Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Njia Mbalimbali za Kujifungua na Faida Zake

Kipindi hiki tofauti na zamani kumekuwa na njia mbali mbali za kujifungua. Hii intokana na maendeleo ya teknolojia na uwepo wa wataalamu mpaka kwenye vituo vya chini kabisa vya afya. Hali hii imesaidia kupunguza kwa kasi vifo vya mama na mtoto. Zifuatazo ni njia mbalimbali zinazotumika kujifungua. Ni vyema kuzitambua na kuzielewa mapema ili uweze kufahamu mapema ni njia gani ambayo itatumika wakati wa kujifungua kwako.

Ukweli Unaotakiwa Kujua Kuhusu Njia za Kujifungua

 • Chaguo zilizopo wakati wa kujifungua ni pamoja na: kujifungua bila msaada (kawaida), kujifungua kwa msaada na kujifungua kwa upasuaji.
 • Unaweza kujifungulia nyumbani, zahanati/kituo cha afya au hospitalini.
 • Kujifungua kwa njia ya kawaida bila dawa hakuna maumivu, ni rahisi kama mama atajifunza mbinu za kupumua wakati wa kusukuma mtoto katika chumba cha kujifungulia.
 • Katika kuhakikisha njia gani ni sahihi kwa mama wakati wa kujifungua upimaji wa faida na hasara za njia hiyo uende sambamba na pendekezo la mjamzito ambalo ni salama kwake.
 • Kila mwanamke ana uzoefu wa kipekee wakati wa kujifungua, wnaawake wengi wanakiri wakati wa kuzaa mtoto kuna amabatana na maumivu. Hata hivyo, maumivu hay ani ya mada mfupi, zipo aina na njia madhubutu za kupunguza ukali wa maumivu wakati wa kujifungua.

Kujifungua kwa Njia ya Kawaida (Kujifungua Bila Msaada- Unassisted birth)

Kujifungua kwa njia ya kawaida

Wewe na familia yako mnaweza kubaini ishara za kawaida za uchungu. Mwanamke anaweza kujifungua siku kadhaa au hata wiki kadhaa kabla au baada ya tarehe iliyotarajiwa, kulingana na tarehe ya kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida. Mwanamke anapofahamu maana ya uchungu, ataweza kufahamu kitakachotokea. Ufahamu huu humsaidia kutulia zaidi na kuwa na ujasiri katika siku au wiki za mwisho za ujauzito.

Yafahamu maagizo dhahiri ya jambo la kufanya pale uchungu unapoanza (kwa mfano ikiwa utakuwa na maumivu ya mkakamao wa misuli ya fumbatio ya tumbo la uzazi au kuvuja kwa kilowevu cha amniotiki, maarufu kama kupasuka chupa). Hakikisha kuwa kuna mtu atakaye mwita mkunga au mtaalamu mwingine ili kukuzalisha haraka iwezekanavyo.

Mkunga wako anafaa kuzingatia maandalizi ya kujifungua na:

 • Kuheshimu chaguo la mama. Anapaswa kumpa mama habari zote zinazohitajika kuhusu uzalishaji safi na salama, lakini hatimaye anapaswa kuheshimu chaguo lake kuhusu mahali pa kujifungulia na mtu angelipenda kuandamana naye.
 • Kukusaidia kutambua mahali pa kupata usaidizi wakati wa kujifungua na kipindi cha baada ya kujifungua kinachofuata punde.
 • Kupangia gharama yoyote ya ziada inayohusiana na kujifungua kwako.
 • Kutayarisha vifaa vya kumtunza mama na mtoto wake atakayezaliwa.

Faida za Kujifungua kwa Njia ya Kawaida

 • Watoto wanaozaliwa kwa njia ya kawaida wanakuwa na matatizo madogo ya upumuaji.
 • Mama anapona haraka na kuepuka aina yeyote ya matatizo yanayohusiana na upasuaji kama vile uchanwaji wa utumbo au ogani za eneo la tumbo wakati wa upasuaji.
 • Njia hii ya kujifungua ina kiasi kidogo cha maambukizi na ukaaji mfupi hospitali au kituo cha afya.

Hasara za Kujifungua kwa Kawaida

 • Kuchanwa eneo kati ya njia ya haja kubwa na uke.

Njia za kujifungua kwa Msaada (Assisted Births)

Kujifungua kwa njia ya kawaida kwa msaada wa vifaa maalumu

Vifaa hivi huwasaidia akina mama na watoto pale watoto wanapotakiwa kuzaliwa haraka. Ni zana muhimu sana kwa mtu mwenye ujuzi wa kuzitumia.

Kifaa cha kunyonyea cha utupu (vacuum extractor) ni kifuniko kidogo cha kunyonyea ambacho hutosha kwenye kichwa cha mtoto kinachotokeza angali akiwa ndani ya uke. Hewa hujazwa ndani ya kile kifuniko ili kiweze kushikilia vizuri ngozi ya kichwa cha mtoto wakati mtaalam anapokivuta. Utaratibu huu unaweza kusababisha damu kuganda kwenye kichwa cha mtoto, kitaalam inaitwa (cephalohematoma)

Koleo hufanana na mikasi mirefu yenye bawaba ambayo mwishoni imejikunja ili kutosha kwenye kichwa cha mtoto. Kifaa hiki kinaweza kuleta madhara makubwa sana kwa watoto na mama vikitumiwa vibaya au vkitumiwa na mtu asiye na ujuzi.

Matumizi ya kifaa cha kunyonyea (vacuum-cup) yameongezeka. Sababu tatu zilizosababisha ongezeko la matumizi ya vifaa hivi ni kwasababu ya:

 • Ongezeko la matumizi ya dawa ya usingizi ya epidural, ambayo hurefusha hatua ya kusukuma
 • Muda maalum wa kusukuma uliotengwa kwa wanawake katika baadhi ya hospitali
 • Jitihada za hospitali kupunguza uwezekano wa kufanyiwa upasuaji.

Kifaa cha kunyonyea (vacuum-cup) mara nyingi hutumiwa pamoja na dawa ya ganzi ya mgongoni (epidural) kwa sababu ganzi huzuia hisia za kusukuma. Kama ulipewa dawa ya ganzi ya mgongoni (epidural), vuta subira mpaka mlango wa kizazi utakapokuwa umeshatanuka vya kutosha. Unaweza pia ukaongeza uwezekano wa kuepuka kujifungua kwa kutumia vifaa hivi au kwa upasuaji kwa kutoanza kusukuma haraka mpaka pale mlango wako wa kizazi unapokuwa umekamilika kutanuka. Kama utasubiri mpaka utakapohisi hali ya kusukuma, au kichwa cha mtoto wako kimezidi kutokeza,utakuwa na nguvu zaidi na unaweza kusukuma vizuri zaidi.

Kabla ya kutumia njia hii kama hakuna dharura yoyote, kaa mikao tofauti ambayo itasaidia kufungua nyonga zako. Jaribu kuchuchumaa au kutekenya chuchu ili kuongeza nguvu uchungu na kupata nguvu zaidi ya kusukuma.

Kuchanwa eneo kati ya uke na njia ya haja ndogo (Episiotomy). Hii ni aina nyingine ya kujifungua kwa njia ya kawaida kwa msaada ambapo madaktari watafanya utaratibu huu ikiwa wanataka kumtoa mtoto haraka.

Kitendo cha kupasua chupa ya maji ya uchungu (Amniotomy). Daktari kifaa maalum chenye muonekano wa ndoana (plastiki) kutengeneza uwazi katika “amniotic sac”.

Kuanzishiwa uchungu (Induced labor)-hali hii inatokea pale daktari anapokuanzishia uchungu kabla haujaanza wenyewe. Kitendo hichi kitapendekezwa ikiwa daktari ana wasiwasi na afya yako au mtoto wako.

Kujifungua kwa upasuaji mkubwa (Cesarean Section)

Kujifungua kwa njia ya upasuaji hutokea kwa sababu kadhaa. Kama mtoto ni mkubwa au mdogo sana, kama unajifungua mapema au baada ya muda wa kujifungua kupita, una umri mkubwa au ni mwoga sana, kuchoka sana kwa sababu ya ujauzito au kuchoka sana kwa sababu ya uchungu, kama una mapacha, kama mtoto alitanguliza makalio, au kama wakati uliopita alijifungua kwa upasuaji.

Kiwango cha watu wanaojifungua kwa njia ya upasuaji mkubwa kimeongezeka sana kwa kipindi cha miaka thelathini iliyopita. Kujifungua kwa upasuaji huhusisha upasuaji mkubwa wa tumbo. Lazima ufanyike hospitalini, mahali ambapo dawa ya nusu kaputi, dawa za kuua bakteria (antibiotiki), na damu ya akiba pia inapatikana. Kujifungua kwa upasuaji ni operesheni zinazookoa maisha wanapofanyiwa wanawake wenye matatizo fulani wakati wa kujifungua, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kitovu (kamba ya kitovu kutangulia kichwa cha mtoto), kondo la nyuma linapoziba mlango wa uzazi (placenta previa), kondo la nyuma kushindwa kufanya kazi yake vizuri na kusababisha mtoto kushindwa kushuka kupitia kwenye fupa nyonga.

Kama unataka kujifungua kwa upasuaji mkubwa, utapelekwa kwenye chumba cha upasuaji, mahali ambapo utachomwa sindano ya dawa ya usingizi au utachomwa sindano ya ganzi kwenye uti wa mgongo (epidural) ili tumbo na miguu yako ife ganzi kabisa. Utaingiziwa Mpira wa kutolea mkojo ili kuhakikisha kibofu chako kinakuwa kitupu. Utaendelea kubaki macho. Kwa nadra sana wakati ambapo upasuaji unatakiwa ufanywe haraka sana, utachomwa sindano ya dawa ya nusu kaputi ili usinzie kwa sababu hufanya kazi kwa haraka zaidi kuliko ya uti wa mgongo (epidural).

Dawa ya nusu kaputi inapoanza kufanya kazi, daktari atakupasua kwa mlalo chini ya tumbo karibia kwenye kinena (Upasuaji wa wima hufanywa kwenye matukio ya dharura), upasuaji mwingine hufanyika tena kwenye misuli ya mlango wa kizazi ili kurahisisha mtoto kutoka. Halafu atamfyonza pua na mdomo mtoto wako, atakibana kitovu na kukikata na kuangalia upumuaji wa mtoto kama ni wa kawaida. Mambo yote yakienda vizuri, wewe na mwenzi wako mnaweza kumshikilia mtoto wenu wakati daktari akiendela kutoa kondo la nyuma na kushona kidonda. Utaratibu mzima huchukua muda wa saa moja. Kujifungua kwa upasuaji mkubwa kunaweza kuokoa maisha na kuboresha afya katika mazingira ya dharura, lakini sio kwamba ni njia ya kawaida tu ya kukimbilia kuchagua.

KUMBUKA

Vifaa vya kujifungua ambavyo mwanamke mjamzito na familia yake wanapaswa kushauriwa watayarishe kabla ya siku ya kujifungua ni:

 • Nguo safi kabisa za mama kulalia na za kumpangusa mtoto mzawa na kumfunika
 • Wembe mpya wa kukata kamba kitovu
 • Uzi safi mpya wa kufungia kitovu au kibana kitovu maalumu
 • Sabuni, kitambaa safi cha kusafishia na ikiwezekana, pombe tiba tiba ili kuepuka maambukizi
 • Maji safi ya kunywa, kumwosha mama mikono na mikono yako.
 • Ndoo tatu kubwa au bakuli.
 • Vifaa vya kutengenezea vinywaji vya kuongeza maji mwilini au chai.
 • Tochi ikiwa hakuna umeme katika eneo husika.

Kumbuka kuwa, matatizo yanayohusiana na ujauzito kama vile shinikizo la juu la damu na kuvuja damu yanaweza kutokea wakati wowote katika ujauzito, na ugonjwa wowote unaweza kutokea wakati wa ujauzito. Hali hizi zinapohisiwa katika awamu yoyote ya ujauzito, unapaswa kupatiwa rufaa mara moja na mkunga atakushauri kumuona  au kutafuta huduma ya kitabibu haraka iwapo dalili za hatari zitaonekana.

Katika hali ya dharura

Hakikisha kuwa wewe na mwenza wako pamoja na watu wengine katika familia wanajua mahali pa kutafuta usaidizi.

 • Fanya utaratibu wa usafiri
 • Akiba ya pesa za usafiri, dawa na matibabu mengine.
 • Nani ataandamana na wewe hadi kwenye kituo cha afya?
 • Nani ataangalia familia wakati mama hayupo.

Mwanamke mjamzito anaweza kuvuja damu kwa wingi wakati wa kujifungua au baada ya kuzaa hivyo anaweza kuhitaji kuongezewa damu. Hakikisha kuwa wewe au mume wako mmewatambua watu wazima wawili wenye afya watakaokubali kukutolea damu ikiwa mama atahitaji.  Na wasiliana na mtaalamu wa afya ili ahakikishe watu waliojitolea kutoa damu kuwa hawataathirika kwa kutoa damu, na kwamba afya yao kwa ujumla itakaguliwa kabla ya kutoa damu.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Kujifungua kwa Msaada wa Vifaa Maalumu

Wakati mwingine inaweza ikashindikana kwa mwanamke kumsukuma mtoto wake atoke, anaweza kuwa kwenye madawa au mwenye uchovu mwingi. Kunaweza kukawa na matatizo yanayosababisha anashindwa kumsukuma mtoto, au dharura imetokea na inalazimu kujifungua kufanikiwe kwa haraka.

Chuma za kujifungulia (Forceps)           

Forceps (chuma za kujifungulia) zinatumiaka kushikilia na kuvuta kichwa cha mtoto kilichokwama ndani ya njia ya kujifungulia. Daktari wako anaweza akapasua kidogo uke wako kuongeza njia ya forceps kuweza kupita na baadae kichwa cha mtoto wako. Wakati wa mkazo wa misuli ya mfuko wako wa uzazi ukiwa unasukuma, daktari atavuta taratibu kwa msaada wa forceps. Kwa kawaida kama majaribio matatu ya kumtoa mtoto yatashindikana utahitajika kufanyiwa upasuaji.

 Kifaa utupu cha kuvutia (Ventouse/Vacuum extractor)

Njia hii inatumia kifaa kinachotumia nguvu ya utupu (vacuum). Kikombe chenye utupu kitawekwa juu ya kichwa cha mtoto wako na kuunganishwa kwenye pampu. Baada ya kufanikiwa kukikamata kichwa vizuri kwa nguvu ya utupu, utaratibu kwa kujaribu kumsaidia mama ajifungue ni kama ilivyo kwenye forceps. Pale mama anapopata maumivu ya kusukuma na daktari pia atakuwa anavuta kichwa cha mtoto taratibu. Kama baada ya majaribio matatu kujifungua kumeshindikana, utahitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura kuweza kujifungua.

Kuchagua Njia na Mahali pa Kujifungulia

Je, naweza kuchagua mahali pa kujifungulia mtoto?

Uchaguzi wa mahali pa kujifungulia unategemea na sehemu unayoishi, na kama wewe na mtoto wako mna afya na ujauzito inaendelea vizuri.

Kwa kawaida chaguo linaweza kuwa kujifungulia:

 • Hospitalini
 • Kituo cha afya chenye mkunga
 • Nyumbani

Ikiwa unaishi mjini unaweza kuwa na chaguo la hospitali au kliniki kubwa za uzazi. Lakini kama unaishi kijijini chaguo lako linaweza kuwa dogo kwasababu ya uchache wa vituo vya kutolea huduma.Ni muhimu kuwasiliana na mkunga wako au mtoa huduma ili kufanya chaguo zuri la wapi ingefaa zaidi kujifungulia.

Lini naweza kwenda nyumbani baada ya kujifungua?

Kuna uwezekano mkubwa wa kurudi nyumbani siku au siku mbili baada ya mtoto kuzaliwa au hata siku hiyohiyo,kama kila kitu kikienda salama. Lakini kama wewe au mtoto wako hamko salama, mnaweza kukaa zaidi hospitali. Kama ulifanyiwa upasuaji, unaweza kukaa hospitali siku tatu hadi nne.

Unaweza kukaa zaidi kama hauko tayari kurudi nyumbani, au kama hakuna mtu wa kukusaidia nyumbani. Unaweza ongea na mkunga wako na kujua lini itafaa zaidi. Baadhi ya kinamama wanapenda kuangaliwa kwa karibu sana na kusikia salama wakiwa hospitali. Wakina mama wengine wanaona shida kulala, au wanagundua mtoto hawezi kulala vizuri kwenye wodi za uzazi kama ilivyo nyumbani.

Mikao Mbalimbali Wakati wa Uchungu

Baadhi ya mikao ambayo unaweza kujaribu ni pamoja na:

 1. Kusimama
 2. Kutembea tembea kadiri uwezavyo
 3. Kukaa
 4. Kuchuchumaa na kuegemea kiti, kitanda au mwenza wako
 5. Kupiga magoti na kuegemea mahali
 6. Kutambaa (Inaweza ikapunguza maumivu makali ya mgongo)

Kama mikao yote hii inakuletea shida na haisaidii na unaona kujilaza kwa mgongo ndio husaidia, jaribu kulala upande upande ukiwa umeweka mto kukusaidia. Vile vile kama ulivyokuwa unalala katika miezi 6 iliyopita.

Mbinu za Kupumua Kipindi cha Uchungu

Kujifunza mbinu za upumuaji zitakazokusaidia wakati wa uchungu ni jambo zuri kwani itakusaidia kuwa makini, kukabiliana na maumivu ya mkazo nyonga, kusaidia uchungu kwenda haraka, na pia kuhifadhi nguvu zako mpaka wakati wa kusukuma.

Wakati unahudhuria kliniki utakuwa umefundishwa mbinu mbali mbali za upumuaji, ikiwemo:

 1. Kuvuta pumzi taratibu ndani na kuitoa nje
 2. Vuta pumzi ndani kwa kutumia pua na utoe pumzi kwa mdomo, hesabu mpaka tatu unapovuta pumzi ndani na pia hesabu mpaka tatu wakati unatoa pumzi nje
 3. Kupumua haraka haraka husaidia wakati wa kusukuma, ukiupa uke wako nafasi ya kujinyoosha wakati mtoto anapita kwenye njia ya kujifungulia.

Kufanya mazoezi haya ya kupumua na mwenza wako mapema ni njia nzuri ya kujitayarisha kwa uchungu.

Matayarisho ya Mwisho Kabla ya Kujifungua

Mpaka sasa utakuwa umeshaandaa begi lako la uzazi utakalokwenda nalo kujifungua. Kuzijua dalili za uchungu ni hatua nyingine muhimu kwa matayarisho, kwani utajua ni wakati gani kuwasiliana na daktari au ni wakati gani uelekee hospitali.

Utahitaji kuwa na mpangilio wa nani atabaki na watoto wengine wakubwa kama unaishi nao nyumbani. Mfanyakazi wa ndani au ndugu yako anaweza akaitwa haraka na kuja kukaa na watoto wako wakati wewe umeenda kujifungua.

Usisahau kubeba pia begi la mtoto ambalo inatakiwa uwe umeshaliandaa pia. Kwenye begi hili utaweka nguo atakazovaa mtoto wako wakati wa kurudi nyumbani, nepi, kanga kadhaa, taulo laini la kumfuta akishazaliwa, chupa kadhaa za kumlishia mtoto kama umeamua hautamnyonyesha mtoto wako.

Pamoja na begi lako la uzazi, utahitaji pia kubeba pedi kadhaa za uzazi, nguo kadhaa za kubadilisha (kumbuka kuchukua nguo kubwa kubwa kwani hautarudi kwenye uzito wako wa kawaida ghafla tu baada ya kujifungua)

Kadiri utakavyojitayarisha vizuri, ndio utakavyokuwa na amani pale uchungu utakapoanza.

Mambo Matano ya Kufanya Kabla ya Kujifungua

Fanya usafi wa nyumba

Inapendeza zaidi nyumba kuwa safi pale ujio wa mwanao utakapowadia. Mnaweza kumuajiri mtu akasafisha nyumba yenu, lakini inaweza kuwa ghali sana. Hivyo unaweza muomba mwenzi wako, ndugu, marafiki au mfanyakazi wa ndani kama unaye kukusaidia kupanga na kusaidia usafi.

Andaa chakula cha kutosha

Mara mwanao atakapowasili, unaweza usipate muda wa kupika hasa kama hauna msaidizi. Ni vyema kuandaa vyakula na kuvihifadhi kwenye friji (kugandisha). Pia ni vyema kununua vyakula rahisi kuandaa ambavyo vitafanya wepesi wa kuandaa. Jaribu kujaza friji yako na vyakula vidogo vidogo vyenye afya kama yogurt, matunda yaliyokatwa vipande vidogo vidogo vitakavyokusaidia wakati umechoka na hauna hamu ya kula.

Jipendezeshe kidogo

Baada ya kujifungua muda wa kupendeza hautapatikana zaidi ya kuoga dakika tano wakati mwanao kalala. Hivyo jipendezeshe sawasawa wakati wa ujauzito kama kutengeneza nywele, kupaka kucha rangi, fanya massage kama unapendelea na mengineyo.

Starehe kidogo

Mnaweza kutumia muda huu wewe na mwenza wako kula chakula cha usiku kwenye mgahawa mzuri ili kurudisha mapenzi kwa mda kidogo, kabla mtoto hajawasili, maana itakua ngumu kufanya hivyo pindi utakapojifungua.

Tafuta daktari au mtaalamu wa afya wa mwanao.

Tafuta daktari mzuri au mtaalamu wa afya ya watoto mapema ili iwe rahisi kufanya miadi ya kukutana nae baada ya kujifungua.

Mambo 14 ya Kujiandaa Kabla ya Ujio wa Mtoto Mchanga

Karibu unakutana na mwanao! Vifuatavyo ni vidokezo vinavyoweza kukusaidia kujiandaa na ujio wa mwanao.

Andika mpango wa kujifungua  

Kama hujajiandaa, ni wazo zuri kuandaa maandishi ya kumwambia mkunga wako njia gani ya kujifungua ungependelea. Andika aina gani ya dawa za maumivu unataka, na iwapo unataka kuchelewa kufunga tumbo.

Mpango wako wa kujifungua unahitaji kuwa rahisi kubadilishwa ikiwa ungependa kuubadilisha au hali ikabadilika siku ya kujifungua. Lakini pia inaweza kuwa muongozo mzuri kwako, mwenza wako na timu nzima inayokujali.

Ongea na mwenzi wako/mzazi mwenzako

Ni muhimu kuhakikisha wewe na mzazi mwenzako mmekubaliana mambo kabla ya ujio wa mtoto. Usidhani mwenza wako anaelewa nafasi yake wakati wa uchungu na kujifungua, au kuhusu majukumu ya ndani ya nyumba baada ya mtoto kuwasili. Hivyo ni vyema kuongea na kuondoa utata na kutoelewana.

Pata ushauri kutoka kwa wamama wengine

Iwe ni mama yako, rafiki zako wenye watoto au jirani yako mwenye mtoto. Hakuna swali la kijinga inapokuja kwenye suala la ujauzito na malezi. Unaweza ukauliza swali lolote pale unapokuwa na wasiwasi na kutaka kujua zaidi kuhusu jambo fulani.

Tumia muda wako na watoto wako wengine wakubwa

Kama una mtoto mkubwa, tumia muda zaidi ukiwa naye sasa, kabla mtoto mdogo hajawasili, maana hutapata muda nae. Baadhi ya wazazi wanahofia huzuni itakayowapata watoto wengine wakihisi upendo wa wazazi kwao umeibiwa na mtoto mpya ndani ya familia. Hivyo tumia muda huu kuungana vizuri na mwanao kabla ya kujifungua, hii itasaidia kumkumbusha jinsi gani unampenda.

Fanya mpango wa kupata msaada zaidi

Wiki za kwanza na mtoto zinaweza kukuelemea. Kama una bahati ya kuwa na marafiki au ndugu waliotayari kukusaidia, ni muhimu kuwasiliana nao sasa. Maana utawahitaji sana wiki chache za kwanza au baada ya likizo ya mwenza wako kuisha (ikiwa alichukua likizo).

 

Fua nguo za mwanao na matandiko yake

Ngozi ya mwanao itakua laini sana. Hivyo ni vizuri kufua nguo zake na matandiko yake ya kulala kwa kutumia sabuni isiyo na kemikali sana, kabla ya kuzitumia. Hii itakua nzuri kwa ngozi ya mwanao na kupunguza uwezekano wa muwasho.

Pika chakula kingi

Wakati mtoto amewasili,itakua ngumu kuandaa na kujipikia chakula, hivyo andaa vyakula vingi sasa na hifadhi kwenye friji(frsehemu ya kugandisha). Hii inaweza kuwa msaada mkubwa katika wiki chache za mwanzo au zaidi baada ya kujifungua.

Safisha nyumba

Muda wa kusaifisha nyumba na kazi nyingine hautapatikana baada ya mtoto kuwasili.lama una bahati na unao uwezo wa kusafisha nyumba, fanya sasa! Ikiwa umechoka jaribu kufanya yale ya muhimu kama kuandaa vitu vya mtoto na malazi yake.

Andaa nepi za kutosha

Utashangazwa kiasi gani cha nepi mwanao atahitaji, hivyo andaa nyingi kadiri uwezavyo. Kama umepanga kutumia diapers andaa 10 mpaka 12 kwa siku. Ikiwa umechagua nepi za kawaida, idadi itategemea na aina ya nepi unayotumia (nzito au nyepesi)

Fungasha begi lako la hospitali sasa

Uchungu unaweza anza muda wowote, hivo ni vizuri kuandaa mahitaji muhimu kidogokidogo mpaka wiki ya 36. Fungasha kila kitu utakachohitaji kipindi cha uchungu na baada ya kujifungua kama mpango wako wa kujifungulia, nepi, nguo za kubadilisha na weka begi karibu na mlango.

Tafuta namba muhimu

Hakikisha una namba zote utakazohitaji kwenye simu yako. Kwa kufanya hivi utaweza kuwsiliana na mkunga wako au mshauri wako wa afya au hospitali ya karibu na wewe mapema. Ni busara pia kumtafuta mtu wa kumpigia ikiwa unahitaji usafiri au mtu wa kuwaangalia watoto wengine.

Andaa gari

Kama una mpango wa kujifungulia hospitali au kliniki jambo la mwisho kabisa kuepuka ni kupata shida ya gari. Hivyo hakikisha kuna mafuta ya kutosha na liko tayari kwa safari. Kama hauna gari basi hakikisha umeshaandaa usafiri utakaokupeleka hospitalini. Unaweza ukawa umeshawasiliana na dereva wa teksi ambaye atakuwa tayari kukufuata na kukupeleka hospitali kwa haraka pale utakapompigia simu ya dharura.

Chaji simu yako

Hakikisha simu imejaa chaji na tembea na chaja yako. Kwa kufanya hivi utaweza kuwapa ndugu na marafiki taarifa na kupiga picha za muhimu.

Kujifungua Watoto Mapacha au Zaidi

Kama una ujauzito wa mapacha au zaidi, inawezekana hautapita zaidi ya wiki 38. Kujifungua kwako kunaweza kukahitazi zaidi ya mtaalamu mmoja wa afya, akiwemo daktari wako, mkunga na mara kwa mara daktari bingwa kwa kila mtoto mmoja atakayezaliwa.

Kujifungua zaidi ya mtoto mmoja ni sawasawa na kujifungua mtoto mmoja, lakini watoto wako watahitaji uangalizi wa ziada, Kama utajifungua kwa njia ya kawaida, pale mtoto wa kwanza atakapozaliwa, wa pili atachukua muda mfupi zaidi kutoka.

Kama unajifungua zaidi ya watoto wawili, uwezekano mkubwa ni kwamba utajifungua kwa upasuaji. Kama ulipata matatizo yoyote katika ujauzito wako, kujifungua kwako huwa kunapangiwa siku maalumu na utaambiwa mapema kabla ya muda. Kutokana na mkao wa watoto wako tumboni pia unaweza kuhitaji kufanyiwa upasuaji. Mara chache huwa pacha wa kwanza anatoka na anayefuata kuhitaji upasuaji wa dharura ili kumuokoa. Lakini hili hutokea mara chache sana.

Madaktari watapendelea ujifungulie kwenye chumba cha upasuaji kama kujitayarisha kwa dharura yoyote itakayohitaji upasuaji. Kwa kawaida kujifungua mapacha huenda vizuri bila matatizo na punde utakuwa unamshika mtoto wako. Kama mapacha wako watakuja mapema kabla ya muda, watahitaji kuwepo hospitali kwa muda. Kwa sababu wamewahi baadhi ya viungo vyao havijakomaa vya kutosha kufanya kazi vyenyewe bila msaada. Mapacha huwa na uzito mdogo kuliko watoto wa kawaida wakati wanazaliwa hivyo ni vyema kuwa kwenye uangalizi mpaka watakapokuwa na afya njema kuruhusiwa kwenda nao nyumbani.

Kupona baada ya upasuaji au baada ya kujifungua kawaida mapacha ni sawa sawa tu na aliyejifungua mtoto mmoja.

Kuanzishiwa uchungu, sababu na faida zake

Kuanzishiwa uchungu

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kusababisha kuanzishiwa uchungu kuwa lazima. Uchungu utatakiwa kuanzishwa iwapo:

1. Umepitiliza siku yako ya kujifungua, mara nyingi utaanzishiwa uchungu kati ya wiki ya 41 na 42
2. Chupa imevunjika lakini uchungu haujaanza
3. Una kisukari; mara nyingi huanzishiwa uchungu mara tu baada ya wiki 38
4. Umepata shinikizo la damu la mimba (pre-eclampsia)
5. Una utokaji wa damu usio wa kawaida
6. Mtoto wako ametambulika kuwa amechoka tayari
7. Mrija wa chakula wa uzazi (placenta) kushindwa kupeleka chakula na oksigeni kwa mtoto
8. Unategemea kujifungua mapacha na daktari wako ameshauri uanzishiwe uchungu

Kama unafikiria ni kwa namna gani utafanikiwa kujifungua kwa kawaida, basi kuna vidokezo kadhaa vya kuzingatia:

1. Achana kabisa na sigara, pombe na madawa yoyote kipindi chote cha ujauzito wako
2. Mara zote wasiliana na daktari wako kabla ya kutumia dawa ya aina yoyote
3. Hudhuria kliniki mara kwa mara
4. Kula mlo bora na kamili
5. Fanya mazoezi mara kwa mara
6. Muone daktari mara moja pale unapopata dalili hatarishi au usiyoielewa

Kumbuka msaada wa kitaalamu wa kukupa uchungu ukihitajika haimaanishi kwamba kuna kitu ulikosea katika ujauzito wako. Wanawake wengi wanakuwa na ujauzito wenye afya kabisa lakini wanakuja kuhitaji kuanzishiwa uchungu wakati wa kujifungua. Kwa makadirio mwanamke mmoja kati ya watatu atahitaji msaada wa kitaalamu wakati wa kujifungua.

Kuanzishiwa uchungu kunaweza kufanyika kwa njia mbali mbali, ikiwemo:

1. Kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep): Moja ya njia maarufu za kuanzishiwa uchungu. Wakati wa tukio hili daktari au mkunga wako atatenganisha nyavunyavu nyembamba zilizozunguka kichwa cha mtoto wako kutoka kwenye mlango wa uzazi. Ni kawaida kwa kitendo hiki kurudiwa mara kwa mara.
2. Prostaglandini: Homoni hii ya kutengeneza maabara inayopatikana kama kimiminika laini au kidonge huingizwa ukeni. Homoni hii husaidia kuivisha mlango wako wa uzazi ili uweze kufunguka na kutanuka kiurahisi. Inaweza ikahitajika kuwekewa dozi kadhaa mpaka ianze kufanya kazi sawasawa.
3. AROM (Artificial rupture of membranes) – Kupasua chupa: Njia hii inahusisha kupasua chupa yako kwa kukusudia. Njia hii ilikuwa ndio njia maarufu zamani lakini kwa sasa inatumika zaidi kuharakisha uchungu kuliko kuanzisha uchungu.
4. Syntocinon: Hii ni kama homoni ya oksitosini iliyotengenezwa maabara. Husaidia kukuharakishia kupata uchungu. Hutumiwa zaidi pale njia ya kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep) pamoja na kutumia homoni ya Prostaglandini zote zimeshindwa kufanya kazi. Dawa hii hutolewa kwa dripu.
5. Kuanzishiwa uchungu kwa njia ya kawaida: Oksitosini ni homoni ambayo inahusishwa moja kwa moja na uchungu. Homoni hii pia huwa inatolewa pale matiti yanapoguswa guswa, kunyonywa n.k. Hivyo basi kwa miaka mingi inafahamika kwamba kufanya mapenzi pia ni njia ya kawaida kabisa inayoweza kukuanzishia uchungu.

Kama taratibu za kukuanzishia uchungu zote hazitafanikiwa, basi itabidi ujifungue kwa upasuaji kadiri itakavyoonekana ni muhimu kiafya. Lakini, wanawake wengi wameanzishiwa uchungu na wakaweza kupata uchungu na kujifungua kawaida.

Imepitiwa: Dec 2017