Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Mtoto Miaka 5 – (Miezi 60)

Jinsi mwanao anavyokua

Heri ya siku ya kuzaliwa! Miaka mitano sasa!

Sasa mwanao atafanya mambo yafuatayo:

  • Ataweza kutengana na wewe bila tatizo, wakati mwingine atakua na shahuku ya kuachana na wewe hasa kama anaenda kwa rafiki yake kucheza.
  • Atajisikia salama akiwa mbali na wewe.
  • Atajifunza thamani ya marafiki.
  • Atakua tayari kusaidia nyumbani, kufanya kazi kama kuandaa meza wakati wa chakula cha pamoja.

Maisha yako sasa

Tafuta usawa kati ya malezi na kumlinda mwanao na hakikisha unampatia mwanao uhuru pia.Mruhusu mwanao kuchunguza na kufanya majaribio ili aweze kuwa na ujasiri katika mazingira mapya kama shuleni. Changamoto uliyo nayo sasa ni kushindwa kujizuia kumsaidia mwanao pale unapomuona anahangaika na kitu kipya.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 11 – (Miezi 59)

Jinsi mwanao anavyokua

Katika umri huu mwano bado anashindwa kujizuia. Itachukua mara moja, mbili mpaka kumi hili somo kulielewa. Kufanya makosa ni moja ya njia anazotumia mwanao kukujaribu.

Uchokozi ni hatua ya kawaida katika umri huu. Chukua hatua haraka na kuwa mtulivu. Anzisha sheria na adhabu nyepesi ya michezo mibaya kama kupiga wenzake mateke na kugonga vitu vya thamani.

Maisha yako sasa

Ni vizuri kuwapatia wageni muda wako wakati wa kusheherekea miaka mitano tangu mwanao amezaliwa, fanya sherehe ndogo ya utulivu kwa mwanao. Akili ya mwanao hajikakua vizuri, anaweza kuelemewa na maandalizi yote ya sherehe yake, ni vizuri kumuandalia sherehe ndogo yeye na marafiki zake wa karibu.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 10 – (Miezi 58)

Jinsi mtoto anavyokua

Watoto ambao hawaanza shule wanaweza kuwa waongeaji zaidi ya watoto wakubwa. Wanapenda kuimba, kuhadithia na kucheza. Wanapenda kuuliza maswali sana. Wanaongea vizuri bila msaada,ila wanahitaji msaada katika kusikiliza jambo unalomwambia. Bado hawajui jinsi gani ya kupata na kuweka usikivu wako, wanaweza kukukatisha pale wanapohitaji na kuendelea iwe unasikiliza na kumjibu au hamsikilizi.

Unaweza kumsaidia mwanao kuelewa maana ya muda- mda gani kitu kinadumu. Kuwa makini na lugha yako ni mwanzo mzuri. Kwa kawaida wazazi wanawaambi watoto “kapige mswaki dakika moja”- ikimaanisha ni mda mfupi. Lakini pia wanapowaambia watoto wao “nipe dakika moja naongea na simu” na dakika moja inabadilika kuwa 20. Kumpatia mtoto muda sahihi kutamsaidia kukuza uelewa mzuri wa muda kwa mtoto.

Maisha yako sasa

Je,nguo za mwanao zinamvuka? Mara kadhaa ingia kabati kwa mwanao chagua nguo zilizomvuka. Kama una mpango wa kuzaa tena, hifadi vizuri nguo zilizomvuka au gawa kwa watoto wasiojiweza na ndugu. Kufanya hivi itakusaidia wewe na mwanao wakati wakutafuta nguo za kuvaa.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 9 – (Miezi 57)

Jinsi mtoto anavyokua

Kujifunza neno samahani ni jambo kubwa katika umri huu. Watoto wenye miaka minne wanajifunza kusikia na kuonyesha huruma, kama nguzo ya kuomba msamaha. Kujipendelea bado ni tabia mwanao aliyo nayo. Hataweza kuwajali wengine kabla yake mpaka atakapofikia umri wa miaka sita au saba. Kwa kusema hayo mwanao anajua pale anapotenda kosa kumuumiza mtu(angalia sura ya hatia atakayoonyesha, sura ya huzuni).

Maisha yako sasa

Kumuwahisha mtoto kulala ni utaratibu mzuri utakao msaidia kuamka mapema siku za usoni atakapoanza kwenda shule. Wakati wengi watoto ambao hawajaanza shule wanaruhusiwa kulala kwa kuchelewa wakisubiria wazazi wanaochelewa kutoka kazini, lakini mara shule zinapoanza mtoto anahitaji kuanza kulala masaa 11 mpaka 12.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 8 – (Miezi 56)

Jinsi mtoto anavyokua.

Mtoto wako anadaka na kuiga tabia anazoziona kwa wakubwa wake. Katika umri wa miaka minne watoto wanaanza majaribio ya kuwa na madaraka na kutumia maneno kupotosha watu.

Kupambana na tabia hii inahitaji uvumilivu na msimamo. Anapo amrisha wenzake mkanye. Anapotaka chakula au kitu kingine kwa nguvu mkumbushe kuomba kwa upole na kushukuru baada ya kupewa. Ikiwa mtoto wako anakua mkaidi kwa rafiki zake, mgeuzie kibao kwake na muulize anajisikiaje mtu akimfanyia hivyo inaweza kumsaidia kupambana na ukaidi.

Maisha yako sasa

Sasa mwanao anaweza kukuonyesha dhahiri chakula asichokipenda, inaweza kukushawishi kuacha kumuanzishia chakula kipya mwanao. Usikate tama endelea kumuanzishia mwanao vyakula vipya, kwa kawida mtoto anapewa vyakula 10 au 20 tofauti tofauti kabla ya kukubali na kukipenda. Mtoto akijifunza kukataa chakula chochote anachopewa italeta changamoto wakati atakapoanza kwenda shuleni. Bado hujachelewa kumuanzishia mtoto vyakula tofauti ili aweze kupata virutubisho vyote muhimu sasa na wakati atakapoanza shule.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 7 – (Miezi 55)

Jinsi mtoto anavyokua

Matamshi ya maneno kwa mwanao bado ni mtihani, jambo hili ni kawaida kwa watoto wa miaka minne. Watoto wengi hawafuzu kutamka maneno vizuri mpaka wanapofika miaka saba au nane. Wakati mwingine mwanao anaposhindwa kutamka neno vizuri inaweza kukufurahisha na ukapenda anavyotamka,usimtie moyo kuendelea kukosea kwa kufurahi anavyotamka neno. Ongea sahihi neno alilokosea itamsaidia kujifunza mara moja.

Michezo ya pamoja imeimarika sasa ukilinganisha na miezi sita iliyopita. Wanaweza kuanzisha michezo yao,kushirikiana zaidi na kuanza kuoneana huruma. Hii inamaanisha muda wa kusuluhisha ugomvi baina yao umepungua.

Hii haimaanishi hautakiwi. Ugomvi unaweza tokea.  Kunyang’anyana midoli.

Maisha yako

Mtoto wako anaweza kukusaidia shughuli nyepesi katika maandalizi ya chakula, kama kukoroga na kutwanga kitunguu saumu jikoni. Watoto wanaohusika katika shughuli za jikoni wanatambulishwa kwenye wingi wa vyakula tofauti kwasababu wana ufahari wa kuandaa na kupendelea kupeleka chakula mezani.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 6 – (Miezi 54)

Jinsi mtoto wako anavyokua

Watoto wengine katika miaka minne wanachukua muda mwingi wakicheza na michezo na mafumbo mbalimbali kuliko walivyokuwa na miaka mitatu. Wananyanyuka kutoka kwenye michezo yao mara chache zaidi na wanajihusisha nayo mpaka wakati mwingine inabidi uingilie kati na kumuondoa.

Ila usiwe na mategemeo makubwa sana. Mtoto wa kawaida wa miaka minne ana umakini na kitu kimoja kwa kati ya dakika tano hadi kumi pekee. Huu unaweza kuonekana kama ni muda mchache lakini kumbuka kuwa mwaka mmoja uliopita ilikuwa ni dakika tatu hadi nne pekee. Hivyo basi kuwa makini kutokuweka muda mrefu sana pale unapokuwa unaandaa matukio ya pamoja na watoto wengine kama sherehe za siku ya kuzaliwa n.k.

Kutokana na kuboreka kwa uwezo wake wa kukamata au kushika vitu, mtoto wako anaweza akashika kalamu, chaki au penseli na kuweza kuanza kuchora michoro ambayo inaanza kuleta maana bila kumlazimisha. Sanaa yake inaanza kutambulika na pia yenye taarifa za kutosha. Na pia anaweza akawa anaanza kujua kwa hakika ni kitu gani anataka kuchora. Mfano, anaweza kusema, “Naenda kuchora picha ya nyumba yetu”.

Maisha yako wakati huu

Utagundua kuwa ukimuuliza mtoto wako kuhusu siku yake ilikuwaje hatakupa majibu au taarifa za kutosha. Kama mtoto wako atatoka kwenye siku ya michezo na watoto wenzake na ukamuuliza ilikuwaje, anaweza akajibu tu kwamba, “Tulicheza”. Jaribu kuligeuza geuza swali na kutaka kujua zaidi. Mfano, “Ni mchezo gani uliupenda zaidi?”, “Mchezo gani haukupenda?” “Ni mchezo gani ungependa ukacheze tena siku nyingine?” Kumbuka pia pamoja na jitihada hizi zote bado unaweza kugundua mtoto wako anakushangaa tuu bila kukupa majibu. Pamoja na kwamba tungependa watoto wetu watuambie zaidi kuhusu walichofanya, kumbuka kuwa ni watoto na wanachofanya ni kucheza tuu hata kama aina ya mchezo au muda atakaocheza hautambui.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 5 – (Miezi 53)

Jinsi mtoto wako anavyokua

Uwezo wa matumizi ya lugha umekomaa karibu kufikia kiwango cha shule ya msingi kwa sasa. Mtoto wako wa miaka minne atakuwa anajifunza maneno manne hadi sita kila siku. Sentesi zake zinaongezeka urefu na kuwa ngumu zaidi, zikiwa na vituo vya kutosha na zenye kuelezea maneno. Watoto wa miaka minne pia wanaweza kuanza kuwa na uelewa wa matokeo ya matendo au matukio. Kwa mfano, “kitu fulani kikitokea, utafanya nini?”

Mtoto wako anaweza akaanza kutumia maongezi yake kuendana na hali iliyopo mbele yake. Kwa mfano anaweza akamwambia mtoto mdogo zaidi yake, “Mama ondoka” ukilinganisha na kumuambia mtu mzima kama mjomba wake, “Mama amekwenda dukani kununua maziwa”

Mtoto wako pia anaanza kuwa na uwezo wa kufuata hatua zenye mfululizo unaofuatana. Kwa mfano, “Unakata kipande kimoja, halafu unakigundisha na gundi na mwenzake” au “Niletee pochi yangu halafu nenda kafungue mlango”

Kwa kawaida mtoto wa miaka minne anaweza akahesabu mpaka kumi, japokuwa anaweza akashindwa kuziweka namba katika mtiririko sahihi kila wakati. Ugumu pekee anaoupata ni kuendelea na zile namba zenye sehemu mbili kama 20. Utofauti wa majina yake hauleti maana kwa mtoto wa miaka minne anayekaribia kuanza shule.

 

Maisha yako wakato huu

Inaweza ikawa ni muda mrefu sana tangu umetoka na marafiki zako. Weka mipango na marafiki zako na uweze kukutana na kubadilishana na mawazo. Kama kuna shughuli au mchezo uliokuwa unapendelea kuufanya kama ni kukimbia, kuhudhuria maktaba, kushiriki kwenye vikundi vya kina mama au vya kidini sasa ndio wakati wa kuanza kuyarudisha maisha yako kwenye mstari kama ilivyokuwa awali.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 4 – (Miezi 52)

Jinsi mtoto wako anavyokua

Watoto wanaokaribia kuanza shule wanapenda kutumia ubunifu wa kufananisha vitu na vitu vingine. Kwa mfano wanaweza wakafananisha na kuchezea fimbo kama mapanga. Mashuka kama mavazi ya kishujaa. Katika miaka minne maono ya mtoto wako yapo kwa wingi sana. Anaweza akawa chochote au yoyote atakayeamua. Anaweza akaamua kuwa daktari, mama au rubani. Ulimwengu wake wa maono unatengeneza hadithi za kusadikika ambazo zinaweza kuwahusisha watu wengine pia. Hivyo, michezo kwa sasa itachukua muda mrefu na wakati mwingine ya kujirudia rudia.

Mazungumzo wakati mwingine yanaweza yakaonekana kama kuhojiwa na mtoto wa miaka minne aliye mdadisi na muongeaji sana. Wakati huu watoto hupenda kuuliza maswali yanayofanana na mifano ifuatayo;

  • Wapi tunakwenda, mama?
  • Tutafika saa ngapi?
  • Tunaenda kuona nini?
  • Kwa nini Baba haendi na sisi?

Ameanza kuelewa kuna sababu vitu vinatokea – na anataka kujua sababu hizi ni zipi.

Sababu nyingine kwa nini mtoto wako anauliza maswali mfululizo bila kikomo ni kwa sababu ameanza kuongeza idadi ya maneno anayoyafahamu, na anataka kuyatumia maneno haya kuutambua ulimwengu unaomzunguka.

 

Maisha yako wakati huu

Wakati mtoto wako anaumwa na mwenye joto kali, unaweza ukatambua hili kabla hata hajapimwa joto kwenye kituo cha afya. Mtoto yule aliyekuwa msumbufu na mwenye kuuliza maswali mfululizo anaweza akawa mkimya na mnyonge. Wakati ukiwa unaendelea kuhangaika kutafuta suluhisho na matibabu kwa mtoto wako, ni vyema kutambua kwamba homa nyingi za watoto ni kutokana na virusi na hivyo dawa za kuua bakteria (antibiotics) hazitasaida.

Usitegemee daktari wako kukupa dawa yoyote kama mtoto wako ana mafua pekee. Inashauriwa kumpa mtoto wako ukaribu zaidi kumkumbatia na kumuelewesha kuwa mwili wake una uwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa na kwa sasa hivi unapambana kweli kweli kuhakikisha anajisikia vizuri mapema.

Mtoto Miaka 4 na Miezi 3 – (Miezi 51)

Jinsi mtoto wako anavyokua

Utaratibu uliozoeleka (ratiba) na uvumilivu kama wa mtume kwenye maswali ya mtoto wako wa miaka minne itamsaidia kuweza kuitambua dunia yake kwa ujumla. Atakuwa makini kujifunza kula kwa kijiko, kuogelea au hata kusaidia kufanya usafi. Zaidi ya haya uwezo wake wa kufikiri unaongezeka kwa kasi.

Mpaka sasa mtoto wako anaweza kukipeleka kijiko mdomoni kwake bila kumwaga akiwa anakula uji au supu na chakula kwa ujumla. Anaweza akatumia uma. Pia anaweza kunywa kutoka kwenye kikombe kisicho na mfuniko bila kumwaga, ijapokuwa unashauriwa kutumia vikombe vidogo visivyovunjika kwa sasa. Mtoto wako bado atahitaji msaada kwenye kukatakata chakula chake.

Maisha yako wakati huu

Je unapungukiwa na shughuli za kufanya na mtoto wako na unaona kama mmeshafanya kila kitu. Jaribu kumpeleka mtoto wako kwenye vituo vya kucheza watoto kama kuchezea maji, kucheza na mchanga, sehemu kama ufukweni, sehemu za kuangalia wanyama kama kuna eneo la ufugaji karibu au hifadhi ya wanyama pori iliyo karibu.

Mtoto wako pia anaweza akapendelea kuona magari makubwa kama magari ya zimamoto, magari ya huduma za kwanza (ambulance) na pia kuona ndege. Hivyo kama upo sehemu karibu na mambo yaliyotajwa hapo juu unaweza ukampeleka mwanao.