Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Usafi wa Kucha za Mtoto

Kucha za mtoto mchanga zinakua haraka sana, inawezekana ukahitajika kuzikata karibia mara 2 hadi 3 kwa wiki. Kucha za miguuni hazihitaji kukatwa mara kwa mar asana.

Ujanja ni kununua vifaa safi na maalumu kumkatia mtoto kucha. Unaweza ukanunua kikatio kucha maalumu kwa watoto. Mmoja anaweza akamshika mtoto asiweze kuhangaika sana huku mwingine akimkata kucha zake kwa makini kwani ngozi ya mtoto ni laini sana. Unaweza ukajaribu kumkata kucha akiwa ananyonya au akiwa amelala kupata urahisi zaidi.

Wakati wa kukata kucha elekeza kikatio kucha mbali na mtoto na kuwa makini usikate ngozi yake. Shikilia kwa nguvu kidole cha mtoto wako ukiwa unakata ili kisitingishike na kumkata bahati mbaya. Kama una wasiwasi sana kwamba unaweza ukamkata mtoto, tumia kikwaruzo kucha badala yake na uwe unazikwaruza kucha taratibu sana kwani ukitumia nguvu na kucha zake ni laini unaweza ukapitiliza na kukwaruza ngozi yake laini.

Kama mtoto wako anajikwarua usoni pamoja na kwamba kucha zake ni fupi, unaweza kumvalisha “gloves” au nguo zenye mikono mirefu inayopitiliza vidole.

Usafi na Uangalizi wa Kibana Kitovu

Baada ya mtoto wako kuzaliwa, mrija wa chakula toka kwa mama utakatwa na kubanwa na kibana kitovu.

Mfunge nepi mtoto wako ikiwa chini ya kitovu, ili kibana kitovu kipate hewa na pia kisipate mkojo. Epuka kumuogesha mtoto wako mpaka kibana kitovu kitakapodondoka.

Hakikisha kibana kitovu kinakuwa safi kadiri uwezavyo kwa muda wote kitakapokuwa kinakauka mpaka kudondoka, mara nyingi kuanzia siku 10 hadi 21. Kikishadondoka kitaacha kijidonda kidogo kibichi kwenye kitovu ambacho kitapona baada ya siku chache zijazo.

Katika maeneo yenye joto au katika kipindi cha joto ni vyema kumuacha mtoto wako akiwa amevaa nepi na T-shirt kubwa kubwakuruhusu hewa kuingia kwani itasaidia kupona kwa kitovu chake. Epuka kumvalisha mtoto wako nguo zenye kubana sana mpaka pale kibana kitovu kitakapodondoka.

Katika kipindi hiki ukisubiria kibana kitovu kidondoke na kitovu cha mtoto wako kupona kabisa, unaweza ukawa unamsafisha kwa kumfuta na kitambaa laini chenye maji ya vuguvugu ukiwa makini kutokuweka maji kwenye kitovu.

Ukurutu Kichwani kwa Mtoto Mchanga

Ukurutu mweupe kichwani ni dalili ya kawaida kwa watoto wachanga. Mtoto wako anaweza akawa ana tatizo dogo tu la ngozi kavu iliyobabuka na kuonekana kama ukurutu au mba au akawa na tatizo kubwa akionekana kuwa na uteute wa njano, mzito, wenye mafuta mafuta na kukatika katika.

Ukurutu huu huweza kutokea wiki mbili hadi miezi mitatu baada ya kuzaliwa na hupotea wenyewe baada ya miezi kadhaa. Mara nyingi huwa sio tatizo baada ya miezi 6 hadi 7. Hakikisha mtaalamu wa afya anamuangalia mtoto wako kama ana tatizo hili. Ukurutu kichwani hutokea pale tezi zinazotengeneza mafuta (sebaceous glands) zinatengeneza mafuta mengi zaidi ambayo baadae hukauka na kubabuka babuka. Wataalamu wengi wanaamini kwamba zile homoni za ziada ambazo mama mjamzito alikuwa anazitoa zilisafiri hadi kwa mtoto wake wakati wa kujifungua na kuziamsha tezi za mtoto kutengeneza mafuta zaidi. Miezi michache baada ya homoni za mtoto wako kuwiana tatizo hili litatoweka.

Njia rahisi kuondoa ukurutu huu ni kwa kuosha nywele za mtoto wako kila siku kwa sabuni zinazoshauriwa kuosha nywele za mtoto. Jaribu kusugua ukurutu huu kwa mikono yako au nguo laini ya kuogeshea watoto kuulainisha ukurutu huu. Kabla ya kuzisuuza nywele zake, mchane kwa kitana laini kuondoa ukurutu uliozidi ndio umsuuze.

Ni Nini cha Kufanya Mtoto Anapocheua

Mtoto wako inabidi acheue kwa sababu huwa anachukua hewa nyingi akiwa ananyonya. Kupunguza kiasi cha hewa anachokiingiza tumboni wakati ananyonya hakikisha yupo kwenye mkao sahihi wa kunyonya na na chuchu imeingia vizuri mdomoni. Midomo yake inabidi iwe imeifunika kabisa chuchu au chupa ya maziwa bila kuacha nafasi wakati ananyonya.

Muweke mtoto wako mabegani mwako. Simama au kaa vizuri, ukiwa umeegemea nyuma kidogo, mshikilie mtoto kwa matakoni ili umbebe vizuri. Hakikisha anaangalia nyuma yako kupitia moja ya mabega yako, kidevu chake kikiwa kimeegemea kwenye kitambaa safi ili kama akicheua usichafuke.

Mpige pige taratibu mgongoni. Msugue kwa mwendo wa chini juu chini juu mgongoni kwake karibu na mabega yake. Kuwa mvumilivu: Inaweza kuchukua dakika 4 hadi 5 mpaka mtoto wako acheue. Hakikisha unaagalia kichwa cha mtoto wako. Watoto wengine hukisukuma kichwa chao nyuma kwa ghafla na kama hakijashikiliwa vizuri anaweza akajiumiza.

Matumizi ya Nepi na Usafi Wake kwa Watoto

Ndani ya siku chache utakuwa umebobea katika swala la kubadilisha nepi mwanao. Unaweza ukawa unambadilisha mtoto wako karibia mara 10 ndani ya saa 24. Kama utagundua mtoto wao amepata vipele vidogo vidogo au kuchubuka kwa ngozi kulikosababishwa na uvaaji wa nepi, zifuatazo ni mbinu mbalimbali za kumsaidia:

  • Hakikisha ngozi ya mtoto ni kavu na ngozi haikutani na choo chake au mkojo.
  • Badilisha nepi kila mtoto anapokojoa au kupata choo. Wakati wa mchana iangalie nepi ya mwanao kila baada ya masaa matatu. Utahitajika kumbadilisha mtoto wako usiku pia ili kuepuka michubuko ya nepi au kusaidia kupona kwake. Ni kawaida kabisa kumbadilisha mtoto nepi hadi mara 8 kwa saa 24.
  • Tumia nepi yenye uwezo mkubwa wa kunyonya majimaji ili kumuacha mtoto wako mkavu muda wote.
  • Taratibu osha eneo lenye vipele au mchubuko kwa maji vuguvugu na kitambaa laini. Suuza vizuri na kausha vizuri.
  • Usitumie sabuni kama eneo hili limechafuliwa na choo cha mtoto wako, hapa unaweza kutumia sabuni kidogo kadiri itakavyohitajika.
  • Usitumie “wipes” za watoto ambazo zina “spirit” au “propylene glycol” kusafishia ngozi iliyochubuka kwani ngozi itazidi kuungua na kusababisha kusambaa kwa bakteria kwenye ngozi.
  • Unaweza ukaacha kumvalisha nepi kwa muda kadiri itakavyowezekana mpaka atakapopona.
  • Weka maziwa ya mama kidogo kwenye mchubuko. Maziwa ya mama yana vimelea vyenye tiba na uwezo wa kupambana na bakteria.

 

Jinsi ya kumbadilisha mtoto nepi (Za kutumia mara moja na kutupa)

Hatua 1: Mlaze mtoto wako kwenye sehemu ya kumbadilishia na hakikisha hataweza kudondoka. Usikae ukamuacha mtoto wako peke yake hata kwa sekunde kadhaa.

Hatua 2: Endelea kumuangalia mtoto wako machoni na endelea kuongea nae atambue kila kitu kiko sawa.

Hatua 3: Ifungue nepi iliyochafu, lakini usiiondoe kwanza.

Hatua 4: Vifunge vifungio vya nepi pamoja ili visijibane kwenye ngozi laini ya mtoto wako.

Hatua 5: Vuta chini mbele ya nepi ya mtoto wako. Kama nepi ya mtoto wako ni chafu unaweza ukaanza kuitumia hiyo hiyo kufutia kiasi kikubwa cha choo cha mtoto wako.

Hatua 6: Nyanyua matako ya mtoto wako juu kwa kuvishika visigino vya miguu yake kwa mkono wako mmoja na kuinyanyua miguu juu.

Hatua 7: Ifunge nepi chafu mara mbili, sehemu safi ikiwa juu.

Hatua 8: Tumia pamba laini na maji vuguvugu kumsafisha mtoto wako.

Hatua 9: Watoto wa kiume inabidi waoshwe kuzunguka korodani zake na uume wake. Ni vyema kuwa makini wakati wa kubadilisha nepi, na hakikisha unaosha kwa uangalifu sehemu zote zenye mikunjo.

Hatua 10: Subiri kwa dakika kadhaa mpaka mtoto wako akauke kwa hewa au umfute kwa kitambaa kikavu na laini. Unaweza ukampaka mafuta ya kinga ya kuchubuka kama daktari wako alishauri.

Hatua 11: Iondoe nepi chafu na fungua nepi safi.

Hatua 12: Taratibu mnyanyue mtoto wako tena juu kidogo kwa kutumia mkono wako mmoja. Ipitishe nepi safi chini ya matako yake.

Hatua 13: Vuta mbele ya nepi hii kuja mbele katikati ya miguu ya mtoto wako. Nusu ya nepi hii itakuja kwa mbele na kuilaza juu ya tumbo la mtoto wako. Lakini hakikisha haifuniki kitovu.

Hatua 14: Tumia mkono mmoja kuishikilia vizuri juu ya tumbo la mwanao. Kwa kutumia mkono mwingine fungua sehemu yenye gundi ya upande mmoja na kuinatisha mbele ya nepi iliyo juu ya tumbo. Fanya hivi kwa upande mwingine pia.

Hatua 15: Kuhakikisha nepi haijakaza sana au kulegea sana hakikisha unaweza kuingiza vidole viwili kwenye sehemu ya mbele ya nepi iliyo juu ya tumbo.

Jifunze Namna ya Kumuogesha Mtoto Mchanga

Muda wa kuoga unaweza kuwa wa furaha sana kwa mtoto wako. Inaweza ikawa ni tukio la kufurahisha hata kwenu wazazi. Lakini pia kumuogesha mtoto inaweza ikawa ni tukio gumu pale ambapo usalama wa mtoto wako ni wa kuzingatiwa. Jifunze namna ya kumuogesha mtoto wako kwa usalama zaidi na wakati huo huo kiwe kitendo cha kufurahia kwako na mtoto wako.

Unapomuogesha mtoto wako kwa mara ya kwanza hakikisha mwenza wako yupo. Kama mwenza hayupo ni vyema kuwe na mtu wa pili wa kukusaidia.

Weka maji ya vuguvugu kwenye beseni au sehemu utakayomuogeshea mtoto wako. Kabla hujamuweka mtoto wako kwenye beseni hakikisha tena joto la maji likoje kwa kutumia mkono wako. Wakati ukiendelea kumuogesha pia uwe makini na maji yanavyoendelea kuwa ya baridi, ukiona mikoni yako imeanza kuyasikia ni ya baridi basi yatakuwa ni ya baridi zaidi kwa mtoto wako, hivyo ni vyema kumaliza kumuogesha haraka zaidi.

Weka kila kitu utakachohitaji karibu yako, sabuni, kitambaa cha kuoshea, taulo, nepi na nguo za kubadilisha kabla hata hujaanza kumuogesha. Hii itakusaidia mkono mmoja uwe umemshikilia mtoto wako muda wote na mkono mwingine ukifanya kazi. Ukishamaliza kumuogesha mfunike haraka kwa taulo ili asipoteze joto lingi. Mkaushe vizuri, ukihakikisha unafuta majimaji yote kwenye sehemu zenye mikunjo kabla ya kumvalisha nepi na nguo.

Watoto wengine huhisi kama maji yanawasisimua, hivyo ni vyema kumuogesha mapema asubuhi. Wengine husinzia wakati wa kuogeshwa, hivyo kumuogesha wakati wa jioni inapendeza zaidi. Mtoto wako hahitaji kuogeshwa kila siku, mara mbili hadi tatu kwa wiki inatosha ilimradi tu kila siku unaosha uso wake, shingo, mikono na eneo linaloguswa na nepi.

Mara tu baada ya kuoga watoto hupenda kula. Unaweza ukamfunika mtoto wako kwa taulo kavu baada ya kumkausha na kumnyonyesha mkiwa mmegusana ngozi kwa ngozi.

Hakikisha umeyamwaga maji uliyotumia kumuogeshea mtoto, kwani ajali ikitokea na mtoto wako akaanguka kwenye maji hayo ukiwa haupo anaweza akazama hata kwenye maji yenye kina kidogo tu cha inchi 1.

.

Fahamu Matunzo Muhimu ya Mtoto kwa Ujumla

Matunzo kwa mtoto wako yanafurahisha, yanachosha na ni yenye hisia nyingi. Hapa tutakupa mbinu mbalimbali za kuweza kufanikiwa kumaliza wiki ya kwanza na kuendelea safari yako ya malezi.

Ngozi

Ngozi ya mtoto wako ni laini sana. Wiki za mwanzoni utaweza kuona chunusi za utotoni na vidoti doti vyeusi. Kila siku mchunguze mtoto wako juu mpaka chini. Chunguza mikunjo wa kwenye shingo, nyuma ya masikio, kwenye kwapa na sehemu zake za siri (Chunguza korodani kwa makini kama mtoto ni wa kiume). Mara nyingi uchafu na ngozi iliyokufa hujazana katika mikunjo hii ya ngozi na huweza kusababisha maambukizi kama “candida” kama hazitafanyiwa usafi vizuri.

Sehemu za siri za mtoto

Unaweza ukagundua kwamba sehemu za siri za mtoto wako zimevimba na kuwa nyekundu. Hii ni kawaida katika wiki kadhaa za mwanzo, na hutokana na kuwepo mda mrefu sehemu yenye homoni za ujauzito.

Kama dalili hizi hazitatoweka ndani ya wiki sita za mwanzo, ni vyema kumshirikisha mtoa huduma za afya utakapoenda kliniki.

Uume uliotahiriwa

Kuhudumia uume uliotahiriwa ni rahisi, unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha ngozi ya uume ni safi na sehemu yenye kidonda inaachwa kavu mpaka itakapopona. Wiki chache za mwanzo baada ya kutahiriwa uume utaonekana kuvimba na wenye maumivu ukiguswa.

Uume usiotahiriwa

Wakati wa kumuosha au kumuogesha mtoto ambaye hajatahiriwa, usijaribu kuirudisha ngozi ya mbele ya uume (govi) ili usafishe chini yake. Osha nje ya uume kama ambavyo unaosha sehemu nyingine ya mwili.

Kutegemea na mtoto wako, inaweza kuchukua wiki, miezi hadi miaka kwa ngozi ya mbele ya uume wake kujitenga na uume wake ili iweze kubenjuka kwa nyuma. Kwa sasa usilazimishe.