Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Mba wa nywele na matibabu yake

Mba ni nini?

Mba katika nywele ni ugonjwa wa ngozi unaowapata watu wengi. Hali hii husababisha kuwepo kwa vipande vidogo vidogo vyeupe vya ngozi kama ukurutu, ambavyo huweza kukudhalilisha. Usiwe na shaka! Tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa matunzo mazuri ya ngozi na kichwa.

Kisayansi, kawaida ngozi hujimenya seli za ngozi ziliyozeeka, na hizi seli hupotea bila kugundulika. Vipande vidogo vya mba vinasababishwa na ongezeko la seli za ngozi katika kichwa, ongezeko hili husababisha pia ongezeko la seli za ngozi zilizozeeka kutolewa. Seli hizi zikikutana na mafuta kwenye nywele na kichwa, pamoja zinaonekana na kufanya mba.

Utagunduaje una mba kichwani?

Kubanduka kwa ngozi ya kichwa kwa kasi ni moja ya dalili ya mba katika kichwa chako. Kubanduka huku kwa ngozi kuna ambatana na kuwashwa kwa ngozi ya kichwa, ambapo inapelekea kuwepo kwa vipande vidogo vidogo vyeupe vya ngozi(ukurutu) kwenye kichwa, nywele na mabega.

Aina za mba wa kichwani

Mba katika kichwa ni hali inayowakuta watu wengi katika jamii zetu. Kuna aina mbili za mba katika kichwa:

  • Mba wa kawaida/ wastani aina hii inaweza kutibika kwa matumizi ya shampoo, na tiba asili za kutengeneza nyumbani kama vile mafuta ya nazi na juisi ya alovera.
  • Mba mkali au uliokithiri, aina hii ya mba katika kichwa inaambatana na kuwashwa kwa kichwa, kuvimba na uwepo wa mba wenye urefu sawa na nyweleza kichwani. Mba katika hatua hii unaweza kutibika kwa dawa zilizoshauriwaa na wataalamu wa afya.

Mba kichwani unasababishwa na nini?

Hakuna chanzo maalumu kinachojulikana cha mba katika kichwa, ila zipi sababu ambazo zinatajwa na watu kuwa vyanzo vya mba kichwani. Miongoni mwa visababishi vya mba katika kichwa ni kama:

Chakula: Ulaji wa vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi nyingi unaweza kusababisha mba kichwani. Pia ulaji wa vyakula vyenye maziwa vinaweza kuchangia kuwepo kwa mba kichwani.

Usafi: usafi duni wa kichwa na nywele ni moja ya sababu za kuwa na mba kichwani, ni vema kusafisha kichwa na nywele mara tatu mpaka nne kwa wiki.

Vyanzo vingine vya mba kichwani vinatajwa kuwa:

  • Msongo wa mawazo
  • Mabadiliko ya homoni
  • Utumiaji wa vipodizi vya nywele sana kama vile jeli za kulaimisha nywele.
  • Kuwa na ngozi ya mafuta sana au kavu sana
  • Kurithi kutoka kwa mzazi.
  • Utumiaji wa hali ya juu wa “chlorinated swimmimg pools”.

Matibabu ya mba wa kichwani

Mba unaweza kupotea ghafla bila matibabu au unaweza kuhitaji kutunza kichwa na nywele kwa kutumia shampoo iliyo na dawa. Mara nyingine mba katika kichwa unaweza kuchukua wiki nyingi kutibika. Baadhi ya matibabu ya mba wa kichwani yanaweza kuwa ya tiba asili au tiba ya kisasa. Inashauriwa zaidi kutumia tiba ya asili kutibu mba wa kichwani, mojawapo wa tiba hizo za asili ni kama:

Matumizi ya mafuta yakupika nyumbani ya nazi na juisi ya kutengeneza ya alovera. Juisi ya alovera inaweza kutumika kama shampoo ya kuosha kichwa na nywele na mafuta ya nazi kwaajili ya kulainisha ngozi na nywele.

Matumizi ya juisi ya limao, juisi ya kimao ina asidi ya citric inayoweza kushambulia fangasi zinazosababisha ukurutu wa ngozi ya kichwa na pia inasaidia kupandisha juu ngozi zilizokufa juu na kuweza kuzisafisha kwa urahisi. Kamua limao na upate juisi ambayo itatumika kusugua kichwani kisha suuza na maji,fanya hivi kila ukitaka kuosha nywele.

Utajikinga vipi usipate mba wa kichwani

Ni vema kchukua hatua ili kuzuia mba kichwani ili usifikie hatua ya hatari zaidi, yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayoweza kufuatwa ili kupunguza au kutokomeza kabisa mba kichwani:

  • Kula kawaida, mlo wenye afya ulio jumuisha matunda na mbogamboga kwa wingi. Punguza vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi kwa wingi.
  • Safisha kichwa na nywele zako walau mara tatu mpaka nne kwa wiki, na suuza kwa maji mengi.

Jaribu tiba asili kwa nywele zako kama mafuta ya kupika nyumbani ya nazi pamoja na juisi ya alovera kutibu nywele zako.

Imepitiwa: Feb 2018

Ugonjwa wa Kichocho

Kichocho ni nini?

Kichocho ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo midogo aina ya Schistosoma au Bilhazia. Minyoo ambayo huingia katika mwili wa binadamu kwa njia ya vitundu vya ngozi na kusababisha mwasho katika viungo mbalimbali vya mwili. Hivyo kupelekea homa, mwili kudhoofu, kupungukiwa kinga mwilini na hatimaye mtu kupoteza maisha.
Pamoja na binadamu kuonekana kuugua ugonjwa wa kichocho pia wanyama wafugwao kama vile Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo hupatwa pia na ugonjwa huu wa kichocho wanapotumia maji yaliyo na vijidudu vya maradhi hayo.

Kichocho kinaenezwaje?

Minyoo aina ya Schistosoma ambayo hueneza Kichocho cha mkojo hasa kwa binadamu inatokea katika Konokono waishio katika maji. Kichocho cha mkojo kwa binadamu husambazwa na konokono wajulikanao kama Bulinus africanus, Bulinus tropicus na Bulinus forskalli, konokono hawa pia husambaza kichocho cha ng’ombe. Kichocho cha matumbo cha binadamu husambazwa na konokono waitwao Biomphalaria pfeiferi.
“Schistosoma lava wakiwa katika maji hutoboa ngozi ya binadamu au mnyama aliyeingia katika maji hayo na kuingia hadi kwenye mishipa ya damu mpaka kufika kwenye maini ambapo hapo hubadilika na kuwa minyoo ambayo itaendelea kukua na kuelekea katika sehemu mahsusi ya mwili ambapo minyoo wakubwa hukaa ” anasema Dkt. Jahashi Nzalawahe kutoka idara ya Vetenari Microbaiolojia na Parasaitolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.

Aina za kichocho

“Kuna aina kuu mbili za kichocho ambazo ni kichocho cha mkojo na kichocho cha tumbo, Kichocho cha mkojo (Urinary schistosomiasis) husababishwa na minyoo inayoitwa Schistosoma haematobium ambao huishi katika mishipa ya damu ya kibofu cha mkojo cha binadamu na Kichocho cha matumbo (Intestinal schistosomiasis) ambacho husababishwa na minyoo iitwayo Schistosoma mansoni ambao hupatikana katika mishipa ya damu ya utumbo”
“Dalili kuu za Kichocho cha mkojo ni kuwepo kwa damu katika mkojo, kujisikia hali ya mwili kuchoka, kuwa na kikohozi kikavu na maumivu ya misuli, pia dalili za Kichocho cha tumbo ni kuharisha kinyesi chenye damu, maumivu ya tumbo na kuvimba tumbo” anaeleza Dkt. Nzalawahe.
Kama nilivyoeleza awali Kichocho huwapata binadamu pamoja na wanyama wafugwao kama Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo kiitwacho (Bovine Schistosomiasis) ambacho husababishwa na minyoo iitwayo Schistosoma bovis waishio katika mishipa ya damu ya utumbo wa wanyama na kupelekea mnyama kupunguza hamu ya kula, kuharisha damu, upungufu wa damu, mnyama kukonda na asipopata tiba mnyama hufa.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kichocho.

Ugonjwa wa kichocho unaweza kuzuiwa kwa urahisi iwapo kanuni za kiafya zitazingatiwa. Hata hivyo hadi sasa hakuna chanjo iliyopatikana ya kudhibiti ugonjwa huo. Si maji yote ni salama kwenye maeneo yaliyo na ugonjwa huu. Sehemu hatari zaidi za ugonjwa huo ni maeneo kama vile kingo za maziwa, mito na mabwawa ambapo maji yametuama na kuna uoto wa mimea. Sehemu salama ni kama vile katika fukwe za bahari na zile zenye mawimbi ambazo si rahisi kukuta konokono wa majini. Mabwawa ya kuogelea ni salama iwapo yatanyunyiziwa dawa ya klorini.

1. Kuacha kujisaidia haja kubwa au ndogo kwenye mabwawa, mito, maziwa na mifereji ya maji. Kwa mtu mwenye kichocho (cha mkojo (Bilhazia) anapokojoa mkojo hutoka na mayai ya kichocho, na kwa kichocho cha tumbo, haja kubwa huwa na mayai ya kichocho ambayo huanguliwa mara tu yanapogusana na maji na vijidudu vilivyo anguliwa huingia mwilini mwa konokono na kuendelea kukua, baada ya wiki tano hutoka na kurudi kwenye maji, ambako huogelea kutafuta mtu aliyepo ndani ya maji na huingia kwenye mwili wa mtu kupitia kwenye ngozi.

2. Kuacha kuoga, kuchota, kufua nguo kwenye maji yaliyotuama kama vile katika mabwawa, mito, maziwa na mifereji ambayo mingi inakuwa na konoko wanaosambaza kichocho. Badala yake watu wawekewe maji ya bomba ambayo huwekewa dawa za kuua vimelea vya maradhi.

3. Kuondoa majani yaliyoota kwenye maji sehemu ambazo watu huenda kuchota maji, kufua, na kuoga katika mabwawa, mito, maziwa, mifereji lengo likiwa ni kuharibu makazi ya konono.

4. Kusafisha mifereji ya umwagiliaji vizuri muda wote ili kupunguza uzalianaji wa konono, na bora zaidi ni kuijenga mifereji kwa mawe na sementi, ili kuharibu kabisa makazi ya konokono.

5. Kwa wakulima wanaofanya kilimo cha umwagiliaji yafaa wavae mabuti na gloves kujikinga na vijidudu vya kichocho kujipenyeza kwenye ngozi. Njia nyingine ni kunyunyizia dawa za kuua konokono kwenye maji (ziwa, mto, bwawa, mfereji), wenye konokono waenezao kichocho.

6. Bila kusahau maji ya kunywa yachemshwe na kuchujwa ili kuuwa vijidudu vya maradhi mbalimbali ikiwemo wadudu wa kichocho.

Ni vyema tujue kuwa, mtu anapaswa kumuona daktari baada ya kuwa na dalili za ugonjwa na yeye ndiye atakayemuainishia dawa za kutumia. Ni matarajio yetu kuwa iwapo tutafuata kanuni na misingi yote hiyo ya kiafya hapo juu, basi tutafanikiwa kushinda vita dhidi ya maradhi ya kichocho. Kwa kufanya hivyo maambuki ya kichocho yanawezwa kuzuiliwa na hatimaye ugonjwa huu kuweza kuteketezwa kabisa

Ugonjwa wa Malaria

Ufahamu ugonjwa wa Malaria

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyojulikana kama Plasmodium.Vimelea hivi huenezwa na mbu jike aina ya anofelesi (anopheles). Lakini watu wengi huelewa kwamba malaria husababishwa na mbu. Mbu huyu husaidia katika usambazaji tuu wa vimelea husika.

Aina ya vimelea ambavyo humdhuru binadamu kati ya vimelea vingi vya Plasmodium ni:
• Plasmodium Vivax
• Plasmodium Falciparum
• Plasmodium Malariae
• Plasmodium Oval

Plasmodium Vivax: Vimelea hivi havina madhara makubwa ingawa vimesambaa sana kuliko vile vya Plasmodium Falciparum.
Plasmodium Falciparum: husababisha vifo vingi na kwa haraka zaidi.
Vimelea vingine kama Plasmodium Malariae na Plasmodium Oval husababisha pia malaria lakini sio kwa ukali na yenye uharibifu kama vile vya Plasmodium Falciparum. Ukurasa huu umejizatiti zaidi kuzungumzia malaria inayosababishwa na Plasmodium Falciparum, kwani ndio inayotushambulia zaidi ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Jinsi mtu anavyopata maambukizi ya malaria

Vimelea (parasites) huingia kwenye mwili wa binadamu baada ya mbu jike aliyeathirika na vimelea hivyo vya malaria wakati akinyonya damu ya binadamu kama mlo wake, atamng`ata na kunyonya damu binadamu mwingine. Ni katika kipindi hiki ambapo mbu huweza kuviacha vimelea alivyovitoa kwa mtu mwingine na kumuathiri mtu huyu. Mbu huyu ana kawaida ya kumdhuru binadamu kwa kumng`ata kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.
Vimelea huzaliana ndani ya utumbo wa mbu na baadae husafiri hadi kwenye tezi za mate yake. Wakati mbu anamng’ata binadamu hutoa mate kama ganzi ili binadamu asigundue kama anang’atwa na hapo ndipo vimelea vya malaria humuingia binadamu.
Baada ya kuingia kwenye mwili wa binadamu vimelea hivi husafiri hadi kwenye ini ambapo huzaliana kwa wingi na hatimaye kuingia kwenye mzunguko wa damu na kusababisha uharibifu wa seli nyekundu za damu. Hapa ndipo mtu huanza kujihisi homa, kutetemeka na dalili nyinginezo za malaria.

Dalili za malaria

Dalili za malaria zinategemea mtu na mtu kutokana na nguvu ya kinga yake. Hata hivyo dalili zinazowapata wagonjwa wa malaria zinatokana na hatua ya ugonjwa aliyonayo mtu aliyeambukizwa.

Kuna aina mbili za malaria:
1. Malaria ya kawaida, isiyokuwa kali au sugu kitaalamu inaitwa “Uncomplicated Malaria”. Hii inakuwa haijasababisha madhara makuwa katika mwili.
2. Malaria sugu, kitaalamu “Complicated Malaria”. Hii imeishasababisha madhara kama kuharibu viungo muhimu mwilini kama, ubongo (kupoteza fahamu – cerebral coma), figo (figo kufeli-renal failure), ini (ini kufeli -liver failure), moyo (moyo kufeli – heart failure), mapafu (mapafu kufeli – pulmonary failure), upungufu wa sukari mwilini (hypoglycaemia). Na pia kuwa na vimelea vingi (hyperparasitaemia).

Dalili za malaria isiyo kali

1. Homa ikiambatana na maumivu ya kichwa
2. Maumivu ya mwili
3. Tumbo kuuma na kuharisha
4. Kichefuchefu na kutapika
5. Kizunguzungu
6. Kutokwa jasho
7. Kutetemeka
8. Kifua kuuma
9. Kukosa hamu ya kula

Dalili za malaria kali

1. Mabadiliko katika mwenendo na tabia (kuchanganyikiwa)
2. Uchovu mkubwa kupita kiasi (mgonjwa hawezi kukaa au kusimama)
3. Upungufu mkubwa wa damu (mgonjwa husikia kizunguzungu sana)
4. Kupoteza fahamu
5. Kupumua kwa shida
6. Degedege/mtukutiko mwili (Kwa watoto wadogo)
7. Kutapika kila kitu, kushindwa kunywa au kunyonya kwa watoto
8. Mzunguko hafifu wa damu, kutokwa damu isiyo ganda kwa urahisi
9. Figo kushindwa kufanya kazi na kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi/kahawia.

Kumbuka:

Malaria hushambulia zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5), wanawake wajawazito na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Hii ni kutokana na kinga zao za mwili huwa chini.

Hizi dalili pia hutokea katika magonjwa yanayoambukizwa na bakteria, kwa mfano:
Homa inaweza kuwa dalili ya UTI, Pneumonia, Typhoid, n.k
Kukohoa kunaweza kuwa sababu ya maambukizi katika mapafu mfano pneumonia, kifua kikuu n.k
Kutapika na kuharisha inaweza kuwa dalili za magonjwa ya maambukizi ya tumbo pia.

Hivyo ni vema ukipata dalili hizi usichukue dawa bila kupata uchunguzi wa kitaalamu na pia ushauri kutoka kwa madaktari. Unapopata dalili hizi wahi hospitali ili wataalamu wakuchunguze na kujua ni ugonjwa gani ulionao.

Matibabu ya Malaria

Kwa malaria isiyosugu/isiyokali, dawa inayopendekezwa kwa sasa kama tiba ya kwanza ni dawa ya Mseto (ALU), pia gonjwa anatumia dawa akiwa nyumbani kwake. Kutokana na dalili za mgonjwa huyu, inawezekana anaweza kula na kunywa vizuri na dalili nyingine pia sio za kushtua sana ndio maana mgonjwa hupewa vidonge na ushauri wa mlo na vitu vya kuepuka akiwa anatumia dawa za malaria, hususani bidhaa za pombe.

Kwa malaria sugu, matibabu yanayopendekezwa kama tiba kwa mgonjwa ni dawa ya Quinine kwa njia ya dripu. Pia mgonjwa anapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Mgonjwa analazwa hospitalini hadi anapopata nafuu na kuweza kula mwenyewe. Wagonjwa wengi wenye malaria kali au sugu, kutokana na hali yao ya kupoteza fahamu, kutapika kila kitu na kushindwa kula, pamoja na dalili zingine kama zilivyoorodheshwa hapo juu, ni vyema walazwe ili wapewe huduma stahiki.

Jinsi ya kujikinga na Malaria

Malaria ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa vifo nchini Tanzania. Ila ni ugonjwa ambao vilevile kwa maamuzi na bidii za binadamu ugonjwa huu unaweza kukwepeka. Hivyo basi, zifuatazo ni namna mbalimbali za kujikinga na malaria:

1. Kutumia chandarua kilicho wekwa dawa ya kuua mbu. Kutumia tu chandarua haitoshi. Ni muhimu kulala kwenye chandarua kilicho na dawa. Chandarua nyingi zinazouzwa madukani kwa muda huu zimeshawekwa dawa tayari, lakini unashauriwa kuuliza na kuwa na uhakika kuwa chandarua unachonunua kimewekwa dawa.

2. Kuweka mazingira safi kwa kufukia madimbwi na mashimo yasababishayo maji kutuama. Maji yanayotuwama huzalisha sana mbu. Mayai ya mbu hupendelea maeneo yenye majimaji lakini yasiyokuwa na kusogea (yaliyotuama), mfano madimbwi ya maji ya mvua yaliyokaa muda mrefu bila kukauka, unyevunyevu vichakani na kwenye nyasi ndefu, makopo yenye uwazi yaliyotelekezwa na kujaa maji ndani yake, magari mabovu yaliyonyeshewa mvua na kukusanya maji ndani, mabwawa madogomadogo kama ya kufugia samaki n.k. Hivyo ni vyema kufukia madimbwi, kufyeka nyasi, kuchoma au kusafisha makopokopo na magaloni na pia kuondoa magari mabovu na chochote kinachoweza kukusanya maji kwa muda mrefu kwa eneo lote linalozunguka nyumba yako. Ukifanya hivi utakuwa umesababisha hatua muhimu ya kisababishi cha malaria (mbu) asizaliwe.

3. Kuteketeza mazalia ya mbu kwa kunyunyuzia dawa ya DDT. Baada ya kufanikisha namba mbili hapo juu, na kuna sehemu ambazo mazalia ya mbu yanaweza kutokea na hakuna jinsi ya kuepuka maji haya yaliyotuama inashauriwa kunyunyuzia dawa ya DDT. Dawa hii ni sumu ambayo pia inaweza ikamdhuru binadamu. Hivyo shughuli ya kunyunyizia dawa hii hufanywa na wataalamu wa afya na mazingira.

4. Kufukuza na kuzuia kung`atwa na mbu. Ni ukweli kwamba pamoja na juhudi zote hapo juu bado kuna uwezekano wa kung`atwa nambu kwani tupo kwenye eneo la tropiki ambalo ndio makazi yao. Hivyo basi njia nyingine za ziada zinahitajika kujikinga using`atwe na mbu waliofanikiwa kuzaliwa.

Kuua mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba. Kuna baadhi ya kampuni wanafanya kazi ya kuua vimelea (fumigation) maeneo mbalimbali.
Kufukuza mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba (Ifahamike kuwa kuna dawa ambazo zina uwezo wa kufukuza pekee na kuna ambazo zinaua kabisa hivyo unavyonunua dawa dukani elewa unanunua dawa ya aina gani ili uitumie kama inavyoelekezwa)
Kuzuia mbu – Dawa za kupaka. Kwa wakati ambao haupo nyumbani inawezekana ukawepo kwenye sehemu yenye mbu, mfano baa, mpirani au hata kazini katika ule muda ambao mbu hung`ata, ni vyema ukajikinga nao kwa kujipaka dawa mbalimbali za kuwafukuza au kuwaua mbu pale wanapokukaribia au kuanza kukung`ata. Dawa hizi zinatoa harufu ambayosio rafiki kwa mbu hawa au zina uwezo wa kuwaua pindi wanapoanza kukuchoma.

5. Kujikinga na ugonjwa wa malaria kwa kina mama wajawazito ni muhimu. Wajawazito wana hatari kubwa zaidi ya kung`atwa na mbu kutokana na mabadiliko yao ya kimwili, mfano joto la mwili kuongezeka, hivyo mbu huweza kuwafikia kwa urahisi zaidi. Inapendekezwa na wizara ya afya kwamba wanawake wajawazito watumie dawa ya malaria aina ya “SP” kabla ya kujifungua. Hii itawasaidia kama kinga dhidi ya malaria kwao na kwa watoto wao tumboni. Dozi ya dawa hizi hutolewa katika vituo vya afya vinavyo toa huduma kwa mama na mtoto.

6. Ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za malaria kwa wagonjwa. Kuzingatia dozi sahihi inaweza ikawa kinga kwa maambukizi mengine yanayokuja. Vilevile kutokumaliza dozi kunamaanisha kuviacha baadhi ya vimelea mwilini ambavyo havikufa tayari mpaka kipindi ulipoacha dozi.

7. Usitumie dawa bila kumuona daktari kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaongeza usugu wa dawa mwilini mwako bila sababu ya msingi na pia unahatarisha maisha yako. Usugu wa dawa za malaria ni hatari na inamaanisha ukipata malaria na vimelea ulivyonavyo vimeshakuwa sugu kwa dawa zilizopo za malaria, maisha yako yanakuwa hatarini kwani madaktari watashindwa kukutibu.

Wito

Malaria ni ugonjwa hatari unaoua kwa haraka hivyo pindi unapohisi una dalili za malaria kama zilivyoorodheshwa hapo awali, wahi katika kituo cha kutoa huduma za afya kilichokaribu na wewe ili upatiwe uchunguzi na kupata tiba sahihi.

Imepitiwa: July 2017

Je Wajua: Saratani ya titi inatibika endapo itatambulika mapema

Saratani ya matiti ni nini?

Saratani ni aina ya ugonjwa unaosababisha ukuaji wa seli za mwili kubadilika na kukua bila mpangilio maalumu.

Saratani ya matiti hutokea kwenye titi ambalo kwa kawaida lina sehemu ya kutengeneza maziwa ijulikanayo kama “lobules” na aina fulani ya mishipa inayounganisha hizi lobules na chuchu za titi. Sehemu kubwa iliyobakia ya matiti inajumuisha mafuta na zile kitaalamu tunazoita “connective” na “lymphatic tissue”. Saratani ya matiti inayotokea kwenye “lobules” huitwa “lobular carcinoma” na ile inayotokea kwenye “ducts” huitwa “ductal carcinoma”.

Vihatarishi vya Saratani

Kuna mambo kadhaa ambayo yameonekana kuwa na uhusiano, ama wa moja kwa moja au kwa kupitia vitu vingine, wa kusababisha saratani ya matiti, au kumfanya mtu au kundi la watu kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huu kuliko wengine. Mambo hayo ni pamoja na:
Jinsia: Ingawa, saratani ya matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.
Umri: Uwezekano wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu. Kadiri umri wa mtu unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa mkubwa. Wanawake walio na umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa (mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45.
Uasili wa mtu (ethnicity): Saratani ya matiti hutokea zaidi kwa wanawake wazungu kuliko wanawake wa kiafrika au wenye asili ya afrika (weusi).
Uzazi: Wanawake ambao hawajazaa au kunyonyesha wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti. Wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 nao pia wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.
Historia ya ugonjwa huu katika familia: Wanawake walio katika familia zenye historia ya ugonjwa huu wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale ambao hawana historia ya ugonjwa huu katika familia zao. Kwa mwanamke aliye na ndugu (mama, dada au mtoto) ambaye aliwahi kupata saratani hii kabla ya umri wa miaka 50, uwezekano wa mwanamke huyu kupata ugonjwa huu ni mara mbili ya yule ambaye hana historia hii.
Umri wa kuvunja ungo: Wanawake wanaovunja ungo (kupata hedhi) kabla ya umri wa miaka 12 wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
Kuacha kupata hedhi: Kwa kawaida wanawake huacha kupata hedhi wafikapo miaka 45, hali ambayo kitaalamu hujulikana kama menopause. Wanawake wanaochelewa kuacha kupata hedhi, kwa mfano wale wanaoendelea kupata hedhi wakiwa na zaidi ya miaka 45, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya matiti.
Historia ya saratani ya matiti: Wanawake ambao wamewahi kupata ugonjwa huu kwenye titi la upande mmoja hapo kabla, wana uwezekano mkubwa wa kupata tena saratani kwenye titi la upande mwingine hapo siku za usoni.
Ulaji wa vyakula venye mafuta mengi: Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake wanaopendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
Kuongezeka uzito: Tafiti nyingine zimeonesha kuwa, wanawake wanene wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale wa uzito mdogo au wa kati.
Uvutaji sigara: Kuna matokeo yenye kukinzana kuhusu uhusiano wa uvutaji sigara na hatari ya kupata saratani ya matiti. Wakati baadhi ya tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya uvutaji sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti, tafiti nyingine zinaonesha majibu yenye kutofautiana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na saratani ya matiti. Hata hivyo, kwa ujumla, wanawake wanaojizuia kuvuta sigara wanakuwa na afya njema zaidi kuliko wale wanaovuta sigara.
Unywaji pombe: Imeonekana kuwa wanawake wanaokunywa pombe zaidi ya chupa moja kwa siku wana uwezekano wa kupata saratani ya matiti kwa asilimia zaidi ya ishirini.
Historia ya tiba ya mionzi: Wanawake ambao wamewahi kupata tiba ya mionzi hususani wakati wa ukuaji wa matiti, wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Hali hii husababishwa na ukweli kuwa mojawapo ya madhara ya mionzi ni kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya aina yoyote.
Matumizi ya dawa za kupanga uzazi: Kuna ushahidi kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya kupanga uzazi.
Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni mwilini: Kwa wale wanaotumia tiba ya homoni inayojulikana kama hormone replacement therapy, kwa sababu nyingine yeyote ile, au wale wenye kiwango kikubwa cha homoni kama vile oestrogen na progesterone mwilini mwao wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti.
Kuwa na matiti makubwa: Wanawake wenye matiti makubwa (dense breast tissue) wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti. Hali hii hutokana na ukweli kuwa wakati mwingine ni vigumu sana kwa madaktari kutambua kama wana saratani au la kutokana na ukubwa wa matiti yao.

Dalili za Saratani ya Matiti

Dalili ya awali inayoweza kutambulisha saratani ya matiti ni kuwepo kwa uvimbe kwenye titi ambao huwa na hali tofauti na sehemu nyingine za titi. Hata hivyo, si kila uvimbe kwenye titi unaashiria uwepo wa saratani ya matiti.
Uvimbe huu huwa mgumu, unaochezacheza kwenye titi, ambapo wakati mwingine unaweza kuwa na maumivu makali au kusiwe na maumivu yeyote. Uvimbe huu huwepo zaidi ya mzunguko mmoja wa hedhi kwa wale ambao hawajaacha kupata hedhi.
Dalili nyingine ni pamoja na:

  • kuwepo kwa uvimbe kwenye sehemu za kwapa
  • Sehemu ya titi kuingia ndani inayoashiria uvimbe usioonekana au usioweza kuhisiwa
  • Mabadiliko kwenye chuchu, kama vile chuchu kuzama ndani au kuwa na nundu ndogo ndogo, chuchu kuwasha, kuhisi kama kuchoma, kidonda kwenye chuchu au chuchu kuwa na kovu ambalo huashiria saratani ya sehemu hiyo
  • Kubadilika kwa umbo la titi, ngozi ya titi kuwa kama ganda la chungwa (peu de orange), ngozi kuwa na rangi nyekundu, na kuongezeka kwa joto kwenye titi. Dalili hizi huashiria kusambaa kwa saratani mwilini.
  • Dalili nyingine ni chuchu kutoa maji yasiyo ya kawaida ambayo hayana rangi. Aidha wakati mwingine, chuchu hutokwa damu au majimaji yenye rangi nyingine tofauti.
  • Ugunduzi wa Saratani ya Matiti

    Pamoja na mgonjwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na wataalamu wa afya kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, anaweza pia kufanyiwa vipimo vifuatavyo ili kusaidia kutambua ugonjwa huu.

  • X-ray ya matiti au Mammogram ambayo ina uwezo wa kuonesha ulipo uvimbe kwenye matiti
  • Ultra-Sonography ni kipimo kinachosaidia kutambua iwapo uvimbe uliopo ndani ya matiti umejaa maji ama la ili ufanyiwe vipimo zaidi
  • Kipimo kinachofanywa kwa kuchukua sehemu ya uvimbe (Aspiration) kwa kutumia aina fulani ya sindano (fine needle) na kisha kupeleka maabara sehemu iliyochukuliwa kwa ajili ya kutafitiwa zaidi ili kugundua uwepo wa saratani. Kwa kitabibu kipimo hiki hujulikana kama Fine Needle Aspiration and Cytology (FNAC)
  • Kipimo kingine ni upasuaji mdogo unaofanywa kwenye titi lililoathirika kwa ajili ya kuchukua sehemu ya titi (surgical biopsy) na kisha kuipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
  • Aidha kwa nchi zilizopiga hatua ya kimaendeleo, mgonjwa anaweza pia kufanyiwa vipimo kama:

  • PET Scan: Hii ni aina mpya ya kipimo ambacho kinahusisha CT Scan na PET kwa pamoja. Kipimo hiki kina uwezo wa kutambua uwepo wa saratani ya matiti, iwapo saratani hiyo imesambaa ama bado, na kama itakuwa imeshasambaa, basi ni sehemu gani ya mwili iliyoathirika.
  • Aidha kipimo hiki, kina uwezo wa kutofautisha tezi au lymph nodes zilizovimba zina uhusiano na saratani (Metastatic lymph nodes) au hazina uhusiano na saratani (Benign lymph nodes).

    Baadhi ya matabibu huwiwa ugumu kutofautisha kati ya kuvimba kwa tezi kunakosababishwa na saratani na kule kunakosababishwa na vitu vingine tofauti na saratani. Hali hii hutokea kwa wagonjwa wa saratani wenye tezi zilizovimba ambao hudhani kuwa kuvimba huko ni sababu ya saratani (metastatic lymph nodes).
    Kipimo hiki pia husaidia madaktari kuwatibu wagonjwa wa saratani kwa kutumia mionzi kwa usahihi zaidi ( Precise Radiotherapy) au kutumia mionzi inayolekezwa na kipimo hiki (PET Scan guided radiotherapy). Aidha, PET Scan huweza pia kutumika kuonesha maendeleo ya mgonjwa wa saratani baada ya kupata tiba ya mionzi (Radiotherapy) au dawa za kutibu saratani (Chemotherapy).

  • Kipimo kingine hujulikana kama DCE MRI (Dynamic contrast MRI). Hiki nacho ni kipimo kipya kwenye ugunduzi na tiba ya saratani. Aina ya kipimo hiki hutofautina na kipimo cha MRI ya kawaida kwani DCE MRI ina uwezo wa kutoa maelezo ya ziada namna uvimbe wa saratani unavyopata damu yake kupitia mishipa ya damu (blood vessels of the tumor) na hivyo kukua na kuongezeka zaidi. Uwezo mwingine wa DCE MRI ni kutoa maelezo mengine sawa na PET Scan.
  • Hata hivyo, vipimo hivi vya PET Scan na DCE MRI kwa sasa havipatikani nchini Tanzania.

    Tiba ya saratani ya matiti

    Upasuaji

    Lengo kuu la upasuaji ni kuondoa saratani kwenye titi pamoja na tezi (lymph nodes). Zipo aina kadhaa za upasuaji unaoweza kufanywa kwenye titi lililogundulika kuwa na saratani.
    Aina hizo ni pamoja na:

    Lumpectomy: Huu ni upasuaji unaofanywa kuondoa sehemu ya saratani pamoja na sehemu ya titi ambayo haijaathirika kwa saratani. Hii hufuatiwa na tiba ya mionzi (radiotherapy) kwa muda wa kati ya wiki 6 au 7. Mgonjwa anayefanyiwa aina hii ya upasuaji anakuwa na uwezekano wa kuishi muda mrefu sawa na anayefanyiwa upasuaji wa kuondoa titi lote lililoathirika.
    Simple au Total mastectomy: Ni aina ya upasuaji inayohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika kwa ugonjwa wa saratani.
    Radical mastectomy: Aina hii ya upasuaji uhusisha uondoaji wa titi lote na kundi la tezi liloathirika kwa saratani, pamoja na misuli ya sehemu za kifua (chest wall muscles). Hata hivyo, upasuaji wa aina hii ni nadra sana kutumika siku hizi.
    Modified radical mastectomy: Ni aina ya upasuaji inayohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika pamoja na kundi lote la tezi (lymph nodes) chini ya mkono (axilla) bila kuhusisha uondoaji wa misuli ya kifua.

    Kwa ujumla, lumpectomy na mastectomy, zote zinahusisha uondoaji wa kundi la tezi ambalo lipo karibu na uvimbe wa saratani (regional lymph nodes).

    Tiba ya mionzi

    Mionzi inaweza kutumika kuharibu seli za saratani zilizobaki kwenye matiti, kifua (chest wall), au/na eneo la chini ya mkono mara baada ya upasuaji kufanyika. Mionzi pia inaweza kutumika kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani kabla ya kufanyika kwa upasuaji.

    Tiba ya saratani kwa njia ya dawa (Systemic therapy)

    Tiba ya aina hii inahusisha matumizi ya kemikali maalum za kutibu saratani (chemotherapy) pamoja na matumizi ya homoni (hormonal therapy).
    Tiba kwa kutumia homoni (Adjuvant hormonal therapy) hutumika ili kuua seli za saratani ambazo hazikugundulika hapo awali na ambazo yawezekana zimesambaa sehemu nyingine za mwili. Tiba hii hutolewa baada ya kufanyika kwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani.
    Aina hii ya tiba hutegemea na ukubwa wa uvimbe, matokeo ya vipimo vya kimaabara vya saratani (histological results), na iwapo saratani imesambaa hadi kwenye tezi za kwenye kwapa la mgonjwa ama la. Tiba hii pia yaweza kutolewa kwa mgonjwa ambaye saratani imeshasambaa mwilini kwake kwa muda mrefu, na ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji.
    Baadhi ya kemikali zinazotumika kutibu saratani ya matiti ni cyclophosphamide, methotrexate, na flouracil. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa kujumuisha dawa 2 au 3 kwa wakati mmoja.
    Ieleweke pia kuwa, kama ilivyo kwa dawa nyingine za kutibu magonjwa mengine tofauti na saratani, kemikali (dawa) hizi za saratani pia zina madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara haya huletwa na ukweli kuwa, pamoja na kuwa kazi kuu ya kemikali hizi ni kuua seli zenye saratani, hutokea pia kuua na kuathiri seli za kawaida yaani zisizo na ugonjwa wa saratani kama vile seli zilizo kwenye mdomo, nywele, pua, kucha, utumbo na hata sehemu za siri za mwanamke.
    Hata hivyo, tofauti na seli za saratani, seli za kawaida huwa na uwezo wa kujizaa tena, kukua na kurudi katika hali yake ya kawaida wakati zile za saratani hazina uwezo huo.
    Madhara ya dawa hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.

    Imepitiwa: July 2017