Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Vifahamu vyakula bora, kupata ujauzito wenye afya

Ni Kipi hasa chakula bora kwa afya?
Kula kwa afya ina maanisha kupata vyakula tofauti tofauti kutoka katika makundi tofauti ya vyakula. Jaribu kujumuisha yafuatayo katika mli wako wa kila siku:

  • Angalau sehemu tano ya matunda na mboga za majani. Matunda na juisi ya mbogamboga na juisi laini(smooth) zianajumuishwa kwenye sehemu hizi. Kumbuka kwamba juisi zinakua na sukari nyingi hivyo basi jaribu kujizuia na kupata 150ml ya glasi kwa siku.
  •  Zingatia mlo wa nafaka zisizokobolewa na viazi, ambavyo vitakupatia wanga na kabohaidreti pamoja na fiba (fibre), pamoja pia na vitamin na madini kwa wingi yenye umuhimu. Hii inajumuisha mkate wa ngano isiyokobolewa, mchele wa kahawia, nafaka zisizokobolewa na tambi.
  • Jumuisha vyakula vya protini katika kila mlo, kama vile nyamana kitimoto, samaki, mayai na maharage. Jaribu kula angalau mara mbili samaki kwa wiki. Mojawapo ya samaki hawa awe wa mafuta, lakini jaribu kula sio zaidi ya mara mbili ya samaki hawa.
  • Baadhi ya vyakula vya maziwa vilivyo na kalsiamu, kama maziwa, mtindi na jibini. Lenga kula mara mbili mpaka tatu kwa siku. Kama uko makini kwenye idadi ya kalori, jaribu kuchagua vyakula vyenye kalori ndogo au zisizo na fati au sukari.
  • Baadhi ya vyakula vyenye wingi wa madini chuma kama nyama nyekundu,matunda, mkate, mboga za kijani na nafaka zisizokobolewa. Hizi hujenga wingi wa madini chuma na kukuandaa kwa ujauzito.
  • Jaribu kula chochote chenye vitamin C kama glasi ya juisi ya matunda, pamoja na vyakula vyenye wingi wa madini chuma. Hii itakusaidia kufyonza madini ya chuma kwa wingi kutoka kwenye vyakula vya tofauti na nyama.

Jipendelee mara moja moja kwa kula vyakula kama keki, tambi, vyakula vya kukaanga na mafuta(kuku na chips), vinywaji vya kiwandani kama juisi na soda. Vyakula hivi vina mafuta, sukari na chumvi kwa wingi. Vinaweza kukushibisha lakini sio vyakula vizuri vya lishe.

Hivyo basi ni vizuri ukajizuia kula vyakula kama hivi kwa wingi. Unaweza ukajiwekea ratiba ya kukuruhusu kula vyakula hivi siku za mapumziko na kula vya kula vya lishe bora wiki nzima, au kila ijumaa kujipendelea kwa kula chokoleti- au vile utakavyoamua wewe.

Kama bado unawaza lini kuanza kuboresha mlo wako, basi jua hakuna wakati mzuri kama sasa. Mlo wenye afya ni muhimu kabla na hata kipindi cha mimba.

Vipi kuhusu uzito wangu?
Jaribu kupata uzito wa kiafya zaidi kabla ya kujaribu kutafuta mtoto. Kinadharia, uzito wako wa mwili (BMI) unatakiwa uwe kati ya 20 mpaka 25. Kuwa na uzito mkubwa sana au pungufu sana kuna punguza uwezo wa wewe kushika mimba.

Uzito pungufu kabla ya kushika mimba kunahusishwa na hatari kubwa ya kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo au njiti. Watoto njiti wana hatari kubwa ya matatizo mbalimbali ya afya wanapoendelea kukua, hivyo basi kuongezeka uzito kidogo kwa sasa ni njia nzuri ya kumpatia maisha bora tangu mwanzo. Kama unapambana kuongeza uzito, muone mshauri wako wa afya anaweza kukupa ushauri wa kitaalamu zaidi.

Uzito mkubwa kabla ya kuzaa unahusishwa na hatari kubwa ya kupata matatizo kipindi una ujauzito. Wanawake wenye uzito mkubwa wana hatari kubwa ya kupata matatizo ya kiafya kama kisukari,shinikizo kubwa la damu na kuwa mwenye huzuni, kuharibika mimba.

Kula pungufu (dieting) haishauriwi kipindi cha ujauzito. Kupungua uzito kupitiliza inaweza kusababisha matumizi yote ya vitamins na madini ndani ya mwili wako, na kupelekea ukosefu wa vitamin na madini ya kutosha kwaajili ya ujauzito wenye afya. Ila kupungua uzito hatua kwa hatua, unaosababishwa na mazoezi na kula kwa afya ni njia nzuri, hivyo basi sasa ni muda muafaka kufanya maamuzi ya kula kwa afya na kudumu nayo mara unapopata mimba.

Mazoezi ni muhimu pia. Jaribu kujijengea mazoea yatakayo ufanyisha mwili kazi ya ziada, mfano kutemebea kwa miguu badala ya kutumia gari, kushuka kituo kimoja au viwili kabla na kutembea mpaka nyumbani au kutumia ngazi badala ya lifti. Ongea na mshauri wako wa afya kama unahitaji ushauri kuhusu ya kubadilisha mlo au kuanza mazoezi.
Kama una uzito mkubwa, jaribu kula kwa afya zaidi na vifuatavyo ni vidokezo vinavyoweza kukusaidia:

  • Kula kifungua kinywa kila asubuhi na jumuisha vyakula vya protini kama mayai na mtindi. Hivi vinakusaidia kuhisi kushiba mda mrefu na kuzuia njaa itakayo kufanya kula vitafuno visivyo na afya.
  • Zingatia kiwango cha chakula katika milo yako. Unaweza gundua kula kwenye sahani ndogo kunsaidia kuweka kiwango chako sawa mda wote.
  • Kula vyakula vyenye afya kama matunda. Kwa njia hii ulaji wa vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi utaepukika.

Je, niache pombe kwa sasa?
Pombe haiwezi kuathiri uzazi wako, ingawa kunywa sana kunaweza kuathiri manii ya mpenzi wako.Hata hivyo, kunywa kunaweza kuwa na hatari kwa ukuaji wa mtoto, hasa katika wiki za mwanzo. Kwa hiyo inapendekezwa kuwa wanawake wanapaswa kuacha kunywa pombe wakati wote wakijaribu kupata mtoto na wakati wa ujauzito.

Je, kahawa inaweza kufanya ugumu kwenye kupata mimba?
Hakuna ushahidi wazi kwamba kahawa husababisha matatizo ya uzazi ikiwa unatafuta mtoto kwa njia ya asili. Hakuna ushahidi wazi kwamba caffeine husababisha matatizo ya uzazi ikiwa unatafuta mtoto kwa kawaida. Hata hivyo, inaweza kuathiri nafasi yako ya mafanikio ikiwa unapokea matibabu ya uzazi wa kupandikiza kama vile IVF (In Vitro Fertilisation).

Mara baada ya kushika mimba,matumizi ya kahawa kwa sana yanaweza kuwa hatari kwa mtoto anayekua. Ili uwe katika usalama, unaweza kupunguza matumizi yako ya kahawa hadi 200mg kwa siku, ambayo ni salama wakati wa ujauzito.

Je, kuna kitu nahitaji kuwa makini katika ulaji au unywaji?
Wakati unapojaribu kumzaa, unaweza kupendelea kuacha vyakula vyovyote ambavyo si salama wakati wa ujauzito. Kwa njia hiyo, unapokuwa na ujauzito, utajua hakuna chochote ambacho kinaweza kumdhuru mtoto wako.

Vyakula vya kuepuka ukiwa mjamzito ni kama:

  • Vyakula vya vitamin A, kama maini
  • Epuka kula zaidi ya mara mbili samaki wenye mafuta kama salmoni (samaki wenye mnofu mwekundu), dagaa wa kigoma, kibua.
  • Jibini
  • Vyalula vyenye hatari kubwa ya sumu kama nyama mbichi, samaki, yai bichi na matunda na mbogamboga zisizosafishwa.

Utagunduaje kama mtoto anayenyonya anashiba

Je, Mtoto wangu anayenyonya anashiba?

Sheria ya kwanza ya kumnyonyesha mtoto ni kumuangalia na sio kuangalia saa. Ili kugundua kama mtoto anayenyonya anashiba ni vyema kujua ni vitu gani muhimu vya kuangalia. Kumuwekea mtoto ratiba ya kunyonya kunaweza kuwa hatari katika upatikanaji wa maziwa yako. Lakini kama utamruhusu mtoto wako kuamua muda gani na mara ngapi ananyonya, utakuwa na uhakika mtoto wako anapata maziwa ya kutosha na upatikanaji na usambasazaji wa maziwa yako kuwa imara. Kama mtoto wako amelala kwenye kifua chako upande mmoja wa bega, mbadilishe kuelekea upande mwingine. Ikiwa mtoto wako bado ana njaa, atakula zaidi. Ikiwa hana njaa, jiandae kwa ulishaji ujao.

Ishara zinazoweza kukujulisha mtoto wako anapata maziwa ya kutosha hujumuisha:

  1. Mtoto wako anapata choo kila siku baada ya kufikisha siku 4.
  2. Kinyesi cha mtoto wako kinabadilika kutoka nyeusi hadi kijani hadi manjano wakati kama anakunywa maziwa vizuri (na inapaswa choo kuwa cha njano baada ya siku 4)
  3. Mtoto wako anatakiwa abadilishe nepi 5-6 nzito zilizo loana kila siku baada ya siku ya nne.
  4. Mtoto wako anaongezeka gramu 112 – 196 kwa wiki baada ya kurejesha uzito wa kawaida wa kuzaliwa (kawaida ndani ya siku 10-14).

Watoto wote wana siku ambazo wananyonya sana na siku nyingine ambazo hawanyonyi. Hizi ni tabia za kawaida za unyonyeshaji na sio ishara kwamba kuna kitu sio sawa. Kwa kuangalia vitu hapo juu unaweza ukatambua kama mtoto anayenyonya anashiba. Pia kushiba kwa mtoto kunategemeana na upatikanaji wa maziwa kutoka kwa mama.

Homoni ya Prolaktini huzalisha maziwa. Ikiwa unanyonyesha mara nyingi, kiwango cha homoni ya prolaktini kitaendelea kukua na kuongezeka kwa wingi. Ikiwa itaongezeka sana na kuwa ya kiwango cha juu, utatengeneza maziwa mengi zaidi na mtoto anayenyonya anashiba na atapata uzito kwa urahisi. Kwa hiyo ni muhimu kuwa unamlisha mara nyingi.

Ikiwa haunyonyeshi mara kwa mara, kwa muda mrefu, ongezeko la homoni ya prolaktini litashuka. Hivyo ni bora kunyonyesha mara nyingi, yaani mara 8-10 katika masaa 24, na ukitumia karibu dakika 15-45 kwa mlisho mmoja.

Imepitiwa: 9/Jan/2018

Faida za kunyonyesha kwa mama aliyejifungua

Je ulishawahi kujiuliza kunyonyesha kuna faida gani kwa mama aliyejifungua? Kwa wanawake wengi waliojifungua, kunyonyesha huwa ndio njia pekee ya kumpatia mtoto virutubisho. Hii ina faida lukuki kwa mtoto. Ila kuna faida nyingi pia kwa mama anayenyonyesha ukilinganisha na yule atakayechagua njia mbadala ya kumpa mtoto wake virutubisho stahiki.

Kunyonyesha baada tu ya kujifungua huwa na faida zifuatazo:

1. Kuepusha kutoka damu kupitiliza baada ya kujifungua
Baada tu ya kujifungua mwili wa mwanamke hupitia mlolongo mrefu sana wa mabadiliko ya homoni. Mabdailiko haya ndio husaidia kurudi kwa mfuko wa mimba katika hali ya kawaida baada ya kujifungua pamoja na kukatika kwa damu. Kunyonyesha husaidia hali hizi kuwahi kufanikiwa kwa haraka zaidi. Kwani kunyonyesha ni kitendo kinachoenda kusisimua utoaji wa homoni zilezile ambazo ni msaada kwa mfuko wa mimba kujirudi na pia damu kukatika. Hivyo basi mama atakayeanza kunyonyesha mtoto wake baada tu ya kujifungua atashuhudia damu kukatika mapema na mfuko wa mimba kurudi kawaida kwa haraka zaidi.

2. Kunyonyesha kunaokoa muda na pesa
Kunyonyesha kunaokoa sana muda na pesa, kwani kitendo cha kunyonyesha hakihitaji muda wowote wa matayarisho kama vile ambavyo ungehitaji kutayarisha maziwa ya “formula”. Mama anaweza akanyonyesha muda wowote, wakati wowote bila kuhitaji kuwa na maji ya moto ya kuchanganya maziwa au purukushani za kusafisha vyombo vya kunyonyeshea kwa njia ya chupa. Lakini pia maziwa ya “formula” ni ya gharama sana na huhitaji kipato kinachoeleweka kuweza kununua maziwa bora ambayo yatakuwa sahihi na salama kwa mtoto wako.

3. Kuepusha hatari ya magonjwa mbalimbali
Kunyonyesha kunahusishwa na kupunguza hatari za kupata magonjwa ya mifupa kuwa laini na kuvunjika kwa haraka. Vile vile mama anayenyonyesha mtoto wake kwa muda unaotakiwa anajilinda pia na magonjwa ya mfumo wa uzazi na pia hatari ya kupata saratani ya titi hupungua kwa wanawake walionyonyesha.

4. Inasaidia kupunguza uzito
Kunyonyesha na yenyewe ni tukio ambalo linaushughulisha mwili, pia kutengenezwa kwa maziwa kunahusishwa na kutumika kwa virutubishi vya kutosha kutoka mwilini kwako. Hivyo kunyonyesha kunahusishwa vile vile na kupungua kwa uzito. Ila si vyema kutumia kunyonyehsa kama njia ya kupungua uzito kwani wakati wa kunyonyesha unashauriwa kula chakula bora na chenye virutubisho vya kutosha na kwa wakati muafaka ili kutengeneza maziwa ya kutosha kwa ajili ya mtoto.

5. Kuendeleza asili ya mzunguko wa kushika mimba, ujauzito na kuzaliwa mtoto.
Kama unanyonyesha, kuachiwa kwa homoni kwenye mwili wako zitakufanya uwe na mzunguko sahihi na salama wa kuweza kupata ujauzito mwingine, na kuzaliwa mtoto mwingine salama zaidi.

Mwisho kabisa kwa wiki chache za mwanzo kunyonyesha usiku inaonekana ni rahisi na yenye usumbufu kidogo kuliko wakati wa mchana.
Kunyonyesha kunakufanya mwenye furaha, pia kunyonyesha kunatoa homoni ambazo zinaongeza ujasiri, kujikubali na kupumzika na kusaidia kuongeza ukaribu wa mama na mtoto. Pia unaweza kusoma makala yetu nyingine kuweza kutambua ni kwa namna gani unaweza kufikia maamuzi ya kumnyonyesha mtoto wako au kutumia maziwa ya “formula”

Imepitiwa: 9/Jan/2018

Kunyonyesha au kutumia maziwa ya formula?

Kunyonyesha au kutumia maziwa ya formula, njia ipi ni bora kwa mtoto?

Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni njia mojawapo ya mafanikio makubwa kabisa ya kufanikisha na kuhakikisha afya ya mtoto. Kama kila mtoto akinyonyeshwa maziwa ya mama kwa ndani ya saa moja toka azaliwe, upewaji pekee maziwa ya mama kwa miezi ya sita ya kwanza katika uhai wa mtoto, na kuendelea kumnyonyesha hadi umri wa miaka miwili kutahakikisha mtoto anakua na afya bora. Huu ndio msingi wa kuimarika kiafya ya mwili na akili kwa watoto wote. Kitakwimu duniani, chini ya asilimia 40 ya watoto wachanga chini ya umri wa miezi sita hawapewi maziwa ya mama.

Ushauri nasaha wa kutosha kuhusu kunyonyesha na huduma ni vitu muhimu kwa ajili ya akina mama na familia katika kuanzisha na kudumisha zoezi hili la kunyonyesha.
Shirika la afya duniani lipo kikamilifu katika kukuza hali ya unyonyeshaji kama chanzo bora cha chakula kwa ajili ya watoto wachanga na watoto wadogo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza:

Kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza katika maisha ya mtoto. Katika miezi sita, vyakula, kama vile matunda kama parachichi, ndizi na mboga, lazima aanze kuwekewa ili kumsaidia katika kipindi anachokuwa akinyonya kwa muda wa miaka miwili au zaidi.

Aidha:
1. Kunyonyesha kunapaswa kuanza ndani ya saa moja baada ya kujifungua.
2. Kunyonyesha lazima kuwe “kwenye mahitaji”, kama mara kwa mara kama mtoto anavyohitaji iwe mchana ama usiku
3. Unyonyeshaji wa chupa hauna budi kuepukwa kadiri iwezekanavyo

Faida za Kunyonyesha

Kwa watoto wachanga
Maziwa ya mama ni chakula bora kwa watoto wachanga na watoto wakuao. Pia huwapa watoto wachanga virutubisho vyote wanavyohitaji kwa ajili ya maendeleo ya afya zao.
Maziwa haya ni salama na yana kinga ambayo husaidia kuwalinda watoto wachanga dhidi ya magonjwa ya kawaida katika utoto kama vile kuhara na homa ya mapafu (pneumonia), ambayo kimsingi ndio sababu kuu mbili za vifo vya watoto wachanga duniani kote.

Maziwa ya mama hupatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu (bure), ambayo husaidia kuhakikisha kwamba watoto wachanga hupata lishe ya kutosha.

Faida za muda mrefu kwa watoto
Kwa zaidi kuna manufaa kwa ajili ya watoto, kwani kunyonyesha maziwa ya mama inachangia kuwa na maisha yenye afya njema.

Vijana na watu wazima ambao walikuwa wananyonya maziwa ya mama walipokuwa watoto wana uwezekano mdogo sana wa kuwa na tatizo la unene na uzito uliopitiliza.
Pia huwa wako katika hali nzuri ya kutokupata uwezekano wa kuwa na aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari na vile vile katika kipimo cha akili huwa wako vizuri.

Faida kwa akina mama
Kunyonyesha pia kuna faida kwa mama. Kunyonyesha maziwa ya mama inahusishwa na njia ya asili kama njia ya uzazi wa mpango (Asilimia 98 huwasaidia katika miezi sita ya kwanza baada ya kujifungua katika kuzuia mimba).

Pia inapunguza hatari ya kupata saratani ya matiti na na saratani ya mifuko ya mayai (ovary) baadaye katika maisha, husaidia wanawake kurudi katika maumbile yao kama kabla ya ujauzito, na husaidia kupunguza viwango vya unene uliopitiliza.

Vipi kuhusu maziwa ya kopo au maziwa ya formula?

Maziwa ya kopo/formula kwa watoto wachanga huwa hayana kingamwili /antibodies ambayo hupatikana katika maziwa ya mama tu. Wakati ambapo maziwa ya kopo/formula hayakutayarishwa vizuri, kuna hatari inayotokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama na pia kutokuwa na vifaa vya kutakasia/kuondoa vijidudu. Hivyo kuwepo uwezo wa bakteria katika maziwa haya.

Utapiamlo pia unaweza kutokea ukisababishwa na uchanganyaji wa maziwa ya unga na maji mengi kuliko kipimo. Kama utaweka mazingira ya kumpa maziwa ya unga kila siku mara kwa mara siku zote, na ikitokia siku hayapo maziwa hayo, na ukawa huna budi kurudi katika kumnyonyesha maziwa ya mama, basi changua hilo halitakuwa sahihi kwa sababu kutakuwa na upungufu wa uzalishaji wa maziwa katika matiti ya mama kwa siku hiyo.

Kwa ushauri wa kisayansi ni vyema kukuchukua maamuzi ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama. Maziwa ya kopo/formula yatumike pale tuu kutakapokuwa na ushauri toka kwa mkunga au daktari kufanya hivyo.

Taratibu za kusimamia maziwa mbadala

Kanuni za kimataifa za kudhibiti masoko ya maziwa mbadala ilipitishwa mwaka 1981 ilikuwa na wito huu:

• Maandiko yote katika maziwa ya kopo/ formula na habari za kuelezea hali ya faida ya kunyonyesha maziwa ya mama na hatari ya afya ya maziwa mbadala/ yakopo au unga lazima zielezwe
• Si ruhusa kufanya matangazo ya maziwa mbadala /maziwa ya kopo ama unga kibiashara
• Si ruhusa sampuli yeyote ya maziwa mbadala kutolewa kwa wanawake wajawazito, mama au familia zao; na
• Si ruhusa kusambaza maziwa mbadala/maziwa ya kopo ama unga kwa bure au ruzuku kwa wafanyakazi wa afya au na vituo vya afya.

Unyonyeshaji sahihi

Unyonyeshaji una hitaji kujifunza na wanawake wengi wanapambana na magumu mengi sana mwanzoni wanapoanza hatua hii. Maumivu ya chuchu, na hofu kwamba hakuna maziwa ya kumtosheleza mtoto ni kawaida.

Vituo vya afya ambayo vinaunga mkono kunyonyesha hufanya mafunzo juu ya kunyonyesha sambamba na upatikana wa ushauri kwa mama wapya katika kunyonyesha. Hii huhamasisha viwango vya juu na uzoefu katika kunyonyesha.

Kutoa msaada huu na kuboresha huduma kwa akina mama na watoto wachanga, kuna hatua kadhaa zimetolewa kama”mama na mtoto” katika kliniki nchini kwetu. Katika mpango huu wa “mama na mtoto” ushauri na taratibu za unyonyeshaji hutolewa bure.

Kufanya kazi na kunyonyesha

Akina mama wengi ambao hurudi kufanya kazi makazini kwao wengi wao huacha kwa muda au kabisa kunyonyesha watoto wao. Sababu kuu ikiwa ni hawana muda wa kutosha, au mahali pa kukaa na kunyonyesha, hujieleza kwa kukosa kuhifadhi ya kusitiri maziwa yao.

Akina mama wanahitaji usalama, hali ya usafi na sehemu ya kujisitiri au sehemu ya karibu na mahali pa kazi yao ili waweze kuendelea kunyonyesha. Pia ili kumwezesha kuendelea na kazi zake, wengi wao hulazimika kuomba likizo ya kulipwa ya uzazi, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kwa ajili ya kutoa na kuhifadhi maziwa kutoka kwenye matiti.

Kumuanzishia mtoto chakula kigumu

Ili kukidhi mahitaji ya kuongezeka kwa watoto katika umri wa miezi sita, chakula kigumu lazima kiazishwe ili kusaidia ukuaji wake wa haraka kipindi hiki. Kwa wakati huu mtoto huyu anatakiwa aendelee kunyonya pia maziwa ya mama. Vyakula vya mtoto vinaweza kuwa vimetengenezwa mahsusi kwa ajili ya mtoto au inashauriwa viwe vinachukuliwa kutoka kwenye milo ya familia za watu wazima kwa kadiri inavyowezekana.

Wataalamu wa afya na vyakula wanasema ya kwamba:

• Kunyonyesha hakupaswi kupungua wakati unaanza kumpatia chakula kingine kigumu
• Mtoto apatiwe chakula akilishwa kwa kutumia kijiko, kikombe na sahani na sio kwatika chupa ya kunyonya.
• Chakula lazima kiwe safi, salama na mtoto alishwe katika mazingira safi.
• Muda wa zaidi na wa kutosha unahitajika kwa ajili ya watoto wadogo kujifunza kula vyakula vingine vigumu.

Imepitiwa: July 2017

Vifahamu vyakula bora na vile vinavyokatazwa kipindi cha ujauzito

Ni vyakula gani vya kuepuka kutumiwa na wajawazito?

Ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema pamoja na akili timamu, akiwa tumboni lazima alishwe lishe bora na mlo sahihi. Mwenye jukumu la kutoa lishe bora na sahihi kwa kiumbe kilichomo tumboni ni mama. Anatakiwa kujua aina ya vyakula anavyopaswa kula. Vivyo hivyo, anatakiwa kujua aina ya vyakula vya kuviepuka.

Katika makala ya leo, tunaangalia orodha ya vyakula vilivyokatazwa. Mama mja mzito haruhusiwi kuvila vyakula vifuatavyo kwa faida ya kiumbe kilichomo tumboni na kwa faida yake mwenyewe:

Nyama mbichi

Epuka kula samaki au nyama mbichi au iliyopikwa lakini haikuiva vizuri. Utajiepusha na uwezekano wa kula bakteria na vijidudu vingine hatari kwa afya ya mtoto tumboni. Mjamzito anapokula nyama, anatakiwa kuhakikisha imeiva sawasawa.

‘Soseji” na “Sandwich”
Mjamzito haruhusiwi kula ‘soseji’, ‘sandwichi’ za nyama na vyakula vingine vilivyotengenezwa kwa nyama. Inaaminika kuwa nyama zinazoandaliwa kwa ajili ya kutengenezea vyakula kama hivyo, huwa vimewekewa vihifadhi vyakula (preservatives) ambavyo vinaweza visiwe vizuri kwa afya ya mtoto.

Samaki wenye zebaki (Mercury)
Wajawazito wamekatazwa kula samaki wenye kiasi kingi cha madini ya zebaki. Ulaji wa zebaji kwa wajawazito umehusishwa na uzaaji wa watoto taahira. Mfano wa samaki hao ni pamoja na Papa, Chuchunge na dagaa wakubwa.

Mayai Mabichi
Ulaji wa mayai mabichi au vyakula vilivyochanganywa na mayai mabichi, mjamzito haruhusiwi kuvila. Kuna baadhi ya ‘Ice Cream’ na ‘mayonaizi’ hutengenezwa kwa kuchanganywa na mayai mabichi. Mjamzito amekatazwa kuvila vyakula hivyo.

Maini
Maini yana kiwango kikubwa cha madini aina ya chuma. Hata hivyo, yana kiasi kikubwa cha Vitamin A ambacho huweza kuwa na madhara kwa mtoto kikizidi.

Maziwa mabichi
Maziwa mabichi huweza kuwa na bakteria ajulikanae kama ‘Listeria’, ambaye huweza kusababisha kuharibika kwa mimba. Unapokunywa maziwa, hakikisha yamechemshwa au kama ni ya paketi hakikisha ni yale yaliyoandikwa‘Pasteurized’ na siyo ‘Unpasteurized’.

Kafeini (Caffeine)
Ingawa baadhi ya utafiti unaonesha kuwa unywaji wa kiasi kidogo cha kafeini hauna madhara, lakini kuna utafiti mwingine unaonesha kuwa unywaji wa kafeini una uhusiano na kuharibika kwa mimba. Kafeini ni aina ya kirutubisho kinachopatikana ndani ya kahawa.

Iwapo mjamzito atakunywa kahawa, basi anywe kiasi kidogo sana kisichozidi kikombe kimoja kwa siku. Kwa kawaida kahawa hukausha maji mwilini, hivyo unywaji wake husaidia kukauka maji mwilini ambayo ni muhimu sana kwa mjamzito.

Utafiti mwingine unaonesha kuwa kafeini inahusishwa pia na uharibikaji wa mimba, uzaaji wa watoto ‘njiti’ na watoto wenye uzito mdogo. Ni vizuri kunywa maji ya kutosha, maziwa na juisi na kuepuka kunywa vinywaji vyenye kahawa.

Pombe
Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa unywaji wa pombe kiasi kidogo wakati wa ujauzito hauna madhara, kwa maana hiyo matumizi ya pombe hayaruhusiwi kabisa wakati wa ujauzito, hata kama ni kidogo.
Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito huweza kuathiri ukuaji mzuri wa mtoto. Kutegemeana na kiasi atakachokunywa mjamzito, pombe inaweza kumsababishia mtoto ugonjwa hatari utokanao na pombe (Fetal Alcohol Syndrome).

Vyakula gani ni muhimu sana kutumiwa na wajawazito?

Lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana, kwani lishe hii hutumika kwa mama na mtoto anaendelea kukua tumboni. kwa kawaida mahitaji ya chakula na virutubisho mwilini mwa mwanamke huongezeka wakati wa ujauzito na kadri ujauzito unavyoendelea kukua, virutubisho hivyo hutumika kujenga mwili wa mama na mtoto. hivyo maamuzi ya lishe au lishe mama anayopata huathiri pia maendeleo ya mtoto anayekua mwilini mwake. tutaona vyakula muhimu vya kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baadhi ya vitu vya kukwepa.

Mlo kamili (balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini:

Nafaka na vyakula vya wanga
Vyakula hivi huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni. Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali(mahindi,mtama,ulezi n.k), viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili(whole grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa; cereals n.k.

Nyama, samaki na vyakula vya protini
Hivi ni muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha miwezi wa 4 mpaka wa 9 ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi, senene, panzi na wanyama wengine ; vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere, karanga,korosho n.k . Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya protini muhimu

Vyakula vya mafuta
Hutumika kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti,senene, panzi, samaki na matunnda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu(cholesterol) nyingi.

Mboga za majani na matunda
Matunda na mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na ufanyaji kazi wa mwili. Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini joto(Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni mwa mama.Vitamini B9 (Foliki asidi) na madini ya chuma hutolewa kama virutubisho ziada kliniki wakati wa ujauzito ili kutosheleza mahitaji ya mwili na kuzuia hatari ya upungufu wa damu kutokea.

Maji
Maji ni muhimu kwenye mmenyenyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI). Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.3 kwa siku, yanaweza kuwa katika chai, juisi, soda, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda.

Mfano wa mpangilio wa mlo

Ili kuhakikisha mlo kamili mjamzito anaweza kufuata mfano wa mpangilio wa mlo ufuatao. Katika mpangilio huu inashauriwa kuchagua aina moja ya chakula kutoka katika kila herufi A mpaka E ili kuweza kuupata mlo kamili.

Mfano:

Mlo wa Asubuhi:
A – Chungwa/ Embe/ Ndizi mbivu/ Parachichi
B – Mkate/ Maandazi/ Chapati/ Vitumbua/ Uji
C – Karoti
D – Mayai
E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya

Mlo wa Mchana:
A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na chungwa
B – Ugali/ Wali/ Ndizi/ Makande/ Tambi
C – Mchicha/ matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji
D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa
E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya.

Mlo wa Usiku:
A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na Chungwa
B – Wali/ Ndizi/ Viazi/ Tambi/ Chapati
C – Mchicha/ Matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji,
D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa
E – Maziwa/Mtindi/Siagi/Maziwa ya Soya.

Imepitiwa: July 2017