Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kumfundisha Mtoto Kujisaidia Mwenyewe

Kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe ni hatua moja uliyokua unaisubiria kwa hamu sana. Japo kuna baadhi ya watoto wanaelewa ndani ya siku chache, kumbuka inaweza kuchukua miezi michache mwanao kuzoea tabia hii, japo kuna changamoto  katika safari hii.

Angalia utayari wa mwanao kujifunza kujisaidia mwenyewe

Hakuna umri maalumu wa kuanza kumfundisha mtoto kujisaidia, kwasababu kila mtoto ni tofauti. Kwa kawaida wazazi wananza kuwafundisha watoto kujisaidia wenyewe kati ya miezi 18 na miaka mitatu. Watoto wengi wanaanza wakiwa kati ya miaka miwili na miaka miwili na nusu.

Usijisikie kumlazimisha mwanao mapema kwasababu ya maneno ya wazazi wengine au familia yako. Angalia ishara kutoka kwa mwanao kama yuko tayari na usianze kabla ya hapo.

Fanya maandalizi ya kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe

Nunua poti la mtoto na chupi mpya. Matumizi ya poti ni njia rahisi ya kuanzia kuliko kutumia choo. Ni rahisi kukaa na kunyanyuka na linaweza kusogezwa sehemu yeyote ndani ya nyumba. Unaweza kutumia picha za kufurahisha na DVD zinazoonyesha matumizi ya poti, ili kumuhamasisha mtoto kuwa tayari zaidi kutumia poti.

Andaa chupi na kaptula za kutosha ambazo zitakua rahisi kuvua na kuvaa. Uvaaji wa chupi una mpa moyo mtoto kutumia poti.

 

Kuwa na msimamo katika njia utakayotumia kumfundisha mwanao kujisaidia mwenyewe

Fanya mambo taratibu unapoanza. Mhamasishe mwanao kukaa kwenye poti mara moja kwa siku,baada ya kifungua kinywa au kabla ya kuoga au wakati anaopendelea kujisaidia.

Mkalishe mwanao kwenye poti baada ya kukojoa kwenye nepi. Hii itamsaidia kumhamasisha kuzoea poti na kukubali ni moja ya utaratibu wake.

Ikiwa hataki kukaa, ni sawa. Usimlazimishe kukaa,mvalishe nepi na weka poti pembeni kwa wiki kadhaa kabla hujajaribu tena.

Ikiwa atakubali kukaa kwenye poti baada ya wiki kadhaa ni vizuri. Ila usimlazimishe kukaa kwenye poti kama hataki. Msubiri mpaka atakapokua tayari na muelekeze anachotakiwa kufanya. Ukimlazimisha mtoto kama hataki atakasirika na kuwa mgumu kutaka kujifunza kutumia poti.

Unaweza kugundua wakati wa kiangazi ni muda mzuri wa kumfundisha mwanao kutumia poti, ikiwa unaishi mji wenye baridi kali na unyevu kipindi kirefu cha mwaka. Wakati huu wa kiangazi nguo zinaweza kufuliwa na kukauka mapema pale mtoto atakapojisaidia.

Wataarifu watu wote wanaobaki na mwanao wakati umeenda kazini juu ya mpango wako wa kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe, ili watumie mfumo huo.

Muonyeshe inavyofanyika

Watoto wanapenda kuiga. Mtoto akiona unatumia choo itamsaidia kuona umuhimu wa kutumia choo. Kama una mtoto wa kiume anza kumfundisha kukojoa kwa kukaa.

Muonyeshe jinsi ya kutumia poti, “toilet paper” au maji kutawaza na jinsi ya kupandisha chupi na suruali mara baada ya kumaliza, kisha kumwaga maji chooni/flash na mwisho kabisa kunawa mikono na kukausha kwenye kitamba kikavu.

Wakati mwingine utamsaidia mtoto kutawaza baada ya kujisaidia haja kubwa. Ila kukuona unafanya itamsaidia hatua kwa hatua kuzoea na kufanya mwenyewe hapo baadae.

Ikiwa mtoto wako ana kaka yake aua dada yake, au rafiki yake ambaye anaweza kujisaidia mwenyewe, akiona wanatumia choo, ataweza kukuza ujuzi wake wa kujisaidia mwenyewe kwasababu anaona jinsi inavyotakiwa kufanyika.

Mhamasishe zaidi, kama yuko tayari kukaa kwenye poti

Mtie moyo mwanao kutumia poti anaposikia haja.  Mpatie maji mengi na mkumbushe akae kwenye poti kila baada ya masaa machache. Lakini mkumbushe kuwa anaweza kukuambia anaposikia kujisaidia, na utamsindikiza kama anataka kujisaidia chooni.

Ukiweza  mruhusu kucheza bila nguo chini na weka poti karibu. Mwambie anaweza kutumia poti kila anapotaka.

Mtoto wako akifanikiwa kutumia poti vizuri mpatie pongezi nyingi, japo ataendelea kuwa na ajali nyingi katika safari hii, ataanza kuelewa kufanikiwa kujisaidia kwenye poti ni moja ya mafanikio.

Kukabiliana na ajali zinzotokea wakati wa kumfundisha mwanao kujisaidia mwenyewe kwa hali ya utulivu

Mtoto atapitia ajali tofauti kabla ya kufanikiwa kujisaidia mwenyewe usiku na mchana. Inaweza kuchosha na kukatisha tama lakini usimuadhibu au kumkasirikia. Kufuzu hatua hii itachukua mda. Akijisaidia pembeni, kwa hali ya utulivu safisha bila kumgombeza ila mkumbushe mara nyingine ajisaidie kwenye poti. Kisha mkalishe kwenye poti baada ya kusafisha na muonyeshe kuwa haja ndogo na kubwa “wee na poo” vinapaswa kuenda kwenye poti.
Ajali ni moja ya utaratibu mzima wa kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe. Lakini ikiwa ajali zitakua nyingi zaidi ya mafanikio, rudi kwenye matumizi ya nepi na acha kumfundisha matumizi ya poti kwa mda. Mwanao anaweza asiwe tayari.

Mafunzo ya kujisaidia mtoto wakati wa usiku

Inaweza kuchukua miezi mingi zaidi hata mwaka mwanao kufuzu kukaa mkavu wakati wa usiku. Hivyo basi,usitupe nepi kwanza. Mwili wake bado haujakua vizuri kumfanya aamke wakati wa usiku mwenyewe na kwenda chooni kujisaidia.

Wazazi wengi wanaanza kuwafundisha watoto wakiwa na miaka mitatu na minne. Unaweza kujaribu kabla ya umri huo,lakini hakikisha unaweka mpira wa kuzuia mkojo chini ya shuka au juu ya shuka.

Usimruhusu mtoto kunywa sana kinywaji chochote wakati wa usiku ili kupunguza nafasi za mtoto kukojoa kitandani wakati wa usiku. Mpatie maji ya kutosha wakati wa mchana kila anapo omba. Unaweza msaidia kwa kumkumbusha anaweza kukuamsha usiku kama atahitaji kujisaidia.

Jinsi ya Kumuhamasisha Mtoto Kukua Kimwili

Mazoezi na michezo ifuatayo kwa mwanao yatamsaidia katika ukuaji wa kimwili ni rahisi kujumuisha mazoezi haya katika utaratibu wa kila siku. Utagundua mwanao anakuwa imara na mwenye furaha.

 • Kupanda, kukwea kitu
 • Kuchora na kuandika haraka bila mpangilio kwenye karatasi
 • Kuvaa na kuvua nguo
 • Kujaza na kumwaga kwenye makopo yake ya kuchezea
 • Kufinyanga/unda na kubomoa
 • Kuvuta na kusukuma
 • Kuviringisha na kuendesha baiskeli
 • Kukimbia na kuruka
 • Kuogelea na kuchezea maji
 • Kurusha na kudaka

Jinsi Gani Nimfundishe Mtoto Kushirikiana na Wenzake

Utamfundishaje mtoto wa miaka miwili kushirikiana na wenzake?

Nini utarajie katika umri huu?

Katika umri huu mtoto wako ataonekana mbinafsi sana, atakua mkali pale ambapo mtoto mwenzake atachukua mdoli wake au kupiga kelele kama mgeni atashika mpira wake anaoupenda.

Katika umri huu watoto wengi hawapendi kushiriki na wengine japo anaweza kuwa na rafiki mmoja ambaye anaweza kumpa biskuti yake. Anaweza kucheza na watoto wengine kama utakua karibu yake sana ukimuangalia, lakini tarajia mikwaruzo ya mara kwa mara kati yao. Kushirikiana ni shughuli ya kujifunza hivo itamchukua muda  ni vizuri kumuelimisha faida za kushirikiana.

Nini ufanye ili kumsaidia mtoto wako kushiriki?

Mfundishe mchezo wa kupeana vitu

Unaweza kumsaidia mtoto wa kumfundisha michezo ya kupeana mfano mchezo wa kusukuma gari chini na kumpa naye asukume hii itamfanya apende michezo ya kupeana na kuelewa kuwa anapotoa vitu vyake haimaanishi kwamba hatavipata tena, mchukue mdoli wake pendwa na kumbusu kisha mpe naye ambusu.

Usimuadhibu mtoto wako

Kama utamwambia mtoto wako ni mbinafsi au kumuadhibu  ili kumlazimisha kushirikiana na wenzake haiwezi kumjenga katika kitendo cha kushirikiana na wenzake. Mshawishi katika njia chanya ili uweze kumjenga kiakili,ili akili yake inapokomaa ajue kushirikiana na rafiki zake ni vema zaidi kuliko kujitenga na vitu vyake.

Zungumza naye
Msaidie mwanao kuelezea hisia zake katika kushirikiana kwa mfano rafiki yake amechukua mdoli wake unaweza kumwambia “sofi anampenda sana mdoli wako anatamani amkumbatie kwa muda” msaidie na yeye kuelezea hisia zake pia, muangalie mtoto wako jinsi atakavyokua mwema anapocheza na wenzake pia muelezee inafurahisha kwa kiasi gani kushirikiana na wenzake.

Mpigishe hatua
Ikiwa kuna watoto wengine wanaocheza naye ni vyema kumwambia mtoto amuweke mbali yule mdoli wake pendwa asijekupotea kisha wahamasishe rafiki zake wanapokuja kucheza kila mmoja aje na vitu vyake vya kuchezea,ili kila mmoja awe na vitu vyake vya kuchezea,na kushirikiana  vitu walivyonavo.

Heshimu vitu vya mwanao
Kama mtoto wako atahisi umetoa nguo zake, midoli au kitu chake chochote kwa mtu mwingine anaweza kujisikia vibaya hivyo ni vema kumuomba ruksa na kuheshimu mawazo yake mpe uhuru achague yeye kusema ndio au hapana, hakikisha vitu vyake vinaheshimiwa na kuangaliwa vizuri.

Muongoze kwa mifano
Njia bora zaidi ni kumfundisha kwa mifano mtoto, hivyo shiriki naye “ice cream” yako, mpatie kitambaa chako avae muonyeshe kuvutiwa kuvaa kofia yake, tumia neno kushirikiana ili kuelezea kile unachokifanya. Kitu kikubwa na bora zaidi mfanye aone unavyochukua na kutoa kwa wengine.

Hatua za Ukuaji kwa Mtoto: Kutembea

Kujifunza kutembea ni moja ya mafanikio makubwa katika maisha ya mtoto, ni hatua kubwa katika maisha yake huru. Mara mtoto atakapoanza kutembea atakua mchunguzaji sana.

Lini mwanangu ataanza kutembea?

Katika mwaka wa kwanza wa mwanao, mwili wake na misuli yake inakuwa na nguvu zaidi. Atajifunza kukaa, kuviringika na kutambaa.

Mtoto wako ataweza kusogea kwa kujiinua. Kati ya miezi saba na mwaka mmoja ataweza kusimama kwa kushika vitu kwa mda mchache. Atapata shida kusimama mda mrefu,hivyo ataishia kudondoka na matako mara anapochoka.

Watoto wengi wanazunguka sana wakikaribia mwaka mmoja. Wanazunguka wakishika vitu kama samani na ukimshika mkono anaweza kutembea hatua chache. Watoto wengi wanaanza kutembea wenyewe wakifika miezi 12 na 17.

Jinsi gani mwanangu atajifunza kutembea?

Mchanga mpaka miezi miwili

Ukimbeba mwanao kwa kumsimamisha na kumshika kichwa chake, utahisi mwanao akijaribu kutumia miguu yake. Kwa sasa miguu yake haina nguvu ya kutosha kumsaidia kusimama.

Miezi mitano mpaka 10

Ifikapo miezi sita mtoto ataweza kuhimili uzito wake na kujiinua kwa kusimama. Ukimsimamisha kwenye mapaja yako ataanza kuruka juu na kutua,kuruka itakua shughuli yake anayoipenda katika umri huu. Ikiwa mwanao hajaweza kuhimili uzito wake kwenye miguu yake akifika miezi nane ongea na mshauri wako wa afya.

Mwanao anapoendelea kujifunza kujiviringisha, kukaa na kutambaa misuli yake inaendelea kunyooka.

Kati ya mwezi wa saba na miezi 12 mwanao atajitahidi kuinuka na kuanza kusimama akiwa anashika samani au mguu wako. Mwanao akianza kusimama vizuri ataanza kuzunguka kwa kushika vitu. Anaweza kuwa jasiri na kuachia na kusimama bila msaada. Mara baada ya mwanao kuwa tayari kuachia kushika samani ataanza kupiga hatua chache ukumshika mkono. Anaweza kuinama akitaka kuokota mdoli wake.

Mwaka mmoja

Mtoto wa mwaka mmoja anaanza kujaribu kukunja magoti na kujifunza kukaa chini baada ya kusimama. Hii ni hatua ngumu zaidi kuliko unavyofikiria.

Mwanao anaweza kuzunguka ndani ya nyumba, kusimama mwenyewe bila msaada na kupiga hatua chache. Lakini watoto wengine wanachukua muda mrefu zaidi kutembea. Kutembea ni jambo la kutatiza! Inahitaji usawa, uratibu na nguvu za misuli.

Mwanao atahitaji mazoezi mengi na atalega mwanzoni. Watoto wengi wanafanikiwa kutembea awali kwa kupanua miguu yao na vidole vyao kuelekezwa ndani au njee. Pia anaweza akaanguka sana.

Nawezaje kumsaidia mwanangu kutembea?

Unaweza kumsaidia mwanao kwa kumpa mazoezi mengi. Mtoto wako anahitaji kuweza kusimama, kutoka kwenye kukaa na kuzunguka kwa kutambaa kabla ya kuanza kutembea kwa ujasiri mwenyewe.

Unaweza kuhifadhi midoli yake mbali na yeye juu ya meza fupi, kwa kufanya hivi kutamsaidia kujivuta na kuifikia. Unaweza kufanya hivyo pia wakati akisimama ili kumpa motisha ya kusonga mbele na kuifuata.

Mwanao akianza kusimama anaweza kuhitaji msaada wa kushuka chini kukaa, hivyo basi mfundishe kukunja magoti ili aweze kukaa kwa urahisi zaidi.

Muhamasishe mwanao kutembea zaidi kwa kuchuchuma au kusimama mbele yake na kumshika mikono yake na kumsaidia kutembea kukuelekea wewe.

Unaweza mtengenezea kigari cha kujifunza kutembelea au kununua vya dukani kama unaweza, kitakachomsaidia kujishika na kusukuma.

Mruhusu mwanao ajifunze kutembea akiwa pekuu (bila viatu) na katika eneo salama(barazani) kama unaweza. Akitembea bila viatu itamsaidia kuimarisha usawa na uwezo wa kusogeza miguu yake kwa urahisi. Mtoto akibanwa na viatu au soksi huku anatembea hawezi kujinyoosha na kukua vizuri.

Hakuna haja ya kumvalisha mwanao viatu, mpaka atakapoweza kutembea kwa ujasiri nje mwenyewe.

Nawezaje kuhakikisha mwanangu anakua salama, sasa ameanza kutembea?

Mara mwanao anapoanza kutembea atazunguka haraka sana! Hakikisha kuna nafasi ya kutosha na sakafu ni tupu itamsaidia kutembea kwa urahisi. Hakikisha ana mazingira salama ya kujifunza kutembea. Hakikisha unaweka usalama ndani ya nyumba yako kama jikoni, bafuni na kwenye nyaya za umeme za televisheni au jokofu. Usimuache mwanao mwenyewe.

Vifuatavyo ni vidokezo vinavyoweza kusaidia nyumba yako ikawa salama kwa mtoto wako:

 • Kama hujatengeneza, weka milango ya usalama jikoni.
 • Hakikisha vitu hatarishi unavitoa kwenye droo anazoweza kufikia sebuleni au jikoni,kama kabati yenye visu,mikasi,dawa na sabuni za maji za kufulia na kudekia.
 • Funika kona zote zilizochongoka kama meza zilizo chini ili kumlinda mwanao asijiumize.

Je, ni sahihi mimi kuwa na wasiwasi mtoto wangu ana miezi 15, na hajaanza kutembea bado?

Watoto wanatofautiana uwezo, baadhi wanakua kwa haraka zaidi ya wengine. Baadhi ya watoto wanatambaa mapema na kuchelewa kutembea, wengine wanatamba na kisha kutembea, wengine hawatambai kabisa. Watoto kukua tofauti ni kawaida kabisa na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

Kama mwanao atafikisha umri wa miezi 18 na hajanza kutembea na una wasiwasi ongea mara moja na daktari au nesi.

Mara nyingi kasi ya mtoto wako kujifunza kusogea inarithiwa kutoka kwa wazazi wake. Ikiwa wewe au mwezi wako mlichelewa kutembea,kuna nafasi mwanao atafanya hivyohivyo.

Kumbuka kama mwanao alizaliwa kabla ya miezi 37 ya ujauzito, anaweza kufikia hatua hii ya kutembea kwa kuchelewa.

Je Mtoto Wako Anaonesha Hasira, Hamaki au Ghadhabu?

Kwanini mtoto wako ana hasira za kuhamaki?

Watoto wenye umri wa mwaka mmoja mpaka miaka mitatu wanakabiliwa na hali hii. Ni hali ya kihisia inayofananishwa na kimbunga wakati wa kiangazi. Dakika moja mwanao anafurahia biskuti yake na dakika mbili baadae analia, analalamika na kupiga kelele kwa sauti ya juu kwasababu biskuti yake imevunjika mara mbili.

Kuwa mvumilivu, mara nyingi watoto wanaokabiliana na hali hii wanakua wamekatishwa tamaa na kitu. Mtoto wako katika umri huu anasikia kila anachoambiwa lakini anakasirika pale anaposhindwa kujielezea anavyojisikia au anachotaka na kwasababu hii anavunjika moyo zaidi.

Jinsi ya kukabiliana na ghadhabu ya mwanao:

1. Usipoteze Uelekeo

Ghadhabu ya mwanao sio muonekano mzuri. Pamoja na kupiga mateke, kupiga kelele au kujiburuza sakafuni, ghadhabu ya mwanao inahusisha kutupa vitu, kujipiga na wakati mwingine kujiumiza kwa kubana pumzi yake. Mwanao akiwa katika hali hii ni vigumu kukusikiliza japo atakujibu kwa kupiga kelele na kukutishia.

Kaa na mwanao wakati wa matukio kama haya inaweza kumsaidia, kushuhudia ghadhabu ya mwanao inaweza kukushtua, lakini anaweza kujisikia salama akikuona uko karibu nae. Wataalamu wanashauri kumbeba mtoto na kumshika kama inawezekana. Wengine wanashauri kumpuuzia mwanao mpaka hasira zitakapoisha kuliko kutetea tabia hiyo mbaya. Kwa kujaribu na kukosea utajua mbinu gani ni sahihi kwa mwanao.

2. Kumbuka wewe ni mtu mzima

Usiwe na wasiwasi watu wengine wanafikiria nini- mtu yeyote ambaye ni mzazi alishapitia hili. Kubaliana na hali halisi. Mwanao atakuwa na wasiwasi kwa alichokitenda. Kitu ambacho hatafurahia kuona ni wewe umekasirishwa zaidi na jambo hili. Ikiwa hasira za mwanao zimefika hatua ya kupiga wenzake na wanyama(paka au mbwa kama unafuga), mtoe kwenye eneo la tukio mpeleke chumbani kwake, mwambie kwanini umempeleka chumbani kwake, na mjuze kwamba utakaa nae mpaka atakapoacha kuhamaki. Ukiwa sehemu yenye umati wa watu wengi kuwa tayari kuondoka na mwanao mpaka atakapoacha kuhamaki.

3. Ongea nae baadae

Anapomaliza kuhamaki, mshike mwanao na ongea nae kuhusu kilichotokea. Kuwa tayari kumuelezea unafahamu kwanini amefanya hivyo na utamsaidia kujifunza kuelezea anavyojisikia wakati mwingine.

4. Jaribu kuepuka hali ya kuleta hamaki

Jaribu kulifanyia kazi tatizo linalosababisha mwanao kuhamaki kabla halijatokea. Kwa mfano kama mwanao anahamaki akiwa na njaa, beba vitafunio na vyakula vyake zaidi kwenye begi wakati unatoka, bila kusahau maji ya kunywa.

Jiangalie mara ngapi unasema HAPANA kwa maombi yake, inaweza kuwa sababu nyingine ya mwanao kuhamaki, jaribu kumruhusu baadhi ya mambo ili kumsaidia mwanao na wewe .

Jinsi ya kuwa baba bora

Sasa wewe ni baba, na kila unapojaribu kupata ufumbuzi wa kilio cha mtoto wako mchanga inakua ngumu. Hivyo inakupasa kujifunza kazi hii! Kukupa mwangaza, kundi kubwa la wanawake waliulizwa ni mambo gani wangependa wenzi wao wawafanyie katika siku za kwanza za uzazi wao na kutaja baadhi ya mambo. Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu kuzingatia ili kuwa baba mkamilifu:

Kuwa Jasiri

Unaweza hisi hofu pale mkunga, daktari na mshauri wa afya wanapoondoka na kukuacha umembeba mtoto wako mwenyewe. Hali hii inaambatana na kulia kwa mtoto kwa sauti kubwa,kuamka kila mara na kupata kwikwi kila anapokua ananyonya. Huu ni mda mzuri wa kutulia na kumkumbusha mwenzi wako kazi nzuri anayoifanya mpaka sasa.

Jua ni nani wa kumuuliza

Hakikisha una namba zote muhimu utakazohitaji: mkunga, daktari au mshauri wa afya. Hii inakusaidia mara unapojitaji ushauri wa haraka unajua ni nani wa kumpigia simu.

Fanya manunuzi ya kutosha

Jaza makabati na jokofu vyakula vya kutosha na rahisi kuandaa.Hii ni kwasababu muda mwingi utatumika kumuhudumia mtoto na kukosa muda wa kuandaa chakula chenu. Kubaliana na jambo hili kwamba kuandaa chakula siku za mwanzo ni ngumu hivyo uwepo wa mahitaji ya kutosha yenye kusaidia kutengeneza chakula rahisi na cha haraka ni muhimu. Pia ni vizuri kuyajua maduka ya karibu yenye mahitaji ya mtoto kama nepi,taulo nyepesi zenye unyevu(wipes), sabuni n.k pale yanapopungua nyumbani.

Kuwa mlinzi wa mlangoni

Kama baba, utahitajika sana nyumbani kipindi cha awali cha ujio wa mtu mpya katika familia yenu. Ndugu, marafiki na majirani watakuja kumuona mtoto na mama. Ingawa ni jambo zuri kupata ugeni lakini pia inachosha kuwa na watu wengi wanaokuja na kuondoka kumuona mtoto. Kuwa tayari kuwarudisha pale mwenzi wako na mtoto wako wanapochoka kupokea wageni.

Dhibiti simu

Simu yako haikomii kuita au kuingia meseji kutoka kwa ndugu, rafiki na wafanyakazi wenzako wakikupongeza na kutaka kujua maendeleo ya mtoto na mama yake. Ikiwa milio hii imezidi zaidi ni vema kuacha na kuwatumia meseji moja yenye kuelezea hali ya mtoto na mama baadae pindi umetulia.

Mbembeleze/ mridhishe mwenzi wako

Kuna njia nyingi unazoweza kufanya na kumuangalia mwenzi wako na kumsaidia maisha kuwa rahisi. Mtayarishie maji bafuni. Mkandekande mabegani na mgongoni. Mpikie chakula chake akipendacho, na mtayarishie vitafunwa(snacks) na kinywaji wakati akinyonyesha.

Baadhi ya wamama wengi wenye watoto wachanga wanakua katika hali ya maumivu, kuchoka na kuwa na hisia kali. Anahitaji msaada wako kuweza kukabiliana na hali. Atashukuru jitihada zako sana itakayopelekea kuimarisha zaidi mahusiano yenu na kufanya mkawa karibu zaidi ya awali.

Ongea na kuwa msikivu

Katika kipindi hiki kuongea na kusikilizana ni jambo ambalo halifanyiki mara kwa mara. Mpatie mwanao na mtoto wako sifa sawia na kuwa mkweli ni jinsi unavyojisikia kuwa mzazi. Lakini kumbuka kitu cha mwisho cha kufanya ni kutilia mkazo jinsi maisha mapya yamekuathiri wewe.

Badala yake, msikilize yeye pia.Elewa kwamba akiwa katika hali ya jazba na kulia kwa wakati mmoja, anachotaka kutoka kwako ni upendo na msaada.

Mpatie pongezi

Katika siku za awali, tendo la ndoa sio jambo la kipaumbele sana kwa mwenza wako. Anaweza kuwa amechoka sana, mwenye huzuni na kuona aibu/ kuushtukia mwili wake baada ya kujifungua.

Jukumu lako ni kumfanya ajisikie anapendwa na bado ana mvuto. Unaweza fanya hivi kwa kumkumbatia sana na kumwambia kila mara jinsi gani ni mzuri. Mpatie sifa hizi pia kwa siku ambazo hajavaa kupendeza na kusuka nywele zake vizuri.

Hakikisha una rafiki wa karibu wa kuongea nae

Usijisahau. Kila mtu anahitaji mtu wa kuzungumza nae pembeni na wanafamilia. Mwenzi wako ana rafiki wengi wa kike, mama na dada zake anaoweza kuzungumza nao. Kwanini usimtafute rafiki yako mmoja utakayezungumza nae juu ya baraka za ujio wa mtoto katika familia yako na wasiwasi ulionao? Hii itakusaidia kukuza akili yako katika safari mpya ya maisha ya kuwa baba bora.

Kumuogesha mtoto mchanga katika hali ya usalama

Mtoto wako anaweza kupendelea zaidi kuchezea maji, lakini kuna kanuni muhimu kufuatwa ili kufanya muda wa kuoga salama na vilevile wa kufurahisha. Kanuni ya kwanza na muhimu ni usimwache mtoto peke yake ndani ya beseni wakati wa kuoga.

Joto gani la maji lafaa kwaajili ya kumuogesha mtoto?

Hakikisha maji ya kuoga ya mtoto wako yana uvuguvugu wa kutosha kabla ya kumuweka mtoto wako. Weka maji ya baridi kwanza, kisha ongeza maji ya moto.

Changanya maji vizuri ili kuhakikisha hakuna maeneo yenye joto zaidi. Hii itapunguza hatari ya kumuunguza mtoto wako. Kamwe usimuweke mtoto ndani ya chombo cha kumuogeshea(beseni) ukiwa unamimina maji. Jotoridi la maji linaweza kubadilika haraka sana na mtoto kuungua ndani ya sekunde chache.

Unaweza kununua kipima joto kuhakikisha jotorii la maji ya kuoga ni sawa. Baadhi ya vipima joto ni midoli mizuri ya kuchezea wakati wa kuoga. Maji ya kuoga ya mtoto yanatakiwa kuwa na joto la digrii 37 za sentigredi mpaka 38, ambalo ni sawa na joto la mwili.

Ikiwa hautumii kipimajoto njia nzuri ya kupima joto la maji kwa haraka ni kwa kutumia kiwiko chako kuliko kiganja cha mkono kujua jotoridi la maji.

Japokua maji ya kuoga yana joto, mtoto anaweza hisi baridi mara umtoapo kwenye maji, hivyo ni vyema kuweka mazingira ya kumpa joto mara atokapo kwenye beseni la maji. Mara umwinuapo mtoto kutoka kwenye maji mfunike kwa taulo kavu na mfute akauke kabla ya kumvalisha nepi kavu na nguo.

Kina gani cha maji ni sawa kwa maji ya mtoto.

Kwa watoto wachanga mpaka miezi 6, jaza maji katika beseni karibu 8sm mpaka 10( inchi 3 mpaka 4). Kamwe usijaze maji kupitiliza na usimuweke mtoto ndani ya beseni kisha umimine maji, kwani joto la maji linaweza kubadilika haraka.

Jinsi gani naweza msaidia mtoto wangu pindi yuko ndani ya maji?

Unapomuweka mtoto ndani ya maji mshike kwa nguvu chini ya matako kwa mkono mmoja. Weka mkono mwingine chini ya shingo yake kwa nyuma karibu na mabega. Mara mtoto wako akikaa vizuri ndani ya beseni au chombo unachomuogeshea, tumia mkono wako uliomshikilia sehemu ya chini ya matako kumwagia maji kuzunguka mwili wake. Kaza mwili wako kwenye mwili wa mtoto na pia msaidie kuweka kichwa chake juu ya maji ili asizame.

Kamwe usimwache mtoto pekee yake ndani ya beseni. Hata kama mtoto wako mwingine mkubwa yupo nae bafuni au kwenye beseni, ni vema kukaa na kumshika au kumwangalia mwanao.

Watoto wadogo wanaweza kuzama ndani ya maji yenye kina cha chini ya 5 sm (2inch) na inachukua sekunde chache tu kwa mtoto kuteleza ndani ya maji au kujizungusha kwenye maji bila msaada. Kawaida watoto hawalii au kupambana mara wanapoingia ndani ya maji, hivyo inakua vigumu kugundua kama hatari imetokea kwa mwanao.

Je, nimwogeshe mwanangu mara ngapi?

Ni uamuzi wako. Kuoga knaweza kuwa wakati wa furaha na kupumzika kwako na mwanao. Lakini kama hupendi kumuogesha mwanao kila siku, ni sawa kumuogesha mara mbili au tatu kwa wiki.

Siku ambazo mtoto haogi unaweza kumfuta kwa kitambaa safi chenye unyevu na kumbadili nguo, pia kuosha uchafu uonekanao tu.

Pindi mtoto wako atakapokua na umri wamiezi michache, itakubidi kuoga kuwe moja ya ratiba yake ya kila siku, asubuhi( midaa ya saa nne mpaka saa tano) na  kabla ya kulala. Lakini pia ratiba hii itegemee hali ya hewa ya eneo. Chagua sabuni nzuri na salama kwa mtoto, ili kusaidia kudumisha mng’ao mzuri wa ngozi ya mwanao.

Ikiwa mtoto wako ana ngozi kavu na yakuwasha, ongeza mafuta ya kuogea (bath emmolient) maalumu yanayosaidia kurudisha mng’ao wa mtoto kwenye maji. Kumbuka kukaza mikono maana mafuta haya maalumu ya kuogea hutelezakwenye ngozi ya mtoto.

Je, nimwoshe mwanangu nywele mara ngapi?

Huitaji kuosha nywele zake kila siku. Nywele zake hutengeneza mafuta kwa kiasikidogo, hivyo basi maramoja au mbili kwa wiki ni sawa.

Kama mtoto wako ana (cradle cap) – ngozi yenye rangi ya unjano au wekundu juu ya kichwa chake inayotokana na uzalishaji wa mafuta(sebum) na kufanya ukoko katika kichwa chake,ni vema kuosha nywele zake mara nyingi kwa sabuni au shampoo maalumu.

Epuka kutumia shampoo kama mtoto wako ana ukavu wa ngozi au muwasho badala yake tumia mafuta maalumu ya kuogea (emollient).

Je, naweza muacha mtoto wangu bafuni kwa dakika chache?

HAPANA. Kamwe usimuache mtoto pekee yake kwenye beseni.

Kabla ya kuanza kumogesha, hakikisha umeandaa kila utakachohitaji katika zoezi hili. Hakikisha taulo, sabuni, nepi safi na nguo ziko karibu na uwepo wako. Kipindi mtoto wako ni mchanga hakikisha una mahitaji ya kutosha maana watoto wanakojoa mara nyingi na kujisaidia haja kubwa wakati wowote na bila kutarajia.

Ikiwa simu yako itaita au mtu akagonga mlangoni, mnyanyue mwano kutoka kwenye maji na mfunike kwa taulo kisha mchukue pamoja na wewe.

Utagunduaje kama mtoto anayenyonya anashiba

Je, Mtoto wangu anayenyonya anashiba?

Sheria ya kwanza ya kumnyonyesha mtoto ni kumuangalia na sio kuangalia saa. Ili kugundua kama mtoto anayenyonya anashiba ni vyema kujua ni vitu gani muhimu vya kuangalia. Kumuwekea mtoto ratiba ya kunyonya kunaweza kuwa hatari katika upatikanaji wa maziwa yako. Lakini kama utamruhusu mtoto wako kuamua muda gani na mara ngapi ananyonya, utakuwa na uhakika mtoto wako anapata maziwa ya kutosha na upatikanaji na usambasazaji wa maziwa yako kuwa imara. Kama mtoto wako amelala kwenye kifua chako upande mmoja wa bega, mbadilishe kuelekea upande mwingine. Ikiwa mtoto wako bado ana njaa, atakula zaidi. Ikiwa hana njaa, jiandae kwa ulishaji ujao.

Ishara zinazoweza kukujulisha mtoto wako anapata maziwa ya kutosha hujumuisha:

 1. Mtoto wako anapata choo kila siku baada ya kufikisha siku 4.
 2. Kinyesi cha mtoto wako kinabadilika kutoka nyeusi hadi kijani hadi manjano wakati kama anakunywa maziwa vizuri (na inapaswa choo kuwa cha njano baada ya siku 4)
 3. Mtoto wako anatakiwa abadilishe nepi 5-6 nzito zilizo loana kila siku baada ya siku ya nne.
 4. Mtoto wako anaongezeka gramu 112 – 196 kwa wiki baada ya kurejesha uzito wa kawaida wa kuzaliwa (kawaida ndani ya siku 10-14).

Watoto wote wana siku ambazo wananyonya sana na siku nyingine ambazo hawanyonyi. Hizi ni tabia za kawaida za unyonyeshaji na sio ishara kwamba kuna kitu sio sawa. Kwa kuangalia vitu hapo juu unaweza ukatambua kama mtoto anayenyonya anashiba. Pia kushiba kwa mtoto kunategemeana na upatikanaji wa maziwa kutoka kwa mama.

Homoni ya Prolaktini huzalisha maziwa. Ikiwa unanyonyesha mara nyingi, kiwango cha homoni ya prolaktini kitaendelea kukua na kuongezeka kwa wingi. Ikiwa itaongezeka sana na kuwa ya kiwango cha juu, utatengeneza maziwa mengi zaidi na mtoto anayenyonya anashiba na atapata uzito kwa urahisi. Kwa hiyo ni muhimu kuwa unamlisha mara nyingi.

Ikiwa haunyonyeshi mara kwa mara, kwa muda mrefu, ongezeko la homoni ya prolaktini litashuka. Hivyo ni bora kunyonyesha mara nyingi, yaani mara 8-10 katika masaa 24, na ukitumia karibu dakika 15-45 kwa mlisho mmoja.

Imepitiwa: 9/Jan/2018

Faida za kunyonyesha kwa mama aliyejifungua

Je ulishawahi kujiuliza kunyonyesha kuna faida gani kwa mama aliyejifungua? Kwa wanawake wengi waliojifungua, kunyonyesha huwa ndio njia pekee ya kumpatia mtoto virutubisho. Hii ina faida lukuki kwa mtoto. Ila kuna faida nyingi pia kwa mama anayenyonyesha ukilinganisha na yule atakayechagua njia mbadala ya kumpa mtoto wake virutubisho stahiki.

Kunyonyesha baada tu ya kujifungua huwa na faida zifuatazo:

1. Kuepusha kutoka damu kupitiliza baada ya kujifungua
Baada tu ya kujifungua mwili wa mwanamke hupitia mlolongo mrefu sana wa mabadiliko ya homoni. Mabdailiko haya ndio husaidia kurudi kwa mfuko wa mimba katika hali ya kawaida baada ya kujifungua pamoja na kukatika kwa damu. Kunyonyesha husaidia hali hizi kuwahi kufanikiwa kwa haraka zaidi. Kwani kunyonyesha ni kitendo kinachoenda kusisimua utoaji wa homoni zilezile ambazo ni msaada kwa mfuko wa mimba kujirudi na pia damu kukatika. Hivyo basi mama atakayeanza kunyonyesha mtoto wake baada tu ya kujifungua atashuhudia damu kukatika mapema na mfuko wa mimba kurudi kawaida kwa haraka zaidi.

2. Kunyonyesha kunaokoa muda na pesa
Kunyonyesha kunaokoa sana muda na pesa, kwani kitendo cha kunyonyesha hakihitaji muda wowote wa matayarisho kama vile ambavyo ungehitaji kutayarisha maziwa ya “formula”. Mama anaweza akanyonyesha muda wowote, wakati wowote bila kuhitaji kuwa na maji ya moto ya kuchanganya maziwa au purukushani za kusafisha vyombo vya kunyonyeshea kwa njia ya chupa. Lakini pia maziwa ya “formula” ni ya gharama sana na huhitaji kipato kinachoeleweka kuweza kununua maziwa bora ambayo yatakuwa sahihi na salama kwa mtoto wako.

3. Kuepusha hatari ya magonjwa mbalimbali
Kunyonyesha kunahusishwa na kupunguza hatari za kupata magonjwa ya mifupa kuwa laini na kuvunjika kwa haraka. Vile vile mama anayenyonyesha mtoto wake kwa muda unaotakiwa anajilinda pia na magonjwa ya mfumo wa uzazi na pia hatari ya kupata saratani ya titi hupungua kwa wanawake walionyonyesha.

4. Inasaidia kupunguza uzito
Kunyonyesha na yenyewe ni tukio ambalo linaushughulisha mwili, pia kutengenezwa kwa maziwa kunahusishwa na kutumika kwa virutubishi vya kutosha kutoka mwilini kwako. Hivyo kunyonyesha kunahusishwa vile vile na kupungua kwa uzito. Ila si vyema kutumia kunyonyehsa kama njia ya kupungua uzito kwani wakati wa kunyonyesha unashauriwa kula chakula bora na chenye virutubisho vya kutosha na kwa wakati muafaka ili kutengeneza maziwa ya kutosha kwa ajili ya mtoto.

5. Kuendeleza asili ya mzunguko wa kushika mimba, ujauzito na kuzaliwa mtoto.
Kama unanyonyesha, kuachiwa kwa homoni kwenye mwili wako zitakufanya uwe na mzunguko sahihi na salama wa kuweza kupata ujauzito mwingine, na kuzaliwa mtoto mwingine salama zaidi.

Mwisho kabisa kwa wiki chache za mwanzo kunyonyesha usiku inaonekana ni rahisi na yenye usumbufu kidogo kuliko wakati wa mchana.
Kunyonyesha kunakufanya mwenye furaha, pia kunyonyesha kunatoa homoni ambazo zinaongeza ujasiri, kujikubali na kupumzika na kusaidia kuongeza ukaribu wa mama na mtoto. Pia unaweza kusoma makala yetu nyingine kuweza kutambua ni kwa namna gani unaweza kufikia maamuzi ya kumnyonyesha mtoto wako au kutumia maziwa ya “formula”

Imepitiwa: 9/Jan/2018

Kunyonyesha au kutumia maziwa ya formula?

Kunyonyesha au kutumia maziwa ya formula, njia ipi ni bora kwa mtoto?

Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni njia mojawapo ya mafanikio makubwa kabisa ya kufanikisha na kuhakikisha afya ya mtoto. Kama kila mtoto akinyonyeshwa maziwa ya mama kwa ndani ya saa moja toka azaliwe, upewaji pekee maziwa ya mama kwa miezi ya sita ya kwanza katika uhai wa mtoto, na kuendelea kumnyonyesha hadi umri wa miaka miwili kutahakikisha mtoto anakua na afya bora. Huu ndio msingi wa kuimarika kiafya ya mwili na akili kwa watoto wote. Kitakwimu duniani, chini ya asilimia 40 ya watoto wachanga chini ya umri wa miezi sita hawapewi maziwa ya mama.

Ushauri nasaha wa kutosha kuhusu kunyonyesha na huduma ni vitu muhimu kwa ajili ya akina mama na familia katika kuanzisha na kudumisha zoezi hili la kunyonyesha.
Shirika la afya duniani lipo kikamilifu katika kukuza hali ya unyonyeshaji kama chanzo bora cha chakula kwa ajili ya watoto wachanga na watoto wadogo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza:

Kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza katika maisha ya mtoto. Katika miezi sita, vyakula, kama vile matunda kama parachichi, ndizi na mboga, lazima aanze kuwekewa ili kumsaidia katika kipindi anachokuwa akinyonya kwa muda wa miaka miwili au zaidi.

Aidha:
1. Kunyonyesha kunapaswa kuanza ndani ya saa moja baada ya kujifungua.
2. Kunyonyesha lazima kuwe “kwenye mahitaji”, kama mara kwa mara kama mtoto anavyohitaji iwe mchana ama usiku
3. Unyonyeshaji wa chupa hauna budi kuepukwa kadiri iwezekanavyo

Faida za Kunyonyesha

Kwa watoto wachanga
Maziwa ya mama ni chakula bora kwa watoto wachanga na watoto wakuao. Pia huwapa watoto wachanga virutubisho vyote wanavyohitaji kwa ajili ya maendeleo ya afya zao.
Maziwa haya ni salama na yana kinga ambayo husaidia kuwalinda watoto wachanga dhidi ya magonjwa ya kawaida katika utoto kama vile kuhara na homa ya mapafu (pneumonia), ambayo kimsingi ndio sababu kuu mbili za vifo vya watoto wachanga duniani kote.

Maziwa ya mama hupatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu (bure), ambayo husaidia kuhakikisha kwamba watoto wachanga hupata lishe ya kutosha.

Faida za muda mrefu kwa watoto
Kwa zaidi kuna manufaa kwa ajili ya watoto, kwani kunyonyesha maziwa ya mama inachangia kuwa na maisha yenye afya njema.

Vijana na watu wazima ambao walikuwa wananyonya maziwa ya mama walipokuwa watoto wana uwezekano mdogo sana wa kuwa na tatizo la unene na uzito uliopitiliza.
Pia huwa wako katika hali nzuri ya kutokupata uwezekano wa kuwa na aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari na vile vile katika kipimo cha akili huwa wako vizuri.

Faida kwa akina mama
Kunyonyesha pia kuna faida kwa mama. Kunyonyesha maziwa ya mama inahusishwa na njia ya asili kama njia ya uzazi wa mpango (Asilimia 98 huwasaidia katika miezi sita ya kwanza baada ya kujifungua katika kuzuia mimba).

Pia inapunguza hatari ya kupata saratani ya matiti na na saratani ya mifuko ya mayai (ovary) baadaye katika maisha, husaidia wanawake kurudi katika maumbile yao kama kabla ya ujauzito, na husaidia kupunguza viwango vya unene uliopitiliza.

Vipi kuhusu maziwa ya kopo au maziwa ya formula?

Maziwa ya kopo/formula kwa watoto wachanga huwa hayana kingamwili /antibodies ambayo hupatikana katika maziwa ya mama tu. Wakati ambapo maziwa ya kopo/formula hayakutayarishwa vizuri, kuna hatari inayotokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama na pia kutokuwa na vifaa vya kutakasia/kuondoa vijidudu. Hivyo kuwepo uwezo wa bakteria katika maziwa haya.

Utapiamlo pia unaweza kutokea ukisababishwa na uchanganyaji wa maziwa ya unga na maji mengi kuliko kipimo. Kama utaweka mazingira ya kumpa maziwa ya unga kila siku mara kwa mara siku zote, na ikitokia siku hayapo maziwa hayo, na ukawa huna budi kurudi katika kumnyonyesha maziwa ya mama, basi changua hilo halitakuwa sahihi kwa sababu kutakuwa na upungufu wa uzalishaji wa maziwa katika matiti ya mama kwa siku hiyo.

Kwa ushauri wa kisayansi ni vyema kukuchukua maamuzi ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama. Maziwa ya kopo/formula yatumike pale tuu kutakapokuwa na ushauri toka kwa mkunga au daktari kufanya hivyo.

Taratibu za kusimamia maziwa mbadala

Kanuni za kimataifa za kudhibiti masoko ya maziwa mbadala ilipitishwa mwaka 1981 ilikuwa na wito huu:

• Maandiko yote katika maziwa ya kopo/ formula na habari za kuelezea hali ya faida ya kunyonyesha maziwa ya mama na hatari ya afya ya maziwa mbadala/ yakopo au unga lazima zielezwe
• Si ruhusa kufanya matangazo ya maziwa mbadala /maziwa ya kopo ama unga kibiashara
• Si ruhusa sampuli yeyote ya maziwa mbadala kutolewa kwa wanawake wajawazito, mama au familia zao; na
• Si ruhusa kusambaza maziwa mbadala/maziwa ya kopo ama unga kwa bure au ruzuku kwa wafanyakazi wa afya au na vituo vya afya.

Unyonyeshaji sahihi

Unyonyeshaji una hitaji kujifunza na wanawake wengi wanapambana na magumu mengi sana mwanzoni wanapoanza hatua hii. Maumivu ya chuchu, na hofu kwamba hakuna maziwa ya kumtosheleza mtoto ni kawaida.

Vituo vya afya ambayo vinaunga mkono kunyonyesha hufanya mafunzo juu ya kunyonyesha sambamba na upatikana wa ushauri kwa mama wapya katika kunyonyesha. Hii huhamasisha viwango vya juu na uzoefu katika kunyonyesha.

Kutoa msaada huu na kuboresha huduma kwa akina mama na watoto wachanga, kuna hatua kadhaa zimetolewa kama”mama na mtoto” katika kliniki nchini kwetu. Katika mpango huu wa “mama na mtoto” ushauri na taratibu za unyonyeshaji hutolewa bure.

Kufanya kazi na kunyonyesha

Akina mama wengi ambao hurudi kufanya kazi makazini kwao wengi wao huacha kwa muda au kabisa kunyonyesha watoto wao. Sababu kuu ikiwa ni hawana muda wa kutosha, au mahali pa kukaa na kunyonyesha, hujieleza kwa kukosa kuhifadhi ya kusitiri maziwa yao.

Akina mama wanahitaji usalama, hali ya usafi na sehemu ya kujisitiri au sehemu ya karibu na mahali pa kazi yao ili waweze kuendelea kunyonyesha. Pia ili kumwezesha kuendelea na kazi zake, wengi wao hulazimika kuomba likizo ya kulipwa ya uzazi, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kwa ajili ya kutoa na kuhifadhi maziwa kutoka kwenye matiti.

Kumuanzishia mtoto chakula kigumu

Ili kukidhi mahitaji ya kuongezeka kwa watoto katika umri wa miezi sita, chakula kigumu lazima kiazishwe ili kusaidia ukuaji wake wa haraka kipindi hiki. Kwa wakati huu mtoto huyu anatakiwa aendelee kunyonya pia maziwa ya mama. Vyakula vya mtoto vinaweza kuwa vimetengenezwa mahsusi kwa ajili ya mtoto au inashauriwa viwe vinachukuliwa kutoka kwenye milo ya familia za watu wazima kwa kadiri inavyowezekana.

Wataalamu wa afya na vyakula wanasema ya kwamba:

• Kunyonyesha hakupaswi kupungua wakati unaanza kumpatia chakula kingine kigumu
• Mtoto apatiwe chakula akilishwa kwa kutumia kijiko, kikombe na sahani na sio kwatika chupa ya kunyonya.
• Chakula lazima kiwe safi, salama na mtoto alishwe katika mazingira safi.
• Muda wa zaidi na wa kutosha unahitajika kwa ajili ya watoto wadogo kujifunza kula vyakula vingine vigumu.

Imepitiwa: July 2017