifungua, ni salama kufanyiwa “massage”. Kufanyiwa massage kutasaidia kuvunjavunja fati iliyopo maeneo ya tumbo na kupunguza majimaji kutoka kwenye vifundo (lymph nodes) vinazopatikana katika shingo, kifua, makwapa, nyonga na tumbo. Lakini, epuka eneo la mshono siku za awali, badala yake zingatia maeneo ya mgongo, mikono na miguu. Wiki nne baada ya mshono kuanza kupona, “massage” eneo la tumbo inaweza kufanyika bila maumivu.

Tembeza mwili wako.

Kuchanwa katika baadhi ya misuli ya tumbo kunapelekea ukusanyikaji wa fati kwenye tumbo lako. Hii inasababisha shinikizo katika misuli yako ya tumboni na sakafu ya nyonga. Hivyo ni muhimu kusubiri wiki 6-8 kabla ya kujaribu mazoezi mazito. Kutembea ni zoezi rahisi linalounguza kalori nyingi kwa njia salama. Nenda kwenye matembezi na mtoto wako angalau mara tatu kwa wiki.

Kula mlo wenye afya

Mama wote wanaonyonyesha wanahitaji nguvu ya kutosha. Hakikisha mlo wako una kabohaidreti kwa wingi, fati kidogo na madini na vitamini muhimu za kutosha. Epuka vitu vitamu na vyakula vya kuangwa na mafuta mengi na soda. Kula matunda mengi, mbogamboga na protini. Inashauriwa kurekodi chakula unachokula kwa siku na kiasi cha kalori, kwa kufanya hivi itakusaidia kudumu katika kipimo cha kueleweka cha chakula chako.

Funga tumbo

Unaweza kufunga tumbo baada ya mshono kupona vizuri.

Kunyonyesha

Hii ni njia rahisi ya kupoteza tumbo. Mnyonyeshe mwanao miezi 6 baada ya upasuaji. Kunyonyesha kunaunguza takribani kalori 500 kwa siku, lakini pia homoni ya “oxytocin” inatolewa wakati wa kunyonyesha inayochochea mibano ya uterasi, na kusaidia uterasai kurudia saizi yake ya awali kabla ya ujauzito.

Kunywa maji na vimiminika vya kutosha

Unywaji maji baada ya kujifungua utakusaidia kuweka uwiano wa maji katika mwili wako, vilevile kuunguza fati iliyozidi kuzunguka kiuno chako. Maji yenye limao ni njia rahisi ya kupunguza uzito wako na kusafisha mwili wako. Changanya juisi ya limao, asali na maji ya moto kisha kunywa mara moja kwa siku, inafaa zaidi asubuhi.

Pata usingizi wa kutosha

Njia nyingine ya kufikia lengo la kupoteza tumbo baada ya upasuaji ni kupata usingizi sio chini ya masaa 5. Ni ngumu lakini, ujanja ni mmoja- lala pale mwanao anapolala! Kufanya hivi kutaimarisha hisia zako pia.

Mazoezi ya yoga

Yoga inakusaidia kukaza na kunyoosha misuli ya tumbo. Inasaidia wamama wapya kukabiliana na msongo wa mawazo na mabadiliko katika maisha. Hata hivyo, unashauriwa kuanza yoga wiki ya 6 mpaka 8 baada ya kujifungua. Ongea na daktari wako kuhusiana na hili kabla ya kuanza.

Mazoezi ya Kupunguza Tumbo Baada ya Kujifungua.

Yapo mazoezi kadhaa ya kupunguza tumbo baada ya kujifungua kwa upasuaji. Unaweza kufuata utaratibu mara utakapopona na daktari wako au mkunga kukuruhusu. Unaweza kuanza mazoezi mepesi taratibu ukahamia kwenye magumu, ukiwa na muongozo wa mtaalamu wa mazoezi. Baadhi ya mazoezi unayoweza kujaribu ni pamoja na:

Zoezi la kwanza: unaweza ukafanya zoezi hili ukiwa umesimama, kaa au kulala chini.

Zoezi la pili: fanya zoezi hili kwa angalau sekunde 30 kisha rudia tena mara tatu.

Zoezi la tatu: lala kwa mgongo kisha nyanyua kiuno na mgongo juu, hakikisha mabega yako yako kwenye sakafu. Shikilia mkao huu kwa sekunde 10 kisha laza mwili wako wote kwenye sakafu. Rudia zoezi hili mara 4-6 ili kunyoosha nyonga na kukaza tumbo.

Zoezi la nne: simama wima kisha taratibu inama kuelekea chini mikono yako ikiwa pembeni mpaka kichwa chako kiwe usawa wa magoti yako. Kaa mkao huo kwa sekunde 10 alafu nyoosha tena mwili wako. Rudia mara 4-5 ili kunyoosha mgongo na kuunguza kalori eneo la tumbo.

Zoezi la tano: bana misuli yako ya sakafu ya nyonga, bana ndani kwa sekunde tano kisha achia. Kumbuka usibane pumzi wakati unafanya zoezi hili. Jaribu tena mara 4 mpaka 5, sekunde 10 za mapumziko. Zoezi hili linanyoosha misuli ya nyonga.

Mazoezi baada ya kujifungua kwa njia ya kawaida ni pamoja na:

 • Kutembea
 • Mazoezi ya kubana pumzi ukiwa unakaza tumbo-ukiwa umekaa kitako wima, anza kupumua kwa kuvuta pumzi ndani. Kaza misuli ya tumbo ukiwa unavuta hewa ndani, kisha shusha pumzi taratibu na achia tumbo. Zoezi hili linakusaidia kutuliza misuli ya tumbo na njia nzuri ya kukaza na kunyoosha misuli ya fumbatio na tumbo lako.

 • Zoezi hili linakusaidia kubana tumbo na misuli ya tumbo.

 • Mazoezi ya shingo- kaa kitako wima, taratibu sogeza kichwa chako upande wa kulia alafu upande wa kushoto. Jaribu kushika bega lako la kushoto kwa sikio lako la kushoto, na sikio la kulia kwenye bega la kulia. Shusha kidevu chako chini, kisha angalia juu kwenye paa. Fanya zoezi hili taratibu, aina yeyote ya kugeuka haraka itapelekea kusikia kizunguzungu. Ikiwa umepata kizunguzungu acha zoezi hili haraka wasiliana na mkunga wako ikiwa dalili hii imechukua mda kupotea. Zoezi hili litaimarisha mkao wa mwili wako unaoweza kujikunja kwasababu ya kumbeba mtoto au kunyonyesha.

KUMBUKA

Mama aliyejifungua kwa njia ya kawaida anaweza kufanya mazoezi ya mama aliyejifungua kwa upasuaji, lakini aliyejifungua kwa upasuaji asijihusishe na mazoezi ya mama aliyejifungua kwa njia ya kawaida bila kujadiliana na mkunga au daktari kwanza ili kupatiwa kibali kama ni salama kwako au sio.

Baada ya mazoezi tumia dakika 5 kupumzika ili mapigo ya moyo yarudi kawaida. Unaweza kunyoosha misuli ili kuepuka kuumwa misuli na viungo. Lala chini kwa utulivu macho yakiwa yamefungwa, baada ya hapo unaweza kuendelea na shughuli zako.

Je, nitawezaje kudumu katika mazoezi mara baada ya kuanza? Weka malengo na mafanikio yanayoweza kufikiwa. Ukiweka malengo makubwa mwanzoni mwa mazoezi na mwili wako haujapona vizuri itakuwa vigumu kuendelea na mazoezi. Jipongeze ikiwa utaweza kufanya mazoezi mara 3 kwa wiki au kuongeza mda wa mazoezi kwa siku hata kwa dakika kumi tu. Epuka kabisa mazoezi ya kukata tumbo (crunches & sit-ups).

Jifunze kujua lini upunguze kasi ya mazoezi, mazoezi kupita kiasi yatasababisha afya yako kudhohofika. Mara uonapo ishara zifuatazo, hakikisha unapunguza kasi ya kufanya mazoezi kabla aina yeyote ya mazoezi haijaathiri afya yako:

 • Kujisikia kuchoka badala ya kujisikia safi (fresh).
 • Misuli yako kuuma kwa mda mrefu na wakati mwingine kutetemeka.
 • Kuongezeka kwa mapigo ya moyo asubuhi- ishara kuwa unafanya mazoezi ya mwili makubwa.
 • Misuli na viungo kuuma au maumivu yanayohusiana na kujifungua kujirudi ukiwa unafanya mazoezi.
 • Kutokwa damu ukeni au uchafu, uchafu unaotoka unakuwa na rangi nyeusi.

Mazoezi baada ya kujifungua hayana athari kwenye kunyonyesha. Ukweli ni kwamba, mazoezi haya yanachangia katika uzima na afya ya mama. Ni mazuri kwasababu yanamsaidia mama kujirudi katika hali yake ya awali baada ya msongo wa mawazo aliopata wakati wa ujauzito na kujifungua. Pia mazoezi haya yanamsaidia mama kuwa mkakamavu, mwenye uwezo wa kusimamia malezi ya mtoto wake na aina yeyote ya majukumu yatakayoongezeka.

IMEPITIWA: AGUSTI,2021.

Utunzaji wa Mshono Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Kama mama, lengo kuu ni mtoto wako kuzaliwa akiwa mwenye afya na salama. Hata kama, inabidi upasuaji kufanyika, ili kumleta kiumbe wako mzuri duniani.

Wakati huohuo, ni jitihada zinazoeleweka kujaribu kila kitu ili kuhakikisha mshono unapona vizuri na kovu linaonekana kwa mbali sana.

Nini cha kufanya ili mshono upone vizuri?

 • Usafi. Jitahidi kuhakikisha sehemu ya mshono inasafishwa vizuri mara moja kwa siku kwa maji na sabuni. Hakuna haja ya kuumwagia mshono maji kila mara na epuka kusugua kwa nguvu. Unapomaliza kusafisha, kausha taratibu kwa taulo.
 • Tumia mafuta. Baadhi ya madaktari wanasema ni vizuri kupaka mafuta ya mgando kisha kukifunika kidonda na kitambaa safi au bandeji bila kukaza; madaktari wengine wanasema ni vizuri kutopaka chochote na kuacha mshono wazi. Ni vizuri ukiongea na daktari wako au mkunga aliyehusika katika upasuaji wako kuhusu njia ipi ni nzuri kwa mshono wako.
 • Ruhusu hewa kwenye eneo la mshono. Wakati wa usiku vaa gauni linaloachia itasaidia sana hewa kuzunguka, kwasababu hewa inahamasisha uponaji wa majeraha katika ngozi.
 • Hudhuria miadi yako na daktari. Hakikisha nyuzi zinatolewa kwa wakati ili kuepusha kovu baya kutokea. Hivyo kabla ya kuondoka hospitali hakikisha unakumbuka kumuuliza mkunga wako au daktari tarehe ya kurudi kutolewa nyuzi.
 • Epuka mazoezi kwa muda. Itakubidi kupunguza mazoezi ili kuruhusu majeraha katika uterasi na tumbo kupona. Hivyo epuka kuinama au kugeuza mwili ghafla, vilevile usinyanyue kitu chochote kizito zaidi ya mtoto wako. Inashauriwa kusubiri daktari akuruhusu kama ni salama kuanza mazoezi.
 • Tembea kila uwezapo. Jitahidi kutembea, inasaidia kuongeza mzunguko wa damu, inasaidia pia kuponya jeraha na kupunguza nafasi ya damu kuganda kwenye mishipa ya miguu au ogani za nyonga, hali ambayo inawapata wamama waliotoka kujifungua. Pale unapoona unaweza kutembea mbebe mwanao kwenye kigari chake (kama unacho) au mfunge mtoto mbeleko kwa mbele kisha fanya matembezi jioni karibu na nyumbani kwako au kuzunguka nyumba yako.

Ishara kuwa mshono wako umepata maambukizi.

Maambukizi haya husababishwa bakteria katika eneo la mshono baada ya upasuaji. Ikiwa unapitia dalili zifuatazo, wasiliana na daktari wako mara moja:

 • Uwekundu au kuvimba eneo la mshono au ngozi kuzunguka eneo hilo.
 • Homa kali zaidi ya (100.4˚F)
 • Harufu mbaya kutoka kwenye mshono
 • Kuvuja au majimji kuzunguka mshono
 • Usaha kutungika katika mshono
 • Kidonda kuwa kigumu au kusikia ongezeko la maumivu kuzunguka kidonda.
 • Maumivu katika sehemu moja ya mshono (kumbuka kuwa wiki za awali baada ya upasuaji maumivu ni kawaida, lakini pia usipuuzie kama eneo moja tu la mshono linakupa maumivu makali)
 • Mshono kuachia.
 • Maumivu wakati wa kukojoa
 • Uchafu wenye harufu mbaya kutoka ukeni
 • Miguu kuvimba au kuuma
 • Kutokwa damu inayojaza pedi ndani ya lisaa. Wakati mwingine damu inayotoka inakuwa mapande ya damu (damu iliyoganda).

Hali Hatari Zinazosababisha Maambukizi Katika Mshono Baada ya Upasuaji.

Baadhi ya wanawake wako katika nafasi ya kupata maambukizi ya bakteria katika eneo la mshono kwa sababu zifuatazo:

 • Unene uliopitiliza
 • Ugonjwa wa kisukari au dosari yeyote katika kinga ya mwili, (mfano HIV)
 • Matumizi ya mda mrefu ya steroidi
 • “Chorioamnionitis”- maambukizo ya bakteria ya papo kwa hapo yanayoathiri utando wa nje, amnion na maji ya amniotic. Hutokea wakati wa ujauzito au uchungu, bila kutibiwa mapema husababisha maambukizo mazito kwa mama na mtoto.
 • Kutohudhuria miadi ya kliniki (mara chache)
 • Kujifungua kwa upasuaji ujauzito zilizopita
 • Ukosefu wa dawa ya tahadhari kabla ya kuchanwa
 • Uchungu au upasuaji uliochukua wa mda mrefu
 • Upotevu mkubwa wa damu wakati wa uchungu, kuzaa au upasuaji

Maambukizi katika eneo la mshono baada ya upasuaji hutibiwa kwa antibaotiki zinazotolewa hospitali, daktari atakuandikia nyingine upate kurudi nazo nyumbani. Daktari atafungua mshono wako kama ulianza kutoa usaha, kisha atatoa usaha wote. Baada ya kusafisha vizuri daktari ataepusha usaha kujikusanya kwa kuweka kitambaa safi chenye antiseptiki ili kuzuia ukuaji wa bakteria katika mshono. Kidonda kinahitajika kuangaliwa mara kwa mara ili kuhakikisha kinapoa vizuri.

Baada ya siku kadhaa za matibabu ya antibaotiki na daktari kuangalia mshono mara kwa mara, kidonda kitaanza kujifunga vizuri au kupona chenyewe.

Jinsi Gani ya Kuzuia Maambukizi ya Mshono Baada ya Upasuaji

Baadhi ya maambukizi katika mshono hayaepukiki. Lakini ikiwa ulifanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, unaweza chukua hatua kupunguza nafasi ya kupata maambukizi tena, baadhi ya hatua hizo ni pamoja na:

 • Tumia dawa ulizoandikiwa na fuata maelekezo ya kuangalia kidonda yaliyotolewa na daktari au mkunga, ikiwa una swali usisite kuwasiliana na daktari.
 • Kama umepewa dawa za kutumia kutibu au kuzuia maambukizi, hakikisha unatumia dozi nzima bila kuruka au kuacha kuzitumia kipindi kizima cha matibabu.
 • Safisha kidonda chako na badili vitambaa vinavyofunga kidonda mara kwa mara.
 • Usivae nguo zinazobana au kupaka losheni juu ya kidonda.
 • Omba ushauri jinsi gani ya kumpakata mtoto wakati wa kumnyonyesha ili kuepuka mgandamizo mbaya katika kidonda.
 • Angalia joto la mwili wako mara kwa mara, tafuta msaada wa kitiba ikiwa jotoridi lako ni zaidi ya 100˚F (37.7˚C)

KUMBUKA

Kama bado haujajifungua kwa upasuaji, hizi ni hatua unazotakiwa kuchukua:

 • Dumisha uzito wenye afya. Kama wewe sio mjamzito, fanya mazoezi na kula mlo wenye afya ili kuepuka uzito uliopitiliza (kiribatumbo) ukiwa mjamzito.
 • Chagua kujifungua kwa njia ya kawaida kama inawezekana. Wanawake wanaojifungua kwa njia ya kawaida hawana nafasi ya kupata maambukizi baada ya kujifungua.
 • Jitahidi kutibu hali yeyote inayoleta dosari katika kinga ya mwili kabla ya kushika mimba. Ni salama kwako na mtoto ikiwa utatibu aina yeyote ya maambukizi au ugonjwa kabla ya kushika ujauzito.

Maambukizi katika eneo la mshono yanayosababishwa na bakteria baada ya upasuaji yanaweza sababisha matatizo makubwa kama: uharibifu wa tishu zenye afya katika ngozi, mshono kuachia na utokaji wa kinyesi baada ya mshono kuachia. Ikiwa mama atapata matatizo haya, upasuaji wa kurekebisha utafanyika. Inaweza kuchukua mda mrefu kupona, kwa wachache inaweza kusababisha kifo.

IMEPITIWA: AGUSTI, 2021.

Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Kujifungua kwa njia ya upasuaji, kwa lugha ya kigeni “C-section” ni njia ya kujifungua mtoto kwa kuchana kuta za sehemu ya chini ya tumbo na mji wa mimba (uterasi) ili kutoa mtoto aliye kwenye mji wa mimba.

Katika kipindi fulani kabla uchungu kutokea mama anajua kwa uhakika atajifungua kwa njia fulani, lakini hali tofauti za kiafya zinaweza kubadilisha mpango huo.

Daktari au mkunga anaweza kuamua utajifungua kwa njia ya upasuaji mara moja ukiwa katika uchungu au ukiwa katika chumba cha kujifungua. Mabadiliko haya ya haraka yanaweza kutokea ikiwa afya yako au mtoto aliyeko tumboni imebadilika ghafla na kuwa mbaya, hivyo kufanya kujifungua kwa njia ya kawaida kuwe hatari kwa afya ya mama.

Ni busara kujifunza anachopitia mama wakati wa kujifungua kwa njia ya upasuaji hata kama sio mpango wako wa kujifungua, itakusaidia ikiwa mabadiliko yatatokea katika chumba cha kujifungulia na kuhitajika upasuaji ili kuokoa maisha yako na mtoto wako.

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni salama kwa mama na mtoto. Lakini ni upasuaji mkubwa, inashauriwa isichukuliwe kimzaha.

Aina za Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Upasuaji Uliopangwa

Ikiwa unajua mapema utajifungua kwa njia ya upasuaji, unapata nafasi ya kujua tarehe ya kujifungua na kutopitia uchungu wa kuzaa. Kabla ya utaratibu huu kufanyika utapata dripu ili mwili wako uwe na dawa na majimaji. Utawekewa pia mpira wa mkojo kusaidia kukusanya mkojo katika kibofu chako kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini.

Kama utajua mapema kuwa utajifungua kwa upasuaji, utapata muda kwa kutosha kujitayarisha, lakini kama ni upasuaji wa dharura inaweza kukushtua. Utachomwa sindano ya kaputi kisha kulazwa kwenye kitanda cha upasuaji. Wakati mwingine inaweza ikahitajika kuchomwa sindano ya kaputi ambapo utakuwa hutambui kinachoendelea mpaka utakapoamka. Faida nyingine ni kwamba utaweza kumuona mtoto wako mara tu anapotolewa tumboni. Daktari atakuruhusu umbebe mara baada ya upasuaji kumalizika. Kama una mpango wa kumnyonyesha mtoto wako, unaweza kujaribu kumlisha mtoto. Lakini sio kila mama anapata nafasi ya kumbeba mtoto wake mara baada ya upasuaji.

Wakati mwingine watoto waliozaliwa kwa njia ya upasuaji wanapata shida ya upumuaji, hali hii inawafanya kuhitaji msaada kutoka kwa madaktari. Usiwe na wasiwasi utaweza kumbeba mtoto wako mara baada ya daktari kuamua kuwa ana afya nzuri na hali yake iko salama.

Baada ya mtoto kuzaliwa, daktari atatoa plasenta yako na kukushona. Utaratibu wote huu utachukua dakika 45 mpaka lisaa limoja tu.

Sababu za Upasuaji Uliopangwa

Daktari au mkunga wako anaweza kukupangia kujifungua kwa upasuaji siku ya kujifungua ikiwa una:

 • Aina fulani ya matatizo ya kiafya. Magonjwa makubwa kama magonjwa ya moyo, kusukari, shinikizo kubwa la damu au tatizo la kibofu cha mkojo ni baadhi ya matatizo yatakayofanya kujifungua kwa kawaida kuwe hatari kwa mwili wa mjamzito.
 • Maambukizi. Ikiwa wewe ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi au una ugonjwa wa zinaa ambao haujapona, upasuaji wakati wa kujifungua ni jambo lisilo epukika. Hii ni kwasababu virusi vinavyosababisha magonjwa haya vinaweza ambukizwa kwa mtoto kipindi cha kujifungua.
 • Afya ya mtoto. Ugonjwa kurithi unaweza fanya safari ya mtoto kupita ukeni kuwa changamoto kwa mtoto wako.
 • Mtoto mkubwa.
 • Uzito wa mjamzito. Kuwa na uzito mkubwa au uzito uliopitiliza kunaongeza nafasi ya mjamzito kujifungua kwa njia ya upasuaji kwa sababu ya shida mbalimbali zinazoambatana na uzito mkubwa kama vile kisukari wakati wa ujauzito, lakini pia kwasababu wanawake wenye uzito mkubwa wa mwili wanapitia uchungu wa kuzaa unaochukua muda mrefu.
 • Mtoto akikaa mkao wa tofauti tumboni (breech position). Mtoto anapotanguliza miguu kwanza na ikashindikana kumgeuza, mkunga wako ataamua upasuaji ni lazima.
 • Ujauzito wa mapacha au zaidi.
 • Tatizo ya kondo la nyuma kujishikiza karibu na mlango wa kizazi. Pale kondo la nyuma limejishikiza karibu na shingo ya uzazi, sio rahisi kujifungua kwa njia ya kawaida kwasababu mtoto hatapita vizuri. Kawaida plasenta ina kazi ya kuingiza virutubisho kwa mtoto, kumpa hewa safi na kuondoa hewa chafu. Ikiwa plasenta imezuia kidogo au sana mlango wa uzazi (placenta previa) upasuaji ni njia pekee salama kwako na mtoto wako.
 • Kondo la nyuma kuachia kabla ya muda wa kujifungua (placenta abruption). Endapo kondo la nyuma limenyofoka au sehemu ndogo kuachana na ukuta wa kizazi, upasuaji wa haraka hauna budi kufanyika ili kuokoa maisha ya mtoto. Upasuaji ukichelewa kufanyika mtoto atazaliwa amechoka au wakati mwingine kufia tumboni kwasababu ya ukosefu wa virutubisho na hewa safi.
 • Matatizo mengine hatari ya kiafya. Matatizo kama ujauzito unaosababisha shinikizo kubwa la damu au shinikizo la damu linalokua taratibu na kuathiri mfumo wa kati wa fahamu na kusababisha mama kupoteza fahamu na wakati huohuo hakuna tiba inayofanya kazi. Mkunga wako atashauri upasuaji ili kulinda afya za wote.
 • Ombi la mama. Mjamzito anaweza kuomba kufanyiwa upasuaji kwasababu za kibinafsi. Mkunga anaweza kumzikiliza mama na kumshauri njia salama kulingana na ombi la mama.
 • Ikiwa ulijifungua kwa upasuaji ujauzito wa awali. Mama aliyejifungua kwa upasuaji ujauzito wake wa awali anaweza kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida endapo kovu limepona vizuri, afya yako iko salama na sababu iliyokufanya ukafanyiwa upasuaji katika ujauzito wako wa awali hazipo.
 • Upasuaji unafanyika ikiwa mtoto ni wa kipekee. Kwa wanandoa ambao wamepata shida katika kutafuta mtoto kwa muda mrefu, wanaweza kuamua upasuaji ufanyike wakati wa kujifungua ili kuhakikisha mama na mtoto hawapati madhara wakati wa kujifungua. Wanawake waliopata mimba ya kwanza kwenye umri mkubwa sana kwa mfano miaka zaidi ya 35, wanawake waliopata shida ya mimba kuharibika sana au mtoto kufariki wakati wa kujifungua huchagua upasuaji wakati wa kujifungua.

Upasuaji wa Dharura

Wakati wa upasuaji wa dharura, mambo machache yatabadilika ikiwa ni pamoja na kasi na uharaka wa operesheni. Daktari anaweza kumzalisha mtoto wako kwa dakika mbili baada ya kuchana uterasi yako (inachuka dakika 10 mpaka 15 kwa upasuaji uliopangwa).

Ikiwa mtoto wako anashida katika upumuaji au mapigo ya moyo hayako sawa, madaktari watahitaji kumtoa haraka ndani ya mji wa mimba na kumuwahisha hosspitali kwaajili ya huduma za kitabibu haraka ili aweze kuwa salama.

Katika upasuaji wa dharura kwa kawaida utachomwa sindano ya uti wa mgongo, itakayokufanya usisikie maumivu kuanzia kwenye nyonga kwenda chini. Au ukapigwa kaputi na kulala upasuaji mzima. Kwa bahati mbaya hutasikia au kumuona mtoto wako akiwa anazaliwa, ila hautasikia maumivu au mkandamizo wowote katika tumbo lako la uzazi. Habari njema ni kwamba, baada ya kuzinduka utaweza kumbeba, kumuona na kumlisha kichanga wako.

Upasuaji wa dharura unafanyika pale:

 • Ikiwa kitovu kitatoka nje kabla mtoto, hali hii itasababisha usambazaji wa hewa ya oksijeni kukatishwa.
 • Uterasi ikichanika.
 • Uchungu umechelewa kuanza au hauendi kama inavyotakiwa. Kutoendelea au kusimama kwa uchungu ni moja ya sababu kubwa inayopelekea wajawazito wengi kujifungua kwa upasuaji. Hali hii inapelekea shingo ya uzazi kutofunguka na kupelekea mtoto kushindwa kutoka. Kwa kawaida mkunga au daktari huangalia hali ya shingo ya kizazi mara kwa mara kwa kuingiza vidole viwili kupitia uke, kwa kufanya hivi atagundua kwa kiasi gani (sentimita) ngapi shingo ya uzazi imetanuka. Hii ni njia mojawapo ya kuangalia maendeleo ya uchungu.
 • Mjamzito kuchoka au mtoto kuchoka. Ikiwa daktari atakuona umechoka au kipimo maalum kinachowekwa kwenye tumbo kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto kuonyesha dalili za mtoto kuchoka daktari ataamua upasuaji wa haraka ufanyike.

 Upasuaji wakati wa kujifungua unachukua muda gani?

Upasuaji ni haraka, procedure yenyewe inachukua dakika 10 au pungufu, ikifuatiwa na dakika nyingine 30 za kushona.

Nini hutokea wakati wa upasuaji?

Iwe ni upasuaji uliopangwa tangu awali au wa dharura, upasuaji wa kawaida unafuata mpango maalum.

Maandalizi na sindano ya nusu kaputi

Utafanyiwa vipimo vya damu ili kuangalia wingi wa dam una kundi la damu ili pale itakapotokea shida baada ya upasuaji damu iongozwe kiurahisi. Upasuaji unaanza kwa utaratibu wa dripu na sindano ya kaputi ili sehemu ya chini ya mwili ili usiweze kusikia maumivu na mgandamizo wowote lakini utakua macho na utafanikiwa kushuhudia pale mwanao anapotolewa ndani ya mji wa mimba. Kisha sehemu cha chini ya tumbo la uzazi litanyolewa (kama inahitajika) na kusafishwa kwa dawa maalum ya kuua vijidudu. Utawekwa mpira wa kukusanya mkojo kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini.

Ikiwa unahitajika kufanyiwa upasuaji wa dharura, utachomwa dawa ya kukufanya ulale kipindi kizima cha upasuaji ambayo mara nyingi huchukua dakika chache. Ukiamka utasikia kusinzia kwasababu ya dawa ya usingizi, utajisikia kichefuchefu na kuchoka sana. Unaweza pia kuwa na koo kavu iliyosababishwa na mrija wa kupeleka hewa kwenye mapafu unaowekwa wakati wa upasuaji.

Kuchanwa na kuzaa

Mara baada ya sehemu ya chini ya mwili kufa ganzi au kulala, daktari atachana kidogo kwenye sehemu ya chini ya tumbo-juu kidogo ya uke. Kovu la mchano huu hupotea kadiri mda unavyoenda ikiwa kazi ilifanyika kwa umakini. Daktari atachana tena ndani sehemu ya chini ya uterasi. Zipo aina mbili za michano:

Mchano mlalo. Unatumika kwa asilimia 95 wakati wa upasuaji, kwasababu misuli chini ya uterasi ni mwembamba hivyo damu kutoka kidogo. Pia sio rahisi kuachia wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida hapo baadae.

Mchano wima. Aina hii ya mchano inafanyika pale mtoto amekaa sehemu ya chini ya uterasi au amekaa katika mkao usio kawaida.

Baada ya hapo maji yanayopatikana tumboni mwa mama mjamzito yanayomzunguka mtoto kwenye hatua zake zote za ukuaji hufyonzwa nje, kisha mtoto wako atatolewa nje. Kwasababu uteute wa ziada haukutolewa vizuri nje ya njia ya hewa ya mtoto wako, ufyonzwaji wa ziada utahitajika ili kuhakikisha mapafu ya mwanao ni safi kabla ya kumsikia mtoto wako akilia kwa mara ya kwanza.

Kumbeba mtoto wako kwa mara ya kwanza

Baada ya kitovu kukatwa, daktari ataondoa placenta, kisha kukagua haraka ogani zako za uzazi kabla ya kuanza kukushona. Kisha ushonaji wa sehemu uliochanwa utafanyika, ambao unachukua dakika 30 au zaidi.

Utapokea dawa ya kupunguza nafasi ya kidonda kupata maambukizi na “oxytocin” ya kudhibiti damu kutoka na kusaidia uterasi kubana na kurudi katika hali yake ya awali katika dripu. Shinikizo lako la damu, mapigo ya moyo na kasi yako ya upumuaji na wingi wa damu inayotoka utaangaliwa mara kwa mara.

Kama utakuwa umejifungua kwa upasuaji utahitaji kuendelea kukaa hospitali kwa siku kadhaa uanze kupona. Kupona baada ya upasuaji ni sawa tu na kupona kwa upasuaji mwingine wa eneo la tumbo. Tofauti kubwa ni kwamba badala ya kupoteza kiungo kimoja kama figo au “appendix” unapata mtoto.

Mojawapo ya matatizo unayoweza kuyaona baada ya kujifungua ambayo ni ya kawaida ni kama hali ya kusikia maumivu kwenye uke, kutokwa na damu nzito nyeusi, matiti kuvimba, nywele kudondoka, uchovu na kutokwa jasho jingi.

Tegemea Yafuatayo Baada ya Kutoka Chumba cha Upasuaji.

Daktari wako atakuchunguza kwa karibu mpaka pale dalili zote za dawa za kuondoa maumivu zimeisha. Kumbukumbu zako zinaweza zikawa zinasumbua kama ulitumia dawa ya usingizi au nusu kaputi. Madhara ya sindano ya nusu kaputi inayochomwa kwenye uti wa mgongo huchukua muda mrefu zaidi kuliko madhara ya dawa za usingizi.

Baada ya dawa ya kuondoa maumivu kuisha utaanza kusikia kidonda kinauma. Ukali wa maumivu unategemea sababu tofauti, ikiwemo uwezo wako wa kusikia maumivu na kama una historia ya kujifungua kwa upasuaji hapo awali, kwani maumivu ya upasuaji wa pili na kuendelea huwa yanaonekana sio makubwa sana kama yale uliyoyasikia kwenye upasuaji wa kwanza. Utapewa dawa za maumivu kupambana na hali hii.

Unaweza ukasikia kichefuchefu, ambapo daktari atakupatia dawa itakayokuzuia kupata kichefuchefu au kutapika.

Nesi atakuwa anakuchunguza mara kwa mara. Atakuwa anachukua vipimo vyako muhimu (joto, shinikizo la damu (BP), na upumuaji). Atakuwa pia anaupima mkojo wako na chochote kinachotoka ukeni. Pia atakuwa anaangalia mfungo wa kidonga chako cha upasuaji, sehemu mfuko wako wa uzazi ulipo na ugumu wake na wakati huo huo akihakikisha mirija ya dripu na mpira wa mkojo ipo sehemu yake.

Kama hali yako itaendelea vizuri, utapelekwa kwenye wodi ndani ya masaa kadhaa baada ya upasuaji kufanyika. Uchunguzi wa vipimo vyako muhimu utafanyika kwa mara nyingine. Kama una uwezo wa kukojoa mwenyewe basi mpira wa mkojo utatolewa masaa 24 baada ya upasuaji.

Unaweza ukawa unasikia maumivu kwenye uke kama mwanamke aliyejifungua kwa njia ya kawaida. Hii isikupe wasiwasi maumivu haya ni kutokana na kukaza kwa misuli ya mfuko wako wa uzazi ukiwa unajirudia kwenye hali yake kabla ya ujauzito.

Dripu za maji zitatolewa na utaruhusuwa kuanza kutumia vinywaji kwa kunywa mwenyewe masaa 24 baada ya upasuaji (Huu ndio muda ambao utumbo wako utakuwa umeshaanza kusogeza chakula kawaida na kufanikiwa kutoa hewa chafu nje kwa njia ya kujamba). Taratibu utaruhusiwa kurudia mlo wako wa kawaida kadiri siku zinavyosogea. Mama wanaonyonyesha inabidi wapate maji ya kutosha mwilini.

Utategemea kutolewa nyuzi zako (Kama sio zile zinazoyeyuka zenyewe) ndani ya siku 4 hadi 6 baada ya upasuaji.

Mwishoni kabisa kama kila kitu kitakuwa kimeenda sawa kwako na mtoto, utaruhusiwa kurudi nyumbani ndani ya siku 3 hadi 7 baada ya upasuaji.

Hali gani hatari za kiafya zinazoweza kutokea baada ya kujifungua kwa upasuaji?

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni salama kabisa, lakini mara chache matatizo ya kiafya yanatokea kwa mama na mtoto baada ya upasuaji kufanyika.

Kwa mama, matatizo haya ni pamoja:

 • Kupoteza damu,
 • Mama kupata maambukizi eneo la mshono.
 • Muitikio mbaya wa dawa zinazotumika kipindi cha upasuaji (dawa za nusu kaputi, dawa za kupunguza maumivu n.k).
 • Kujeruhiwa wakati wa upasuaji,
 • Damu kuganda kwenye mishipa ya damu haswa miguuni,viungo ndani ya nyonga na mapafu. Huku madaktari wakifanya kila namna kuhakikisha hali hii haitokei, ni vizuri ukatembea baada ya upasuaji kama unaweza.
 • Mara chache sana, uterasi inaweza kuvimba au kuwasha.
 • Maambukizi katika kuta za kizazi
 • Mama kupata hatari ya kujifungua kwa upasuaji upasuaji unaofuata.

Hatari za kiafya za muda mrefu ni pamoja na: kupata kovu baya kwenye eneo la mshono na kuchanika kizazi kwenye ujauzito unaofuata.

Mtoto aliyezaliwa kwa njia ya upasuaji anaweza:

 • Kupitia kipindi cha mpito cha kupumua haraka haraka, kitakachodumu kwa siku chache baada ya kujifungua, hali hii inasababishwa na mabaki ya maji (yanayopatikana ndani ya mji wa mimba kumzunguka mtoto kipindi chote cha ujauzito) ndani ya mapafu ya mtoto.
 • Kama upasuaji umefanyika kabala ya wiki ya 39 ya ujauzito, mtoto atakuwa katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kupumua ikiwa mapafu yake hayajakua vizuri-lakini kumbuka daktari atakua karibu nawe kumuangalia kwa ukaribu zaidi na kutibu aina yoyote ya tatizo litakalozuka ukiwa bado hospitalini.

Kumbuka

Ukishuhudia ongezeko la maumivu ya nyonga, kutokwa uchafu usio wa kawaida au homa baada ya mtoto kuzaliwa, wasiliana na daktari wako mara moja.

IMEPITIWA: AGUSTI, 2021.

Leba ya Uongo (The Braxton Hicks Contractions)

Uchungu ni mwendelezo wa mchakato wa mimba tangu ilipotungwa. Uchungu wa mjamzito ni wa kipekee na hubadilika kutokana na mambo mengi ikiwemo: maumbile yako (fiziolojia), ukubwa na mkao wa mtoto wako, afya na historia ya maradhi yako, matarajio na hisia zako, watu unaoishi nao na wanaokusaidia, mtaalam atakayekuhudumia, na mahali utakapojifungulia mtoto wako. Hatua za uchungu hutofautiana kati ya mwanamke mmoja hadi mwingine.

Kuelekea mwishoni mwa ujauzito au hata mapema zaidi kwa baadhi ya wanawake-wanaweza kuhisi mji wa mimba ukikaza mara chache bila kuhisi maumivu yoyote, kitendo hiki huitwa “Braxton-Hicks contractions” au (leba ya uongo). Kukaza kwa mji wa mimba ni hali ya kawaida ambayo haitokei katika mpangilio maalum, na wala haisababishi mlango wa kizazi kufunguka.  Mikazo hii ni njia ya asili ya mwili kujiandaa kwa ujio wa uchungu halisi wa kuzaa.Utahisi kuongezeka kwa msukumo kwenye nyonga na kibofu cha mkojo kadiri mtoto anavyozidi kusogea chini zaidi.

Mkazo wa aina hii katika mji wa mimba ni maarufu sana kwa wajawazito katika kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito, lakini inaweza kuanza mapema zaidi muda wowote baada ya wiki ya 20 ya ujauzito.

Mjamzito Anayepitia Leba ya Uongo (Braxton Hicks Contractions) Anahisije?

Kwa ujumla wanawake wengi waliopitia uchungu huu wameripoti mikazo hii kutokuwa na maumivu ila inasababisha mikazo ya tumbo inayodumu kati ya sekunde 30 mpaka 60 na kwenda mpaka dakika 2 kwa muda. Mikazo hii inaweza kuleta wasiwasi kwa wajawazito lakini ikumbukwe haisababishi uchungu halisi kuanza au kufunguka kwa mlango wa uzazi (cervix). Ukilinganisha na uchungu halisi wa kujifungua, aina hii ya uchungu:

 • Hausababishi maumivu.
 • Unatofautiana, hutokea kawaida au bila mpangilio.
 • Unaachana sana kati ya mkazo mmoja na mwingine.
 • Unadumu kwa muda mfupi.
 • Kwa kawaida hutokea kwa saa chache na baadaye kuacha- wakati mwingine hata siku kadhaa.
 • Unaacha ukibadilisha mkao au shughuli unayoifanya.
 • Mikazo yake inasikika katika tumbo.

Nini Husababisha Leba ya Uongo?

Chanzo halisi cha mikazo hii hakijulikani. Watafiti wa kuaminika wa afya wameafiki kuwa kuna baadhi ya shughuli na hali zinazoweza kumsumbua mtoto ndani ya mji wa mimba. Mikazo hii katika mji wa mimba inaweza kusaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenye plasenta na kumpatia mtoto hewa ya oksijeni zaidi.

Vyanzo vya hali hii ni pamoja na:

 • Upungufu wa maji mwilini. Wajawazito wanahitaji vikombe 10 mpaka 12 vya maji na vinywaji vingine kama maziwa au juisi ya matunda safi kila siku, jitahidi kunywa maji ya kutosha.
 • Unaweza kushuhudia mikazo katika mji wa mimba baada ya kusimama muda mrefu au kufanya shughuli nyingi za nyumbani au kufanya kuupa mwili zoezi kidogo.
 • Tendo la ndoa. Kufika kilele wakati wa tendo la ndoa (orgasm), inaweza kusababisha misuli ya uterasi kukaza. Hii ni kwasababu mwili unaachia “oxytocin” baada ya kufika kileleni. Kichocheo hichi husababisha mkazo wa mawimbi wa mara kwa mara.
 • Kibofu cha mkojo kilichojaa. Kibofu cha mkojo kilichojaa kinapeleka mgandamizo katika uterasi na kusababisha mikazo au maumivu ya misuli ya tumbo.

Unawezaje Kutofautisha Leba ya uongo na Leba ya ukweli?

Wakati

Leba ya uongo

 • Hutokea baada ya wiki ya 20 ya ujauzito.

Leba ya ukweli

 • kawaida hutokea kati ya wiki ya 37 na 40 ya ujauzito.

Marudio ya mikazo

Leba ya uongo

 • Yanatofautiana, hutokea kawaida au bila mpangilio.
 • Unaachana sana kati ya mkazo mmoja na mwingine.

Leba ya ukweli

 • Inakuwa na mpangilio maalumu
 • Uchungu unakuwa mkali, kuongezeka kadiri mda unavyoendelea.

Muda

Leba ya uongo

 • Sekunde 30-60 mpaka dakika
 • Kila mkazo unabadilika kwa muda.

Leba ya ukweli

 • Maumivu yanayopanda na kushuka yanayoachana kwa muda wa dakika tano na kudumu kwa sekunde 45 mpaka 60 na huwa ni makali sana.

Ukali

Leba ya uongo

 • Hausababishi maumivu lakini inakufanya ujisikie vibaya tu.
 • Makali ya mikazo ya mji wa mimba hayaongezeki.
 • Yanapotea ukibadilisha mkao.

Leba ya ukweli

 • Maumivu yanayopanda na kushuka huwa ni makali sana kiasi kwamba hushindwa hata kuongea kadiri muda unavyoenda.
 • Makali hayapungui hata ukibadilisha mkao.

Eneo

Leba ya uongo

 • Hutokea sehemu ya chini ya fumbatio na ukeni.

Leba ya ukweli

 • Huanza mgongoni na kusogea sehemu ya mbele.

Je, Kuna Tiba Zozote za Leba ya Uongo “Braxton Hicks Contractions”?

Baada ya kuthibitisha na daktari unapitia leba ya uongo na sio leba halisi, unaweza kupumzika bila wasiwasi.

Hakuna haja ya matibabu ya kidaktari kwaajili ya aina hii ya uchungu. Jaribu kujikita katika kupumzika, kunywa maji ya kutosha na kubadilisha mkao-hata ikibidi kusogea kutoka kitandani kwenda kwenye kochi.

Jitahidi:

 • Kwenda maliwatoni kujisaidia haja ndogo (ikiwa haufanyi hivyo kila baada ya saa moja).
 • Kunywa glasi tatu mpaka nne za maji au kinywaji kingine kama maziwa, au juisi ya matunda safi.
 • Lala kwa ubavu wa kushoto, ulalaji huu unaimarisha mtiririko mzuri wa damu kwenye uterasi, figo na plasenta.
 • Mara nyingi uchungu huanza usiku. Wakati mwingine kuoga kwa maji ya moto ya bomba la mvua husaidia kupunguza maumivu, na kukufanya upate usingizi.
 • Hakikisha unakula na kupumzika.
 • Ili kupunguza maumivu, wajawazito wengine hupenda kutembea kunasaidia kupunguza uchungu.
 • “Massage” inasaidia pia.

Ikiwa mbinu hizi hazifanyi kazi kupunguza uchungu wa mapema unaopitia, usisite kumuuliza daktari au mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako matibabu mengineyo yanayofaa. Ijapokuwa utatuaji wa hali za kila siku za maisha zinashauriwa kutumika, ila kuna baadhi ya dawa zinazoweza kusaidia kupunguza mikazo na mibano katika mji wa mimba.

KUMBUKA

Wasiliana na mkunga wako au daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako mara moja ikiwa una dalili kama:

 • Unatokwa damu ukeni
 • Unavuja maji maji au kama chupa yako ya maji ya uchungu imevunjika.
 • Mikazo ya nguvu kila dakika tano ndani ya saa moja.
 • Maumivu yasiyovumilika.
 • Mtoto kucheza tumboni tofauti kuliko kawaida, au kama mtoto hachezi mara 6-10 ndani ya saa moja.
 • Maumivu ya mgongo yanayoendelea.
 • Dalili zozote za uchungu halisi kabla ya wiki ya 37 ya ujauzito.

IMEPITIWA: JULAI,2021.

Uchungu wa Uzazi wa Muda Mrefu (Prolonged Labor)

Iwe ni mara ya kwanza kujifungua au ulishawahi kujifungua, kuzaa mtoto ni tukio la kipekee kwa kila mwanamke. Kila mwanamke ana uchungu wa uzazi tofauti na hii ni kawaida. Uchungu wa uzazi wenye afya unaweza kuwa wa haraka sana au kuchukua mda mrefu. Hata hivyo, baadhi ya watoto hukwama na kuishia kuzaliwa kwa upasuaji au kwa msaada wa vifaa maalum.

Kuna wakati mtoto anakuja haraka sana na wakati mwingine anachelewa. Ujio wa kichanga wako unategemea vitu vingi, kimoja wapo ni kwa kasi gani uchungu wako unatokea.

Uchungu wa uzazi ni nini?

Uchungu wa uzazi ni kubana na kuachia kwa kujirudia rudia kwa misuli katika tumbo la uzazi. Utahisi misuli kubana na kuachia sehemu ya chini ya mgongo na eneo la tumbo. Misuli inavyobana na kuachia taratibu husababisha kufunguka kwa mlango wa tumbo la uzazi (cervix). Vile vile mibano hii ya misuli inasaidia mtoto kusukumwa nje ya mfuko wa uzazi. Baada ya mlango mzima kufunguka, mtoto anaweza kutoka nje ya tumbo la uzazi na hatimaye nje kupitia uke wa mama.

Kubana na kuachia kwa misuli huanza polepole mwanzoni mwa ujauzito, kawaida haichukui mda mrefu-huachia mama anapopumzika inajulikana kama uchungu wa uongo “Braxton-hick contractions”. Uchungu wa uzazi wa ukweli unaanza kwa nguvu, ukianza huja mara kwa mara, na kwa taratibu kila baada ya dakika chache. Uchungu huu hauachi hata mama akilala chini au kupumzika.

Kwa mama anayejifungua kwa mara ya kwanza uchungu unadumu kwa takribani masaa 12 mpaka 18 kwa wastani. Ila kwa mama mzoefu, uchungu unaenda haraka sana, kawaida nusu ya masaa ya mama anayejifungua kwa mara ya kwanza.

Uchungu wa uzazi wa muda mrefu ni nini?

Uchungu wa uzazi unaochukua muda mrefu sana ni uchungu wa zaidi ya masaa 12 kwa mama mzoefu au zaidi ya saa 24 (usiku na mchana) kwa mama anayejifungua kwa mara ya kwanza.

Kama mtoto wako hajazaliwa baada ya takribani masaa 20 ya mibano ya kawaida ya tumbo la uzazi, utakuwa unapitia uchungu wa mda mrefu. Baadhi ya wataalamu wa afya wanasema inatokea baada ya masaa 18 mpaka 24. Kama una ujauzito wa mapacha au zaidi uchungu wako utadumu kwa masaa zaidi ya 16.

Mara nyingi husababisha majeraha kwa mama na matatizo kwa mtoto, iwapo maji ya uzazi yataanza kutoka lakini uchungu wa uzazi ukachelewa kuanza baada ya saa 12, hali hii inaweza kusababisha maambukizi.

Uchungu wa uzazi wa muda mrefu unasababishwa na nini?

Uchungu utachukua mda mrefu endapo:

 • Mtoto ni mkubwa na hawezi kupita katika mlango wa uzazi.
 • Mtoto amekaa vibaya, kwa kawaida kichwa cha mtoto kinatangulia chini huku akiangalia mgongo wako. Tofauti na hapo uchungu utachukua mda mrefu kuliko kawaida.
 • Mibano na mikazo ya mfuko wa uzazi ni hafifu, hali hii itapunguza kasi ya mjamzito kuanza kusukuma mtoto wakati wa kujifungua.

Dalili na ishara za uchungu wa uzazi wa muda mrefu

Dalili na ishara za aina hii ya uchungu ni pamoja na

 • Uchungu wa zaidi ya masaa 18, kuchelewa ni moja ya ishara kuu.
 • Mama kuchoka na kuishiwa nguvu.
 • Dalili nyingine za kimwili ambazo hazivumiliki ni kama maumivu ya mgongo, mapigo ya juu moyo na maumivu katika misuli ya tumbo la uzazi hata ukigusa kidogo
 • Ukosefu wa maji na nguvu mwilini.

Mambo gani yanayochangia kuongezeka nafasi ya kupata uchungu wa uzazi wa muda mrefu?

Unene sana (Obesity)

Kisukari wakati wa ujauzito au shinikizo la damu kipindi cha ujauzito vinavyoambatana na unene uliopitiliza sana unaweza kuongeza ukubwa wa mtoto. Matatizo haya ya kiafya yanaweza kumfanya mama awe dhaifu, na fati kuzunguka mlango wa uzazi inaweza kusababisha matatizo wakati wa kujifungua.

Uzito duni

Ukosefu wa virutubisho muhimu kwa mama inapelekea ukosefu wa virutubisho kwa kiumbe ndani ya tumbo na mfuko wa uzazi, hivyo kusababisha matatizo katika mlango wa uzazi na kusababisha mtoto kuchelewa kuzaliwa. Udogo wa mwili unamaanisha udogo wa nyonga, ambayo itasababisha mtoto kuchelewa kupita kwasababu ya njia kuwa ndogo mtoto kupita. Hivyo basi, ni muhimu kuangalia afya yako vizuri.

Kupungua kwa wingi wa misuli

Moja ya sababu ya kupungua kwa wingi wa misuli wakati wa ujauzito ni ukosefu wa mazoezi na kuufanyisha mwili kazi ndogo ndogo. Kusukuma mtoto ni utaratibu wenye kuhitaji nguvu nyingi, na inahitaji misuli mizuri kwa kazi kufanyika bila vipingamizi. Upungufu wa misuli utapunguza nguvu na kuongeza nafasi ya uchungu kuchukua mda mrefu.

Kubeba ujauzito ukiwa na umri mkubwa au umri mdogo

Umri mzuri ambao mwanamke anaweza kujifungua vizuri bila vipingamizi vyovyote vya mwili ni kuanzia miaka 25 mpaka 35. Miaka kabla ya hapo na baada ya hapo mwili unakua haujajiandaa vizuri. Kina mama wanaozaa kwa mara ya kwanza katika umri mkubwa wanahitaji kuwa imara kimwili, kinyume na hapo watapata matatizo ya kiafya kama kisukari kinachosababishwa na kubeba mimba.

Nini hutokea ikiwa uchungu wa uzazi unaenda taratibu?

Wanawake wengi wanatamani uchungu wa uzazi unaoenda haraka na kujifungua haraka bila kutaabika. Lakini kama uchungu wa uzazi unaonekana kwenda taratibu, njia pekee ya kukabiliana na hali hii ni kujaribu kutulia kadiri uwezavyo kihisia na kimwili. Jambo kubwa wanalofanya wahudumu wa afya pale inapoonekana mama mjamzito anapitia hali hii ni kuhakikisha mama anatulia kiakili na kihisia kwa kumpatia mama hali ambayo itampunguzia msongo wa mawazo ikiwa ni pamoja na kuwepo karibu nao wakati wote na kumpatia njia ya kupunguza maumivu (inaweza kuwa dawa au njia ya asili ya kupunguza maumivu).

Baadhi ya vipimo vinaweza kufanyika katika muda huu na watoa huduma ili kuchunguza:

 • Mara ngapi misuli ya tumbo la uzazi inabana na kuachia
 • Kwa kiasi gani wa mibano na mikazo “contractions” katika tumbo la uzazi ni imara.

Vipimo hivyo vinavyoweza kufanywa ni pamoja na:

 • “Intrauterine Pressure Catheter Placement (IUPC)”- ni mrija mdogo wa uchunguzi unaoingizwa ndani ya uterasi pembeni ya mtoto unao muonyesha dakatari jinsi “contractions” zinavyotokea na kiasi gani “contractions” hizi ni imara.
 • Kipimo cha kuchunguza mapigo ya moyo ya mtoto.

Je, uchungu wa uzazi wa muda mrefu unatibiwaje?

Ikiwa uchungu wa uzazi unaenda taratibu, unaweza kushauriwa kupumzika kwa muda kidogo. Wakati mwingine dawa hutolewa kupunguza maumivu na kukusaidia kupumzika. Unaweza kujisikia kama kubadilisha mkao wa mwili ili kupata nafuu zaidi.

Matibabu ya ziada yanategemea na chanzo cha uchungu wako kuenda polepole. Ikiwa mtoto yuko tayari kwenye mlango wa uzazi (cervix), daktari au mkunga anaweza kutumia zana maalum zinazoitwa “forceps” au kifaa chenye utupu kusaidia kumvuta mtoto nje kupitia uke.

Ikiwa daktari wako anahisi kama unahitaji mikazo na mibano zaidi au yenye nguvu, unaweza kupatiwa dawa. Dawa hii inaharakisha mikazo na kuifanya imara. Ikiwa baada ya njia zote hizi bado uchungu unachelewa, unaweza kuhitaji upasuaji ili kumtoa mtoto ndani kabla hajapata matatizo ya kiafya.

Ikiwa mtoto ni mkubwa sana, au dawa haifanyi kazi kuharakisha utaratibu ya kujifungua utahitaji upasuaji pia.

Madhara ya uchungu wa uzazi wa muda mrefu

Uchungu wa uzazi wa muda mrefu unaongeza nafasi ya kuhitaji upasuaji ili kujifungua. Hali hii ni hatari kwa mtoto kwasababu inaweza kusababisha:

 • Viwango vidogo vya hewa ya oksijeni kwa mtoto.
 • Mapigo ya moyo yasio ya kawaida kwa mtoto.
 • Maambukizi katika mji wa mimba (uteras).
 • Mtoto kuzaliwa akiwa mfu (stillbirth)

Mama anaweza kupata:

 • Maambukizi.
 • Kupasuka au kuchanika kwa mji wa uzazi (uterine rupture).
 • Ugonjwa wa fistula ambao husababisha shimo kubwa kati ya njia ya uzazi na njia ya mkojo unaotokana na mama kuwa na uchungu wa muda mrefu bila matibabu.

Je, unawezaje kupunguza nafasi ya kupata uchungu wa uzazi wa muda mrefu?

Unaweza kupunguza hatari za kupata uchungu wa uzazi ambao ni taratibu kwa kuchukua tahadhari zifuatazo:

 • Jitahidi kuishi mtindo wa afya wa kimaisha: fanya mazoezi kuwa imara na mkakamavu, kula mlo kamili wenye afya, siku zote kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara.
 • Jitahidi kupunguza msongo wa mawazo: zuia kila aina ya woga na wasiwasi wowote, jitahidi kuzungukwa na shughuli na watu wenye mawazo chanya. Kila wakati jikumbushe jinsi gani utakua mwenye furaha na fahari kumpakata mwanao mkononi mwako.
 • Hali ya umasikini ya maisha ni chanzo kikuu cha magonjwa ya ziada wakati wa uchungu wa uzazi. Inashauriwa kufanya miadi ya kila mwezi na mkunga wako ili shida kama unene uliopitiliza au ukosefu wa misuli ya kutosha kugundulika mapema. Kwa kuchukua taadhari na mikakati sahihi unaweza kupunguza uchungu wa uzazi wa muda mrefu.

IMEPITIWA: JUNI, 2021.

Umuhimu wa Asidi ya Foliki Kipindi cha Ujauzito.

Asidi ya foliki ni shujaa katika mimba! Kumeza vitamini kabla ya kupata ujauzito kwa kiwango kinachokubalika cha mikrogramu 400mcg kabla na wakati wa ujauzito huweza kusaidia matatizo ya kuzaliwa nayo kwenye ubongo, mgongo na uti wa mgongo wa mtoto wako. Ni vyema kumeza kidonge cha asidi ya foliki kila siku kama unategemea au wewe ni mjamzito tayari.

Asidi ya foliki (Folic acid) ni nini?

Asidi ya foliki ni aina ya vitamini B inayoitwa “folate” inayotengenezwa na mwanadamu maabara (inajulikana kama vitamini B9). “Folate” inafanya kazi muhimu kwenye utengenezaji wa chembe damu nyekundu na pia husaidia katika kukinga dhidi ya kasoro katika neva za fahamu na hivyo kuepusha dosari za kimaumbile katika ubongo, mgongo na uti wa mgongo. Chakula bora chenye wingi wa asidi ya foliki ni “fortified cereals”. Folati hupatikana zaidi kwenye mbogamboga zenye rangi kijani iliyokolea na matunda jamii ya chungwa.

Ni lini uanze kutumia asidi ya foliki?

Matatizo ya kuzaliwa nayo (dosari katika neva za fahamu) huanza kutokea ndani ya wiki ya 3-4 ya ujauzito (siku 28) baada ya mimba kutungwa, kabla hata mama kujua kuwa ni mjamzito. Hivyo ni muhimu kuwa na “folate” tayari kwenye mzunguko wa mwili wako kwenye kipindi hiki muhimu cha mwanzoni ambapo ndio ubongo na uti wa mgongo wa mtoto wako unajijenga.

Kama ulizungumza na daktari wako kipindi ulichokuwa unataka kupata ujauzito, inawezekana alishakushauri tayari kuanza kutumia vitamini na asidi ya foliki. Tafiti moja ilionesha wanawake waliotumia asidi ya foliki kwa kuanzia mwaka kabla ya kupata ujauzito walipunguza uwezekano wa kujifungua mapema kabla ya muda (kabla ya wiki 37) kwa asilimia 50 au zaidi.

Tafiti zinaonesha nusu ya mimba zote hazikuwa zimepangwa hivyo inapendekezwa kuwa mwanamke yeyote anayetarajia kupata ujauzito atumie mickrogramu 400 za vidonge vya foliki asidi kila siku, akianza kabla ya kupata ujauzito na kuendelea namna hiyo kwa wiki 12 za ujauzito. Muda huu wa wiki 12 za mwanzo wa ujauzito ndiyo muda ambao ubongo na mfumo wa neva unajengwa na kukua

Shirika la kuzuia magonjwa la Marekani (CDC) linashauri Vilevile shirika wanawake wote walio kwenye umri wa kuweza kuwa wajawazito kutumia asidi ya foliki kila siku. Hivyo hata ukiamua kuanza kutumia asidi ya foliki mapema zaidi ni vyema zaidi.

Kama utaamua kununua nyongeza ya vitamini wewe mwenyewe, ni vyema ukazungumza pia na daktari wako baada ya kupata ujauzito ili kuwa na uhakika kuwa nyongeza hiyo ya vitamini ina mjumuisho wa kila kitu unachotakiwa ukipate kwa ujauzito wako ikiwemo asidi ya foliki.

Kiasi gani cha asidi ya foliki nitumie?

Dozi inayoelekezwa kwa wanawake wote waliopo kwenye umri wa kuweza kupata ujauzito ni mikrogramu 400 au 400mcg za folati kila siku. Ikiwa wewe ni mjamzito au unajaribu kupata ujauzito unashauriwa kutumia foliki asidi mapema kadiri uwezavyo na ndani ya wiki 12 za kwanza za ujauzito. Kufanya hivi kutamsaidia mtoto kukua vizuri na kawaida.

Daktari anaweza kukushauri kutumia dozi kubwa zaidi ya foliki asidi ikiwa uko katika hatari kubwa ya kupata dosari katika neva za fahamu (neural tube defects) wakati wa ujauzito.

Huu ndio mchanganuo wa kiasi cha asidi ya foliki kinachoelekezwa kwa wanawake wajawazito kwa siku

 • Ukiwa unataka kupata ujauzito – 400mcg
 • Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito – 400mcg
 • Kuanzia mwezi wa 4 hadi wa 9 wa ujauzito – 600mcg
 • Ukiwa unanyonyesha – 500mcg.

Mama ambaye tayari amepata mtoto mwenye dosari katika neva za nyuroni (mfumo wa fahamu) anahitaji ajadiliane na daktari wake kama atahitaji vidonge vya foliki na dozi yake itakuwa ni ipi. Tafiti zinaonesha kwamba matumizi ya mikrogramu 4,000 kwa mwezi mmoja kabla na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito zinaweza kusaidia kutatua tatizo hili. Tafadhali usitumie dawa hizi mwenyewe bila kujadiliana na daktari kwanza.

Asidi ya foliki ina faida gani?

Bila kuwa na asidi ya foliki ya kutosha, dosari katika neva za fahamu na hivyo kuepusha kasoro za kimaumbile katika ubongo, mgongo na uti wa (neural tube defects). Magonjwa haya ni kama:

 • Spina bifida: Kutokukamilika ukuaji wa uti wa mgongo au pingili za uti wa mgongo.
 • Anencephaly: Kutokukamilika kwa ukuaji wa sehemu kubwa ya ubongo.

Watoto wenye “Anencephaly” mara nyingi hawaishi muda mrefu na wale wenye “spina bifida” huwa na ulemavu maisha yao yote. Habari njema ni kwamba kutumia nyongeza ya asidi ya foliki kipindi cha ujauzito inaweza kumuepusha mtoto wako kupata magonjwa haya kwa zaidi ya asilimia 50.

Kama utatumua kabla na wakati wa ujauzito, asidi ya foliki inaweza kumkinga mtoto wako dhidi ya:

 • Mdomo sungura
 • Kuzaliwa kabla ya muda (Njiti)
 • Kuzaliwa na uzito mdogo
 • Mimba kutoka
 • Ukuaji dhaifu tumboni

Asidi ya foliki pia inahusishwa na kupunguza hatari ya kupata:

 • Matatizo kwenye ujauzito
 • Magonjwa ya moyo
 • Kiharusi
 • Aina baadhi ya saratani
 • Ugonjwa wa “Alzheimer”

Je, kuna vyanzo vingine vya folati?

Vyakula vilivyo na foliki asidi katika kiwango kiubwa ni kama:

 • Mboga za majani kama spinachi, kabichi, loshu, broccoli
 • Mimea jamii ya kunde kama maharage, mbaazi, njegere, njugu
 • Karanga, njugumawe, nazi na korosho
 • Matunda jamii ya sitrusi kama machungwa, machenza, limao n.k
 • Nafaka zisizokobolewa
 • Maini na samaki
 • Vyakula vilivyoongezwa foliki asidi.

Kumbuka

 • Kichefuchefu, kupoteza hamu ya kulan a kuvimbiwa ni madhara yanayoweza kutokea kwa mjamzito kama matokeo ya kutumia vidonge hivi. Ulaji wa chakula kidogo kidogo badala ya kula milo mikubwa mitatu kwa siku, kula na kunywa taratibu na kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara yanaweza kusaidia dalili hizi unazoweza kupata kama matokeo ya kutumia asidi ya foliki. Ikiwa dalili hizi zinaendelea kuwa mbaya, wasiliana na daktari/mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako mara moja.
 • Mtoto tumboni yuko katika hatari ya kupata dosari katika mfumo wa fahamu ikiwa: mama mjamzito aliwahi kupata ujauzito ulipata dosari katika mfumo wa neva za fahamu, wewe au mwezi wako ana kasoro katika neva za fahamu aliyozaliwa nayo,katika familia yako au mwezi wako kuna historia ya watu kuzaliwa na dosari katika neva za fahamu, mjamzito ana kisukari,mjamzito ana uzito mkubwa uliopitiliza na mjamzito ana ugonjwa wa siko seli.
 • Mama ambaye hakutumia foliki asidi kabla au miezi ya awali ya ujauzito ajadiliane na daktari/mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wake, wataweza kukushauri nini kifanyike na dozi kiasi gani itumike kuokoa maisha ya mtoto tumboni. Tafadhali usitumie dawa hizi mwenyewe bila kujadiliana na daktari kwanza.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Umuhimu wa Lishe Bora kwa Mjamzito Kabla ya Kujifungua.

Vitamini unazotumia kabla ya kujifungua zina virutubisho vingi mtoto wako anavyohitaji, hivyo basi kuna umuhimu gani waa mama mjamzito kuangalia kwa makini lishe yake?

Inaathiri afya ya mtoto wako maishani: Kila unachokula ukiwa mjamzito kinamuathiri mtoto na maisha yake kwa ujumla, hivyo ni muhimu kula vizui kwa manufaa ya mtoto hapo baadae. Kuna baadhi ya tafiti zinazoshauri ulaji wa vyakula vyenye chumvi, mafuta na sukari vinaathiri mapendekezo ya ladha ya mtoto hapo baadae. Hii inaweza kumsababisha mtoto kupata changamoto katika ulaji, afya na uzito kutokana na aina ya lishe uliyomtambulisha ukiwa mjamzito.

Chakula kinasaidia mwili kufyonza virutubisho vyenye afya: Ikiwa unakula mlo kamili mwili wako una nafasi kubwa ya kupata na kufyonza virutubisho na madini yanayohitajika katika mwili.

Chakula bora kinasaidia mwili kufanya kazi vizuri: Ukiwa unakula vizuri mwili wako utakushukuru. Utakuwa na nguvu ya kutosha, utajisikia vizuri na pengine kuepuka kero, usumbufu na maumivu ya kawaida ya ujauzito.

Aina za Matunda Mazuri Wakati wa Ujauzito

Ndizi

Ndizi ni chakula kizuri sana wakati wa ujauzito. Zinashibisha na zina viwango vikubwa vya madini ya kalishiamu na potasiamu ambayo yanasaidia matatizo ya misuli ya miguu kukaza. Ikiwa una hamu ya kitu chenye sukari kilicho salama kwako na mtoto tumboni, ndizi za kuiva ni chaguo sahihi. Lakini kama una kisukari kilichosababishwa na ubebaji mimba, chagua kula ndizi za kupikwa (mbichi).

Tufaha (apple)

Matunda haya yana vitamini A na C, maji ya kutosha na nyuzinyuzi (fiber) zitakazokusaidia kulainisha choo.

Tikiti Maji

Tunda hili lina kiwango kikubwa cha maji kuliko tunda linguine lolote-92%. Ikiwa unapambana na tatizo la kukosa maji mwili wakati wa ujauzito, unashauriwa kula tunda hili. Tikiti maji lina madini ya potasiamu, zinki na foliki asidi kwaajili ya kupambana na misuli ya miguu kukaza wakati wa usiku na kusaidia ukuaji wa uti wa mgongo wa mtoto tumboni.

Machungwa

Chungwa linaweza kuwa tamu au chachu, ladha hizi zina pendwa na wanawake wengi ambao wanasubuliwa na kichefuchefu wakati wa ujauzito. Yana kiwango kikubwa cha maji, ni chanzo kizuri sana cha vitamini C. Vitamini hii inachangia kukuza kinga yako na mtoto tumboni, na pia inasaidia kujenga tishu muhimu kwa ajili ya ukuaji wa kimwili wa mtoto.

Parachichi

Parachichi lina madini chuma,magnesiamu, potasiamu na nyuzinyuzi (fiber). Madini chuma yanayotumika kuzuia anemia, magnesiamu na potasiamu yanasaidia tatizo la misuli ya miguu kukaza na kichefuchefu. Parachichi ni chanzo cha fati unayotakiwa kupata ukiwa mjamzito.

Peasi

Ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi zinazosaidia kupambana na tatizo la kukosa choo. Ni chanzo kizuri pia cha vitamini C, pamoja na madini chuma, magnesiamu na foliki asidi.

Embe

Ni chanzo kizuri cha vitamini C na A, inayosaidia kukuza kinga ya mtoto.

Faida za Matunda Wakati wa Ujauzito

Je, unataka ujauzito salama na wenye afya?

Kuna sababu nyingi za kula matunda ukiwa mjamzito, nazo ni pamoja na:

Yanatoa virutubisho muhimu: Mtoto wako anahitaji virutubisho fulani ili kukua vizuri. Virutubisho vinavyotolewa na matunda ni pamoja na vitamini C na foliki. Vitamini C ni muhimu kujenga tishu, inasaidia kukuza kinga ya mwili ya mtoto na kuruhusu uhifadhi wa madini chuma yanayotumika kuzuia anemia. Foliki inasaidia kujenga uti wa mgongo na pia kumkinga mtoto anayekua dhidi ya kasoro katika neva za fahamu na hivyo kuepusha dosari katika ubongo, mgongo na uti wa mgongo (neural tube defects).

Yanasaidia kukidhi hamu ya vyakula vitamu: Utofauti mmojawapo wa matunda ni kuwa matamu au machachu, ladha zote hizi ni pendwa kwa wajawazito. Kuchagua tunda badala ya peremende au biskuti itakusaidia kumaliza hamu katika njia ya kuridhisha na salama kwa afya.

Ni chaguo zuri ukisikia kichefuchefu: Ikiwa unapata changamoto ya kichefuchefu wakati wa ujauzito, ni ngumu kuweka chakula tumboni kwa muda mrefu. Vyakula vitamu na baridi ni vizuri ikiwa una pambana na magonjwa ya asubuhi, hakikisha unatunza matunda ya kutosha kwenye friji kwaajili ya kifungua kinywa.

Yanasaidia kudhibiti sukari katika damu: Matunda yana nyuzinyuzi (fiber) zinazosaidia kuratibu ufyonzaji wa sukari katika mfumo wa damu.

Matunda yanakufanya uwe na maji ya kutosha mwilini: Unahitaji kunywa maji ya kutosha ukiwa mjamzito. Tunda lina zaidi ya asilimia 80 ya maji, hivyo ikiwa umechoka kunywa maji kila saa unaweza kuchagua kula matunda kuhakikisha mwili wako unakaa na maji.

Yanasaidia kukabiliana na tatizo la kukosa choo: Ukiwa mjamzito, umeng’enyaji wa chakula unakua polepole, hali hii inaweza sababisha kukosa choo- lalamiko la kawaida kipindi cha ujauzito. Ikiwa unatumia virutubisho vyenye madini ya chuma yanaweza kusababisha kukosa choo. Tatizo kubwa la kukosa choo linaweza kusababisha “hemorrhoids”. Njia nzuri ya kuondokana na tatizo la kukosa choo ni ulaji wa vyakula ambavyo ni vyanzo vizuri vya nyuzi nyuzi na kunywa maji (matunda yana vyote viwili-maji na nyuzi nyuzi).

Kiasi Gani cha Matunda Nile Nikiwa Mjamzito?

Ingawa ulaji wa matunda ni afya, lakini ikumbukwe matunda ni chanzo cha sukari, ambayo inatakiwa kuwekwa kikomo ukiwa mjamzito. Inashauriwa mjamzito kula matunda mara 2-4 kwa siku.

Je, Kuna Matunda Natakiwa Nisile Wakati wa Ujauzito?

Hakuna kikomo cha kula matunda ikiwa limeiva na safi. Ni muhimu kuhakikisha unasafisha vizuri matunda kabla ya kula ili kuepuka uchafu utakaosababisha ugonjwa. Mchanganyiko wa maji na vinegar ni mzuri na salama kusafishia matunda hasa yaliyokuzwa kwa kemikali za kiwandani (nyanya, tufaha, zabibu, peasi, strawberi n.k)

Kumbuka

 • Nanasi limepata sifa ya kusababisha mimba kutoka na kusadikika kuchochea uchungu kabla ya mda wa kujifungua. Ijapokuwa hakuna ushahidi wa kisayansi kuunga mkono madai haya, nanasi linajulikana kama tunda salama kutumia katika viwango sahihi wakati wa ujauzito.
 • Tunda pekee linalotakiwa kuepukwa ni papai bichi, papai ambalo halijaiva lina dutu ambayo inachochea mikazo ya mfuko wa mimba.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Tatizo la Kukosa Choo Kipindi cha Ujauzito

Tumbo kujaa gesi, kuvimbiwa, hali ya kujisikia umebanwa na haja kubwa ni malalamiko ya kawaida kipindi cha ujauzito.

Tatizo la kukosa choo ni hali isiyopendeza, kwa bahati mbaya ni hali ya kawaida sana wakati wa ujauzito- baadhi ya ripoti zinasema karibia asilimia 40 ya wanawake wanapitia hali hii. Kadiri tumbo linavyozidi kukua ndivyo mkandamizo wa mfuko wa mimba unavyoongezeka katika eneo la haja kubwa na kuzidisha tatizo hili.

Lini tatizo la kukosa choo linaanza wakati wa ujauzito?

Tatizo la kukosa choo linaanza mapema kadiri viwango vya projesteroni vinavyoongezeka, karibu na mwezi wa pili hadi wa tatu wa ujauzito. Inaweza kuwa mbaya zaidi wakati ujauzito unavyoendelea na uterasi yako inavyokua.

Ni moja ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwasumbua wajawazito wengi hasa katika miezi ya awali ya ujauzito na miezi ya mwisho ya ujauzito.

Nini chanzo cha tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito, nazo ni pamoja na:

Viwango vya homoni ya projesteroni: homoni hii huzalishwa kwa wingi wakati wa ujauzito,homoni hii hujulikana kulegeza misuli ya tumbo la chakula hivyo kusababisha chakula kupita taratibu katika utumbo. Mabaki ya chakula hukaa kwa muda mrefu tumboni bila ya kutolewa nje kama taka,kadiri mabaki hayo yanavyo zidi kubaki tumboni ndivyo maji yaliyo katika mabaki hayo huendelea kufyonzwa na utumbo hivyo kusababisha kukosa choo kwa muda na vilevile kupata choo kigumu.

Matumizi ya vidonge vya kuongeza madini ya chuma mwilini: ijapokuwa madini ya chuma ni muhimu wakati wa ujauzito kwa ukuaji wa mtoto, kukosa choo kwa mjamzito inaweza kuwa athari ya kutumia sana vidonge hivi. Ni vema kuongea na mkunga wako kuhusu jambo hili, anaweza kukushauri kubadilisha vidonge hivi, dozi yake au mara ngapi uvitumie. Hakikisha unafuata maelekezo kwasababu ukosefu wa damu ya kutosha (anemia) hutokea sana wakati wa ujauzito na inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa mama na mtoto.

Ukosefu wa maji ya kutosha mwilini: wakati wa ujauzito mama anakabiliwa na tatizo la upungufu wa maji mwilini, kwasababu mwili unatumia maji zaidi kusaidia kutengeneza plasenta na “amniotic sac” (kifuko cha amnion-mfuko wa maji yanayomlinda mtoto na hupasuka kabla mtoto hajazaliwa. Ikiwa utakuwa na upungufu wa maji mwilini, mwili wako utashindwa kufanya kazi muhimu na kupelekea kupata shida kubwa sana za kiafya.

Msongo wa mawazo: ujauzito unaweza kuleta msongo wwa mawazo hasa unapokaribia siku ya kujifungua. Epuka kuwa na wasiwasi sana, hali hii inaweza kuathiri mfumo wa umeng’enyaji wa chakula na utoaji taka (kukosa choo).

Ukuaji wa tumbo la uzazi: kuongezeka kwa ukubwa wa tumbo la uzazi hutokea zaidi katika miezi ya mwisho ya ujauzito,ukubwa wa tumbo la uzazi kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa mtoto tumboni husababisha mkandamizo mkubwa kwenye tumbo la chakula,hivyo kupunguza kasi ya usafirishwaji wa mabaki ya chakula nje ya tumbo,hivyo kusababisha mwili kufyonza maji katika mabaki hayo na kuleta choo kigumu.

Mwili kutofanyishwa kazi na mazoezi: kadiri tumbo linavyozidi kuwa kubwa, inakuwa ngumu kwa mama kuwa imara katika ufanyaji kazi na mazoezi. Ufanyaji wa mazoezi huchochea misuli ya tumbo kufanya kazi yake ya kutoa taka nje ya mwili, mjamzito anavyo kuwa hafanyi mazoezi misuli ya tumbo nayo hushindwa kufanya kazi yake vizuri na kusababisha mama kukosa choo.

Wakati mwingine kukosa choo kunasababishwa na ulaji wa bidhaa za maziwa sana (dairy products), dawa mpya unayotumia au ulaji mdogo wa vyakula vyenye nyuzi nyuzi (fibre) kama matunda na mboga mboga za majani. Fiber hupatikana katika vyakula vya mimea: mboga, matunda, mboga, nafaka, karanga.

Baadhi ya vyakula unavyotakiwa kuacha ikiwa unasumbuliwa na tatizo la kukosa choo ni pamoja na ndizi, vyakula vya kukaangwa, viazi vya kukaanga, nyama nyekundu, mkate mweupe, wali mweupe, pasta na vyakula vya maziwa kama jibini.

Je, nini unapaswa kufanya ukipata tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Hakuna haja ya kuteseka miezi yote tisa kwa tatizo hili. Zipo mbinu nyingi zitakazo kusaidia kupambana na tatizo la kukosa choo, nazo ni pamoja na:

 • Kula vyakula vyenye nyuzi nyuzi kwa wingi, vyakula hivi vinasaidia kutoa mabaki ya chakula kwenye utumbo kwa urahisi zaidi. Hakikisha unakula nafaka zisizokobolewa, vyakula jamii ya kunde, matunda safi na mboga za kijani za majani (mboga mbichi au iliyopikwa kidogo).
 • Kunywa maji ya kutosha. Maji mengi yatakusaidia kutoa mabaki ya chakula nje ya mwili kwa haraka zaidi. Hakikisha unakunywa angalau glasi 8 za maji kwa siku. Maji yanaweza kusaidia tatizo la kukosa choo lililosababishwa na matumizi ya vidonge vya madini chuma. Ikiwa unaishi eneo lenye hali ya hewa ya joto, kunywa zaidi maji (zaidi ya glasi 8)
 • Fanya mazoezi. Kutembea, kuogelea na yoga ni mazoezi mazuri kwa mwili wa mwanamke mwenye ujauzito. Mwili unapofanyishwa mazoezi unasaidia utembeaji wa mabaki ya chakula kuelekea nje ya mwili.
 • Oga kwa maji ya moto. Maji ya moto yanasaidia kupumzisha misuli na kuhamasisha taka kutoka nje ya mwili. Kama una bafu la kulala (bathtub) jiloweke kwa lisaa moja au zaidi.
 • Kunywa maji yenye limao. Chukua juisi ya limao nusu, changanya kwenye glasi ya maji, kisha kunywa kabla ya kwenda kulala. Maji yatasaidia kulainisha kinyesi, limao lina kiwango kikubwa cha asidi kitakachosaidia kusafirisha kinyesi.
 • Kula vyakula vyenye magnesiamu ya kutosha. Magnesiamu yanasaidia kuelekeza maji kwenye utumbo na kusaidia kinyesi kulainika na kusafirishwa nje kwa urahisi. Hakikisha unapata miligramu 350 kwa siku kwa kula vyakula kama samaki, spinachi, karanga na chokoleti nyeusi.
 • Epuka nafaka zilizokobolewa kila unapoweza, nafaka hizi zinachangia kukosa choo. Kwa mfano badala ya kula mkate mweupe, kula mkate wa kahawia (broen bread).
 • Jaribu kula milo sita midogo midogo kwa siku badala ya milo mitatu mikubwa, kwa kufanya hivi unaweza kuepuka kuvimbiwa na tumbo kujaa gesi.
 • Jisaidie haja kubwa kila unapoisikia, kubana haja kubwa mara kwa mara kunafanya misuli ya kuzuia utokaji wa kinyesi kuwa hafifu na kusababisha tatizo la kukosa choo.
 • Zingatia virutubisho na dawa zako. Jambo la kushangaza ni kwamba, virutubisho na dawa nyingi ambazo hufanya mwili wa mjamzito kuwa na afya kwa mfano; vitamini za kutumia kabla ya kuzaa, virutubisho vya kalsiamu na chuma zinaweza kuzidisha tatizo la kukosa choo. Kwa hivyo jadiliana na daktari wako kuhusu njia mbadala au marekebisho ya dozi za virutubisho hivi hadi hali itakapoboreka. Muulize pia daktari wako juu ya kutumia zaidi virutubisho vyenye madini ya magnesiamu kusaidia kupambana na tatizo la kukosa choo.
 • Ongea na daktari wako. Pale ambapo mbinu hizi za nyumbani hazifanyi kazi vizuri, mshirikishe daktari wako anaweza kukusahauri dawa au mbinu nyingine za kidaktari.

Je, naweza kuzuia kupata tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Tabia ya kula kiafya na mazoezi ya kawaida huhimiza mfumo wa haraka wa kumeng’enya chakula, ambao unaweza kusaidia kuzuia tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito.

Kutumia vyakula vingi vyenye nyuzi nyuzi (kama; matunda, mboga, nafaka nzima, dengu), kunywa maji ya kutosha na kuupa mwili mazoezi vyote kwa pamoja vinazuia tatizo la kukosa choo.

Lini nitarajie tatizo la choo kuisha nikiwa mjamzito?

Kwa wanawake wengine, tatizo la kukosa choo hudumu katika kipindi chote cha ujauzito kadri viwango vya projesteroni vinapopanda. Walakini, ukibadilisha tabia yako ya kula na kuwa na tabia ya kufanya mazoezi kila mara, mambo huanza kusonga vizuri. Na unaweza kuchukua hatua za kupambana na tatizo hili la kukosa choo wakati wowote wa ujauzito.

Kumbuka

Utafurahi kujua kwamba vitamini unazotumia kabla ya kujifungua pia zinaweza kusaidia tatizo la kukosa choo, haswa asidi ya folic. Manufaa ya “vitamini B complex” na “vitamini B5” sio tu kutatua tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito, bali inasaidia kupunguza maumivu ya miguu wakati wa ujauzito. Unaweza kuipata kutoka kwa viini vya mayai, nafaka nzima, parachichi, viazi vitamu, mbegu za alizeti, broccoli.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Kutoka Uchafu Ukeni Kipindi cha Ujauzito

Moja ya njia muhimu ya kutunza mfumo wa uzazi wa mwanamke ni kupitia uchafu unaotoka ukeni. Uchafu huu huweka uke wa mwanamke kuwa na afya nzuri ingawa wakati mwingine huweza kuleta shida. Maji yaliyotengenezwa na tezi ndani ya uke na mlango wa uzazi hubeba seli zilizokufa na bakteria nje ya mwili. Tendo hili linaweka uke safi na kusaidia kuukinga na maambukizi.

Wanawake wote hutokwa na uchafu ukeni, ingawa kiwango hutofautiana. Mara nyingi uchafu unaotoka ukeni ni kawaida kabisa. Unatofautiana kwa harufu,uzito, na rangi kulingana na mzunguko wako wa hedhi. Kwa mfano unaweza kutoka uchafu mwingi ukeni kama uko kwenye siku za yai lako kupevushwa, unanyonyesha au ashiki (hamu ya kujamiana). Uchafu huu unaweza kutoa harufu ya tofauti ukiwa mjamzito au unaposhindwa kujisafisha vizuri. Wanawake waliokomaa (menopause women) hupata uchafu huu kwa kiwango kidogo sana.

Mabadiliko haya yasikupe wasiwasi ni kawaida. Isipokuwa kama una dalili zifuatazo unaweza kuwa na tatizo la maambukizi ya vijidudu vya maradhi katika uke wako, ni vema kuwahi kituo cha afya kupatiwa uchunguzi zaidi na tiba sahihi:

 • Kutokwa uchafu ukeni kunakoambatana na kuwashwa au vipele.
 • Kutokwa uchafu ukeni ambako ni endelevu na kiwango kinaongezeka kila siku.
 • Maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo.
 • Kutoka uchafu mweupe, mzito kama jibini.
 • Kutoka uchafu wa kijivu/mweupe au njano/kijani unaotoa harufu mbaya.
 • Unajikuna, kuchomwa au hata uvimbe kwenye uke.
 • Maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Nini chanzo cha uchafu ukeni usio wa kawaida kwa mwanamke?

Badiliko lolote katika uwiano sawa wa bakteria wa asili wanaopatikana ukeni linaweza kuathiri harufu, rangi na muonekano wa uchafu unaotoka ukeni. Hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea uchafu ukeni kwa mwanamke yeyote:

 • Matumizi ya antibaotiki au virutubisho vya kikemikali (steroid)
 • Maambukizi yanayosababishwa na bakteria “bacterial vaginosis” – yanawapata wajawazito sana au wanawake walio na wapenzi zaidi ya mmoja.
 • Njia za mpango wa uzazi-vidonge
 • Kansa ya kizazi
 • Magonjwa ya zinaa kama klamedia au kisonono
 • Kutumia sabuni zenye marashi makali kusafishia uke/kutumia mafuta yenye harufu kali ukeni
 • Maambukizi katika mfumo wa uzazi baada ya upasuaji wakati wa kujifungua.
 • Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
 • Ugonjwa wa malengelenge sehemu za siri (trichomoniasis), unaosababishwa baada ya kufanya ngono zembe.
 • Uke kuwa mkavu kwa wanawake waliofikia ukomo wa kuzaa
 • Ugonjwa wa fangasi ukeni (yeast infection)

Aina ya uchafu unaotoka ukeni na chanzo chake

Aina ya uchafu Maana yake ni nini? Dalili nyingine
Rangi ya damu au kahawai(hudhurungi) Ishara ya mzunguko wa hedhi uliovurugika (irregular menstrual cycle), kansa ya kizazi au kansa katika mfuko wa uzazi. Utokaji wa damu ukeni usio wa kawaida, maumivu ya nyonga.
Rangi yenye mawingu au njano (cloudy or yellow) Kisonono Damu kabla na baada ya siku yako ya hedhi, maumivu ya nyonga,kushindwa kuzuia mkojo.
Uchafu wenye rangi njano au kijani unaotoka kama povu na wenye harufu mbaya. ugonjwa wa trichominiasis Maumivu na muwasho kila unapokojoa.
Uchafu wenye rangi ya pinki. Tabaka lililojishika ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi linatoka nje ya mwili baada ya kujifungua (lochia-kutokwa damu baada ya kujifungua)  
Uchafu mzito, mweupe, unaofanania jibini Ugonjwa wa fangasi ukeni. Maumivu na kuvimba kuzunguka uke (vulva), muwasho, maumivu wakati wa kujamiana.
Uchafu mweupe, rangi ya kijivu, au njano wenye harufu ya shombo ya samaki. Bakteria ukeni Muwasho au kuungua, wekundu na kuvimba uke au ndani ya uke (vagina au vulva)

 Chanzo cha uchafu kutoka ukeni kipindi cha ujauzito ni nini?

Ujauzito unaweza kukuchanganya kadiri unavyoendelea kukua, sio rahisi kujua mabadiliko yapi ni kawaida na yapi yanahitaji uharaka wa kuwasiliana na mkunga wako au kutembelea kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi. Mojawapo ya mabadiliko haya ni kutokwa uchafu ukeni, ambao unabadilika katika muda wa kutokea,mara ngapi unatokea,muonekano, kiasi,na uzito wake kipindi cha ujauzito.

Moja ya ishara za awali za ujauzito ni ongezeko la uchafu unaotoka ukeni, hali hii inaendelea kipindi chote cha ujauzito. Kwa kawaida uchafu unaotoka ukeni (leukorrhea) ni mwembamba, unaonekana vizuri (clear) au una rangi ya maziwa meupe na unatoa harufu kidogo.

Mabadiliko ya viwango vya homoni mara baada ya kuwa mjamzito yanasababisha mabadiliko ya uchafu unaotoka ukeni. Mabadiliko ya mlango wa uzazi kipindi cha ujauzito yanachangia kuathiri uchafu unaotoka ukeni. Kulainika kwa mlango wa uzazi na ukuta ndani ya uke, kunasababisha mwili kutoa uchafu zaidi ili kujikinga na maambukizi. Unapokaribia mwisho wa ujauzito kichwa cha mwanao kinaweza kuleta mgandamizo katika mlango wa uzazi na kupelekea ongezeko la uchafu unaotoka ukeni.

Kipindi chote cha ujauzito inategemewa mama mjamzito kupitia dalili kama mkojo kuvuja, kutoka uchafu, kuwashwa, na kuona damu katika nguo za ndani.

Katika makala hii utaweza kujua aina gani ya uchafu unaotoka ukeni ni kawaida na upi una ashiria tatizo linalohitaji kumuona daktari. Ili kujua aina gani ya uchafu unaotoka ukeni wakati wa ujauzito ni kawaida, tujifunze zaidi kuhusu vyanzo vyake:

Uchafu wa kawaida ukeni

Matone ya damu katika nguo zako za ndani

Hakuna kitu kinacho ogopesha kama kutokwa damu bila kutarajia. Wanawake wengi wanaona damu kidogo katika nguo zao za ndani katika kipindi cha miezi mitatu ya awali baada ya kufanya tendo la ndoa au uchunguzi wa mfumo wa uzazi katika miadi. Mara nyingi hali hii inaashiria yai lililo rutubishwa limefanikiwa kupandikizwa kwenye ukuta wa mfuko wa mimba (implantation) au muwasho katika mlango wa kizazi.

Kuona damu katika nguo zako za ndani kipindi cha mwisho cha ujauzito inahusiana na kuwa na kiasi cha ziada cha damu na homoni zinazopelekea mishipa iliyopo kwenye mlango wa uzazi kutoa damu. Wakati mwingine ina ashiria kujifungua kuna karibia, lakini pia inaweza kuashiria tatizo kubwa la kiafya kama- kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa. Kila unapoona matone ya damu kwenye nguo zako za ndani yasio kawaida (rangi nyekundu inayong’aa) mjulishe mkunga wako.

Unyevu katika nguo za ndani(chupi)

Je, unyevu kwenye nguo za ndani ni ishara chupa yako imepasuka? Inawezekana ni mkojo, ikiwa unavuja kila unapo cheka, piga chafya au kukohoa. Kuvuja mkojo ni kawaida kipindi cha ujauzito, inatokea kwasababu ya mgandamizo wa uterasi inayoendelea kukua. Mazoezi maalumu- “kegel” yanasaidia wanawake wengi kuweza kudhibiti vibofu vyao. Unaweza kufanya utaratibu wa kuwahi chooni dakika chache kabla ya kubanwa mkojo vizuri. Kumbuka usiache kunywa maji ya kutosha hata kama unavuja mkojo bila kutarajia. Ikiwa unahisi maji yanayovuja sio mkojo bali chupa ya uchungu imepasuka, fanya utaratibu wa kuwasiliana na mkunga wako au wahi kituo cha afya.

 Uchafu usio kawaida ukeni.

Ugonjwa wa fangasi ukeni

Maambukizi haya yana ambatanana muwasho, wekundu na kuvimba kuzunguka uke, baadhi ya wanawake wanapata maumivu wakati wa tendo la ndoa na kuungua wakati wa kukojoa. Uchafu huu una rangi ya njano au nyeupe inayofanana na jibini. Fangasi wanaishi ndani ya mwili na kwenye uke muda wote, lakini ujauzito unatengeneza mazingira ya fangasi kuzaliana.

Muone daktari akupatie ushauri wa dawa sahihi kwaajili ya maambukizi haya. Punguza sukari kwenye mlo wako (fangasi wanapenda sukari) na hakikisha unabadilisha nguo yako ya ndani (chupi) mara kwa mara.

Bakteria ukeni (Bacterial vaginosis-BV)

Maambukizi haya yanasababishwa na kukosekana kwa uwiano sawa wa bakteria asili wanaopatikana ukeni. Uchafu huu unaonekana zaidi baada ya kufanya tendo la ndoa,unaambatana na muwasho au kuungua kila unapojisaidia. Vile vile unakua na harufu ya shombo ya samaki ukiwa mjamzito. Maambukizi haya yasipotibiwa vizuri yanaweza kusababisha matitizo makubwa kwenye ujauzito. Kawaida maambukizi haya yanaanza katika uke, lakini baadae yanapanda kwenye uterasi na kusababisha kuraruka membreni mapema na kujifungua kabla ya wiki ya 37.

Ikiwa unahisi una dalili za maambukizi haya, muone daktari haraka. Dawa sahihi zinaweza tokomeza dalili zote bila kuhatarisha mtoto tumboni na kupunguza nafasi ya kujifungua kabla ya wiki 37.

Magonjwa ya zinaa

Wakati mwingine uchafu wenye rangi ya njano wakati wa ujauzito unaashiria kisonono, na uchafu unaotoka kama povu wenye rangi ya kijani au njano wakati wa ujauzito unaonyesha ugonjwa wa “trichomoniasis” zaidi ya hayo, uchafu ulio na harufu unasababishwa na klamedia. Maambukizi haya matatu ya zinaa yanaweza sababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa au kujisaidia. Kuwa na magonjwa ya zinaa wakati wa ujauzito inapelekea kujifungua kabla ya wiki 37 na maambukizi ya mfuko wa mimba baada ya kujifungua.

Baadhi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa haya ya zinaa vinaweza penya kupitia plasenta na kuathiri kijusi, mengine yanaweza kusambazwa kwa mtoto wakati wa kujifungua.

Ikiwa unahisi una maambukizi ya magonjwa ya zinaa wahi kituo cha afya mara moja, ukapimwe na daktari na kupatiwa antibaotiki sahihi. Habari njema ni kuwa magonjwa haya mengi yanaweza kutibika kwa antibaotiki sahihi.

Jinsi gani uchafu unaotoka ukeni unatibiwa?

Aina ya matibabu yatategemea na nini chanzo cha uchafu. Kwa mfano maambukizi ya fangasi ukeni yanatibiwa na dawa za antifungal zinazowekwa ndani ya uke. BV inatibiwa na antibaotiki. Ugonjwa wa malengelenge sehemu za siri  unatibiwa na madawa kama “metronidazole(Flagyl) au tinidazole (Tindamax).

Vifuatavyo ni vidokezo kwa wanawake wote(wajawazito na wasio wajawaazito) vya kuzuia maambukizi ukeni ambayo yanapelekea uchafu usio kawaida ukeni:

 • Weka uke wako safi kwa kusafisha taratibu, sabuni kidogo na maji vuguvugu kwa nje. Hakuna haja ya kutumia sabuni moja kwa moja kwenye uke.
 • Epuka kuosha uke kwa kutumia sabuni zenye manukato au mbinu yoyote ile kwa sababu huongeza kujikuna. Uke wenye afya hauhitaji marashi au manukato.
 • Baada ya kutoka bafuni, siku zote jifute kuanzia mbele kurudi nyuma kuepuka bakteria kuingia ukeni na kusababisha maambukizi.
 • Ongeza mtindi katika mlo wako ili kukuza bakteia wenye afya.
 • Tumia chupi iliyotengenezwa kwa pamba au chupi ambayo haitakuchoma na badilisha chupi kila siku.
 • Usivalie nguo za kukubana kwa sababu zinafanya mwili kuwa na unyevu na kisha husababisha vidudu kusambaa kwa haraka.
 • Osha chupi kwa maji moto na sabuni kisha ukamue chupi hizo kwa maji masafi kabla ya kuanikwa.
 •  Badilisha nguo zenye unyevunyevu baada ya kuogelea au nguo za michezo baada ya mchezo bila kukawia.

Kumbuka

Ni muhimu kuwasiliana na daktari au mkunga anayesimamia ujauzito wako kama unatokwa uchafu usio wa kawaida ukeni, maana inaweza kuwa ishara ya maambukizi au tatizo kwenye ujauzito wako.

CDC (Centre for diseases control and prevention) wanashauri wajawazito wote kuchunguzwa magonjwa ya zinaa katika miadi ya kwanza ya kliniki.

Uchafu usio wa kawaida unaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa kwenye ujauzito wako. Wasiliana na mkunga anayesimamia ujauzito wako ikiwa utaona uchafu ukeni wenye rangi nyekundu inayong’aa. Inaweza kuwa ishara ya tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa au placenta previa (kondo la nyuma hujipachika katika sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi)

IMEPITIWA: MEI,2021.

Kuvimba Miguu na Vifundo cha Miguu Kipindi cha Ujauzito (Edema).

Mwili wa mjamzito unabadilika kwa kasi sana na kumfanya asijisikie vizuri na kukosa utulivu wa mwili na akili. Moja ya mabadiliko ya mwili ambayo wajawazito wengi wanapata wasiwasi nayo kipindi cha ujauzito ni ni miguu na vifundo vya miguu kuvimba. Edema inaathiri karibia robo tatu ya wanawake wajawazito. Mara nyingi inaanza wiki ya 22 mpaka 27, inaweza kubaki hata baada ya kujifungua.

Katika makala hii tutajadili kwanini miguu inavimba kipindi cha ujauzito, lini unaweza kuona hali hii, lini umuone daktari, na vidokezo rahisi vinavyoweza kukusaidia kukabiliana na hali hii.

Nini chanzo cha miguu kuvimba kwa wajawazito?

Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

Ongezeko la kasi la viwango vya homoni ya projesteroni hupunguza kasi ya umeng’enyaji wa chakula. Hii inaweza kusababisha kuvimbiwa tumboni, vilevile unaweza ona mikono, miguu au uso wako umevimba kiasi.

Ikiwa utashuhudia mikono, miguu na uso wako kuvimba sana mapema hii, haswa kama uvimbaji huu unaambatana na dalili nyingine kama kizunguzungu, kuumwa kichwa au kutoka damu, ni jambo la hekima kuwasiliana na mkunga au daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Miezi mitatu ya pili ya ujauzito

Kipindi hiki kinaanza na wiki ya 13 ya ujauzito. Ni kawaida kuanza kushuhudia miguu kuvimba kipindi hasa ikiwa una simama mda mrefu au hali ya hewa ya sehemu unayoishi ni joto.

Uvimbe huu unasababishwa na kuongezeka kwa kiasi cha damu na majimaji ndani ya mwili. Kiasi cha damu huongezeka kwa karibia asilimia 50 kipindi cha ujauzito, ukiunganisha na uhifadhi mwingi wa maji ya homoni (hormonal fluid retention).

Maji haya ya ziada yatasaidia kuandaa na kulainisha mwili wako kwaajili ya kujifungua. Punguza wasiwasi maji haya ya ziada yatapungua kwa kasi baada ya kichanga wako kuzaliwa.

Kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito

Wajawazito wengi wanapatwa na tatizo hili la miguu kuvimba kipindi hichi, kinachoanza wiki ya 28. Kadiri wiki zinavyosonga mbele na kukaribia wiki ya 40, ndivyo vidole vyako vya miguuni vitakavyozidi kuvimba.

Edema inatokea pale majimaji ya mwili yanapo ongezeka ili kuhakikisha mtoto na mama mjamzito wanaendelea kukua vizuri, majimaji haya yanachukua nafasi katika tishu na kusababisha mwili kuvimba. Ukuaji wa uterasi unasababisha mgandamizo kwenye mishipa ya nyonga na venakava (mshipa mkubwa unaopatikana upande wa kulia unaohusika na kurudisha damu moyoni kutoka miguuni), hali hii inaweza kupunguza kasi ya mzunguko wa damu kutoka kwenye miguu kurudi kwenye moyo (usiwe na wasiwasi, hali hii sio hatari-itakufanya usiwe katika hali ya utulivu tu). Matokeo yake miguu, mikono na vifundo vya miguu kuzidi huvimba.

Sababu nyingine zinachangia miguu kuvimba kipindi hichi ni pamoja na:

 • Hali ya hewa-joto.
 • Kuongezeka uzito kwa kasi.
 • Kukosa mlo kamili.
 • Unywaji wa kahawa na bidhaa zenye kafeini.
 • Kutembea kwa miguu au kusimama mda mrefu.
 • Kutokunywa maji ya kutosha.

Je, kuna hali za hatari zinazohusiana na kuvimba kwa miguu na vifundo vya miguu?

Hata hivyo ikiwa mikono au uso wako ukavimba na kudumu zaidi ya siku bila kupungua (ndani ya usiku mmoja) wasiliana na daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Kuvimba kupita kiasi kunaweza kuwa ishara ya kifafa cha mimba-huwa inaambatana na dalili nyingine kama shinikizo kubwa la damu, kuongezeka uzito kwa kasi na uwepo wa protini katika mkojo. Ikiwa shinikizo na mkojo wako vitaonekana kuwa kawaida (kila miadi unachunguza), hakuna haja ya kupata wasiwasi.

Kuvimba kwa mguu mmoja (mguu wa kulia) ni ishara ya hali inayoweza hatarisha maisha “DVT” (deep vein thrombosis)-inatokea pale damu inapoganda katika mshipa ulio ndani(deep) .Ishara nyingine ni pamoja na uzito au maumivu ya mguu yanayozidi kila ukisimama, ngozi ya mguu inakua nyekundu na moto pale unapoigusa. Ikiwa umeoona ishara hizi wasiliana na mkunga wako mara moja.

Muda mwingi, miguu kuvimba ni ishara nyingine ya kazi nzito mwili wako unafanya kukuza maisha mapya ya mtoto anayekua tumboni. Hata hivyo wakati mwingine miguu kuvimba ni ishara ya hali hatari sana. Moja ya hali hizi ni kifafa cha mimba. Hali hii huanza wakati wa ujauzito na kusababisha shinikizo kubwa la damu ambalo ni hatari.

Muone daktari ikiwa utaona ishara zifuatazo:

 • Kuvimba ghafla kwa miguu,mikono, uso na kuzunguka macho.
 • Kuvimba kupita kiasi.
 • Kizunguzungu au kushindwa kuona vizuri.
 • Maumivu makali ya kichwa
 • Kuchanganyikiwa
 • Shida katika upumuaji.
 • Ikiwa utashuhudia mguu mmoja umevimba, ukiambatana na maumivu, kubadilika rangi na kuwa wa moto.

Jinsi gani ya kukabiliana na kuvimba kwa miguu na vifundo vya miguu.

 • Weka kikomo cha ulaji wa chumvi. Moja ya njia ya kupunguza miguu kuvimba kipindi cha ujauzito ni kuweka kikomo katika ulaji wa vyakula vyenye sodiamu (chumvi). Chumvi inafanya mwili utunze maji ya ziada. Jaribu kuepuka kula vyakula vilivyohifadhiwa kwenye makopo-vina viwango vikubwa vya sodiamu. Epuka pia kuongeza chumvi kwenye chakula mezani. Tumia viungo kama majani ya “rosemary”, giligilani, tangawizi kuongeza ladha kwenye chakula chako.
 • Kunywa maji ya kutosha. Kunywa maji glasi 8 mpaka 10 kwa siku itakusaidia kuondoa sodiamu ya ziada na taka mwili nyingine.
 • Ongeza ulaji wa vyakula vyenye potasiamu. Potasiamu inasaidia mwili kufanya uwiano wa kiasi cha majimaji unayotunza. Virutubisho unavyotumia kipindi cha ujauzito vina potasiamu ya kutosha kwaajii ya mama mjamzito, lakini vilevile ni muhimu kula vyakula vyenye potasiamu ya kutosha. Baadhi ya vyakula vyenye asilia ya kuwa na patasiamu nyingi ni pamoja na: viazi mviringo na maganda yake, viazi vitamu na maganda yake,ndizi, spinachi, maharagwe, juisi za matunda (chungwa, karoti, pasheni, na komamanga), mtindi na samaki aina ya “salmon. 
 • Epuka kukaa au kusimama kwa muda mrefu. Ikiwa unafanya shughuli inayokutaka kusimama kwa muda mrefu, chukua mapumziko mara kwa mara na kaa kitako. Ikiwa unakaa sana, tumia dakika 5 kwa kila saa, kusimama na kutembea kidogo.
 • Tembea. Matembezi ya hata dakika 5 mpaka 10 kwa siku yanaweza kuboresha mzunguko wa damu na kusaidia kupunguza miguu kuvimba. Hii pia ni njia nzuri ya kufanya mazoezi wakati wa ujauzito.
 • Vaa viatu visivyokubana. Viatu vinavyokuacha huru ni muhimu katika kupunguza uvimbe wa miguu, vile vile hukinga matatizo ya mgongo na nyonga yanayoletwa na mabadiliko ya mkao (centre of gravity) na kuongezeka uzito.
 • Ogelea. Hakuna utafiti unaothibitishakuwa mgandamizo wa maji unapunguza kuvimba kwa miguu wakati wa ujauzito, lakini wanawake wengi wanapata kutulizwa wakitumia muda wao kwenye maji. Jaribu kusimama au kuogelea kwenye maji yenye kina kirefu (kama unaweza). Angalau unaweza kusikia mwepesi,mwili kupoa na pia kuupa mwili wako mazoezi. Utagundua pia miguu yako imepungua kuvimba.
 • Pata “massage”.Kwa msaada ya mwenza wako au sehemu maalum zenye kutoa huduma hii. Kukanda miguu kwa kutumia mafuta maalum inasaidia kusambaza majimaji ambayo yanajikusanya miguuni. Ikiwa unakaribia kujifungua, mweza wako ahakikishe anaepuka kusugua sehemu (acupressure points) ambazo zinahusiana na mikazo ya kujirudia ya mfuko wa uzazi (uterine contractions). Ni busara kumpata mtu aliye na ujuzi wa masaji kukusaidia.
 • Lala kwa ubavu wa kushoto. Ulalaji huu unaweza kuboresha mzunguko wa damu, ambayo inaweza kupunguza miguu kuvimba. Kulala kwa ubavu wa kushoto kuna ondoa mgandamizo wa uterasi kwenye mshipa mkubwa wa damu unaorudisha damu kwenye moyo kutoka miguuni.
 • Weka miguu yako juu. Kama inawezekana kila unapokaa kitako hakikisha miguu imeinuliwa juu, unaweza kutumia kiti kingine, kigoda au ndoo kama egemeo.
 • Epuka soksi au taiti zinazobana. Lengo lako ni kuhakikisha dam una majimaji yanasafiri kwa urahisi (soksi zinazoacha alama ya kubanwa kwenye mguu ni ishara kuwa zinabana).
 • Punguza matumizi ya kafeini. Unywaji sana wa kahawa unachukuliwa kama hatari kubwa kwa mtoto. Inaweza pia kusababisha mguu na vifundo vya miguu kuvimba zaidi. Jaribu chai yenye majani ya mitishamba kama mnana, mchaichai, n.k.
 • Vaa nguo zisizobana. Nguo zinazobana hasa kwenye viwiko, kiuno na vifundo vya miguu inaweza kufanya uvimbe kuongezeka zaidi. Kimsingi, inafanya damu isisambae kwa urahisi. Jaribu kuvaa mavasi yanayoachia mwili- madera na magauni mapana yanayoachia mwili huru, suruali pana zisizobana kwenye kiuno na miguuni ikiwa unaishi eneo lenye baridi.

Kumbuka

Miguu kuvimba ni hali ya kawaida sana kipindi cha ujauzito. Uvimbe huu unasabishwa na ongezeko la kiasi cha maji kwenye mwili, vilevile upungufu wa usambazaji wa maji maji haya.

Ikiwa unapata uvimbe wa miguu uliopitiliza ghafla, ni muhimu kuwasiliana na daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako, kwasababu inaweza kuwa ishara ya tatizo lingine kubwa. Lakini miguu kuvimba kidogo ni kawaida.

Unaweza kuepuka kuvimba miguu kila mara kwa kufanya mzoezi mepesi kwa mjamzito kila mara kama vile kutembea, kunywa maji ya kutosha, pumzika na kula mlo kamili.

IMEPITIWA: MEI,2021.