Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kiungulia Wakati wa Ujauzito.

Kipindi cha ujauzito mabadiliko mbalimbali hutokea katika mwili wa mjamzito ili kuruhusu ukuaji na maendeleo ya mtoto aliye tumboni, mabadiliko haya vilevile ni maandalizi ya mtoto kuzaliwa. Kiungulia ni miongoni mwa matatizo yanayowapata wanawake wengi wanapobeba mimba, tatizo hili huwapata wajawazito mara nyingi katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito na kwa wengine miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.

Kiungulia hutokea wakati kiwambo (valvu) kilichopo kati ya tumbo na koromeo la chakula (esophagus) kinapolegea na kushindwa kuzuia tindikali (acid) ya tumbo isipenye na kurudi katika koromeo la chakula na kusababisha maumivu makali kifuani. Ujauzito huongeza nafasi ya mama kupata kiungulia kwasababu homoni ya projesteroni hulegeza kiwambo hicho na kusababisha tindikali (acid) inayozalishwa tumboni hasa baada ya kula kurejea katika koromeo la chakula na kusababisha kiungulia.

Je, Kiungulia Kinasababishwa na Nini Wakati wa Ujauzito?

Ili kuelewa njia na mbinu za kuzuia kiungulia kisitokee ni vizuri kufahamu kiungulia kinasababishwa na ni nini wakati wa ujauzito.

Mabadiliko ya homoni

Wakati wa ujauzito kiwango cha homoni ya projesteroni huongezeka zaidi ili kuhakikisha mtoto tumboni anakua vizuri, lakini pia homoni hii inafanya misuli ilegee. Hali hii inaweza kupelekea misuli ya koo la juu kulegea zaidi na kuruhusu tindikali inayozalishwa tumboni kurudi kwenye koromeo la chakula na kusababisha maumivu makali kifuani.

Ukuaji wa mtoto tumboni/ Kuongezeka ukubwa tumbo la uzazi

Katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito kiungulia hutokea kwasababu ya ukubwa wa mfuko wa uzazi unaosababisha kubana utumbo mdogo na tumbo. Kadiri mtoto anavyoendelea kukua tumboni ndivyo mfuko wa uzazi unavyokua mkubwa na kusababisha kuongezeka kwa mkandamizo tumboni. Mbano huu hupeleka vilivyoko tumboni kusukumwa upande wa koromeo la chakula.

Baadhi ya mambo na hali zinazochangia kiungulia kutokea wakati wa ujauzito ni pamoja na:

 • Kula chakula kingi na kunywa maji mengi wakati wa kula
 • Ulaji wa vyakula vyenye mafuta, pilipili na viungo vingi
 • Ulaji wa chakula kingi wakati mmoja
 • Kula chakula masaa machache kabla ya kwenda kulala
 • Kuvaa mavazi yakubana wakati wa ujauzito inaweza kuchangia kiungulia kutokea
 • Matumizi ya kahawa au vinywaji vyenye kahawa
 • Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito
 • Uvutaji sigara wakati wa ujauzito.

Ishara na Dalili za Kiungulia Wakati wa Ujauzito.

Kawaida dalili zinatokea baada ya kula au kunywa, vilevile unaweza kupata dalili hizi wakati wowote kipindi cha ujauzito lakini mara nyingi zinatokea sana wiki ya 27 ya ujauzito na kuendelea. Miongoni mwa dalili hizo ni pamoja na:

 • Kujisikia kuungua, kuchoma au maumivu kifuani kutokana na tindikali za tumboni kurudi kwenye umio (esophagus)
 • Tumbo kujaa gesi
 • Uchachu mdomoni
 • Kujisikia kuumwa
 • Kubeua mara kwa mara
 • Kukohoa mara kwa mara
 • Kupata malengelenge kwenye mdomo
 • Kujisikia kutapika.

Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kufanya Nyumbani ili Kupunguza Kiungulia Wakati wa Ujauzito

 • Kuwa makini na chakula unachokula. Hakikisha unaepuka vyakula vyenye tindikali na pilipili kama vile nyanya, vitunguu maji, vitunguu swaumu, kahawa, soda, chokoleti. Kaa mbali na vyakula vyenye mafuta mengi na viungo vingi, aina hii ya vyakula vinachelewesha umeng’enyaji wa chakula tumboni.
 • Kula milo midogo midogo badala ya milo mikubwa mitatu ya kawaida. Hii inasaidia kuepuka tumbo kujaa sana
 • Kaa wima kila unapokula, inasaidia chakula kutulia tumboni.
 • Hakikisha usile mlo mkubwa (mfano:chakula cha usiku) masaa matatu kabla ya kwenda kulala. Unaweza kula mlo mwepesi ambao utalifanya tumbo lako kuwa tupu na kuepusha kiungulia.
 • Usivute sigara na kunywa pombe wakati wa ujauzito. Kemikali zinazopatikana katika sigara na pombe zinasababisha kiwambo (valvu) kulegea, valvu hii inafanya chakula chote kilicho tumboni kutulia, lakini mara baada ya kulegea chakula ambacho hakijameng’enywa na tindikali inayopatikana tumboni zinapata uhuru wa kurudi kwenye koromro la chakula na kusababisha kiungulia.
 • Vaa nguo zisizobana wakati wa ujauzito. Nguo za kubana huongeza mkandamizo tumboni hivyo kuwa rahisi kwa tindikali za tumboni kurudi kwenye koromeo la chakula (oesophagus).
 • Unapoenda kulala hakikisha sehemu za juu za mwili zimeinuliwa juu kidogo kwa kuweka mto.
 • Kunywa maji dakika 30 baada ya kumaliza kula siyo katikati ya mlo.
 • Ongea na daktari au mkunga wako juu ya dawa sahihi kwaajili ya kiungulia. Hali ikiwa mbaya hakikisha unaenda hospitali, kulingana na hali yako ya ujauzito daktari atapendekeza dawa sahihi za kutumia. Usitumie dawa bila kupata ushauri wa daktari maana zinaweza kukudhuru wewe na mtoto tumboni.
 • Unapohisi kiungulia kunywa glasi ya maziwa au kunywa maji moto yaliyowekwa kijiko kimoja cha asali.
 • Mjamzito alale kwa ubavu wa kushoto, tafiti zinaonyesha kulala kwa ubavu wa kulia kunasababisha kiungulia kwasababu ni rahisi tindikali za tumboni kurudi kooni.
 • Kula papai au nanasi mara kwa mara kwa sababu matunda haya yana enzaimu (kemikali maalum) zinazosaidia tumbo kumeng’enya chakula.

IMEPITIWA: NOVEMBA, 2021.

Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito.

Ikiwa wewe ni mjamzito na unapata maumivu ya kichwa mara kwa mara, hauko pekee yako. Ripoti moja ya matibabu iliyotathiminiwa ilionyesha asilimia 39 ya wanawake wajawazito na waliotoka kujifungua hupata maumivu ya kichwa.

Ijapokuwa kipindi cha ujauzito utakuwa na maumivu ya kichwa tofauti na yale uliyozoea, ikumbukwe maumivu haya wakati wa ujauzito hayana madhara.

Maumivu ya kichwa wakati wa kipindi cha kwanza cha ujauizto yanaweza kutokea kwa sababu tofauti ukilinganisha na maumivu katika kipidni cha pili cha ujauzito. Kwa baadhi ya kesi, maumivu ya kichwa yanaweza kuwa ishara ya matatizo mengine ya kiafya wakati wa ujauzito.

Mwambie daktari au mkunga wako kuhusu maumivu haya ya kichwa kabla,wakati na baada ya ujauzito. Ni busara pia kuweka kumbukumbu ya mara ngapi unapata maumivu haya na kwa kiasi gani maumivu yanakuwa makali. Kwa kuongezea, weka kumbukumbu ya aina ya dalili nyingine unazopita.

Aina za Maumivu ya Kichwa.

Maumivu mengi ya kichwa yanayowapata wajawazito hutokea yenyewe. Hii sio dalili au ishara ya tatizo au hitilafu nyingine katika ujauzito. Haina budi kujifunza baadhi ya aina kuu za maumivu haya ya kichwa ili kukusaidia kujua aina gani ya maumivu ya kichwa inakutokea, aina hizo ni pamoja na:

Maumivu ya kichwa ya kuvuta “tension headache”. Ikiwa una msongo wa mawazo, njaa au maumivu ya shingo au mabega unaweza kupata aina hii ya maumivu ya kichwa. Ni moja ya aina kuu ya maumivu ya kichwa.

Maumivu ya kichwa kama kinagongwa gongwa “migraine attacks”. Aina hii ya maumivu unaweza pitia maumivu wastani na kuwa makali yanayogonga gonga na kudumu kwa masaa au hata siku. Wanawake wenye aina hii ya maumivu hupitia dalili kama kushindwa kuona vizuri, kufa ganzi na kichefuchefu.

“Sinus headache”. Mkandamizo kuzunguka macho, mashavu na kichwa pamoja na kubanwa mafua ni ishara za aina hii ya maumivu ya kichwa. Aina hii huchanganywa na “migraines”, maumivu haya huongezeka kila unapoinama au kulala.

“Cluster headache”. Unaweza kusikia kama maumivu juu ya maumivu yanayoanza haraka na kuwa makali sana yanayodumu kwa siku au zaidi. Maumivu haya yanajikita katika jicho moja au kuathiri upande mmoja wa kichwa. Habari njema ni kwamba, aina hii ya maumivu huwapata wanaume sana kuliko wanawake, hivyo ni nadra sana kuwapata wanawake.

Maumivu ya kichwa ya kudumu “chronic headaches”. Ikiwa unapata maumivu ya kichwa zaidi ya siku 15 ndani ya mwezi, maumivu haya yanaweza kuchukuliwa kama ya kudumu.

Je, Dalili na Ishara za Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito ni Zipi?

Maumivu ya kichwa yanatofautiana kutoka kwa mtu mmojaa na mwingine. Unaweza kupata dalili kama:

 • Maumivu kidogo/yasiyo makali
 • Kichwa kugonga gonga au maumivu ya kubana na kuachia kwa nguvu katika kichwa
 • Maumivu makali upande mmoja au pande zote mbili za kichwa
 • Maumivu ya makali nyuma ya jicho moja au yote
 • Kichefuchefu
 • Kutapika
 • Kushindwa kuona vizuri

Kwa baadhi ya wanawake wanapata shida wakiwa katika mwanga na sauti kubwa “light and sound sensitivity” wanapopata maumivu ya kichwa aina ya “migraine”. Maumivu yanakuwa makali zaidi wakisogea sehemu moja kwenda nyingine.

Nini Chanzo cha Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito?

Vichocheo (homoni) ni sababu kuu ya maumivu ya kichwa, japo zipo sababu nyingine nyingi za maumivu ya kichwa kila hatua ya ujauzito.

Kipindi cha kwanza cha ujauzito (first trimester)

Maumivu ya kichwa ya kuvuta hutokea sana kipindi hichi. Hii hutokea kwasababu mwili wa mjamzito unapitia mabadiliko mbalimbali. Mabadiliko yafuatayo yanapelekea maumivu ya kichwa:

 • Mabadiliko ya homoni
 • Kiwango kikubwa cha damu
 • Mabadiliko ya uzito wa mwili

Vilevile maumivu ya kichwa kipindi hichi yanasababishwa na: ukosefu wa maji ya kutosha mwilini, kichefuchefu na kutapika, msongo wa mawazo, ukosefu wa usingizi, kuacha kutumia kahawa, lishe duni, viwango vidogo vya damu, kiasi kidogo cha mazoezi au kazi za mwili na unyeti wa mwanga na sauti (sound and light sensitivity).

Vipo baadhi ya vyakula vinasababisha maumivu ya kichwa. Vyakula hivi vinabadilika kipindi cha ujauzito, baadhi ya vyakula hivi vinavyoweza kusababisha maumivu ya kichwa kwa baadhi ya watu ni pamoja na:

 • Maziwa
 • Chokoleti
 • Jibini
 • Mikate iliyotengenezwa na hamira
 • Nyanya
 • Nyama iliyosindikwa
 • Pombe
 • Karanga

Kipindi cha pili na cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito (second and third trimester)

Maumivu ya kichwa katika vipindi hivi yanaweza sababishwa na:

 • Uzito ziada wa mwili
 • Mkao (jinsi mjamzito anavyobeba mwili wake)
 • Kiasi kidogo cha usingizi
 • Mlo
 • Misuli kukaza na kubana
 • Shinikizo kubwa la damu: baada ya wiki ya 20 ya ujauzito, maumivu makali ya kichwa yanahusishwa na shinikizo kubwa la damu. Hali hii inaongeza nafasi ya kupata baadhi ya matatizo katika ujauzito wako kama vile kujifungua kabla ya wiki 37 ya ujauzito, kifafa cha mimba (pre-elampsia,eclampsia), tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto hajazaliwa, kiasi kidogo cha oksijeni inayoenda kwa mtoto, mtoto kuzaliwa na uzito duni na kiharusi
 • Kisukari

Sababu nyingine za maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito ni pamoja na maambukizi ya kawaida na magonjwa makubwa zaidi kama vile:

 • Kuvimba kwa mizizi ya hewa kwenye mifupa karibu na pua na macho “sinus infection”
 • Shinikizo dogo la damu
 • Tatizo la “blood clot” linalosababishwa na unene, kukaa mda mrefu, ujauzito, kuvuta sigara, njia za uzazi wa mpango n.k. “Blood clot” inatokea pale damu inapobadilika kutoka hali ya ukimiminika na kuwa katika hali yabisi (bonge la damu).
 • Kutoka damu
 • Ugonjwa wa selimundu (sickle cell anemia)
 • Tatizo la uvimbe kwenye ubongo (brain tumor)
 • Uvimbe (aneurysm)
 • Kiharusi
 • Matatizo ya moyo
 • Ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo.

Matibabu ya Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito.

Wakati wa ujauzito, inasahuriwa kutuliza maumivu haya kwa kutumia njia za asili kama inawezekana, ingawa mkunga au daktari wako anaweza kukushauri dawa sahihi kutumia. Ongea na daktari kabla ya kutumia dawa zako za kutuliza maumivu wakati wa ujauzito. Usitumie asprin na ibuprofen (Advil, motrin,mitishamba), Acetaminophen (tylenol) inaweza kutumika kuleta unafuu na pia inaaminika kuwa salama kwa ujauzito.

CDC (Centre for Disease Control and Prevention) wameonya kuwa matumizi ya dawa za kupunguza maumivu zinaweza kuwa na madhara kwa mtoto anayekua, haswa kama zitatumika kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya ujauzito. Daktari anaweza kukushauri njia mbadala za matibabu ya kutibu maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito na dawa za asili za maumivu ya kichwa kama vile:

 • Kunywa maji na vimiminika vya kutosha
 • Ikiwa una maumivu yaliyosababishwa na “sinus infection” tumia taulo/kitambaa cha moto kukanda kuzunguka eneo la macho na pua.
 • Kama maumivu yako ya kichwa ni yakuvuta, chukua barafu zifunge kwenye kitambaa au taulo kisha weka kwenye shingo yako
 • Pumzika kwenye chumba kilicho na mwanga hafifu (giza) kisha jaribu kuvuta pumzi ndani na kuachia kuondoa msongo mwilini.
 • Oga kwa maji ya moto
 • Tafuta mkao mzuri wa kubeba mwili wako haswa kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito
 • Pumzika vya kutosha
 • Fanya zoezi la kutembea kisha kunywa maji ya kutosha
 • Pata masaji
 • Fanya mazoezi na kujinyoosha mara kwa mara.

Tafuta huduma ya haraka ikiwa una dalili zifuatazo:

 • Homa
 • Kichefuchefu na kutapika
 • Kushindwa kuona vizuri
 • Maumivu makali
 • Maumivu ya kichwa yanayodumu zaidi ya masaa kadhaa
 • Maumivu ya kila mara ya kichwa
 • Kuzimia
 • Mshtuko wa moyo
 • Maumivu ya kichwa yanayoambatana na kuongezeka uzito ghafla, maumivu upande wa kulia juu ya fumbatio na kuvimba mikono na uso.

Daktari anaweza kukushauri kufanya vipimo na uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha maumivu ya kichwa. Vipimo hivi ni pamaoja na;

 • Shinikizo la damu
 • Kipimo cha damu
 • Kipimo cha kiwango cha sukari katika damu
 • Kipimo cha kuona
 • Ultrasound ya kichwa na shingo
 • Kipimo cha uchunguzi wa moyo na kichwa
 • Afya ya jicho kwa kutumia hadubini

Je, Ninaweza Kuzuia Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito?

Ijapokuwa baadhi ya maumivu ya kichwa hayaepukiki, vidokezo sahihi na hatua chache zinaweza kuchukuliwa ili kuzuia kutokea hapo baadae. Baadhi ya vidokezo hivyo ni pamoja na:

 • Kula mara kwa mara. Kuruka milo kunapelekea kiwango kidogo cha sukari katika damu ambacho kinasababisha maumivu ya kichwa. Hakikisha unakula chakula kwa muda sahihi, ikiwezekana beba matunda au vitafunio vyenye afya kila uendapo ili kuufanya mwili upate virutubisho sahihi kwa wakati sahihi.
 • Lala vizuri. Pata mapumziko ya kutosha ni muhimu katika kipindi cha kwanza na cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito, lakini kumbuka usilale sana maana kufanya hivyo kutafanya kichwa kuuma.
 • Punguza matumizi ya kahawa
 • Pata hewa ya kutosha. Epuka maeneo yaliyo na joto sana, msongamano, harufu nzito. Ukiwa ndani kumbuka kufungua dirisha ili hewa safi ipenye ndani. Angalau mara chache pata hewa safi nje kwa kutembea jioni au asubuhi.
 • Tafuta eneo lenye amani na utulivu. Makelele yanapelekea maumivu ya kichwa, eneo tulivu linaweza kusaidia kuepuka maumivu ya kichwa sasa n ahata baadae.
 • Hakikisha mwili wako unadumu katika mkao ambao ni salama kwako. Jaribu kutojikunja au kuinama unapotembea au kukaa kazini.
 • Jaribu kufanya yoga, mazoezi ya kupumua kwa kuvuta pumzi ya nguvu kwa ndani na kuachia taratibu.

KUMBUKA

Maumivu ya kichwa ni kawaida wakati wa ujauzito. Unaweza ukapata maumivu ya kuvuta ya kichwa katika kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya ujauzito. Hali hii inaweza kutokea kwasababu ya mabadiliko yanayopitiwa na mwili kwa kipindi cha mda mfupi.

Maumivu haya ya kichwa yanaweza kutokea katika kipindi cha pili na cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito kwasababu nyinginezo. Baadhi ya sababu zinazosababisha maumivu ya kichwa katika kipindi cha katikati na mwisho wa ujauzito zinaweza kuwa kubwa na hatari kwa afya.

Shinikizo kubwa la damu ni sababu kubwa hatari ya maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito. Wakati wowote katika ujauzito wako unaweza kupata tatizo hili. Unaweza usiwe na dalili zozote zile. Angalia shinikizo lako la damu angalau mara moja kwa siku ukiwa nyumbani kwa kutumia kifaa maaalum.

Mtaarifu daktari katika miadi yako ya kliniki ikiwa unapata maumivu haya mara kwa mara. Mjulishe daktari mara moja ikiwa kuna historia katika familia yenu ya watu kusumbuliwa na shinikizo kubwa la damu, kisukari, maumivu makali ya kichwa aumshtuko wa moyo.

Tumia dawa na matibabu kama ulivyoelekezwa na daktari wako. Fuata mlo mzuri na mazoezi salama kwa hali yako. Muone daktari kwaajili ya uchunguzi au ufuatiliaji wa matibabu kila unapopaswa kwenda. Sababu za maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito zinatibika au kuzuilika kwa kuzingatia huduma sahihi.

IMEPITIWA: OKTOBA, 2021.

Tatizo la Kondo la Nyuma (Placenta) Kuachia Kabla ya Mtoto Kuzaliwa (Placenta Abruption)

Tatizo hili linaweza kutokea ghafla wakati wa ujauzito. Inaweza kuwa hatari kwako na mtoto wako hivyo msaada wa haraka unahitajika. Kwa bahati nzuri sio tatizo linalowapata wajawazito wote.

Kondo la nyuma (placenta) inakua ndani ya mfuko wa uzazi ukiwa mjamzito. Kiungo hiki kinatumika kumlisha mtoto akiwa tumboni kwa mama yake kwa kutuma chakula virutubisho na hewa ya oksijeni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na kutoa taka mwili zinazojijenga katika damu ya mtoto. Kondo la nyuma limejishikilia kwenye ukuta wa uterasi na mtoto wako amejishikilia kwenye kondo la nyuma kwa kutumia kiunga mwana (umbilical cord). Katika hali ya kawaida, kondo la nyuma hujitenga na ukuta wa mfuko wa uzazi mara baada ya mtoto kuzaliwa. Ukipata tatizo hili, kondo la nyuma hujitenga na ukuta wa mfuko wa uzazi kabla hata mtoto kuzaliwa (placenta abruption), ambapo husababisha mama kupoteza damu nyingi, kufariki kwa mtoto na hata mama mwenyewe.

Dalili na Ishara za Kondo la Nyuma Kuachia Kabla Mtoto Kuzaliwa (Placenta Abruption).

Tatizo hili linaathiri takribani asilimia moja ya wajawazito. Linatokea mda wowote baada ya wiki 20 za ujauzito, lakini pia linatokea sana katika kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito (third trimester).

Tatizo hili hutokea ghafla unaweza kuona damu ikitoka ukeni. Kiasi cha damu inayotoka ukeni kinatofautiana. Wakati mwingine kiasi kidogo cha damu hutoka ukeni kwasababu damu hunaswa ndani ya mfuko wa uzazi. Hivyo usidharau tatizo kwasababu kiasi cha damu kilichotoka ni kidogo, pata msaada wa haraka ikiwa dalili hiyo ya damu kutoka ukeni imeambatana na dalili hizi nyingine:

 • Maumivu katika tumbo au mgongo
 • Mibano na mikazo ya haraka au taratibu katika mfuko wa uzazi
 • Matatizo katika mapigo ya moyo ya mtoto

Tatizo la kuachia kondo la nyuma linaweza kutokea kidogo kidogo “chronic abruption”. Unaweza shuhudia:

 • Damu nyepesi kutoka na kuacha ukeni
 • Kiwango kidogo cha “amniotic fluid”
 • Mtoto aliye tumboni hakui haraka kama anavotakiwa.

Tatizo Hili la Kuachia Kondo la Nyuma Linasababishwa na Nini?

Wakati mwingi, madktari hawajui chanzo. Lakini unywaji wa pombe au matumizi ya madawa ya kulevya ukiwa mjamzito inaweza kuongeza hatari ya kupata tatizo hili. Vitu vingine vinavyochangia ni pamoja na:

 • Ulipata tatizo hili katika mimba zilizopita. Kama tatizo hili lilishawahi kukupata hapo awali una nafasi ya takribani asilimia kumi tatizo hili kutokea tena katika ujauzito wa sasa.
 • Uvutaji sigara. Utafiti mmoja ulionyesha wanawake waliokuwa wanavuta sigara kabla ya kushika ujauzito waliongeza nafasi ya kupata tatizo la kondo la nyuma kuachia kwa asilimia 40 kila mwaka waliovuta sigara.
 • Matumizi ya kokeni au madawa mengine ya kulevya. Tatizo hili linatokea kwa asilimia 10 ya wanawake wanaotumia madawa haya katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito (third trimester).
 • Shinikizo kubwa la damu kabla na baada ya kupata ujauzito, hakikisha mnalitafutia ufumbuzi tatizo hili wewe na mkunga wako ili liweze kudhibitiwa. Takribani ya nusu ya vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na tatizo hili vinasababishwa na shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito.
 • Matatizo ya kifuko cha maji yanayopatikana katika mfuko wa uzazi. Kifuko hichi cha maji kinatumika kumlinda mtoto ndani ya mfuko wa uzazi. Ikiwa kitu chochote kitapasua au kusababisha kuvuja kabla hujawa tayari kujifungua, nafasi ya kupata tatizo la kondo la nyuma kuachia inaongezeka.
 • Kushika ujauzito ukiwa na umri mkubwa. Nafasi ya kupata tatizo hili huongezeka kama una umri wa miaka 35 au zaidi. Mara nyingi kama mama ana umri zaidi ya mika 40.
 • Ukishika ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja. Wakati mwingine kujifungua mtoto wa kwanza kunafanya plasenta ijiachie kabla mtoto mwingine hajawa tayari kuzaliwa.
 • Kuumia eneo la tumbo. Inaweza kutokea kama ulidondoka au kupata kipigo kikali tumboni. Inaweza kutokea kama ulihusika katika ajali ya gari, kumbuka kufunga mkanda wa gari kila mara.

Haiwezekani kuzuia tatizo la kondo la nyuma kuachia, lakini kuna vitu unaweza kuepuka kama vile tumbaku, pombe na madawa ya kulevya ili kupunguza nafasi ya kupata tatizo hili.

Mwambie mkunga au daktari wako anayesiamamia maendeleo ya ujauzito wako ikiwa ulipata tatizo hili katika mimba zako za awali. Watakuangalia kwa ukaribu zaidi. Watakushauri njia unazoweza kujikinga ili lisitoke tena.

Vipimo na Uchunguzi wa Tatizo la Kondo la Nyuma Kuachia.

Ikiwa unatoka damu ukeni au maumivu ya tumbo unahitaji kumuona daktari mara moja. Watakufanyia kipimo cha mwili na vipimo vya damu, pia watakufanya kipimo cha ultrasound kuona ndani ya mfuko wa uzazi (kipimo cha ultrasound hakionyeshi tatizo la kondo la nyuma kuachia).

Matibabu ya Tatizo la Kondo la Nyuma Kuachia.

Kondo la nyuma haliwezi kujifunga tena kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi, chaguo la matibabu linategemea na umri wa ujauzito wako, ukubwa wa tatizo na hali ya mama na mtoto.

Ikiwa una ujauzito chini ya wiki 34, utalazwa hospitali kwaajili ya kuangaliwa kwa ukaribu kama mapigo ya moyo ya mtoto ni kawaida na tatizo la kuachia kondo la nyuma sio kubwa. Ikiwa mtoto wako ataonekana kuendelea vizuri na damu ikacha kutoka unaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Ikiwa una ujauzito wa zaidi ya wiki 34, unaweza kujifungua kwa njia ya kawaida kama tatizo sio kubwa sana. Kama tatizo ni kubwa na limehatarisha afya yako na mtoto, upasuaji utahitajika kufanyika haraka. Pia unaweza kuhitaji kuongezewa damu.

Matatizo Yanayosababishwa na Tatizo la Kondo la Nyuma Kuachia.

Ikiwa sehemu ndogo ya kondo la nyuma itaachia, inaweza isisababishe matatizo mengi. Lakini kama sehemu kubwa au yote imeachia inaweza kusababisha athari kubwa kwako na mtoto wako. Kwa mjamzito inaweza kusababisha:

 • Kupoteza damu nyingi inayoweza kusababisha mshtuko au kuhitaji kuongezewa damu
 • Matatizo ya damu kuganda
 • Figo au ogani nyingine kushindwa kufanya kazi
 • Kifo- mama au mtoto.

Kwa mtoto matatizo yanayoweza kumpata ni kama:

 • Mtoto kuzaliwa kabla ya mda (kabla ya wiki ya 37).
 • Matatizo katika ukuaji wake. Watoto njiti wanaozaliwa kwasababu ya tatizo hili wanapatwa na matatizo mengi ya kiafya mwanzo na mwisho katika maisha yao.
 • Mtoto kufariki akiwa tumboni baada ya angalau wiki ya 20 ya ujauzito.

IMEPITIWA: OKTOBA,2021.

Tatizo la Kukosa Choo Kipindi cha Ujauzito

Tumbo kujaa gesi, kuvimbiwa, hali ya kujisikia umebanwa na haja kubwa ni malalamiko ya kawaida kipindi cha ujauzito.

Tatizo la kukosa choo ni hali isiyopendeza, kwa bahati mbaya ni hali ya kawaida sana wakati wa ujauzito- baadhi ya ripoti zinasema karibia asilimia 40 ya wanawake wanapitia hali hii. Kadiri tumbo linavyozidi kukua ndivyo mkandamizo wa mfuko wa mimba unavyoongezeka katika eneo la haja kubwa na kuzidisha tatizo hili.

Lini tatizo la kukosa choo linaanza wakati wa ujauzito?

Tatizo la kukosa choo linaanza mapema kadiri viwango vya projesteroni vinavyoongezeka, karibu na mwezi wa pili hadi wa tatu wa ujauzito. Inaweza kuwa mbaya zaidi wakati ujauzito unavyoendelea na uterasi yako inavyokua.

Ni moja ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwasumbua wajawazito wengi hasa katika miezi ya awali ya ujauzito na miezi ya mwisho ya ujauzito.

Nini chanzo cha tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito, nazo ni pamoja na:

Viwango vya homoni ya projesteroni: homoni hii huzalishwa kwa wingi wakati wa ujauzito,homoni hii hujulikana kulegeza misuli ya tumbo la chakula hivyo kusababisha chakula kupita taratibu katika utumbo. Mabaki ya chakula hukaa kwa muda mrefu tumboni bila ya kutolewa nje kama taka,kadiri mabaki hayo yanavyo zidi kubaki tumboni ndivyo maji yaliyo katika mabaki hayo huendelea kufyonzwa na utumbo hivyo kusababisha kukosa choo kwa muda na vilevile kupata choo kigumu.

Matumizi ya vidonge vya kuongeza madini ya chuma mwilini: ijapokuwa madini ya chuma ni muhimu wakati wa ujauzito kwa ukuaji wa mtoto, kukosa choo kwa mjamzito inaweza kuwa athari ya kutumia sana vidonge hivi. Ni vema kuongea na mkunga wako kuhusu jambo hili, anaweza kukushauri kubadilisha vidonge hivi, dozi yake au mara ngapi uvitumie. Hakikisha unafuata maelekezo kwasababu ukosefu wa damu ya kutosha (anemia) hutokea sana wakati wa ujauzito na inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa mama na mtoto.

Ukosefu wa maji ya kutosha mwilini: wakati wa ujauzito mama anakabiliwa na tatizo la upungufu wa maji mwilini, kwasababu mwili unatumia maji zaidi kusaidia kutengeneza plasenta na “amniotic sac” (kifuko cha amnion-mfuko wa maji yanayomlinda mtoto na hupasuka kabla mtoto hajazaliwa. Ikiwa utakuwa na upungufu wa maji mwilini, mwili wako utashindwa kufanya kazi muhimu na kupelekea kupata shida kubwa sana za kiafya.

Msongo wa mawazo: ujauzito unaweza kuleta msongo wwa mawazo hasa unapokaribia siku ya kujifungua. Epuka kuwa na wasiwasi sana, hali hii inaweza kuathiri mfumo wa umeng’enyaji wa chakula na utoaji taka (kukosa choo).

Ukuaji wa tumbo la uzazi: kuongezeka kwa ukubwa wa tumbo la uzazi hutokea zaidi katika miezi ya mwisho ya ujauzito,ukubwa wa tumbo la uzazi kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa mtoto tumboni husababisha mkandamizo mkubwa kwenye tumbo la chakula,hivyo kupunguza kasi ya usafirishwaji wa mabaki ya chakula nje ya tumbo,hivyo kusababisha mwili kufyonza maji katika mabaki hayo na kuleta choo kigumu.

Mwili kutofanyishwa kazi na mazoezi: kadiri tumbo linavyozidi kuwa kubwa, inakuwa ngumu kwa mama kuwa imara katika ufanyaji kazi na mazoezi. Ufanyaji wa mazoezi huchochea misuli ya tumbo kufanya kazi yake ya kutoa taka nje ya mwili, mjamzito anavyo kuwa hafanyi mazoezi misuli ya tumbo nayo hushindwa kufanya kazi yake vizuri na kusababisha mama kukosa choo.

Wakati mwingine kukosa choo kunasababishwa na ulaji wa bidhaa za maziwa sana (dairy products), dawa mpya unayotumia au ulaji mdogo wa vyakula vyenye nyuzi nyuzi (fibre) kama matunda na mboga mboga za majani. Fiber hupatikana katika vyakula vya mimea: mboga, matunda, mboga, nafaka, karanga.

Baadhi ya vyakula unavyotakiwa kuacha ikiwa unasumbuliwa na tatizo la kukosa choo ni pamoja na ndizi, vyakula vya kukaangwa, viazi vya kukaanga, nyama nyekundu, mkate mweupe, wali mweupe, pasta na vyakula vya maziwa kama jibini.

Je, nini unapaswa kufanya ukipata tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Hakuna haja ya kuteseka miezi yote tisa kwa tatizo hili. Zipo mbinu nyingi zitakazo kusaidia kupambana na tatizo la kukosa choo, nazo ni pamoja na:

 • Kula vyakula vyenye nyuzi nyuzi kwa wingi, vyakula hivi vinasaidia kutoa mabaki ya chakula kwenye utumbo kwa urahisi zaidi. Hakikisha unakula nafaka zisizokobolewa, vyakula jamii ya kunde, matunda safi na mboga za kijani za majani (mboga mbichi au iliyopikwa kidogo).
 • Kunywa maji ya kutosha. Maji mengi yatakusaidia kutoa mabaki ya chakula nje ya mwili kwa haraka zaidi. Hakikisha unakunywa angalau glasi 8 za maji kwa siku. Maji yanaweza kusaidia tatizo la kukosa choo lililosababishwa na matumizi ya vidonge vya madini chuma. Ikiwa unaishi eneo lenye hali ya hewa ya joto, kunywa zaidi maji (zaidi ya glasi 8)
 • Fanya mazoezi. Kutembea, kuogelea na yoga ni mazoezi mazuri kwa mwili wa mwanamke mwenye ujauzito. Mwili unapofanyishwa mazoezi unasaidia utembeaji wa mabaki ya chakula kuelekea nje ya mwili.
 • Oga kwa maji ya moto. Maji ya moto yanasaidia kupumzisha misuli na kuhamasisha taka kutoka nje ya mwili. Kama una bafu la kulala (bathtub) jiloweke kwa lisaa moja au zaidi.
 • Kunywa maji yenye limao. Chukua juisi ya limao nusu, changanya kwenye glasi ya maji, kisha kunywa kabla ya kwenda kulala. Maji yatasaidia kulainisha kinyesi, limao lina kiwango kikubwa cha asidi kitakachosaidia kusafirisha kinyesi.
 • Kula vyakula vyenye magnesiamu ya kutosha. Magnesiamu yanasaidia kuelekeza maji kwenye utumbo na kusaidia kinyesi kulainika na kusafirishwa nje kwa urahisi. Hakikisha unapata miligramu 350 kwa siku kwa kula vyakula kama samaki, spinachi, karanga na chokoleti nyeusi.
 • Epuka nafaka zilizokobolewa kila unapoweza, nafaka hizi zinachangia kukosa choo. Kwa mfano badala ya kula mkate mweupe, kula mkate wa kahawia (broen bread).
 • Jaribu kula milo sita midogo midogo kwa siku badala ya milo mitatu mikubwa, kwa kufanya hivi unaweza kuepuka kuvimbiwa na tumbo kujaa gesi.
 • Jisaidie haja kubwa kila unapoisikia, kubana haja kubwa mara kwa mara kunafanya misuli ya kuzuia utokaji wa kinyesi kuwa hafifu na kusababisha tatizo la kukosa choo.
 • Zingatia virutubisho na dawa zako. Jambo la kushangaza ni kwamba, virutubisho na dawa nyingi ambazo hufanya mwili wa mjamzito kuwa na afya kwa mfano; vitamini za kutumia kabla ya kuzaa, virutubisho vya kalsiamu na chuma zinaweza kuzidisha tatizo la kukosa choo. Kwa hivyo jadiliana na daktari wako kuhusu njia mbadala au marekebisho ya dozi za virutubisho hivi hadi hali itakapoboreka. Muulize pia daktari wako juu ya kutumia zaidi virutubisho vyenye madini ya magnesiamu kusaidia kupambana na tatizo la kukosa choo.
 • Ongea na daktari wako. Pale ambapo mbinu hizi za nyumbani hazifanyi kazi vizuri, mshirikishe daktari wako anaweza kukusahauri dawa au mbinu nyingine za kidaktari.

Je, naweza kuzuia kupata tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Tabia ya kula kiafya na mazoezi ya kawaida huhimiza mfumo wa haraka wa kumeng’enya chakula, ambao unaweza kusaidia kuzuia tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito.

Kutumia vyakula vingi vyenye nyuzi nyuzi (kama; matunda, mboga, nafaka nzima, dengu), kunywa maji ya kutosha na kuupa mwili mazoezi vyote kwa pamoja vinazuia tatizo la kukosa choo.

Lini nitarajie tatizo la choo kuisha nikiwa mjamzito?

Kwa wanawake wengine, tatizo la kukosa choo hudumu katika kipindi chote cha ujauzito kadri viwango vya projesteroni vinapopanda. Walakini, ukibadilisha tabia yako ya kula na kuwa na tabia ya kufanya mazoezi kila mara, mambo huanza kusonga vizuri. Na unaweza kuchukua hatua za kupambana na tatizo hili la kukosa choo wakati wowote wa ujauzito.

Kumbuka

Utafurahi kujua kwamba vitamini unazotumia kabla ya kujifungua pia zinaweza kusaidia tatizo la kukosa choo, haswa asidi ya folic. Manufaa ya “vitamini B complex” na “vitamini B5” sio tu kutatua tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito, bali inasaidia kupunguza maumivu ya miguu wakati wa ujauzito. Unaweza kuipata kutoka kwa viini vya mayai, nafaka nzima, parachichi, viazi vitamu, mbegu za alizeti, broccoli.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Kutoka Uchafu Ukeni Kipindi cha Ujauzito

Moja ya njia muhimu ya kutunza mfumo wa uzazi wa mwanamke ni kupitia uchafu unaotoka ukeni. Uchafu huu huweka uke wa mwanamke kuwa na afya nzuri ingawa wakati mwingine huweza kuleta shida. Maji yaliyotengenezwa na tezi ndani ya uke na mlango wa uzazi hubeba seli zilizokufa na bakteria nje ya mwili. Tendo hili linaweka uke safi na kusaidia kuukinga na maambukizi.

Wanawake wote hutokwa na uchafu ukeni, ingawa kiwango hutofautiana. Mara nyingi uchafu unaotoka ukeni ni kawaida kabisa. Unatofautiana kwa harufu,uzito, na rangi kulingana na mzunguko wako wa hedhi. Kwa mfano unaweza kutoka uchafu mwingi ukeni kama uko kwenye siku za yai lako kupevushwa, unanyonyesha au ashiki (hamu ya kujamiana). Uchafu huu unaweza kutoa harufu ya tofauti ukiwa mjamzito au unaposhindwa kujisafisha vizuri. Wanawake waliokomaa (menopause women) hupata uchafu huu kwa kiwango kidogo sana.

Mabadiliko haya yasikupe wasiwasi ni kawaida. Isipokuwa kama una dalili zifuatazo unaweza kuwa na tatizo la maambukizi ya vijidudu vya maradhi katika uke wako, ni vema kuwahi kituo cha afya kupatiwa uchunguzi zaidi na tiba sahihi:

 • Kutokwa uchafu ukeni kunakoambatana na kuwashwa au vipele.
 • Kutokwa uchafu ukeni ambako ni endelevu na kiwango kinaongezeka kila siku.
 • Maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo.
 • Kutoka uchafu mweupe, mzito kama jibini.
 • Kutoka uchafu wa kijivu/mweupe au njano/kijani unaotoa harufu mbaya.
 • Unajikuna, kuchomwa au hata uvimbe kwenye uke.
 • Maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Nini chanzo cha uchafu ukeni usio wa kawaida kwa mwanamke?

Badiliko lolote katika uwiano sawa wa bakteria wa asili wanaopatikana ukeni linaweza kuathiri harufu, rangi na muonekano wa uchafu unaotoka ukeni. Hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea uchafu ukeni kwa mwanamke yeyote:

 • Matumizi ya antibaotiki au virutubisho vya kikemikali (steroid)
 • Maambukizi yanayosababishwa na bakteria “bacterial vaginosis” – yanawapata wajawazito sana au wanawake walio na wapenzi zaidi ya mmoja.
 • Njia za mpango wa uzazi-vidonge
 • Kansa ya kizazi
 • Magonjwa ya zinaa kama klamedia au kisonono
 • Kutumia sabuni zenye marashi makali kusafishia uke/kutumia mafuta yenye harufu kali ukeni
 • Maambukizi katika mfumo wa uzazi baada ya upasuaji wakati wa kujifungua.
 • Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
 • Ugonjwa wa malengelenge sehemu za siri (trichomoniasis), unaosababishwa baada ya kufanya ngono zembe.
 • Uke kuwa mkavu kwa wanawake waliofikia ukomo wa kuzaa
 • Ugonjwa wa fangasi ukeni (yeast infection)

Aina ya uchafu unaotoka ukeni na chanzo chake

Aina ya uchafu Maana yake ni nini? Dalili nyingine
Rangi ya damu au kahawai(hudhurungi) Ishara ya mzunguko wa hedhi uliovurugika (irregular menstrual cycle), kansa ya kizazi au kansa katika mfuko wa uzazi. Utokaji wa damu ukeni usio wa kawaida, maumivu ya nyonga.
Rangi yenye mawingu au njano (cloudy or yellow) Kisonono Damu kabla na baada ya siku yako ya hedhi, maumivu ya nyonga,kushindwa kuzuia mkojo.
Uchafu wenye rangi njano au kijani unaotoka kama povu na wenye harufu mbaya. ugonjwa wa trichominiasis Maumivu na muwasho kila unapokojoa.
Uchafu wenye rangi ya pinki. Tabaka lililojishika ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi linatoka nje ya mwili baada ya kujifungua (lochia-kutokwa damu baada ya kujifungua)  
Uchafu mzito, mweupe, unaofanania jibini Ugonjwa wa fangasi ukeni. Maumivu na kuvimba kuzunguka uke (vulva), muwasho, maumivu wakati wa kujamiana.
Uchafu mweupe, rangi ya kijivu, au njano wenye harufu ya shombo ya samaki. Bakteria ukeni Muwasho au kuungua, wekundu na kuvimba uke au ndani ya uke (vagina au vulva)

 Chanzo cha uchafu kutoka ukeni kipindi cha ujauzito ni nini?

Ujauzito unaweza kukuchanganya kadiri unavyoendelea kukua, sio rahisi kujua mabadiliko yapi ni kawaida na yapi yanahitaji uharaka wa kuwasiliana na mkunga wako au kutembelea kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi. Mojawapo ya mabadiliko haya ni kutokwa uchafu ukeni, ambao unabadilika katika muda wa kutokea,mara ngapi unatokea,muonekano, kiasi,na uzito wake kipindi cha ujauzito.

Moja ya ishara za awali za ujauzito ni ongezeko la uchafu unaotoka ukeni, hali hii inaendelea kipindi chote cha ujauzito. Kwa kawaida uchafu unaotoka ukeni (leukorrhea) ni mwembamba, unaonekana vizuri (clear) au una rangi ya maziwa meupe na unatoa harufu kidogo.

Mabadiliko ya viwango vya homoni mara baada ya kuwa mjamzito yanasababisha mabadiliko ya uchafu unaotoka ukeni. Mabadiliko ya mlango wa uzazi kipindi cha ujauzito yanachangia kuathiri uchafu unaotoka ukeni. Kulainika kwa mlango wa uzazi na ukuta ndani ya uke, kunasababisha mwili kutoa uchafu zaidi ili kujikinga na maambukizi. Unapokaribia mwisho wa ujauzito kichwa cha mwanao kinaweza kuleta mgandamizo katika mlango wa uzazi na kupelekea ongezeko la uchafu unaotoka ukeni.

Kipindi chote cha ujauzito inategemewa mama mjamzito kupitia dalili kama mkojo kuvuja, kutoka uchafu, kuwashwa, na kuona damu katika nguo za ndani.

Katika makala hii utaweza kujua aina gani ya uchafu unaotoka ukeni ni kawaida na upi una ashiria tatizo linalohitaji kumuona daktari. Ili kujua aina gani ya uchafu unaotoka ukeni wakati wa ujauzito ni kawaida, tujifunze zaidi kuhusu vyanzo vyake:

Uchafu wa kawaida ukeni

Matone ya damu katika nguo zako za ndani

Hakuna kitu kinacho ogopesha kama kutokwa damu bila kutarajia. Wanawake wengi wanaona damu kidogo katika nguo zao za ndani katika kipindi cha miezi mitatu ya awali baada ya kufanya tendo la ndoa au uchunguzi wa mfumo wa uzazi katika miadi. Mara nyingi hali hii inaashiria yai lililo rutubishwa limefanikiwa kupandikizwa kwenye ukuta wa mfuko wa mimba (implantation) au muwasho katika mlango wa kizazi.

Kuona damu katika nguo zako za ndani kipindi cha mwisho cha ujauzito inahusiana na kuwa na kiasi cha ziada cha damu na homoni zinazopelekea mishipa iliyopo kwenye mlango wa uzazi kutoa damu. Wakati mwingine ina ashiria kujifungua kuna karibia, lakini pia inaweza kuashiria tatizo kubwa la kiafya kama- kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa. Kila unapoona matone ya damu kwenye nguo zako za ndani yasio kawaida (rangi nyekundu inayong’aa) mjulishe mkunga wako.

Unyevu katika nguo za ndani(chupi)

Je, unyevu kwenye nguo za ndani ni ishara chupa yako imepasuka? Inawezekana ni mkojo, ikiwa unavuja kila unapo cheka, piga chafya au kukohoa. Kuvuja mkojo ni kawaida kipindi cha ujauzito, inatokea kwasababu ya mgandamizo wa uterasi inayoendelea kukua. Mazoezi maalumu- “kegel” yanasaidia wanawake wengi kuweza kudhibiti vibofu vyao. Unaweza kufanya utaratibu wa kuwahi chooni dakika chache kabla ya kubanwa mkojo vizuri. Kumbuka usiache kunywa maji ya kutosha hata kama unavuja mkojo bila kutarajia. Ikiwa unahisi maji yanayovuja sio mkojo bali chupa ya uchungu imepasuka, fanya utaratibu wa kuwasiliana na mkunga wako au wahi kituo cha afya.

 Uchafu usio kawaida ukeni.

Ugonjwa wa fangasi ukeni

Maambukizi haya yana ambatanana muwasho, wekundu na kuvimba kuzunguka uke, baadhi ya wanawake wanapata maumivu wakati wa tendo la ndoa na kuungua wakati wa kukojoa. Uchafu huu una rangi ya njano au nyeupe inayofanana na jibini. Fangasi wanaishi ndani ya mwili na kwenye uke muda wote, lakini ujauzito unatengeneza mazingira ya fangasi kuzaliana.

Muone daktari akupatie ushauri wa dawa sahihi kwaajili ya maambukizi haya. Punguza sukari kwenye mlo wako (fangasi wanapenda sukari) na hakikisha unabadilisha nguo yako ya ndani (chupi) mara kwa mara.

Bakteria ukeni (Bacterial vaginosis-BV)

Maambukizi haya yanasababishwa na kukosekana kwa uwiano sawa wa bakteria asili wanaopatikana ukeni. Uchafu huu unaonekana zaidi baada ya kufanya tendo la ndoa,unaambatana na muwasho au kuungua kila unapojisaidia. Vile vile unakua na harufu ya shombo ya samaki ukiwa mjamzito. Maambukizi haya yasipotibiwa vizuri yanaweza kusababisha matitizo makubwa kwenye ujauzito. Kawaida maambukizi haya yanaanza katika uke, lakini baadae yanapanda kwenye uterasi na kusababisha kuraruka membreni mapema na kujifungua kabla ya wiki ya 37.

Ikiwa unahisi una dalili za maambukizi haya, muone daktari haraka. Dawa sahihi zinaweza tokomeza dalili zote bila kuhatarisha mtoto tumboni na kupunguza nafasi ya kujifungua kabla ya wiki 37.

Magonjwa ya zinaa

Wakati mwingine uchafu wenye rangi ya njano wakati wa ujauzito unaashiria kisonono, na uchafu unaotoka kama povu wenye rangi ya kijani au njano wakati wa ujauzito unaonyesha ugonjwa wa “trichomoniasis” zaidi ya hayo, uchafu ulio na harufu unasababishwa na klamedia. Maambukizi haya matatu ya zinaa yanaweza sababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa au kujisaidia. Kuwa na magonjwa ya zinaa wakati wa ujauzito inapelekea kujifungua kabla ya wiki 37 na maambukizi ya mfuko wa mimba baada ya kujifungua.

Baadhi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa haya ya zinaa vinaweza penya kupitia plasenta na kuathiri kijusi, mengine yanaweza kusambazwa kwa mtoto wakati wa kujifungua.

Ikiwa unahisi una maambukizi ya magonjwa ya zinaa wahi kituo cha afya mara moja, ukapimwe na daktari na kupatiwa antibaotiki sahihi. Habari njema ni kuwa magonjwa haya mengi yanaweza kutibika kwa antibaotiki sahihi.

Jinsi gani uchafu unaotoka ukeni unatibiwa?

Aina ya matibabu yatategemea na nini chanzo cha uchafu. Kwa mfano maambukizi ya fangasi ukeni yanatibiwa na dawa za antifungal zinazowekwa ndani ya uke. BV inatibiwa na antibaotiki. Ugonjwa wa malengelenge sehemu za siri  unatibiwa na madawa kama “metronidazole(Flagyl) au tinidazole (Tindamax).

Vifuatavyo ni vidokezo kwa wanawake wote(wajawazito na wasio wajawaazito) vya kuzuia maambukizi ukeni ambayo yanapelekea uchafu usio kawaida ukeni:

 • Weka uke wako safi kwa kusafisha taratibu, sabuni kidogo na maji vuguvugu kwa nje. Hakuna haja ya kutumia sabuni moja kwa moja kwenye uke.
 • Epuka kuosha uke kwa kutumia sabuni zenye manukato au mbinu yoyote ile kwa sababu huongeza kujikuna. Uke wenye afya hauhitaji marashi au manukato.
 • Baada ya kutoka bafuni, siku zote jifute kuanzia mbele kurudi nyuma kuepuka bakteria kuingia ukeni na kusababisha maambukizi.
 • Ongeza mtindi katika mlo wako ili kukuza bakteia wenye afya.
 • Tumia chupi iliyotengenezwa kwa pamba au chupi ambayo haitakuchoma na badilisha chupi kila siku.
 • Usivalie nguo za kukubana kwa sababu zinafanya mwili kuwa na unyevu na kisha husababisha vidudu kusambaa kwa haraka.
 • Osha chupi kwa maji moto na sabuni kisha ukamue chupi hizo kwa maji masafi kabla ya kuanikwa.
 •  Badilisha nguo zenye unyevunyevu baada ya kuogelea au nguo za michezo baada ya mchezo bila kukawia.

Kumbuka

Ni muhimu kuwasiliana na daktari au mkunga anayesimamia ujauzito wako kama unatokwa uchafu usio wa kawaida ukeni, maana inaweza kuwa ishara ya maambukizi au tatizo kwenye ujauzito wako.

CDC (Centre for diseases control and prevention) wanashauri wajawazito wote kuchunguzwa magonjwa ya zinaa katika miadi ya kwanza ya kliniki.

Uchafu usio wa kawaida unaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa kwenye ujauzito wako. Wasiliana na mkunga anayesimamia ujauzito wako ikiwa utaona uchafu ukeni wenye rangi nyekundu inayong’aa. Inaweza kuwa ishara ya tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa au placenta previa (kondo la nyuma hujipachika katika sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi)

IMEPITIWA: MEI,2021.

Kuvimba Miguu na Vifundo cha Miguu Kipindi cha Ujauzito (Edema).

Mwili wa mjamzito unabadilika kwa kasi sana na kumfanya asijisikie vizuri na kukosa utulivu wa mwili na akili. Moja ya mabadiliko ya mwili ambayo wajawazito wengi wanapata wasiwasi nayo kipindi cha ujauzito ni ni miguu na vifundo vya miguu kuvimba. Edema inaathiri karibia robo tatu ya wanawake wajawazito. Mara nyingi inaanza wiki ya 22 mpaka 27, inaweza kubaki hata baada ya kujifungua.

Katika makala hii tutajadili kwanini miguu inavimba kipindi cha ujauzito, lini unaweza kuona hali hii, lini umuone daktari, na vidokezo rahisi vinavyoweza kukusaidia kukabiliana na hali hii.

Nini chanzo cha miguu kuvimba kwa wajawazito?

Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

Ongezeko la kasi la viwango vya homoni ya projesteroni hupunguza kasi ya umeng’enyaji wa chakula. Hii inaweza kusababisha kuvimbiwa tumboni, vilevile unaweza ona mikono, miguu au uso wako umevimba kiasi.

Ikiwa utashuhudia mikono, miguu na uso wako kuvimba sana mapema hii, haswa kama uvimbaji huu unaambatana na dalili nyingine kama kizunguzungu, kuumwa kichwa au kutoka damu, ni jambo la hekima kuwasiliana na mkunga au daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Miezi mitatu ya pili ya ujauzito

Kipindi hiki kinaanza na wiki ya 13 ya ujauzito. Ni kawaida kuanza kushuhudia miguu kuvimba kipindi hasa ikiwa una simama mda mrefu au hali ya hewa ya sehemu unayoishi ni joto.

Uvimbe huu unasababishwa na kuongezeka kwa kiasi cha damu na majimaji ndani ya mwili. Kiasi cha damu huongezeka kwa karibia asilimia 50 kipindi cha ujauzito, ukiunganisha na uhifadhi mwingi wa maji ya homoni (hormonal fluid retention).

Maji haya ya ziada yatasaidia kuandaa na kulainisha mwili wako kwaajili ya kujifungua. Punguza wasiwasi maji haya ya ziada yatapungua kwa kasi baada ya kichanga wako kuzaliwa.

Kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito

Wajawazito wengi wanapatwa na tatizo hili la miguu kuvimba kipindi hichi, kinachoanza wiki ya 28. Kadiri wiki zinavyosonga mbele na kukaribia wiki ya 40, ndivyo vidole vyako vya miguuni vitakavyozidi kuvimba.

Edema inatokea pale majimaji ya mwili yanapo ongezeka ili kuhakikisha mtoto na mama mjamzito wanaendelea kukua vizuri, majimaji haya yanachukua nafasi katika tishu na kusababisha mwili kuvimba. Ukuaji wa uterasi unasababisha mgandamizo kwenye mishipa ya nyonga na venakava (mshipa mkubwa unaopatikana upande wa kulia unaohusika na kurudisha damu moyoni kutoka miguuni), hali hii inaweza kupunguza kasi ya mzunguko wa damu kutoka kwenye miguu kurudi kwenye moyo (usiwe na wasiwasi, hali hii sio hatari-itakufanya usiwe katika hali ya utulivu tu). Matokeo yake miguu, mikono na vifundo vya miguu kuzidi huvimba.

Sababu nyingine zinachangia miguu kuvimba kipindi hichi ni pamoja na:

 • Hali ya hewa-joto.
 • Kuongezeka uzito kwa kasi.
 • Kukosa mlo kamili.
 • Unywaji wa kahawa na bidhaa zenye kafeini.
 • Kutembea kwa miguu au kusimama mda mrefu.
 • Kutokunywa maji ya kutosha.

Je, kuna hali za hatari zinazohusiana na kuvimba kwa miguu na vifundo vya miguu?

Hata hivyo ikiwa mikono au uso wako ukavimba na kudumu zaidi ya siku bila kupungua (ndani ya usiku mmoja) wasiliana na daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Kuvimba kupita kiasi kunaweza kuwa ishara ya kifafa cha mimba-huwa inaambatana na dalili nyingine kama shinikizo kubwa la damu, kuongezeka uzito kwa kasi na uwepo wa protini katika mkojo. Ikiwa shinikizo na mkojo wako vitaonekana kuwa kawaida (kila miadi unachunguza), hakuna haja ya kupata wasiwasi.

Kuvimba kwa mguu mmoja (mguu wa kulia) ni ishara ya hali inayoweza hatarisha maisha “DVT” (deep vein thrombosis)-inatokea pale damu inapoganda katika mshipa ulio ndani(deep) .Ishara nyingine ni pamoja na uzito au maumivu ya mguu yanayozidi kila ukisimama, ngozi ya mguu inakua nyekundu na moto pale unapoigusa. Ikiwa umeoona ishara hizi wasiliana na mkunga wako mara moja.

Muda mwingi, miguu kuvimba ni ishara nyingine ya kazi nzito mwili wako unafanya kukuza maisha mapya ya mtoto anayekua tumboni. Hata hivyo wakati mwingine miguu kuvimba ni ishara ya hali hatari sana. Moja ya hali hizi ni kifafa cha mimba. Hali hii huanza wakati wa ujauzito na kusababisha shinikizo kubwa la damu ambalo ni hatari.

Muone daktari ikiwa utaona ishara zifuatazo:

 • Kuvimba ghafla kwa miguu,mikono, uso na kuzunguka macho.
 • Kuvimba kupita kiasi.
 • Kizunguzungu au kushindwa kuona vizuri.
 • Maumivu makali ya kichwa
 • Kuchanganyikiwa
 • Shida katika upumuaji.
 • Ikiwa utashuhudia mguu mmoja umevimba, ukiambatana na maumivu, kubadilika rangi na kuwa wa moto.

Jinsi gani ya kukabiliana na kuvimba kwa miguu na vifundo vya miguu.

 • Weka kikomo cha ulaji wa chumvi. Moja ya njia ya kupunguza miguu kuvimba kipindi cha ujauzito ni kuweka kikomo katika ulaji wa vyakula vyenye sodiamu (chumvi). Chumvi inafanya mwili utunze maji ya ziada. Jaribu kuepuka kula vyakula vilivyohifadhiwa kwenye makopo-vina viwango vikubwa vya sodiamu. Epuka pia kuongeza chumvi kwenye chakula mezani. Tumia viungo kama majani ya “rosemary”, giligilani, tangawizi kuongeza ladha kwenye chakula chako.
 • Kunywa maji ya kutosha. Kunywa maji glasi 8 mpaka 10 kwa siku itakusaidia kuondoa sodiamu ya ziada na taka mwili nyingine.
 • Ongeza ulaji wa vyakula vyenye potasiamu. Potasiamu inasaidia mwili kufanya uwiano wa kiasi cha majimaji unayotunza. Virutubisho unavyotumia kipindi cha ujauzito vina potasiamu ya kutosha kwaajii ya mama mjamzito, lakini vilevile ni muhimu kula vyakula vyenye potasiamu ya kutosha. Baadhi ya vyakula vyenye asilia ya kuwa na patasiamu nyingi ni pamoja na: viazi mviringo na maganda yake, viazi vitamu na maganda yake,ndizi, spinachi, maharagwe, juisi za matunda (chungwa, karoti, pasheni, na komamanga), mtindi na samaki aina ya “salmon. 
 • Epuka kukaa au kusimama kwa muda mrefu. Ikiwa unafanya shughuli inayokutaka kusimama kwa muda mrefu, chukua mapumziko mara kwa mara na kaa kitako. Ikiwa unakaa sana, tumia dakika 5 kwa kila saa, kusimama na kutembea kidogo.
 • Tembea. Matembezi ya hata dakika 5 mpaka 10 kwa siku yanaweza kuboresha mzunguko wa damu na kusaidia kupunguza miguu kuvimba. Hii pia ni njia nzuri ya kufanya mazoezi wakati wa ujauzito.
 • Vaa viatu visivyokubana. Viatu vinavyokuacha huru ni muhimu katika kupunguza uvimbe wa miguu, vile vile hukinga matatizo ya mgongo na nyonga yanayoletwa na mabadiliko ya mkao (centre of gravity) na kuongezeka uzito.
 • Ogelea. Hakuna utafiti unaothibitishakuwa mgandamizo wa maji unapunguza kuvimba kwa miguu wakati wa ujauzito, lakini wanawake wengi wanapata kutulizwa wakitumia muda wao kwenye maji. Jaribu kusimama au kuogelea kwenye maji yenye kina kirefu (kama unaweza). Angalau unaweza kusikia mwepesi,mwili kupoa na pia kuupa mwili wako mazoezi. Utagundua pia miguu yako imepungua kuvimba.
 • Pata “massage”.Kwa msaada ya mwenza wako au sehemu maalum zenye kutoa huduma hii. Kukanda miguu kwa kutumia mafuta maalum inasaidia kusambaza majimaji ambayo yanajikusanya miguuni. Ikiwa unakaribia kujifungua, mweza wako ahakikishe anaepuka kusugua sehemu (acupressure points) ambazo zinahusiana na mikazo ya kujirudia ya mfuko wa uzazi (uterine contractions). Ni busara kumpata mtu aliye na ujuzi wa masaji kukusaidia.
 • Lala kwa ubavu wa kushoto. Ulalaji huu unaweza kuboresha mzunguko wa damu, ambayo inaweza kupunguza miguu kuvimba. Kulala kwa ubavu wa kushoto kuna ondoa mgandamizo wa uterasi kwenye mshipa mkubwa wa damu unaorudisha damu kwenye moyo kutoka miguuni.
 • Weka miguu yako juu. Kama inawezekana kila unapokaa kitako hakikisha miguu imeinuliwa juu, unaweza kutumia kiti kingine, kigoda au ndoo kama egemeo.
 • Epuka soksi au taiti zinazobana. Lengo lako ni kuhakikisha dam una majimaji yanasafiri kwa urahisi (soksi zinazoacha alama ya kubanwa kwenye mguu ni ishara kuwa zinabana).
 • Punguza matumizi ya kafeini. Unywaji sana wa kahawa unachukuliwa kama hatari kubwa kwa mtoto. Inaweza pia kusababisha mguu na vifundo vya miguu kuvimba zaidi. Jaribu chai yenye majani ya mitishamba kama mnana, mchaichai, n.k.
 • Vaa nguo zisizobana. Nguo zinazobana hasa kwenye viwiko, kiuno na vifundo vya miguu inaweza kufanya uvimbe kuongezeka zaidi. Kimsingi, inafanya damu isisambae kwa urahisi. Jaribu kuvaa mavasi yanayoachia mwili- madera na magauni mapana yanayoachia mwili huru, suruali pana zisizobana kwenye kiuno na miguuni ikiwa unaishi eneo lenye baridi.

Kumbuka

Miguu kuvimba ni hali ya kawaida sana kipindi cha ujauzito. Uvimbe huu unasabishwa na ongezeko la kiasi cha maji kwenye mwili, vilevile upungufu wa usambazaji wa maji maji haya.

Ikiwa unapata uvimbe wa miguu uliopitiliza ghafla, ni muhimu kuwasiliana na daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako, kwasababu inaweza kuwa ishara ya tatizo lingine kubwa. Lakini miguu kuvimba kidogo ni kawaida.

Unaweza kuepuka kuvimba miguu kila mara kwa kufanya mzoezi mepesi kwa mjamzito kila mara kama vile kutembea, kunywa maji ya kutosha, pumzika na kula mlo kamili.

IMEPITIWA: MEI,2021.

Maumivu ya Mgongo Wakati wa Ujauzito

Habari njema ni kuwa mtoto wako anaendelea kukua. Maumivu makali katika mgongo kipindi hichi yanasababishwa na ukuaji wa mtoto tumboni.

Kumbuka sio wewe tu unayepitia hali hii,wajawazito wengi wanaanza kupatwa na hali hii mara nyingi kuanzia kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito.

Makala hii itakupa nafasi ya kufahamu vidokezo vitakavyokusaidia kupunguza maumivu ya mgongo kipindi cha ujauzito.

Chanzo cha maumivu ya mgongo kwa mama wajawazito

Kawaida maumivu ya mgongo wakati wa ujauzito yanatokea sehemu ambayo nyonga na uti wa mgongo vinakutana (sacroiliac joint)

Maumivu ya mgongo yanachangiwa na mambo mengi.  Zifuatazo ni sababu zinazoongeza nafasi ya maumivu ya mgongo kutokea kwa wajawazito:

 • Kuongezeka uzito. Wakati wa ujauzito ambao ni salama, kawaida wanawake huongezeka uzito (kilo 11-16). Kazi ya kuhimili uzito huu inafanywa na uti wa mgongo. Hii inaweza kusababisha maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo. Uzito wa mtoto anayekua na uterasi vinasababisha mgandamizo kwenye mishipa na mirija ya damu inayopatikana katika nyonga na mgongo.
 • Mabadiliko ya mkao. Uzani wa mtoto, uterasi na kiowevu cha amnioni hubadili mkao wak na kuweka mkazo kwenye mifupa na misuli ya mgongo wa mama mjamzito.Taratibu bila hata kujua utaanza kubadilisha mkao wako na jinsi unavyotembea,hali hii inaweza kusababisha maumivu ya mgongo.
 • Mabadiliko ya homoni. Wakati wa ujauzito, mwili unatengeneza homoni iitwayo “relaxin” ambayo inaruhusu ligamenti katika nyonga kupumzika na viungo kulegea kwaajili ya maandalizi ya kujifungua. Homoni hii inasababisha ligamenti zinazosaidia uti wa mgongo kufanya kazi vizuri kulegea pia, hali hii inasababisha maumivu.
 • Msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo unaweza kusababisha mvutano wa misuli inayopatikana kwenye mgongo,hali hii inaweza kusababisha maumivu ya mgongo kwa mama mjamzito.

Matibabu kwaajili ya maumivu ya mgongo kwa mama mjamzito

Habari njema zaidi: maumivu ya mgongo yanaweza kupungua taratibu kabla ya kujifungua isipokuwa kama ulikuwa na matatizo ya kudumu ya mgongo kabla ya kubeba ujauzito.

Wakati huohuo, yapo mambo mengi unaweza kufanya kutibu sehemu ya chini ya mgongo wako au kupunguza maumivu haya:

 • Kufanya mazoezi kila mara, mazoezi salama kwa mjamzito kama kutembea, kuogelea yanaweza kunyoosha misuli na kupunguza mvutano katika uti wa mgongo. Mkunga wako anaweza kukushauri mazoezi ya kunyoosha mgongo na fumbatio ambayo ni salama kwako na ujauzito wako.
 • Tumia vitu vya baridi au joto kutuliza maumivu ya mgongo. Zungumza na mkunga au daktarin wako anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako kama ni salama kutumia njia hii. Unaweza kuanza kwa kuweka kitu cha baridi (mfuko wenye barafu au njegere zilizoganda) kwa dakika 20 eneo lenye maumivu. Baada ya siku mbili au tatu ukabadilisha na kuweka chupa ya plastiki au mpira maalumu wa maji ya moto eneo lenye maumivu. Kuwa makini usisababisha maumivu kwenye fumbatio wakati wa ujauzito.
 • Imarisha mkao wako. Kuchechema kunaumiza uti wako wa mgongo. Hivyo basi, mkao mzuri wakati unafanya kazi, kaa kitako au kulala ni hatua nzuri. Kwa mfano, wakati wa kulala-lala kwa upande kwa msaada wa mto katikati ya magoti ili kutoa mkazo mgongoni. Ukiwa umekaa kwenye dawati ofisini, weka mto au taulo iliyoviringishwa vizuri nyuma ya mgongo wako kuupa msaada mgongo. Vilevile pumzisha miguu yako juu ya vitabu kadhaa ulivyovipanga au kigoda kisha kaa kwa kunyooka, mabega yako yakirudi nyuma. Ikiwezekana vaa mkanda maalumu unasaidia.
 • Ushauri nasaha. Ikiwa maumivu yako ya mgongo yanahusiana na msongo wa mawazo, kuongea na rafiki yako unayemwamini au mshauri nasaha inaweza kukusaidia.
 • Matibabu ya kutumia sindano(acupuncture) hii ni aina ya dawa kutoka China ambapo sindano nyembamba zinatumika kuchomwa kwenye ngozi katika maeneo fulani. Utafiti unaonyesha aina hii ya matibabu inaweza kutuliza maumivu ya mgongo wakati wa ujauzito. Ongea na daktari wako kama ni salama kwako na upatikanaje wake.

Vidokezo zaidi:

 • Ikiwa unataka kuokota kitu chini, tumia miguu yako kuchuchumaa kuliko kuinama.
 • Usivae viatu vyenye kisigino kirefu.
 • Usilale kwa mgongo

Ikiwa maumivu yako yatazidi, ni busara zaidi kumuona dakatari, ili kuona kama kuna hatua nyingine inaweza kuchukuliwa. Hakikisha unapata maelekezo au ushauri kutoka kwa daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako kabla ya kutumia dawa yeyote kutumiza maumivu. Acetaminophen (Tylenol) ni salama kwa mama mjamzito. Dawa kama Asprin na dawa nyinginezo za maumivu kama ibuprofen (Advil,Motrin) au naproxen(Aleve) hazishauriwi kutumika kwa mama mjamzito.

Kwa baadhi ya wanawake, maumivu ya mgongo sio sababu pekee ya kuwasiliana au kumuona daktari. Lakini inakubidi umuone daktari haraka iwezekanavyo ikiwa utapata dalili zifuatazo:

 • Maumivu makali sana
 • Ongezeko la maumivu haya makali au maumivu yanayoanza ghafla.
 • Shida kukojoa au kuhisi hali ya kuchomwa na pini au sindano kwenye mikono na miguu.
 • Maumivu yanayofuatana katika fumbatio.

KUMBUKA

Katika hali nadra, maumivu makali ya mgongo yanaweza kuhusishwa na shida kama vile ugonjwa wa mifupa “osteoporosis”-hali ambayo mifupa inakua dhaifu na yenye kuvunjika kwa urahisi. Maumivu yanayofuatana inaweza kuwa ishara ya uchungu wa kujifungua kabla ya muda. Kwa hivyo ikiwa unapata shida hizi, ni muhimu kuchunguzwa na daktari wako hospitalini.

IMEPITIWA: APRILI, 2021.

Maambukizi ya Njia ya Mkojo (UTI) Wakati wa Ujauzito

UTI ni kifupi cha urinary tract infection au kwa lugha rahisi maambukizi katika njia ya mkojo, ambayo inajumuisha figo, ureta (mirija ya figo inayobeba mkojo kutoka kwenye figo mpaka kwenye kibofu), kibofu cha mkojo na urethra (mrija mfupi unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu mpaka nje ya mwili). Ogani zote hufanya kazi pamoja ili kuondoa uchafu kutoka kwenye damu. Kwanza figo husafisha damu na kugeuza uchafu kuwa mkojo. Halafu mkojo huteremka kwenda kwenye kibofu kwa msaada wa mirija ya figo-ureta ambapo hapo hutunzwa na baadaye kutolewa nje ya mwili kupitia mrija wa urethra.

Maambukizi haya yanasababishwa na bakteria. Mtu yeyote anaweza kuyapata. Mwanamke anaweza kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo wakati wa ujauzito kuliko nyakati zingine zote. Ikiwa utahisi una UTI,ongea na daktari wako mapema. Kwa huduma na matibabu mazuri wewe na mtoto wako mtakuwa salama.

Mara nyingi maambukizi haya ushambulia zaidi kibofu cha mkojo na urethra. Lakini wakati mwingine yanaweza kupelekea maambukizi ya figo, maambukizi haya kwenye figo yanaweza pelekea mama kujifungua kabla ya muda au kujifungua mtoto mwenye uzito duni. Ndio maana ni muhimu kuchunguza dalili na ishara za maambukizi katika kila miadi ya kliniki kwa mjamzito.

Aina za Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI)

Cystitis or Bladder infection: Aina hii hutokea pale bakteria wanakusanyika kwenye kibofu cha mkojo na kusababisha uvimbe.

Maambukizi ya figo: bakteria wanaweza kupita kutoka kwenye kibofu cha mkojo kupitia mirija ya mkojo (ureter) na kuathiri figo moja au zote mbili, ugonjwa unaojulikana kama ‘pyelonephritis’. Ugonjwa huu unawaathiri sana wajawazito na huweza kusambaa kwenye damu. Madhara huwa makubwa kwa mama mjamzito na huweza kusababisha mtoto kuzaliwa njiti.

Asymptomatic bacteriuria: Mara nyingine bakteria katika njia ya mkojo hawaonyeshi dalili zozote.

Dalili za Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI)

Ikiwa una UTI, unaweza kuwa na dalili kama:

 • Kubanwa na mkojo haraka au kwenda kujisaidia haja ndogo kila mara
 • Shida wakati wa kukojoa
 • Kujisikia hali ya kuungua au maumivu sehemu ya chini ya misuli ya mgongo au tumbo la chini
 • Kujisikia hali ya kuungua kila unapojisaidia haja ndogo.
 • Mkojo kubadilika rangi au kuwa na harufu kali.
 • Maumivu wakati wa tendo la ndoa.
 • Damu kwenye mkojo, ambayo itaubadikisha rangi na kuwa pinki inayong’aa au rangi ya cocacola

Ikiwa una maambukizi ya figo unaweza ukawa na dalili kama:

 • Homa kali
 • Kichefuchefu
 • Kutapika
 • Maumivu ya sehemu ya juu ya mgongo, mara nyingi upande mmoja.

Kama una dalili za maambukizi ya figo, muone daktarin haraka katika kituo cha afya kilicho karibu na wewe. Bila matibabu sahihi, maambukizi haya yanaweza kuenea ndani ya mfumo wako wa damu na kusababisha hali za kutishia maisha.

Kwanini UTI Inatokea Mara kwa Mara Wakati wa Ujauzito

Homoni ni moja ya sababu. Kipindi cha ujauzito, homoni zinasababisha mabadiliko katika njia ya mkojo na kumfanya mwanamke awe katika hatari ya kupata maambukizi. Mabadiliko ya homoni yanapelekea hali ambayo mkojo unarudi kwenye kibofu cha mkojo kisha kwenye figo (vesicoureteral reflux), hali hii inaweza kusababisha UTI.

Ukiwa na ujauzito, mkojo wako una sukari zaidi, protini na homoni ndani yake. Mabadiliko haya pia yana kuweka katika hatari kubwa ya kupata UTI.

Kwasababu ya ujauzito, ukuaji wa uterasi unaoendelea kadiri ujauzito unavyokua hugandamiza kibofu cha mkojo. Hali hii inazuia mkojo wote ulio kwenye kibofu kutoka, mkojo unaobaki unaweza kuwa chanzo cha maambukizi.

Sababu/Chanzo cha UTI ni pamoja na:

“Escherichia coli” ni bakteria wanaotoka kwenye kinyesi chako: E.Coli ni chanzo kikubwa cha UTI na anaweza kuhama kutoka kwenye sehemu ya haja kubwa (mkundu) mpaka kwenye urethra ikiwa baada ya kujisaidia unajisafisha kuanzia nyuma kwenda mbele.

Shughuli zinazohusiana na tendo la ndoa. Vidole, uume wa mwenza wako, au vifaa vinavyotumika wakati wa tendo la ndoa vinaweza kusogeza bakteria karibu na urethra yako ku

“Group B streptococcus” baktari huyu anapatikana katika uke na utumbo mkubwa wa chakula, anaweza kusababisha UTI. Maambukizi haya yanaweza kupatiwa kwa watoto wachanga pia kutoka kwa mama zao. Katika wiki kati ya 36 mpaka 37 ya ujauzito daktarin atafanya kipimo kwa mama mjamzito kuchunguza aina hii ya bakteria. Ikiwa utapatikana na bakteria huyu, daktarin wako atakupatia dawa wakati wa kujifungua.

Jinsi Gani Maambukizi Katika Njia ya Mkojo Yanachunguzwa?

 • Kipimo cha mkojo kitachukuliwa. Inapendekezwa kupima mkojo wa kwanza wa asubuhi, ikiwa mkojo una chembechembe nyeupe za damu nyingi huashiria maambukizi.
 • Kipimo cha damu
 • Kipimo cha “urine culture” ni kipimo cha kugundua vijidudu vinavyoleta maambukizi kama vile bakteri kwenye mkojo. Sampuli ya mkojo huongezwa kwenye dutu ambayo inasababisa vijidudu kukua. Ikiwa hakuna vijidudu vinavyokua, basi kipimo ni (-ve), ikimaanisha hakuna bateria ndani ya mkojo. Uchunguzi huu ndio bora zaidi na unafaa kufanywa kabla ya kutumia dawa za antibayotiki.
 • Wakati mwingine kipimo cha Ultrasound hutumika kwa mgonjwa anayepata ugonjwa huu mara kwa mara.

Matibabu ya UTI Wakati wa Ujauzito

Utatumia dawa alizokuandika daktari kwa siku 3 mpaka 7. Ikiwa maambukizi yako yatakufanya ujisikie vibaya daktari wako anaweza kukuanzishia matibabu hata kabla majibu ya mkojo kutoka.

Dalili za UTI zinazokusumbua zitaanza kupotea siku ya tatu baada ya kuanza dozi. Tumia dawa zote ulizoandikiwa kwa wakati. Usiache kutumia dawa mapema hata kama dalili zimepotea.

Baadhi ya antibiotiki zinazotumika kutibu maambukizi ya njia mkojo ni pamoja na: amoxicillin, erythromycin na penicillin, dawa hizi ni salama kwa wanawake wajawazito. Daktari ataepuka kukuandikia dawa ambazo zinaweza kuathiri ukuaji wa mtoto ambazo ni pamoja na ciprofloxacin (Cipro), sulfamethoxazole, na tetracycline.

Matatizo Yanayoweza Kusababishwa na UTI Wakati wa Ujauzito

Maambukiz ya njia ya mkojo yanayoathiri figo yanajulikana kama “pyelonephritis”. Ikiwa wewe ni mjamzito aina hii ya maambukizi inaweza sababisha mambo yafuatayo:

 • Kujifungua kabla ya muda
 • Maambukizi makali
 • Anemia
 • Maambukizi ya mda mrefu ya njia ya mkojo (UTI sugu)

Nitajikingaje Dhidi ya Maambukizi Katika Njia ya Mkojo Wakati wa Ujauzito?

Ili kujaribu kuepuka UTI mambo yafuatayo hayana budi kufuatwa:

 • Kunywa maji ya kutosha angalau glasi 8 kwa siku. Maji huzimua mkojo na kusaidia kutoa bakteria kwenye kibofu cha mkojo kwa njia ya mkojo.
 • Ukimaliza kujisaidia jifute kuanzia mbele kurudi nyuma
 • Jisaidie haja ndogo kabla na baada ya kufanya tendo la ndoa na usisahau kujifuta sehemu za siri baada ya tendo la ndoa, ukianzia mbele kurudi nyuma. Pia inashauriwa kunywa glasi moja ya maji.
 • Epuka sabuni zenye marashi makali zinazoweza sababisha muwasho katika kusafisha sehemu zako za siri.
 • Kula vyakula vyenye vitamini C kama vile matunda(ubuyu, machungwa, machenza,nk)mkojo wenye asidi hupunguza bakteria
 • Vaa nguo za ndani zilizotengenezwa na pamba ili kuruhusu mzunguko wa hewa.
 • Usivae nguo za ndani zinazokubana
 • Jisaidie haja ndogo kila mara, angalau baada ya saa mbili au tatu. Usibane mkojo kwa muda mrefu, hali hii huwapa bakteria nafasi ya kukua
 • Epuka pombe, vyakula vyenye pilipili, kahawa na vyakula vyote vinavyoweza sababisa muwasho katika kibofu chako.

IMEPITIWA: APRIL 2021

Virusi Vya Corona COVID19 na Ujauzito

 

Je, wajawazito na kina mama wanaonyonyesha wanahitaji kujua nini kuhusu virusi vya corona?

Kuna mengi yasiyofahamika kuhusu madhara ya virusi vya corona kwa wajawazito na kina mama wanaonyonyesha. Lakini uelewa wa madhara ya virusi hivi utaongezeka kadiri muda unavyoenda.

Kuwa mjamzito huleta wasiwasi na hali ya sintofahamu kwa wamama wengi watarajiwa, hata kama kila kitu kinaenda sawa.

Wanahitaji kuepuka aina fulani ya vyakula mfano samaki wasiopikwa vizuri na jibini laini. Hii ni kwasababu miili yao inabadilika kwa kiasi kikubwa kila siku na utaratibu wake wa kawaida unaweza kuvurugika.

Taifa la Uingereza ni moja ya nchi ambazo hivi karibuni zimewahusisha wanawake wajawazito katika kundi la watu walio katika hatari za kupata maambukizi haya. Inashauriwa wanawake wajawazito kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ili kupunguza nafasi za kushika virusi vya Corona. Inaeleweka, wajawazito wengi na familia zao wana wasiwasi na wamechaganyikiwa kwasababu ya ujio huu wa Virusi vya Corona.

Pamoja yote hayo, ukweli unabaki kuwa hatuna ufahamu wa kutosha kuhusu madhara ya virusi hivi vya Corona COVID-19 kwa wajauzito. Kuwepo kwa ufahamu wa kutosha husaidia kuchukua hatua za uhakika. Uwepo mdogo wa wanawake wajawazito waliopata maambukizi haya pamoja na ufahamu wa kutosha wa Virusi hivi vya Corona kwa ujumla utatusaidia kutoa ushauri wa ziada kwa wanawake wajawazito kuchukua tahadhari mapema.

Mfumo Dhaifu wa Kinga ya Mwili

Mwanzoni ilidhaniwa kipindi cha ujauzito kinga ya mwili ya mwanamke inadhoofika na kumfanya kuwa katika hatari ya kupata maambukizo. Hata hivyo, kama ilivyo vitu vingi vinavyohusiana na mwili wa binadamu ushahidi mpya unaonesha kuwa kinga mwili ya mjamzito hupanda kipindi cha ujauzito, na wakati mwingine huwa ni ya kubadilika badilika.

Mabadiliko haya ya kinga ya mwili kipindi cha ujauzito ni muhimu kwa ajili ya kumpa nafasi mtoto anayeendelea kukua katika hatua tofauti za ujauzito. Kwa mfano katika hatua za kwanza za ujauzito kinga ya mwili inabadilika ili kuruhusu upandikizaji katika mwili. Wakati mwingine mfumo wa kinga unahitaji kujirekebisha katika njia tofauti, mfano mzuri ni wakati mwili wa mwanamke unajiandaa kupata uchungu wa kujifungua.

Jambo la muhimu katika maelezo yote haya ni kwamba kuwa na mfumo wa kinga wenye kubadilika badilika inakuweka katika hatari kubwa ya matatizo ya Virusi vya Corona kama vile shida katika upumuaji na hata homa ya mapafu (pneumonia).

Kitu cha kwanza cha kutiliwa mkazo ni wanawake wajawazito waendelee kuhudhuria miadi yao ya kliniki katika hospitali isipokuwa kama wameambiwa vinginevyo na mkunga au daktari wao.

Kwa sasa hakuna sababu ya kubadilisha mpango wako wa kujifungua, kama uliandaa hapo awali. Mpango wa kujifungua unahusisha mahali unapotarajia kujifungulia (hospitali, zahanati, kituo cha afya, au nyumbani) na aina gani ya dawa za maumivu unatarajia kupata.

Walakini, ikiwa umeonekana na dalili zinazoashiria maambukizi ya Virusi vya Corona, kama kikohozi kikavu au joto kubwa la mwili, kubanwa kifua na kupumua kwa shida,  ni lazima ujitenge (self-isolation) na wasiliana na daktari au mkunga wako haraka.

Vilevile, kwa wanawake wajawazito wenye matatizo mengine ya kiafya wanahitaji kuwa makini zaidi na kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ikiwezekana kufikiria kujitenga (self-isolation) kipindi cha ujauzito. Wanawake waliopata ugonjwa wa kisukari, aina ya ugonjwa wa kisukari ambayo ni matokeo ya ujauzito ijulikanayo “Ugonjwa wa Kisukari kipindi cha Ujauzito” (gestational diabetes), wanatakiwa kuchukua tahadhari na kupunguza migusano na watu.

Kuwa mgonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito ni kundi la hatari hata bila kupata Virusi vya Corona, kwasababu ugonjwa huu wa kisukari unaongeza ugumu wakati wa ujauzito na kujifungua. Zaidi ya hapo, viwango vikubwa vya sukari katika damu kwa mda mrefu bila kutibiwa na kuangaliwa vizuri vinaweza kudhoofisha mfumo wa kinga zaidi.

Kutokana na mfumo wa kinga unaobadilika kila hatua wakati wa ujauzito ni vizuri wanawake wasio na matatizo ya kiafya kuchukua tahadhari na kukaa mbali na watu pale inapobidi.

Kama ilivyo wajawazito wengi wanaishi na wenzi wao au mara nyingine mtoto/watoto wao wengine, ushauri huu ni vizuri kufuatwa ili kupunguza nafasi ya kuweka afya ya mama mjamzito katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Corona.

Tahadhari hizo ni pamoja na kufanya kazi ukiwa nyumbani kwa wale wanaoweza, kataa mgusano wa aina yeyote na watu na epuka sehemu za mikusanyiko.

Mwisho kabisa, ili kuwasaidia wajawazito kuwa na ujauzito wenye afya na kinga ya mwili nzuri katika kipindi hiki, ni vizuri kuzingatia mlo bora wenye madini chuma kwa wingi (kama mboga za majani zenye kijani kilichokolea, samaki na mayai) na madini ya foliki ambayo yanapatikana kwenye maharage, kunde, maharage ya kijani n.k. Bila kusahau vidonge vya vitamini vya kila siku ulivyoandikiwa na daktari wako vinasaidia pia.

Je, ninaweza kumpatia mtoto wangu Virusi vya Corona?

Je, kuna uwezekano wa mama mjamzito aliyepata maambukizi ya Virusi vya Corona kumpatia mtoto anayeendelea kukua ndani ya mwili wake?  Hili ni moja ya swali linalowaumiza wajawazito wengi na familia zao.

Ukweli ni kwamba kuna maambukizi mengi ya virusi, bakteria na fangasi ambayo yanaweza kupatiwa mtoto kipindi cha ujauzito, kama vile Virusi vya Ukimwi, Homa ya Manjano, Tetekuwanga, Rubela na Toxoplasmosis (maambukizi yanayosababishwa kwa kula nyama isiyopikwa vizuri na iliyogusana na kinyesi cha paka).

Hakuna ushahidi unaoonyesha Virusi vya Corona vinaweza kumpata mtoto aliye tumboni kama mama mjamzito anayo maambukizi. Ila kwa sababu virusi hivi ni vipya wanasayansi wanaendelea kuusoma ugonjwa huu taratibu na tutegemee taarifa zaidi hapo mbeleni.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la kujitegemea la Kidaktari liitwalo “The Lancet” ambalo liliwafuatilia wanawake 9 waliopatikana na maambukizi ya virusi hivi baada ya kufanyiwa vipimo nchini China, waligundua hakuna mtoto hata mmoja aliyezaliwa na maambukizi haya (ikumbukwe wanawake hawa wote walijifungua kwa njia ya upasuaji). Ijapokuwa idadi ni ndogo ila inatia matumaini.

Pia hakuna ushahidi ulioonyesha kulikuwa na virusi ndani ya kimiminika cha amnion “Amniotic fluid” hichi ni kimiminika kinachomzunguka na kumlinda mtoto wakati wa ujauzito. Pia hakuna ushaidi uliopatikana ndani ya sampuli za damu zilizochukuliwa kutoka katika kitovu cha kila mtoto. Hali hii inaweza kupendekeza kujifungua kwa njia ya kawaida kwa mjamzito aliye na maambukizi ni njia salama, lakini hatuna majibu ya uhakika kuhusu hili kwasababu idadi ya tafiti zilizofanywa ni ndogo sana.

Kwa tafiti zote hizi inaonyesha kuna ushahidi kidogo kuwa watoto wanaweza kupata maambukizi ya virusi hivi kutoka kwa mama zao wakati wa ujauzito.

Je, ninaweza kumpatia mtoto wangu maambukizi kwa njia ya kunyonyesha?

Hakuna uwazi wa kutosha katika suala la maziwa ya mama, hata hivyo hatuwezi fanya hitimisho kama maziwa ya mama yanabeba virusi au la!

Baadhi ya virusi, kama virusi vya UKIMWI vinajulikana kuenezwa kwa njia ya maziwa ya mama, lakini mpaka tulipofikia hakuna ushahidi kuwa Virusi vya Corona COVID-19 vinaweza kuenezwa kwa njia hii pia.

Ushauri uliopo ni kuwa wamama ambao hawana maambukizi haya waendelee kuwanyonyesha watoto wao ila wakumbuke kunawa mikono yao vizuri kabla na baada ya kuwanyonyesha.

Ikiwa mama ataonekana na dalili za kukohoa au joto kubwa la mwili, ni vizuri atumie njia mbadala ya kunyonyesha (mf: vifaa maalumu vya kukamua maziwa) na kumpatia mtu mwingine asiye na maambukizi kumlisha mtoto mpaka atakapo pona.

Kuna ushahidi wa kutosha kuwa maziwa ya mama ni mazuri kwa kuongeza kinga mwili ya mtoto, hivyo kusitisha moja kwa moja kumnyonyesha mtoto wako kunaweza kumuweka katika  hatari ya kupata maambukizi kwa urahisi.

Kadiri muda unavyokwenda, haitaepukika na tutarajie kushuhudia wanawake wengi wajawazito wakipata virusi vya corona COVID-19, hii itapelekea wanasayansi kuweza kutambua zaidi jinsi kirusi hiki kinafanya kazi na ni kwa namna gani kinamuathiri mjamzito. Kwa sasa kuchukua hatua za kujikinga ni muhimu – kuosha mikono kwa maji tiririka, kuepuka kukaa karibu karibu sana ikiwemo kuepuka maeneo yenye mikusanyiko ya watoto, kukaa nyumbani, kuepuka wageni ni njia zinazohitaji kufuatwa kuweza kuwa salama.

 

IMEPITIWA: 19 MARCH 2020

 

 

Kwanini chunusi hutokea na namna ya kupambana nazo

Chunusi ni nini?

Chunusi ni ugonjwa wa ngozi unaowaathiri watu wengi katika kipindi fulani cha maisha yao. Ugonjwa huu husababisha vipele vidogo vidogo vya mafuta kwenye ngozi na wakati mwingine hufanya ngozi kuwa na maumivu au kuhisi kuungua. Viupele hivi hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinapozibwa kwa mafuta na seli za ngozi zilizokufa au wadudu yaani bakteria. Mara nyingi chunusi hutokea usoni, mgongoni, kifuani na shingoni. Chunusi huwaathiri takribani asilimia 80% ya watu wenye umri kati ya miaka 11-30. Ugonjwa huu hutokea zaidi wasichana kuanzia miaka 14-17 na wavulana kuanzia miaka 16-19.

Jinsi gani chunusi hutokea?

Kawaida ngozi ina vishimo vidogo vidogo vya kutolea jasho,mafuta na seli zilizozeeka kutoka ndani ya mwili. Katika ngozi pia kuna tezi ya mafuta iitwayo ‘sebacous gland’ inayotoa mafuta yaitwayo sebum. Uzalishaji wa sebum nyingi na seli za ngozi zilizokufa husababisha kuziba kwa vishimo vidogo vidogo vya ngozi vinapitisha jasho katika ngozi na kusababisha kuvimba na mara nyingine kujaa kwa usaa na kusababisha chunusi. Licha ya hayo chunusi pia huchangiwa na sababu nyinginezo kama:

 • Mabadiliko ya homoni
 • Bakteria
 • Matibabu
 • Kizazi(genetics)

Jinsi gani ya kupambana na chunusi?

Kuna njia nyingi za matibabu za kupunguza chunusi zikijumuisha kubadili hali ya maisha, taratibu na dawa. Kula kabohidrati chache na zinazomeng’enywa kwa urahisi, kama vile sukari, kunaweza kusaidia. Usijaribu kuviminya au kuvisugua kwa nguvu viupele kwasababu hufanya ngozi kuuma na kutengeneza makovu ya kudumu. Jiepushe kutumia manukato au vipodozi kwenye ngozi yenye chunusi. Tumia bidhaa za urembo zisizoziba matundu madogo madogo ya ngozi yako.

Chunusi pia huweza kutibiwa kwa matumizi ya tiba asili kama matumizi ya matunda na viungo kama vitunguu swaumu, mdalasini na vingine. Hii ni njia nzuri ya kupatia ngozi unafuu na tiba mbadala na rafiki kwa ngozi yako. Zifuatazo ni baadhi ya tiba asili za chunusi na salama kwa ngozi yako:

Mdalasini wa unga na asali.

Kwa wale ambao wanasumbuliwa sana na chunusi iwe, usoni, kifuani, mgongoni n.k wanaweza tumia mchanganyiko mzuri wa asali na mdalasini wa unga kwa kupaka angalau mara moja kwa siku. AsaliI na mdalasini  zinasaidia kuponyesha kwasababu zina tabia za ANTI-BACTERIAL (zinaua na kuzuia mazalia ya bacteria) Jinsi ya kufanya:

 1. Chukua vijiko vitatu (3) vya chai vya asali
 2. Chukua nusu kijiko cha chai cha mdalasini wa unga safi
 3. Changanya pamoja kupata uji uji mzuri
 4. Paka sehemu yenye chunusi na kisha kaa nayo kwa angalau dakika 10-30 kisha osha kwa maji ya uvuguvugu.

ANGALIZO: MDALASINI unaweza kuwasha kwenye ngozi hivyo unashauriwa ujaribu kupaka kidogo kwenye kiganja cha mkono kwanza ili kupata uhakika kua haitakusumbua.

Matango:

Unaweza kutumia tango kwa kuondoa chunusi na hata kuondoa mabaka mabaka katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuonekana yenye afya na yenye kuvutia. Matango ni mazuri sana kwa kusafishia uso na haswa ukiwa na chunusi. Kata tango na kisha liponde ponde (unaweza kutumia blenda) kisha paka au kandika usoni. Acha likae kwa muda wa dakika 15 hadi 20 hivi, kisha suuza kwa maji baridi. Unaweza kurudia kwa siku mara mbili mpaka mara tatu hadi utakapopona.

Asali:

Matumizi ya asali kutibu chunusi huwezesha ngozi, iwe na afya na nyororo. Kwa sababu kwenye asali kuna virutubisho vingi vyenye kazi ya kuua vimelea (bacteria) na kuzuia uchafu na kusinyaa kwa ngozi. Weka asali kidogo sehemu ilio athirika na iache kwa muda mrefu kadri uwezavyo. Vilevile unaweza kupaka uso mzima au hata mwili mzima ukitaka. Sababu asali inarutubisha ngozi ya mwili na kuifanya iwe na afya na mwonekano mzuri. Ukisha ridhika na muda wa asali kwenye ngozi yako unaweza kusafisha kwa kutumia maji ya vuguvugu.

Papai:

Unaweza kushangaa, lakini matumizi ya papai yameonyesha matokeo mazuri sana katika kuondoa chunusi usoni na kusafisha sehemu zingine za mwili. Ponda ponda kiasi kidogo cha papai na upakae sehemu yenye chunusi, kisha liache kwa muda mrefu kadri uwezavyo. Ukisha ridhika na muda unaweza kujisafisha kwa kutumia maji ya kawaida. Unaweza kurudia mara kadhaa kila siku kama unataka.

 

Imepitiwa: Feb 2018