Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kunyonyesha Ukiwa Mjamzito

Je, ni Sawa Kuendelea Kunyonyesha Mtoto Wakati una Mimba Nyingine?

Kunyonyesha kunasaidia kuzuia kupata ujauzito, lakini sio mara zote. Inategemea na vitu kama vile mara ngapi unanyonyesha mwanao na umri wa mtoto wako. Kumbuka, inawezekana kushika mimba tena huku unanyonyesha mtoto wako.

Ikiwa utagundua wewe ni mjamzito tena, iwe ulipanga au bila kupanga, utakuwa na maswali mengi- kama kuendelea kumnyonyesha mtoto kutaathiri ujauzito wako mpya, mtoto anayenyonya, utokaji wa maziwa na mwili wako.

Ikiwa mama akagundua kuwa ni mjamzito wakati bado ananyonyesha. Mtoto anayenyonyeshwa anaweza kuwa mdogo hajafikia umri wa kuachishwa au mama mwenyewe anakuwa bado anapenda kumnyonyesha mtoto wake. Ikiwa mimba ni ya kawaida na yenye afya, inapendekezwa kuwa ni salama kabisa kuendelea kunyonyesha katika kipindi chote cha ujauzito. Katika makala hii utajifunza mambo muhimu na mikakati thabiti unayotakiwa kujua kuhusu unyonyeshaji ukiwa mjamzito.

Je, Nimuachishe Mtoto Kunyonya Mara Baada ya Kugundua Nina Ujauzito Mwingine?

Ujauzito mpya ni sababu iliyozoeleka ya kumuachisha mtoto kunyonya. Baadhi ya watoto wanaacha wenyewe na baadhi ya kina mama wanawahamasisha watoto wao kuacha kunyonya ili kujiandaa kwa ujio wa mtoto mpya atakayezaliwa. Lakini ikumbukwe hakuna haja ya kumuachisha mtoto kwasababu umeshika ujauzito mwingine. Unaweza kuendelea kumnyonyesha. Unaweza pia kuamua kuwanyonyesha wote wawili- mtoto mkubwa na kichanga wako atakayezaliwa.

Usalama wa Kunyonyesha Wakati wa Ujauzito

Kama umegundua umeshika ujauzito mwingine, hakikisha unaongea na mkunga au daktari wako juu ya historia ya afya yako. Daktari atakusaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu kuendelea kunyonyesha au kumuachisha mwanao.

Kawaida kunyonyesha baada ya kugundua una ujauzito mpya ni salama kabisa. Ikiwa una afya nzuri na ujauzito wako hausababishi matatizo yeyote ya kiafya, unaweza kuendelea kunyonyesa. Ingawa, zipo baadhi ya hali daktari akizishuhudia katika afya yako atakushauri umwachishe mwano kunyonya.

Wakati unanyonyesha mwili wako unatoa kichocheo kinachoitwa “oxytocin”. Homoni hii inawaunganisha mtoto na mama na kuleta upendo, vilevile homoni hii inasababisha mibano na mikazo ya mfuko wa uzazi (uterasi). Mibano na mikazo (The Braxton Hicks Contractions) hii sio hatari kwa ujauzito wa kawaida na wenye afya.

Sababu Ambazo Daktari Atakushauri Umuachishe Mtoto Kunyonya

Daktari anaweza kuwa na wasiwasi na kukushauri umwachishe mtoto kunyonya kama:

  • Ujauzito wako uko katika hatari kubwa ya kutoka
  • Ulishapitia tatizo la mimba changa kuharibika au kutoka
  • Ulijifungua kabla ya mda katika ujauzito uliopita (kabla ya wiki ya 37)
  • Unapata maumivu ya tumbo yanayoambatana na kutoka damu ukeni
  • Una ujauzito wa mapacha au zaidi
  • Hauongezeki uzito sahihi wenye afya.

Je, Kunyonyesha Kunaweza Athiri Mtoto Aliye Tumboni?

Hakuna ushahidi kuwa kunyonyesha ukiwa mjamzito kutaumiza ujauzito wako mpya au kuingilia ukuaji na maendeleo ya mtoto anayekuwa tumboni. Mwili wako unaweza kutengeneza maziwa ya mtoto anaye endelea kunyonya huku ukimtoa virutubisho vyote anavyohitaji mtoto aliye tumboni. Vifuatavyo vidokezo muhimu unavyotakiwa kukumbuka:

  • Mwili wako unahitaji nishati ya kutosha ili kutengeneza maziwa, kutoa virutubisho muhimu kwaajili ya mtoto anayekua tumboni, na kukuweka mwenye afya na imara. Ili mwili wako kuwa na nguvu na kuepusha upungufu wa aina yeyote ya virutubisho muhimu, kunywa maji ya kutosha, kula mlo kamili ulio na nyongeza ya kalori zenye afya, na pata mapumziko ya ziada.
  • Ongea na daktari wako ikiwa una tatizo lolote la kiafya kama vile kisukari au anemia, ili kuhakikisha unapata virutubisho muhimu na kalori sahihi unazohitaji.
  • Hudhuria miadi yako kila mwezi na fanya uchunguzi mara kwa mara kila unapoweza, ni muhimu ili kuwa na uhakika kuwa ujauzito wako unaendelea vizuri na unaongezeka uzito kama inavyotakiwa.

Je, Ujauzito Wako Mpya Unaweza Kumuathiri Mtoto Anayenyonya?

Mabadiliko katika ladha ya maziwa na kupungua kwa kiwango cha maziwa huweza kumuathiri mtoto anayenyonya. Mambo haya mawili yanaweza kusababisha mtoto mwenyewe kukataa kunyonya. Ikiwa mtoto wako yuko chini ya mwaka mmoja, mabadiliko haya yaangaliwe kwa umakini zaidi ili kuhakikisha mtoto anapata virutubisho vya kutosha. Endelea kumnyonyesha ili asikose virutubisho muhimu kutoka kwenye maziwa ya mama. Lakini, ikiwa mtoto wako ni mkubwa na tayari kaanza kula vyakula vigumu na kula mwenyewe, mabadiliko ya ladha na kiwango cha maziwa hayawezi kumuathiri.

Mabadiliko ya ladha ya maziwa

Wakati mtoto wako amezaliwa, atapokea maziwa ya kwanza yanayoitwa “colostrum”. Kadiri ujauzito wako unavyoendelea kukua ndivyo ladha ya maziwa itakavyobadilika kuelekea kwenye “colostrum” kwaajili ya ujio wa mtoto mpya. Mambo machache unayotakiwa kujua kuhusu mabadiliko haya ni kuwa:

  • “Colostrum” imejaa kingamwili na virutubisho, hivyo ni nzuri kwa mtoto mkubwa anayenyonya. Lakini, mwili hautengenezi “colostrum” nyingi hakikisha kichanga wako anapata kwa wingi maziwa haya yenye kingamwili na virutubisho vya kutosha haswa kama utaamua kunyonyesha mtoto mkubwa na kichanga wako baada ya kujifungua.
  • Mtoto anaweza kuendelea kunyonya bila tatizo hata baada ya mabadiliko ya ladha ya maziwa, au anaweza asipende utofauti wa ladha na kuacha mwenyewe kunyonya.
  • Maziwa haya ya awali “colostrum” yanamsaidia mtoto mchanga kutoa kinyesi cha kwanza nje ya miili yao “meconium”, vilevile kwa mtoto mkubwa ambaye bado ananyonya anaweza kupata dalili za kuharisha kutokana na maziwa haya ya awali yaliyojaa virutubisho na kingamwili za kutosha.

Mabadiliko ya kiwango cha maziwa

Ujauzito ni moja ya sababu ya upungufu wa kiwango cha maziwa. Mambo machache unayotakiwa kujua ni kwamba:

  • Unaweza kuona kupungua kwa kiwango cha maziwa mara baada ya kushika ujauzito au baadae kidogo.
  • Ikiwa mtoto wako anayenyonya yuko chini ya mwaka mmoja na umegundua upungufu wa kiwango cha maziwa ongea na mkunga wako. Inaweza kukuhitaji kutumia maziwa ya fomula sambamba na kunyonyesha ili kuhakikisha mtoto anapata virutubisho anavyohitaji.
  • Kama mtoto wako ana umri zaidi ya mwaka mmoja, hakikisha anapata virutubisho anavyohitaji kutoka kwenye vyakula mbalimbali vigumu anavyokula. Unaweza kuendelea kumnyonyesha kama afya yako inaruhusu na mwanao yuko tayari kunyonya.
  • Upungufu wa kiwango cha maziwa unasababisha maziwa kutoka taratibu kwenye titi. Baadhi ya watoto wanakatishwa tamaa na hali hii na kuacha kunyonya wenyewe.

Je, Ujauzito Mpya Unaweza Kumuathiri Mama Anayenyonyesha?

Ingawa inawezekana kuendelea kunyonyesha wakati wa ujauzito, zipo changamoto. Zipo njia nyingi ambazo ujauzito unaweza kukuathiri kama mama anayenyonyesha. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto unazoweza kupitia wakati wa kunyonyesha na vidokezo vitakavyokusaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Kuvimba kwa matiti na chuchu.

Ujauzito unaweza kurejesha tatizo la kunyonyesha la zamani. Mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa ujauzito yanaweza kusababisha tena maumivu ya chuchu na matiti. Kunyonyesha huku chuchu zimevimba kunaweza kuwa kugumu au kusababisha maumivu. Kwa bahati mbaya, suluhisho la chuchu zilizovimba wakati wa kunyonyesha halifanyi kazi wakati wa awali wa ujauzito kwasababu chanzo cha chuchu kuvimba ni mabadaliko ya vichocheo. Suluhisho la hali hii ni kuwa mvumilivu. Hali hii itadumu kwa miezi mitatu ya kwanza, japo kwa baadhi ya kina mama hali hii inaweza kuendelea kipindi chote cha ujauzito.

Unaweza kufanya yafuatayo ili kukabiliana na hali hii:

  • Weka kitu cha baridi juu ya chuchu zako
  • Vaa sidiria inayokufanya uwe huru (isikubane sana)
  • Jitahidi kumnyonyesha mtoto katika mazingira matulivu yatakayomfanya mtoto apunguze kuhangaika ili asisababishe kuvuta chuchu. Badala ya kumnyonyeshea sebuleni ambapo anaweza kubabaishwa na kelele za luninga au ndugu zake, nenda chumbani ambapo hakuna kelele au watu.
  • Jaribu mikao tofauti ya kunyonyesha.

Kuchoka

Ni kawaida kusikia uchovu kuliko kawaida ukiwa mjamzito kwasababu ya mabadiliko yote ya homoni yanayoendelea katika mwili wako. Kumlea mtoto mwingine na kumnyonyesha inaongezea uchovu huo. Kama unaweza, pata mapumziko ya kutosha. Inaweza kuwa ngumu haswa kama una mtoto anayetambaa au kukimbia kimbia, lakini fanya jitihada ya:

  • Kulala wakati mwanao akilala
  • Kaa kitako au lala kisha nyoosha miguu yako juu ukiwa unanyonyesha
  • Usiruke milo na kumbuka kunywa maji ya kutosha

Kadiri ujauzito unavyoendelea kukua, inakuwa ngumu kupata mkao mzuri wa kunyonyeshea mtoto wako. Fanya majaribio na tafuta mkao mpya utakaokupa unafuu wewe na mwanao. Pia unaweza kunyonyesha ukiwa umelala kwa ubavu.

Kumbuka

Wanawake wengi wanacha kunyonyesha mara baada ya kugundua wameshika ujauzito mwingine. Ikiwa hauko tayari, na daktari wako amekuhakikishia hakuna tatizo la kiafya linalokukabili hauna haja ya kumuachisha mwanao. Unaweza kuendelea kumnyonyesha mtoto wako kipindi chote cha ujauzito kwa usalama. Unaweza pia kuendelea kunyonyesha mwanao mkubwa hata baada ya kichanga wako kuzaliwa. Inaitwa “tandem nursing” kwa lugha ya kigeni.

Ni kweli, ujauzito unaleta kuvimba na maumivu ya matiti, kupungua kwa kiwango cha maziwa na uhitaji wa nishati ya zaidi mwilini. Ni rahisi kuchoka na kuelemewa. Unaweza kuamua kumuachisha mtoto wako kunyonya, na hii ni sawa kabisa. Ikumbukwe pia kuwa kipindi cha ujauzito kumuachisha mtoto kunyonya ni rahisi zaidi kwasababu ya mabadiliko ya ladha na kiwango cha maziwa, hivyo unaweza kuamua ni mda mzuri wa kuacha kunyonyesha. Fanya kile ambacho ni sahihi kwako na familia yako na usisikie hatia juu ya hilo.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Uchungu wa Uzazi wa Muda Mrefu (Prolonged Labor)

Iwe ni mara ya kwanza kujifungua au ulishawahi kujifungua, kuzaa mtoto ni tukio la kipekee kwa kila mwanamke. Kila mwanamke ana uchungu wa uzazi tofauti na hii ni kawaida. Uchungu wa uzazi wenye afya unaweza kuwa wa haraka sana au kuchukua mda mrefu. Hata hivyo, baadhi ya watoto hukwama na kuishia kuzaliwa kwa upasuaji au kwa msaada wa vifaa maalum.

Kuna wakati mtoto anakuja haraka sana na wakati mwingine anachelewa. Ujio wa kichanga wako unategemea vitu vingi, kimoja wapo ni kwa kasi gani uchungu wako unatokea.

Uchungu wa uzazi ni nini?

Uchungu wa uzazi ni kubana na kuachia kwa kujirudia rudia kwa misuli katika tumbo la uzazi. Utahisi misuli kubana na kuachia sehemu ya chini ya mgongo na eneo la tumbo. Misuli inavyobana na kuachia taratibu husababisha kufunguka kwa mlango wa tumbo la uzazi (cervix). Vile vile mibano hii ya misuli inasaidia mtoto kusukumwa nje ya mfuko wa uzazi. Baada ya mlango mzima kufunguka, mtoto anaweza kutoka nje ya tumbo la uzazi na hatimaye nje kupitia uke wa mama.

Kubana na kuachia kwa misuli huanza polepole mwanzoni mwa ujauzito, kawaida haichukui mda mrefu-huachia mama anapopumzika inajulikana kama uchungu wa uongo “Braxton-hick contractions”. Uchungu wa uzazi wa ukweli unaanza kwa nguvu, ukianza huja mara kwa mara, na kwa taratibu kila baada ya dakika chache. Uchungu huu hauachi hata mama akilala chini au kupumzika.

Kwa mama anayejifungua kwa mara ya kwanza uchungu unadumu kwa takribani masaa 12 mpaka 18 kwa wastani. Ila kwa mama mzoefu, uchungu unaenda haraka sana, kawaida nusu ya masaa ya mama anayejifungua kwa mara ya kwanza.

Uchungu wa uzazi wa muda mrefu ni nini?

Uchungu wa uzazi unaochukua muda mrefu sana ni uchungu wa zaidi ya masaa 12 kwa mama mzoefu au zaidi ya saa 24 (usiku na mchana) kwa mama anayejifungua kwa mara ya kwanza.

Kama mtoto wako hajazaliwa baada ya takribani masaa 20 ya mibano ya kawaida ya tumbo la uzazi, utakuwa unapitia uchungu wa mda mrefu. Baadhi ya wataalamu wa afya wanasema inatokea baada ya masaa 18 mpaka 24. Kama una ujauzito wa mapacha au zaidi uchungu wako utadumu kwa masaa zaidi ya 16.

Mara nyingi husababisha majeraha kwa mama na matatizo kwa mtoto, iwapo maji ya uzazi yataanza kutoka lakini uchungu wa uzazi ukachelewa kuanza baada ya saa 12, hali hii inaweza kusababisha maambukizi.

Uchungu wa uzazi wa muda mrefu unasababishwa na nini?

Uchungu utachukua mda mrefu endapo:

  • Mtoto ni mkubwa na hawezi kupita katika mlango wa uzazi.
  • Mtoto amekaa vibaya, kwa kawaida kichwa cha mtoto kinatangulia chini huku akiangalia mgongo wako. Tofauti na hapo uchungu utachukua mda mrefu kuliko kawaida.
  • Mibano na mikazo ya mfuko wa uzazi ni hafifu, hali hii itapunguza kasi ya mjamzito kuanza kusukuma mtoto wakati wa kujifungua.

Dalili na ishara za uchungu wa uzazi wa muda mrefu

Dalili na ishara za aina hii ya uchungu ni pamoja na

  • Uchungu wa zaidi ya masaa 18, kuchelewa ni moja ya ishara kuu.
  • Mama kuchoka na kuishiwa nguvu.
  • Dalili nyingine za kimwili ambazo hazivumiliki ni kama maumivu ya mgongo, mapigo ya juu moyo na maumivu katika misuli ya tumbo la uzazi hata ukigusa kidogo
  • Ukosefu wa maji na nguvu mwilini.

Mambo gani yanayochangia kuongezeka nafasi ya kupata uchungu wa uzazi wa muda mrefu?

Unene sana (Obesity)

Kisukari wakati wa ujauzito au shinikizo la damu kipindi cha ujauzito vinavyoambatana na unene uliopitiliza sana unaweza kuongeza ukubwa wa mtoto. Matatizo haya ya kiafya yanaweza kumfanya mama awe dhaifu, na fati kuzunguka mlango wa uzazi inaweza kusababisha matatizo wakati wa kujifungua.

Uzito duni

Ukosefu wa virutubisho muhimu kwa mama inapelekea ukosefu wa virutubisho kwa kiumbe ndani ya tumbo na mfuko wa uzazi, hivyo kusababisha matatizo katika mlango wa uzazi na kusababisha mtoto kuchelewa kuzaliwa. Udogo wa mwili unamaanisha udogo wa nyonga, ambayo itasababisha mtoto kuchelewa kupita kwasababu ya njia kuwa ndogo mtoto kupita. Hivyo basi, ni muhimu kuangalia afya yako vizuri.

Kupungua kwa wingi wa misuli

Moja ya sababu ya kupungua kwa wingi wa misuli wakati wa ujauzito ni ukosefu wa mazoezi na kuufanyisha mwili kazi ndogo ndogo. Kusukuma mtoto ni utaratibu wenye kuhitaji nguvu nyingi, na inahitaji misuli mizuri kwa kazi kufanyika bila vipingamizi. Upungufu wa misuli utapunguza nguvu na kuongeza nafasi ya uchungu kuchukua mda mrefu.

Kubeba ujauzito ukiwa na umri mkubwa au umri mdogo

Umri mzuri ambao mwanamke anaweza kujifungua vizuri bila vipingamizi vyovyote vya mwili ni kuanzia miaka 25 mpaka 35. Miaka kabla ya hapo na baada ya hapo mwili unakua haujajiandaa vizuri. Kina mama wanaozaa kwa mara ya kwanza katika umri mkubwa wanahitaji kuwa imara kimwili, kinyume na hapo watapata matatizo ya kiafya kama kisukari kinachosababishwa na kubeba mimba.

Nini hutokea ikiwa uchungu wa uzazi unaenda taratibu?

Wanawake wengi wanatamani uchungu wa uzazi unaoenda haraka na kujifungua haraka bila kutaabika. Lakini kama uchungu wa uzazi unaonekana kwenda taratibu, njia pekee ya kukabiliana na hali hii ni kujaribu kutulia kadiri uwezavyo kihisia na kimwili. Jambo kubwa wanalofanya wahudumu wa afya pale inapoonekana mama mjamzito anapitia hali hii ni kuhakikisha mama anatulia kiakili na kihisia kwa kumpatia mama hali ambayo itampunguzia msongo wa mawazo ikiwa ni pamoja na kuwepo karibu nao wakati wote na kumpatia njia ya kupunguza maumivu (inaweza kuwa dawa au njia ya asili ya kupunguza maumivu).

Baadhi ya vipimo vinaweza kufanyika katika muda huu na watoa huduma ili kuchunguza:

  • Mara ngapi misuli ya tumbo la uzazi inabana na kuachia
  • Kwa kiasi gani wa mibano na mikazo “contractions” katika tumbo la uzazi ni imara.

Vipimo hivyo vinavyoweza kufanywa ni pamoja na:

  • “Intrauterine Pressure Catheter Placement (IUPC)”- ni mrija mdogo wa uchunguzi unaoingizwa ndani ya uterasi pembeni ya mtoto unao muonyesha dakatari jinsi “contractions” zinavyotokea na kiasi gani “contractions” hizi ni imara.
  • Kipimo cha kuchunguza mapigo ya moyo ya mtoto.

Je, uchungu wa uzazi wa muda mrefu unatibiwaje?

Ikiwa uchungu wa uzazi unaenda taratibu, unaweza kushauriwa kupumzika kwa muda kidogo. Wakati mwingine dawa hutolewa kupunguza maumivu na kukusaidia kupumzika. Unaweza kujisikia kama kubadilisha mkao wa mwili ili kupata nafuu zaidi.

Matibabu ya ziada yanategemea na chanzo cha uchungu wako kuenda polepole. Ikiwa mtoto yuko tayari kwenye mlango wa uzazi (cervix), daktari au mkunga anaweza kutumia zana maalum zinazoitwa “forceps” au kifaa chenye utupu kusaidia kumvuta mtoto nje kupitia uke.

Ikiwa daktari wako anahisi kama unahitaji mikazo na mibano zaidi au yenye nguvu, unaweza kupatiwa dawa. Dawa hii inaharakisha mikazo na kuifanya imara. Ikiwa baada ya njia zote hizi bado uchungu unachelewa, unaweza kuhitaji upasuaji ili kumtoa mtoto ndani kabla hajapata matatizo ya kiafya.

Ikiwa mtoto ni mkubwa sana, au dawa haifanyi kazi kuharakisha utaratibu ya kujifungua utahitaji upasuaji pia.

Madhara ya uchungu wa uzazi wa muda mrefu

Uchungu wa uzazi wa muda mrefu unaongeza nafasi ya kuhitaji upasuaji ili kujifungua. Hali hii ni hatari kwa mtoto kwasababu inaweza kusababisha:

  • Viwango vidogo vya hewa ya oksijeni kwa mtoto.
  • Mapigo ya moyo yasio ya kawaida kwa mtoto.
  • Maambukizi katika mji wa mimba (uteras).
  • Mtoto kuzaliwa akiwa mfu (stillbirth)

Mama anaweza kupata:

  • Maambukizi.
  • Kupasuka au kuchanika kwa mji wa uzazi (uterine rupture).
  • Ugonjwa wa fistula ambao husababisha shimo kubwa kati ya njia ya uzazi na njia ya mkojo unaotokana na mama kuwa na uchungu wa muda mrefu bila matibabu.

Je, unawezaje kupunguza nafasi ya kupata uchungu wa uzazi wa muda mrefu?

Unaweza kupunguza hatari za kupata uchungu wa uzazi ambao ni taratibu kwa kuchukua tahadhari zifuatazo:

  • Jitahidi kuishi mtindo wa afya wa kimaisha: fanya mazoezi kuwa imara na mkakamavu, kula mlo kamili wenye afya, siku zote kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara.
  • Jitahidi kupunguza msongo wa mawazo: zuia kila aina ya woga na wasiwasi wowote, jitahidi kuzungukwa na shughuli na watu wenye mawazo chanya. Kila wakati jikumbushe jinsi gani utakua mwenye furaha na fahari kumpakata mwanao mkononi mwako.
  • Hali ya umasikini ya maisha ni chanzo kikuu cha magonjwa ya ziada wakati wa uchungu wa uzazi. Inashauriwa kufanya miadi ya kila mwezi na mkunga wako ili shida kama unene uliopitiliza au ukosefu wa misuli ya kutosha kugundulika mapema. Kwa kuchukua taadhari na mikakati sahihi unaweza kupunguza uchungu wa uzazi wa muda mrefu.

IMEPITIWA: JUNI, 2021.

Zifahamu chanjo sahihi. Je, Mtoto wako anazipata kwa wakati?

Chanjo ni nini?

Chanjo huokoa maisha ya hadi watoto milioni 3 kila mwaka. Chanjo hukinga maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.
Kisayansi chanjo ni kitendo cha kupewa kinga mwili kwa njia ya kuamsha vitoa kinga viwe tayari kupambana na adui ambaye wanamjua tayari.

Umuhimu wa chanjo

Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo. Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii. Kinga ya utotoni ni muhimu sana hasa kwa ukuaji wa baadae. Hivyo basi, chanjo kwa mtoto katika mwaka wake wa kwanza na katika mwaka wa pili ni muhimu sana.
Ni muhimu pia, kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa. Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto.
Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu kuwa kutoa chanjo kwa mtoto mgonjwa kidogo au mwenye ulemavu au mwenye upungufu wa lishe ni salama.

Ukweli kwa ajili ya familia na jamii kuhusu chanjo

1. Chanjo ni jambo la lazima. Kila mtoto ni lazima apate chanjo zote zilizopendekezwa. Kinga ya utotoni ni muhimu sana; chanjo katika mwaka wa kwanza na wa pili zina umuhimu wa pekee. Wazazi wote au walezi wengine wanapaswa kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu muda wa kukamilisha chanjo zinazohitajika.

2. Chanjo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mengi hatarishi. Mtoto ambaye hajapata chanjo yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi, ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha.

3. Mama wote wajawazito pamoja na watoto wao wanapaswa kukingwa dhidi ya pepopunda. Hata kama mama aliwahi kupata chanjo kabla , anapaswa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu kama bado anahitaji kupewa chanjo ya pepopunda.

4. Sindano mpya hazina budi kutumika kwa kila mtu anayepata chanjo. Kila mtu anapaswa kudai sindano mpya kwa kila chanjo anayopewa.

5. Ugonjwa huweza kuenea haraka watu wengi wanapokuwa wamekusanyika pamoja. Watoto wote wanaoishi katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa , hasa katika mazingira ya wakimbizi au ya watu waliojikusanya kutokana na janga fulani, wanapaswa kupewa chanjo haraka.

6. Kadi ya chanjo ya mtoto (au ya mtu mzima) haina budi kuwasilishwa kwa mtoa chanjo kabla ya kutolewa kwa chanjo.

Aina za chanjo

BCG (Bacile Calmette-Guérin)
Watoto wote wanastahili kupokea chanjo itwayo BCG (Bacile Calmette-Guérin) vaccine. Hii huumpa mtoto kinga dhidi ya aina zingine za kifua kikuu na ukoma.

DTP au DPT (Dondakoo, Pepopunda na Kifaduro)
Watoto wote wanastahili chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro kupitia aina ya chanjo iitwayo DTP au DPT vaccine. Viini vya dondakoo husababisha maambukizi ya njia ya kuingizia hewa na huenda ikasababisha shida za kupumua na hata kifo. Pepopunda nayo husababisha kukauka kwa misuli na maumivu makali yanayo sababishwa na mkazo wa misuli. Mkazo huo wa misuli unaweza sababisha kifo. Kifaduro huathiri njia ya kuigizia hewa na kusababisha kikohozi kinachoweza dumu wiki nne hadi nane na ni hatari sana kwa watoto wachanga.

Wanawake wote waja wazito na watoto wachanga wanahitaji chanjo ya pepopunda.

Surua
Watoto wote wanastahili kupokea chanjo dhidi ya surua. Maradhi ya surua husababisha utapiamlo, udhaifu wa maendeleo ya ubongo na huweza kufanya mtoto kiziwi au kipofu. Ishara zinazoelekeza kuwa mtoto anaweza kuwa anaugua surua ni pamoja na kuongezeka kwa joto mwilini, upele, kikohozi, kumwaga kamasi na macho kubadilika na kuwa mekundu. Tahadhari, mtoto anaweza kufa kutokana na surua.

Polio
Watoto wote wanastahili chanjo dhidi ya polio. Dalili za polio ni utepe kwenye mguu au mkono na udhaifu wa kukitumia kiungo kilicho athirika. Kwa kila watoto mia mbili wanaoambukizwa maradhi ya polio, mmoja atapata ulemavu wa maisha.

Ratiba za chanjo hutofautiana kulingana na nchi au sehemu ya nchi unayoishi. Ni muhimu kufuatilia ratiba ya chanjo kwa mujibu wa mwongozo wa taifa. Watoto wanastahili kupokea chanjo kwa umri unaostahili na kwa muda unaostahili.
Pamoja na kutofautiana huku kwa ratiba za chanjo kati ya nchi na nchi, unaweza kufuatilia utaratibu uliopendekezwa na CDC (Centre for Disease Control) hapa chini.

Ufuatao ni mtiririko wa chanjo husika na wakati muafaka ambao mtoto wako anatakiwa awe ameshapatiwa.

UMRIAINA YA CHANJOINATOLEWAJEMUHIMU KUJUA
0 – AnapozaliwaKifua Kikuu (BCG)  Sindano bega la kulia  Ni lazima kovu lotokee kwenye bega la kulia baada ya muda  
 Polio (OPV 0)Matone mdomoniChanjo ya ugonjwa wa kupooza ya kuanzia
    
Wiki ya 6Polio (OPV 1)Matone mdomoniChanjo ya kwanza ya ugonjwa wa kupooza
 DTB-HepB-Hib1 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B)Sindano paja la kushotoChanjo ya kwanza ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja.
 PCV 1Sindano paja la kuliaChanjo ya Nimonia ya kwanza
 Rota 1Matone mdomoniChanjo ya Kuhara ya kwanza
    
Wiki ya 10Polio (OPV 2)Matone mdomoniChanjo ya pili ya ugonjwa wa kupooza
 DTB-HepB-Hib2 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B)Sindano paja la kushotoChanjo ya pili ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja.
 PCV 2Sindano paja la kuliaChanjo ya Nimonia ya pili
 Rota 2Matone mdomoniChanjo ya kuhara ya pili
    
Wiki ya 14Polio (OPV 3)Matone mdomoniChanjo ya mwisho ya ugonjwa wa kupooza
 DTB-HepB-Hib3 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B)Sindano paja la kushotoChanjo ya tatu ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja.
 PCV 3Sindano paja la kuliaChanjo ya Nimonia ya tatu
    
Miezi 9Measles (MR 1)Sindano bega la kushotoChanjo ya kwanza ya surua
    
Miezi 15Measles (MR 2)Sindano bega la kushotoChanjo ya pili ya surua

IMEPITIWA: 26 MAY 2020

Faida za kunyonyesha kwa mama aliyejifungua

Je ulishawahi kujiuliza kunyonyesha kuna faida gani kwa mama aliyejifungua? Kwa wanawake wengi waliojifungua, kunyonyesha huwa ndio njia pekee ya kumpatia mtoto virutubisho. Hii ina faida lukuki kwa mtoto. Ila kuna faida nyingi pia kwa mama anayenyonyesha ukilinganisha na yule atakayechagua njia mbadala ya kumpa mtoto wake virutubisho stahiki.

Kunyonyesha baada tu ya kujifungua huwa na faida zifuatazo:

1. Kuepusha kutoka damu kupitiliza baada ya kujifungua
Baada tu ya kujifungua mwili wa mwanamke hupitia mlolongo mrefu sana wa mabadiliko ya homoni. Mabdailiko haya ndio husaidia kurudi kwa mfuko wa mimba katika hali ya kawaida baada ya kujifungua pamoja na kukatika kwa damu. Kunyonyesha husaidia hali hizi kuwahi kufanikiwa kwa haraka zaidi. Kwani kunyonyesha ni kitendo kinachoenda kusisimua utoaji wa homoni zilezile ambazo ni msaada kwa mfuko wa mimba kujirudi na pia damu kukatika. Hivyo basi mama atakayeanza kunyonyesha mtoto wake baada tu ya kujifungua atashuhudia damu kukatika mapema na mfuko wa mimba kurudi kawaida kwa haraka zaidi.

2. Kunyonyesha kunaokoa muda na pesa
Kunyonyesha kunaokoa sana muda na pesa, kwani kitendo cha kunyonyesha hakihitaji muda wowote wa matayarisho kama vile ambavyo ungehitaji kutayarisha maziwa ya “formula”. Mama anaweza akanyonyesha muda wowote, wakati wowote bila kuhitaji kuwa na maji ya moto ya kuchanganya maziwa au purukushani za kusafisha vyombo vya kunyonyeshea kwa njia ya chupa. Lakini pia maziwa ya “formula” ni ya gharama sana na huhitaji kipato kinachoeleweka kuweza kununua maziwa bora ambayo yatakuwa sahihi na salama kwa mtoto wako.

3. Kuepusha hatari ya magonjwa mbalimbali
Kunyonyesha kunahusishwa na kupunguza hatari za kupata magonjwa ya mifupa kuwa laini na kuvunjika kwa haraka. Vile vile mama anayenyonyesha mtoto wake kwa muda unaotakiwa anajilinda pia na magonjwa ya mfumo wa uzazi na pia hatari ya kupata saratani ya titi hupungua kwa wanawake walionyonyesha.

4. Inasaidia kupunguza uzito
Kunyonyesha na yenyewe ni tukio ambalo linaushughulisha mwili, pia kutengenezwa kwa maziwa kunahusishwa na kutumika kwa virutubishi vya kutosha kutoka mwilini kwako. Hivyo kunyonyesha kunahusishwa vile vile na kupungua kwa uzito. Ila si vyema kutumia kunyonyehsa kama njia ya kupungua uzito kwani wakati wa kunyonyesha unashauriwa kula chakula bora na chenye virutubisho vya kutosha na kwa wakati muafaka ili kutengeneza maziwa ya kutosha kwa ajili ya mtoto.

5. Kuendeleza asili ya mzunguko wa kushika mimba, ujauzito na kuzaliwa mtoto.
Kama unanyonyesha, kuachiwa kwa homoni kwenye mwili wako zitakufanya uwe na mzunguko sahihi na salama wa kuweza kupata ujauzito mwingine, na kuzaliwa mtoto mwingine salama zaidi.

Mwisho kabisa kwa wiki chache za mwanzo kunyonyesha usiku inaonekana ni rahisi na yenye usumbufu kidogo kuliko wakati wa mchana.
Kunyonyesha kunakufanya mwenye furaha, pia kunyonyesha kunatoa homoni ambazo zinaongeza ujasiri, kujikubali na kupumzika na kusaidia kuongeza ukaribu wa mama na mtoto. Pia unaweza kusoma makala yetu nyingine kuweza kutambua ni kwa namna gani unaweza kufikia maamuzi ya kumnyonyesha mtoto wako au kutumia maziwa ya “formula”

Imepitiwa: 9/Jan/2018

Huduma ya Kwanza: Mtu aliyekabwa kwenye koo la hewa – choking

Huduma ya kwanza: Mtu aliyekabwa kwenye koo la hewa – Choking

Kukabwa kwenye koo la hewa hutokea pale kitu kinapokwenda na kubana koo la hewa kwenye koromelo na kuzuia kupita kwa hewa kuelekea na kutoka kwenye mapafu. Kwa watu wazima mara nyingi vipande vya chakula ndio husababisha. Kwa watoto wadogo mara nyingi huwa ni vitu vidogo vidogo wanavyochezea na kuvimeza kwa bahati mbaya. Kwa sababu kukabwa kwa koo huzuia oksijeni kuelekea kwenye ubongo ni vyema kupata huduma ya kwanza mara moja.

Alama ya kimataifa ya mtu aliyekabwa koo la hewa ni mikono kuonekana imeishikilia shingo kwa nguvu. Kama mtu aliyekabwa koo la hewa hatoi ishara hii, ziangalie pia ishara zifuatazo:

Kushindwa kuongea
Kupumua kwa tabu au kwa kelele
Kushindwa kukohoa kwa nguvu
Midomo na kucha kuwa za bluu
Kupoteza fahamu

Mtu aliyekabwa koo la hewa:

Shirika la huduma ya kwanza – Red Cross linaelekeza kutumia mufumo wa “tano – kwa – tano” kuweza kutoa huduma ya kwanza:
Toa mapigo matano 5 mgongoni: kwa kutumia upande wa mkono ambao ungetumia kupiga kofi ila kwa nguvu zaidi piga mara tano mgongoni. Sehemu sahihi ya kupiga ni katikati ya mabawa mebega kwa nyuma mgongoni.
Toa mapigo matano 5 kwenye tumbo: Toa mapigo matano ya tumboni ambayo kwa jina lingine ni kufaitilia mfumo wa Heimlich “Heimlich maneuver”
Pishana kati ya mapigo matano mgongoni na matano tumboni: mpaka kilichokaba kimetoka na kuachia koo la hewa.

Kuutumia mfumo wa Heimlich “Heimlich Maneuver”

Kwa mtu mwingine:

Simama nyuma ya mtu husika. Zungusha mikono yako kukizunguka kiuno chake. Msogeze mutu mhusika aegemee mbele zaidi kidogo.
Tengeneza ngumi kwa mkono mmoja. Iweke ngumi hii juu kidogo ya kitovu chake.
Ikamate ngumi hii kwa mkono mwingine. Bonyeza kwa nguvu tumboni kwa mpigo wa haraka kuelekea juu – Kana kwamba unataka kumnyanyua mtu huyu juu.
Toa mapigo haya ya tumboni mara 5, kama itahitajika. Kama kilichomkaba bado hakitoki, rudioa mzunguko wote wa tano-kwa-tano kama uluvyoelezewa awali.

Kama upo peke yako fanya kwanza mzunguko wa mapigo ya mgongo na tumbo kabla ya kupika simu ya dharura kuomba msaada. Kama kuna mtu mwingine karibu, muelekeze mtu huyu kupiga simu kuomba msaada wakati wewe unatoa huduma ya kwanza.
Kama mhusika ataonekana anapoteza fahamu, inashauriwa kumfanyia huduma ya kwanza ya CPR inayojumuisha kukisukuma kifua na kutoa pumzi mdomoni. (Makala nyingine inayohusu huduma hii ya kwanza itafuata baadae)

Kwako mwenyewe:

Kwanza kama upo mwenyewe na umekabwa koo la hewa, piga 112 au namba ya dharura ya sehemu ulipo haraka iwezekanavyo. Halafu, ijapokuwa unaweza ukashindwa kujipiga mgongoni ila bado una uwezo wa kutumia mfumo wa kupiga tumboni na kukiondoka kinachokukaba.
Weka ngumi juu kidogo ya kitovu
Ishike ngumi hii kwa mkono mwingine na egemea sehemu ngumu – upande wa meza au egemeo la kiti itafaa.
Iingize ngumi yako ndani ya tumbo kuelekea juu

Kwa mwanamke mjamzito au mwenye umbile kubwa
Iweke mikono yako juu zaidi kuliko mfumo wa Heimlich wa kawaida, chini kidogo ya chembe cha moyo, pale mbavu za chini kabisa zinapokutana kufuani.
Endelea kutumia mfumo wa Heimlich kwa kubonyeza kwa nguvu kuelekea kifuani, kwa mapigo ya haraka.
Rudia mpaka chakula au kilichokuwa kimekaba kimetoka au mhusika anapoteza fahamu

Namna ya kuifungua njia ya hewa kwa mtu aliyepoteza fahamu:

Mlaze mtu kwa mgongo kwenye sakafu
Fungua njia ya hewa. Kama unakiona kilichomkaba nyuma kabisa ya koo la mhusika, ingiza kidole mdomoni na ukisafishe kinachomkaba kitoke nje. Kuwa muangalifu usikisukume chakula au chochote kinachomkaba ndani zaidi, kwani inaweza kutokea kwa urahisi zaidi kwa watoto.
Anza mapigo ya uhai (Cardiopulmonary Resescitation – CPR) kama kinachomkaba kinaendelea kumkaba na mtu haoneshi dalili ya kupata nafuu. Mapigo ya uhai ya CPR yanaweza yakasababisha kinachomkaba kikatoka. Kumbuka kuangalia mdomo mara kwa mara.

Mtoto mdogo chini ya mwaka mmoja:

Chuchumaa kama upo kwenye mkao wa kukaa. Mbebe mtoto kicha kikiwa kinaangalia chini kwenye mkono wako, ambao umelala juu ya paja lako.
Mbonyeze kwa kiganja chako kichanga huyu mara tano katikati ya mgongo wake. Kwa mkao huu na mapigo haya ya mgongoni yatatosha kukiondoa kitu kinachomkaba.
Mshike mtoto uso ukiwa unaangalia juu kwenye mkono wako, katika mkao ambao kichwa kipo chini kuliko kiwiliwili kama njia hapo juu haikusaidia. Kwa kutumia vidole viwili vilivyowekwa kwenye chembe cha moyo cha mtoto, toa mapigo matano ya kukibonyeza kifua.
Rudia mapigo ya mgongoni na msukumo wa kifua. Kama kupumua hakutarudi. Piga simu kuomba msaada wa matibabu ya haraka.
Anza kufanya mapigo ya uhai (CPR). Kama moja ya njia hizi zimefungua njia ya hewa lakini mtoto huyu bado hajaanza kupumua

Mtoto mdogo juu ya mwaka mmoja:

• Toa mapigo ya tumbo pekee

Kujiweka tayari kwa tatizo kama hili au kwa matatizo mengine ambayo huduma ya kwanza inaweza ikawa ndio msaada pekee utakaosaidia kuokoa maisha ya mtu wako wa karibu. Ni vyema ukajifunza au kujisomea kuhusu namna mbali mbali za kutoa huduma ya kwanza. AFYAPLUS itakuwa inatoa makala moja kila wiki inayohusiana na huduma ya kwanza.

Imepitiwa: July 2017

Teknolojia: Matumizi ya “drones” kusafirisha dawa vijijini

Matumizi ya “drone” kusafirisha dawa

Katika karne hii ya ishirini na moja, maendeleo ya kiteknolojia ni makubwa sana kuliko baadhi yetu tunavyoweza kuamini. Dunia imefikia kwenye muongo wa mabadiliko makubwa ya kisayansi na teknolojia. Katika sekta ya usafiri, teknolojia pia imekua kwa haraka sana hivi punde.

“Drone” ni nini?

Kifaa kinachoitwa “drone” ni mfano wa ndege ndogo inayoweza kupaa na kusafiri bila kuwa na rubani ndani yake. Drones zinaweza kuwa na ukubwa tofauti tofauti kulingana na uwezo wake wa kufanya kazi. Vindege hivi vidogo huwa vinaendeshwa na muongozaji au rubani ambaye huwa anatumia kompyuta au simu ya mkononi iliyounganishwa na mtandao na GPS ya drone husika.

Matumizi mbalimbali ya “drones”

Matumizi ya drones yapo ya aina mbalimbali. Kwa muda mrefu drone zimekuwa zikitumika kuchukua picha au video za maeneo husika kwa kupiga picha zikiwa angani. Ila pia zimekuwa zikitumiwa na wataalamu wa ardhi kuweza kupima na kutengeneza ramani za mashamba, ranchi na pia hifadhi za mali asili. Kwa baadhi ya nchi zilizoendelea matumizi ya drone yamekua na hutumika pia na majeshi ya ulinzi na usalama kwa matumizi mbalimbali.

Matumizi ya “drone” kusafirisha mizigo

Ndani ya miaka mitano iliyopita kampuni kubwa duniani kwa uuzaji wa bidhaa mbalimbali ya Amazon na kampuni za usafirishaji kama UPS, FEDEX na DHL zimekuwa zikitafiti njia rahisi, salama na ya haraka zaidi kuweza kuifikisha mizigo sehemu husika kwa kutumia drones. Matatizo kadhaa yameorodheshwa ikiwa ni changamoto zinazoweza kujitokeza katika aina hii ya usafiri. Kwanza ni usalama wa anga inayotumiwa na ndege za kawaida za abiria na mizigo. Ukizingatia kuwa “drones” zenye uwezo wa kupaa na kufikia au kuweza kukutana na ndege za kawaida, hali ya usalama lazima itakuwa ni changamoto. Changamoto ya pili ni usalama wa matumizi ya drones kufanya uhalifu wa aina nyingine. Kwa mfano mapema mwaka 2016 watu wasiojulikana walifanikiwa kusafirisha na kufikisha madawa ya kulevya kwenye jela moja huko Uingereza. Pia kuna changamoto nyingine kama namna drone itakavyoweza kuutua mzigo baada ya kuufikisha kwenye anuani husika. Pamoja na changamoto hizi ni ukweli usiofichika kwamba miaka michche ijayo tutashuhudia matumizi makubwa zaidi na kwa wingi zaidi ya drone katika sekta mbalimbali.

Matumizi ya drone kusafirisha dawa

Nchini Rwanda, matumizi ya drone kwenye sekta ya afya yalianza rasmi mwaka 2016 baada ya serikali ya Rwanda kwa kushirikiana na kampuni ya kimarekani ya ZIPLINE walianza shughuli za usafirishaji wa damu na madawa au vifaa tiba muhimu kuweza kuzifikia hospitali zilizopo kijijini. Ifahamike kwamba kwa nchi kama Rwanda yenye miundombinu haba ya usafiri vijijini inaweza kuchukua hadi masaa manne kwa gari kufikisha bidhaa kama damu inayohitajika kwa dharura kutoka hospitali moja kwenda nyingine. Teknolojia ya kutumia drone inaweza kufanikisha safari hii kwa muda wa dakika 15 pekee.

Nchi ya Rwanda imekuwa ya kwanza Afrika na inawezekana ya kwanza duniani kuanza kuruhusu matumizi ya drone kwa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali. Matumizi ya drone yamepokelewa tofauti na nchi mbalimbali duniani, nyingine zikihitaji mlolongo wa vibali na sheria za kuweza kusimamia shughuli zake huku nchi nyingine kama Morocco, Kenya na Uganda wamezuia utumiani wa drone katika shughuli mbalimbali na sheria kali zinasimamia hili. Nchini Ghana watumiaji wa drone wanaweza wakafungwa kifungo cha hadi miaka 30 kama hawataandikisha “drones” zao.

Miaka ijayo

Ni sahihi kukubali kuwa miaka michache ijayo teknolojia na matumizi ya drones na vifaa vingine vitakavyogundulika itakuwa sio hiari tena ila ni lazima kwani matumizi yake yatakuwa salama zaidi na bei rahisi kulinganisha na njia mbadala. Ni wakati mzuri sasa kwa serikali na nchi za bara la Afrika kuandaa na kutengeneza miswada na sheria zitakazowezesha serikali kuwa tayari kukumbatia teknolojia mbalimbali zinazokuja na kutoa mwongozo haraka iwezekanavyo. Kitendo cha kufungia au kukataza matumizi fulani ya teknolojia kadiri zinavyobuniwa ni kudorosha na kurudisha nyuma ubunifu na maendeleo ya nchi husika katika karne hii ya uchuni wa kidigitali.

Imepitiwa: 24 July 2017