Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Umuhimu wa Kunywa Maji Wakati wa Ujauzito.

Ninywe Maji Kiasi Gani Kila Siku Wakati wa Ujauzito?

Uhitaji wa maji wakati wa ujauzito ni mkubwa zaidi ili kuhakikisha mfumo wa mwili unaosimamia maisha ya viumbe wawili unafanya kazi vizuri. Ijapokuwa utofauti upo wa kiasi gani cha maji unywe kwa siku kutokana na sababu mbalimbali kama aina na ukubwa wa mwili wako na kwa kiasi gani unaushughulisha mwili wako, kwa ujumla angalau glasi 8 mpaka 12 za maji kwa siku.

Inashauriwa ukiwa unakunywa maji, kunywa kidogo kidogo badala ya kugugumia maji mengi kwa wakati mmoja hali ambayo inaweza kukufanya kujisikia vibaya. Unaweza kujaza chupa mbili za maji asubuhi na kuhakikisha uko karibu nazo kila wakati itakusaidia kukumbusha kunywa maji kila utakapoiona.

Hakikisha unakunywa maji kabla, wakati na baada ya mazoezi. Kumbuka kiu ni ishara mwili wako unaelekea kupata upungufu wa maji.

Faida za Kunywa Maji Wakati wa Ujauzito

Maji yanasaidia kuzuia kukosa choo

Sasa wewe ni mjamzito, kumbuka unakula na kutoa taka za watu wawili. Hii ina maanisha utoaji taka mwilini ni mkubwa kuliko hapo awali. Maji ya kutosha mwili yatasaidia kuyeyusha takamwili na mabaki, kisha kuzisafirisha nje ya mwili. Unywaji wa maji ya kutosha unasaidia kutoa haraka nje ya mwili mabaki ya chakula baada ya kumeng’enywa kupitia njia ya mfumo wa umeng’enyaji. Ikumbukwe tatizo la kukosa choo linawapata wajawazito wengi bila kusahau athari zake ambazo zinahusisha kuota nyama sehemu ya haja kubwa (hemorrhoids).

Maji yanasaidia kuzuia maambukizi katika njia ya mkojo (UTI)

Unywaji wa maji ya kutosha unazimua mkojo, hali ambayo inasaidia mkojo kutolewa nje haraka na kuzuia bakteria zinazosababisha maambukizi katika kibofu kuzaliana (bakteria hizi zinazaliana mkojo unapobanwa kwa muda mrefu kwenye kibofu). Pia mama anayekunywa maji ya kutosha hana hatari ya kupata maambukizi katika kibofu na figo.

Maji yanapunguza joto la mwili.

Ni kweli ukiwa mjamzito joto la mwili ni kubwa. Lakini ukinywa maji ya kutosha wakati wa ujauzito unasaidia kupooza mwili na kufanya mwili kufanya kazi vizuri.

Maji yanapambana dhidi ya uchovu.

Moja ya ishara za awali za upungufu wa maji mwilini ni uchovu. Unywaji wa maji ya kutosha unasaidi kuhakikisha tatizo la uchovu wakati wa ujauzito linadhibitiwa, vilevile maumivu ya kichwa (ishara nyingine ya upungufu wa maji mwilini). Pia maji yanasiadia mwili kutoa sodiamu iliyozidi mwilini- hali ambayo itapunguza miguu kuvimba “edema”.

Je, Vinywaji Gani Vingine Mjamzito Anaweza Kutumia?

Maji ndio kinywaji cha kwanza kizuri na salama kwa mjamzito, lakini vipo vimiminika vingine vinavyoweza kutumiwa na mjamzito kusaidia mwili wake uwe na maji ya kutosha:

  • Maziwa
  • Maji yaliyotiwa ladha (ladha ya limao)
  • Juisi safi na salama ya matunda na mbogamboga (kuwa makini na sukari inayoongezwa katika juisi ya matunda)
  • Chai zisizo na kafeini.

Kwa hali yeyote, weka kikomo cha unywaji wa soda na vinywaji vingine vilivyo na kafeini kwasababu vina dutu inayosababisha kasi na kiwango cha kukojoa kuongezeka.

Kumbuka pia, karibia asilimia 20 za maji yanayoingia mwilini yanatoka kwenye vyakula. Matunda yana maji ya kutosha.

Ishara Mwili Wako Una Upungufu wa Maji.

Mwili wako utakuonyesha hauna maji ya kutosha kwa kuangalia ishara zifuatazo:

  • Kiu na njaa
  • Midomo kukauka na kuchanika.
  • Mabadiliko ya rangi ya mkojo. Mwili ukiwa na maji ya kutosha mkojo wako utakuwa na rangi ya njano ya kupauka (yaani “pale-yellow color”). Wakati mkojo wenye rangi ya njano iliyokolea ni ishara ya kukosa maji ya kutosha mwilini.
  • Kupungua kwa safari za kwenda uwani
  • Kutotoka jasho hata wakati wa joto
  • Tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu
  • Uchovu, kizunguzungu na maumivu ya kichwa. Upungufu wa maji mwilini unasababisha uchovu na maumivu ya kichwa, hakikisha unakunywa maji ya kutosha kutunza nguvu uliyo nayo kwasababu ujauzito ni kazi kubwa inayohitaji nishati ya kutosha haswa miezi ya kwanza.
  • Kusahau, kuchanganyikiwa kushindwa kuelewa na kukosa mwelekeo ni baadhi ya dalili za mtu mwenye hali inayoitwa “brain fog”.
  • Ngozi mwili kukauka.
  • Baadhi ya wajawazito wanapitia leba ya uongo (Braxton Hicks contractions)

Dalili kama kizunguzungu na kuchanganyikiwa, mapigo kasi ya moyo, mabadiliko ya kucheza kwa mtoto tumboni,shinikizo dogo la damu, mshtuko na ogani kushindwa kufanya kazi zinawapata wajawazito walio na tatizo kubwa la ukosefu wa maji.

Vidokezo Vitakavyokusaidia Kuhakikisha mwili una Maji ya Kutosha Muda Wote

Zipo baadhi ya siku unaweza kuhitaji msaada kuhakikisha unafikia dozi yako ya kila siku ya maji. Vifuatavyo ni vidokezo vitakavyokusaidia kuendelea kunywa maji:

  • Ongeza ladha, unaweza kuongeza kipande cha tango, limao majani ya mnanaa (mint) katika maji.
  • Jaribu chai zenye majani ya mitishamba, hakikisha daktari au mkunga wako anakupa kibali cha kutumia kiungo hicho.
  • Hakikisha una chupa ya maji mkononi mwako. Ni rahisi kufuatilia unywaji wako wa maji ukiwa na chupa yako ya maji mkononi nyakati zote.
  • Anza siku kwa kunywa glasi moja ya maji. Kunywa maji mara baada ya kuamka ni njia nzuri ya kujijengea tabia ya kunywa maji.
  • Kula vyakula vyenye maji kwa wingi kama vile supu, tikitimaji, nanasi n.k.

Kumbuka

Ukosefu wa maji ya kutosha mwilini wakati wa ujauzito unaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto tumboni.Inaweza kusababisha matatizo makubwa na hatari kwa afya kama vile:

  • Kupungua viwango vya maji yanayomzunguka mtoto ndani ya uterasi “amniotic fluid” ambayo ni muhimu katika maendeleo na ukuaji wa mtoto.
  • Mama kujifungua kabla ya wiki 37 za ujauzito kwasababu ya kupungua kwa “amniotic fluid”.
  • Mtoto kuzaliwa na kasoro za mirija ya neva za fahamu
  • Kiasi kidogo cha uzalishaji wa maziwa
  • Mtoto kuzaliwa na kasoro kwasababu ya ukosefu wa maji na virutubisho muhimu vya kumsaidia mtoto.
  • Mara chache,kukosa maji ya kutosha kunaweza hatarisha uhai au kusababisha mama kulazwa chumba cha wagonjwa mahutihuti.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Kunyonyesha Ukiwa Mjamzito

Je, ni Sawa Kuendelea Kunyonyesha Mtoto Wakati una Mimba Nyingine?

Kunyonyesha kunasaidia kuzuia kupata ujauzito, lakini sio mara zote. Inategemea na vitu kama vile mara ngapi unanyonyesha mwanao na umri wa mtoto wako. Kumbuka, inawezekana kushika mimba tena huku unanyonyesha mtoto wako.

Ikiwa utagundua wewe ni mjamzito tena, iwe ulipanga au bila kupanga, utakuwa na maswali mengi- kama kuendelea kumnyonyesha mtoto kutaathiri ujauzito wako mpya, mtoto anayenyonya, utokaji wa maziwa na mwili wako.

Ikiwa mama akagundua kuwa ni mjamzito wakati bado ananyonyesha. Mtoto anayenyonyeshwa anaweza kuwa mdogo hajafikia umri wa kuachishwa au mama mwenyewe anakuwa bado anapenda kumnyonyesha mtoto wake. Ikiwa mimba ni ya kawaida na yenye afya, inapendekezwa kuwa ni salama kabisa kuendelea kunyonyesha katika kipindi chote cha ujauzito. Katika makala hii utajifunza mambo muhimu na mikakati thabiti unayotakiwa kujua kuhusu unyonyeshaji ukiwa mjamzito.

Je, Nimuachishe Mtoto Kunyonya Mara Baada ya Kugundua Nina Ujauzito Mwingine?

Ujauzito mpya ni sababu iliyozoeleka ya kumuachisha mtoto kunyonya. Baadhi ya watoto wanaacha wenyewe na baadhi ya kina mama wanawahamasisha watoto wao kuacha kunyonya ili kujiandaa kwa ujio wa mtoto mpya atakayezaliwa. Lakini ikumbukwe hakuna haja ya kumuachisha mtoto kwasababu umeshika ujauzito mwingine. Unaweza kuendelea kumnyonyesha. Unaweza pia kuamua kuwanyonyesha wote wawili- mtoto mkubwa na kichanga wako atakayezaliwa.

Usalama wa Kunyonyesha Wakati wa Ujauzito

Kama umegundua umeshika ujauzito mwingine, hakikisha unaongea na mkunga au daktari wako juu ya historia ya afya yako. Daktari atakusaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu kuendelea kunyonyesha au kumuachisha mwanao.

Kawaida kunyonyesha baada ya kugundua una ujauzito mpya ni salama kabisa. Ikiwa una afya nzuri na ujauzito wako hausababishi matatizo yeyote ya kiafya, unaweza kuendelea kunyonyesa. Ingawa, zipo baadhi ya hali daktari akizishuhudia katika afya yako atakushauri umwachishe mwano kunyonya.

Wakati unanyonyesha mwili wako unatoa kichocheo kinachoitwa “oxytocin”. Homoni hii inawaunganisha mtoto na mama na kuleta upendo, vilevile homoni hii inasababisha mibano na mikazo ya mfuko wa uzazi (uterasi). Mibano na mikazo (The Braxton Hicks Contractions) hii sio hatari kwa ujauzito wa kawaida na wenye afya.

Sababu Ambazo Daktari Atakushauri Umuachishe Mtoto Kunyonya

Daktari anaweza kuwa na wasiwasi na kukushauri umwachishe mtoto kunyonya kama:

  • Ujauzito wako uko katika hatari kubwa ya kutoka
  • Ulishapitia tatizo la mimba changa kuharibika au kutoka
  • Ulijifungua kabla ya mda katika ujauzito uliopita (kabla ya wiki ya 37)
  • Unapata maumivu ya tumbo yanayoambatana na kutoka damu ukeni
  • Una ujauzito wa mapacha au zaidi
  • Hauongezeki uzito sahihi wenye afya.

Je, Kunyonyesha Kunaweza Athiri Mtoto Aliye Tumboni?

Hakuna ushahidi kuwa kunyonyesha ukiwa mjamzito kutaumiza ujauzito wako mpya au kuingilia ukuaji na maendeleo ya mtoto anayekuwa tumboni. Mwili wako unaweza kutengeneza maziwa ya mtoto anaye endelea kunyonya huku ukimtoa virutubisho vyote anavyohitaji mtoto aliye tumboni. Vifuatavyo vidokezo muhimu unavyotakiwa kukumbuka:

  • Mwili wako unahitaji nishati ya kutosha ili kutengeneza maziwa, kutoa virutubisho muhimu kwaajili ya mtoto anayekua tumboni, na kukuweka mwenye afya na imara. Ili mwili wako kuwa na nguvu na kuepusha upungufu wa aina yeyote ya virutubisho muhimu, kunywa maji ya kutosha, kula mlo kamili ulio na nyongeza ya kalori zenye afya, na pata mapumziko ya ziada.
  • Ongea na daktari wako ikiwa una tatizo lolote la kiafya kama vile kisukari au anemia, ili kuhakikisha unapata virutubisho muhimu na kalori sahihi unazohitaji.
  • Hudhuria miadi yako kila mwezi na fanya uchunguzi mara kwa mara kila unapoweza, ni muhimu ili kuwa na uhakika kuwa ujauzito wako unaendelea vizuri na unaongezeka uzito kama inavyotakiwa.

Je, Ujauzito Wako Mpya Unaweza Kumuathiri Mtoto Anayenyonya?

Mabadiliko katika ladha ya maziwa na kupungua kwa kiwango cha maziwa huweza kumuathiri mtoto anayenyonya. Mambo haya mawili yanaweza kusababisha mtoto mwenyewe kukataa kunyonya. Ikiwa mtoto wako yuko chini ya mwaka mmoja, mabadiliko haya yaangaliwe kwa umakini zaidi ili kuhakikisha mtoto anapata virutubisho vya kutosha. Endelea kumnyonyesha ili asikose virutubisho muhimu kutoka kwenye maziwa ya mama. Lakini, ikiwa mtoto wako ni mkubwa na tayari kaanza kula vyakula vigumu na kula mwenyewe, mabadiliko ya ladha na kiwango cha maziwa hayawezi kumuathiri.

Mabadiliko ya ladha ya maziwa

Wakati mtoto wako amezaliwa, atapokea maziwa ya kwanza yanayoitwa “colostrum”. Kadiri ujauzito wako unavyoendelea kukua ndivyo ladha ya maziwa itakavyobadilika kuelekea kwenye “colostrum” kwaajili ya ujio wa mtoto mpya. Mambo machache unayotakiwa kujua kuhusu mabadiliko haya ni kuwa:

  • “Colostrum” imejaa kingamwili na virutubisho, hivyo ni nzuri kwa mtoto mkubwa anayenyonya. Lakini, mwili hautengenezi “colostrum” nyingi hakikisha kichanga wako anapata kwa wingi maziwa haya yenye kingamwili na virutubisho vya kutosha haswa kama utaamua kunyonyesha mtoto mkubwa na kichanga wako baada ya kujifungua.
  • Mtoto anaweza kuendelea kunyonya bila tatizo hata baada ya mabadiliko ya ladha ya maziwa, au anaweza asipende utofauti wa ladha na kuacha mwenyewe kunyonya.
  • Maziwa haya ya awali “colostrum” yanamsaidia mtoto mchanga kutoa kinyesi cha kwanza nje ya miili yao “meconium”, vilevile kwa mtoto mkubwa ambaye bado ananyonya anaweza kupata dalili za kuharisha kutokana na maziwa haya ya awali yaliyojaa virutubisho na kingamwili za kutosha.

Mabadiliko ya kiwango cha maziwa

Ujauzito ni moja ya sababu ya upungufu wa kiwango cha maziwa. Mambo machache unayotakiwa kujua ni kwamba:

  • Unaweza kuona kupungua kwa kiwango cha maziwa mara baada ya kushika ujauzito au baadae kidogo.
  • Ikiwa mtoto wako anayenyonya yuko chini ya mwaka mmoja na umegundua upungufu wa kiwango cha maziwa ongea na mkunga wako. Inaweza kukuhitaji kutumia maziwa ya fomula sambamba na kunyonyesha ili kuhakikisha mtoto anapata virutubisho anavyohitaji.
  • Kama mtoto wako ana umri zaidi ya mwaka mmoja, hakikisha anapata virutubisho anavyohitaji kutoka kwenye vyakula mbalimbali vigumu anavyokula. Unaweza kuendelea kumnyonyesha kama afya yako inaruhusu na mwanao yuko tayari kunyonya.
  • Upungufu wa kiwango cha maziwa unasababisha maziwa kutoka taratibu kwenye titi. Baadhi ya watoto wanakatishwa tamaa na hali hii na kuacha kunyonya wenyewe.

Je, Ujauzito Mpya Unaweza Kumuathiri Mama Anayenyonyesha?

Ingawa inawezekana kuendelea kunyonyesha wakati wa ujauzito, zipo changamoto. Zipo njia nyingi ambazo ujauzito unaweza kukuathiri kama mama anayenyonyesha. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto unazoweza kupitia wakati wa kunyonyesha na vidokezo vitakavyokusaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Kuvimba kwa matiti na chuchu.

Ujauzito unaweza kurejesha tatizo la kunyonyesha la zamani. Mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa ujauzito yanaweza kusababisha tena maumivu ya chuchu na matiti. Kunyonyesha huku chuchu zimevimba kunaweza kuwa kugumu au kusababisha maumivu. Kwa bahati mbaya, suluhisho la chuchu zilizovimba wakati wa kunyonyesha halifanyi kazi wakati wa awali wa ujauzito kwasababu chanzo cha chuchu kuvimba ni mabadaliko ya vichocheo. Suluhisho la hali hii ni kuwa mvumilivu. Hali hii itadumu kwa miezi mitatu ya kwanza, japo kwa baadhi ya kina mama hali hii inaweza kuendelea kipindi chote cha ujauzito.

Unaweza kufanya yafuatayo ili kukabiliana na hali hii:

  • Weka kitu cha baridi juu ya chuchu zako
  • Vaa sidiria inayokufanya uwe huru (isikubane sana)
  • Jitahidi kumnyonyesha mtoto katika mazingira matulivu yatakayomfanya mtoto apunguze kuhangaika ili asisababishe kuvuta chuchu. Badala ya kumnyonyeshea sebuleni ambapo anaweza kubabaishwa na kelele za luninga au ndugu zake, nenda chumbani ambapo hakuna kelele au watu.
  • Jaribu mikao tofauti ya kunyonyesha.

Kuchoka

Ni kawaida kusikia uchovu kuliko kawaida ukiwa mjamzito kwasababu ya mabadiliko yote ya homoni yanayoendelea katika mwili wako. Kumlea mtoto mwingine na kumnyonyesha inaongezea uchovu huo. Kama unaweza, pata mapumziko ya kutosha. Inaweza kuwa ngumu haswa kama una mtoto anayetambaa au kukimbia kimbia, lakini fanya jitihada ya:

  • Kulala wakati mwanao akilala
  • Kaa kitako au lala kisha nyoosha miguu yako juu ukiwa unanyonyesha
  • Usiruke milo na kumbuka kunywa maji ya kutosha

Kadiri ujauzito unavyoendelea kukua, inakuwa ngumu kupata mkao mzuri wa kunyonyeshea mtoto wako. Fanya majaribio na tafuta mkao mpya utakaokupa unafuu wewe na mwanao. Pia unaweza kunyonyesha ukiwa umelala kwa ubavu.

Kumbuka

Wanawake wengi wanacha kunyonyesha mara baada ya kugundua wameshika ujauzito mwingine. Ikiwa hauko tayari, na daktari wako amekuhakikishia hakuna tatizo la kiafya linalokukabili hauna haja ya kumuachisha mwanao. Unaweza kuendelea kumnyonyesha mtoto wako kipindi chote cha ujauzito kwa usalama. Unaweza pia kuendelea kunyonyesha mwanao mkubwa hata baada ya kichanga wako kuzaliwa. Inaitwa “tandem nursing” kwa lugha ya kigeni.

Ni kweli, ujauzito unaleta kuvimba na maumivu ya matiti, kupungua kwa kiwango cha maziwa na uhitaji wa nishati ya zaidi mwilini. Ni rahisi kuchoka na kuelemewa. Unaweza kuamua kumuachisha mtoto wako kunyonya, na hii ni sawa kabisa. Ikumbukwe pia kuwa kipindi cha ujauzito kumuachisha mtoto kunyonya ni rahisi zaidi kwasababu ya mabadiliko ya ladha na kiwango cha maziwa, hivyo unaweza kuamua ni mda mzuri wa kuacha kunyonyesha. Fanya kile ambacho ni sahihi kwako na familia yako na usisikie hatia juu ya hilo.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Kujifungua kwa Njia ya Kawaida Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji (VBAC)

Ikiwa unajiuliza kama kujifungua kwa njia ya kawaida inawezekana baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji ujauzito uliopita, jibu ni kwamba inawezekana kwa wanawake wengi lakini kuna sababu zitakazo wasaidia wewe na daktari wako kufikia hitimisho kama inawezekana kwako au la.

Usalama kwako na mtoto wako ni jambo muhimu la kuzingatia. Kujifungua kwa kawaida baada ya kujifungua kwa upasuaji sio salama kwa kila mwanamke.

Ikiwa unajaribu kujifungua kwa njia ya kawaida unakuwa katika hatari kubwa ya kupata matatizo, ambayo yanaweza kusababisha utata wa afya ya wewe na mtoto wako- baadhi kuhatarisha maisha. Ndiyo maana ni muhimu kuongea na daktari wako kuhusu hatari hizi.

Ili daktari na wewe kufikiria uwezekano wa kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji, inakubidi wewe na mtoto wako muwe katika afya njema. Unaweza kujaribu kujifungua kwa kawaida hata ukiwa na ujauzito wa mapacha, cha msingi ni daktari kuhakikisha na kusema wote mko katika afya nzuri ya kuhimili zoezi zima.

Sababu hatari ambazo daktari hatakuruhusu kujifungua kwa kawaida baada ya kujifungua kwa upasuaji ujauzito uliopita ni pamoja na:

  • Uzito uliopitiliza (kama BMI yako ni 30 au zaidi)
  • Shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito (Pre-eclampsia)
  • Umri mkubwa (kawaida zaidi ya 35)
  • Upasuaji wako wa awali ulifanyika miezi 19 iliyopita.
  • Mtoto wako tumboni ni mkubwa sana.
  • Kama wakati wa upasuaji ulichanwa kwa wima (vertical cut) hauruhusiwi kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida. Kuna nafasi kubwa ya mshono wako kuachia wakati wa kusukuma mtoto, hali ambayo italeta madhara makubwa kwako na mtoto wako. Itakubidi kufanyiwa upasuaji tena.

 Faida za Kujifungua kwa Njia ya Kawaida Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Asilimia 70 ya wanawake wanaojaribu kujifungua kwa njia ya kawaida wanafanikiwa, wengine inashindikana kwasababu ya dharura zinazotekea wakati wa kujaribu, wanaishia kufanyiwa upasuaji.

Unaweza kutamani kujaribu kujifungua kwa kawaida baada ya upasuaji kwasababu ya sababu mbalimbali, jaribio hili likifanikiwa kuna faida ambazo ni:

  • Hakuna upasuaji utakaofanyika
  • Kiasi kidogo cha damu kitapotea
  • Uponaji wa haraka
  • Inapunguza nafasi ya maambukizi
  • Sio rahisi kusumbuka na kidonda kwenye kibofu, utumbo au ogani nyingine.
  • Inapunguza nafasi ya kuwa na matatizo makubwa wakati wa kujifungua kwa ujauzito ujao.

Kumbuka

Sio kila hospitali inatoa huduma ya mjamzito kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji katika ujauzito wake wa awali, hivyo katika mpango wako wa kujifungua hakikisha unahusisha hospitali unayotarajia katika mkakati wako ili kujua kama inatoa huduma hiyo. Hata kama nafasi ya mshono uliopita kuachia wakati wa kusukuma ni ndogo, hospitali inatakiwa kujiandaa kwa hali yeyote ya dharura inayoweza kutokea. Baadhi ya hospitali hazina utayari wa vifaa na watu wenye ujuzi kukabiliana na hali ya dharura.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Njia Mbalimbali za Kujifungua na Faida Zake

Kipindi hiki tofauti na zamani kumekuwa na njia mbali mbali za kujifungua. Hii intokana na maendeleo ya teknolojia na uwepo wa wataalamu mpaka kwenye vituo vya chini kabisa vya afya. Hali hii imesaidia kupunguza kwa kasi vifo vya mama na mtoto. Zifuatazo ni njia mbalimbali zinazotumika kujifungua. Ni vyema kuzitambua na kuzielewa mapema ili uweze kufahamu mapema ni njia gani ambayo itatumika wakati wa kujifungua kwako.

Ukweli Unaotakiwa Kujua Kuhusu Njia za Kujifungua

  • Chaguo zilizopo wakati wa kujifungua ni pamoja na: kujifungua bila msaada (kawaida), kujifungua kwa msaada na kujifungua kwa upasuaji.
  • Unaweza kujifungulia nyumbani, zahanati/kituo cha afya au hospitalini.
  • Kujifungua kwa njia ya kawaida bila dawa hakuna maumivu, ni rahisi kama mama atajifunza mbinu za kupumua wakati wa kusukuma mtoto katika chumba cha kujifungulia.
  • Katika kuhakikisha njia gani ni sahihi kwa mama wakati wa kujifungua upimaji wa faida na hasara za njia hiyo uende sambamba na pendekezo la mjamzito ambalo ni salama kwake.
  • Kila mwanamke ana uzoefu wa kipekee wakati wa kujifungua, wnaawake wengi wanakiri wakati wa kuzaa mtoto kuna amabatana na maumivu. Hata hivyo, maumivu hay ani ya mada mfupi, zipo aina na njia madhubutu za kupunguza ukali wa maumivu wakati wa kujifungua.

Kujifungua kwa Njia ya Kawaida (Kujifungua Bila Msaada- Unassisted birth)

Kujifungua kwa njia ya kawaida

Wewe na familia yako mnaweza kubaini ishara za kawaida za uchungu. Mwanamke anaweza kujifungua siku kadhaa au hata wiki kadhaa kabla au baada ya tarehe iliyotarajiwa, kulingana na tarehe ya kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida. Mwanamke anapofahamu maana ya uchungu, ataweza kufahamu kitakachotokea. Ufahamu huu humsaidia kutulia zaidi na kuwa na ujasiri katika siku au wiki za mwisho za ujauzito.

Yafahamu maagizo dhahiri ya jambo la kufanya pale uchungu unapoanza (kwa mfano ikiwa utakuwa na maumivu ya mkakamao wa misuli ya fumbatio ya tumbo la uzazi au kuvuja kwa kilowevu cha amniotiki, maarufu kama kupasuka chupa). Hakikisha kuwa kuna mtu atakaye mwita mkunga au mtaalamu mwingine ili kukuzalisha haraka iwezekanavyo.

Mkunga wako anafaa kuzingatia maandalizi ya kujifungua na:

  • Kuheshimu chaguo la mama. Anapaswa kumpa mama habari zote zinazohitajika kuhusu uzalishaji safi na salama, lakini hatimaye anapaswa kuheshimu chaguo lake kuhusu mahali pa kujifungulia na mtu angelipenda kuandamana naye.
  • Kukusaidia kutambua mahali pa kupata usaidizi wakati wa kujifungua na kipindi cha baada ya kujifungua kinachofuata punde.
  • Kupangia gharama yoyote ya ziada inayohusiana na kujifungua kwako.
  • Kutayarisha vifaa vya kumtunza mama na mtoto wake atakayezaliwa.

Faida za Kujifungua kwa Njia ya Kawaida

  • Watoto wanaozaliwa kwa njia ya kawaida wanakuwa na matatizo madogo ya upumuaji.
  • Mama anapona haraka na kuepuka aina yeyote ya matatizo yanayohusiana na upasuaji kama vile uchanwaji wa utumbo au ogani za eneo la tumbo wakati wa upasuaji.
  • Njia hii ya kujifungua ina kiasi kidogo cha maambukizi na ukaaji mfupi hospitali au kituo cha afya.

Hasara za Kujifungua kwa Kawaida

  • Kuchanwa eneo kati ya njia ya haja kubwa na uke.

Njia za kujifungua kwa Msaada (Assisted Births)

Kujifungua kwa njia ya kawaida kwa msaada wa vifaa maalumu

Vifaa hivi huwasaidia akina mama na watoto pale watoto wanapotakiwa kuzaliwa haraka. Ni zana muhimu sana kwa mtu mwenye ujuzi wa kuzitumia.

Kifaa cha kunyonyea cha utupu (vacuum extractor) ni kifuniko kidogo cha kunyonyea ambacho hutosha kwenye kichwa cha mtoto kinachotokeza angali akiwa ndani ya uke. Hewa hujazwa ndani ya kile kifuniko ili kiweze kushikilia vizuri ngozi ya kichwa cha mtoto wakati mtaalam anapokivuta. Utaratibu huu unaweza kusababisha damu kuganda kwenye kichwa cha mtoto, kitaalam inaitwa (cephalohematoma)

Koleo hufanana na mikasi mirefu yenye bawaba ambayo mwishoni imejikunja ili kutosha kwenye kichwa cha mtoto. Kifaa hiki kinaweza kuleta madhara makubwa sana kwa watoto na mama vikitumiwa vibaya au vkitumiwa na mtu asiye na ujuzi.

Matumizi ya kifaa cha kunyonyea (vacuum-cup) yameongezeka. Sababu tatu zilizosababisha ongezeko la matumizi ya vifaa hivi ni kwasababu ya:

  • Ongezeko la matumizi ya dawa ya usingizi ya epidural, ambayo hurefusha hatua ya kusukuma
  • Muda maalum wa kusukuma uliotengwa kwa wanawake katika baadhi ya hospitali
  • Jitihada za hospitali kupunguza uwezekano wa kufanyiwa upasuaji.

Kifaa cha kunyonyea (vacuum-cup) mara nyingi hutumiwa pamoja na dawa ya ganzi ya mgongoni (epidural) kwa sababu ganzi huzuia hisia za kusukuma. Kama ulipewa dawa ya ganzi ya mgongoni (epidural), vuta subira mpaka mlango wa kizazi utakapokuwa umeshatanuka vya kutosha. Unaweza pia ukaongeza uwezekano wa kuepuka kujifungua kwa kutumia vifaa hivi au kwa upasuaji kwa kutoanza kusukuma haraka mpaka pale mlango wako wa kizazi unapokuwa umekamilika kutanuka. Kama utasubiri mpaka utakapohisi hali ya kusukuma, au kichwa cha mtoto wako kimezidi kutokeza,utakuwa na nguvu zaidi na unaweza kusukuma vizuri zaidi.

Kabla ya kutumia njia hii kama hakuna dharura yoyote, kaa mikao tofauti ambayo itasaidia kufungua nyonga zako. Jaribu kuchuchumaa au kutekenya chuchu ili kuongeza nguvu uchungu na kupata nguvu zaidi ya kusukuma.

Kuchanwa eneo kati ya uke na njia ya haja ndogo (Episiotomy). Hii ni aina nyingine ya kujifungua kwa njia ya kawaida kwa msaada ambapo madaktari watafanya utaratibu huu ikiwa wanataka kumtoa mtoto haraka.

Kitendo cha kupasua chupa ya maji ya uchungu (Amniotomy). Daktari kifaa maalum chenye muonekano wa ndoana (plastiki) kutengeneza uwazi katika “amniotic sac”.

Kuanzishiwa uchungu (Induced labor)-hali hii inatokea pale daktari anapokuanzishia uchungu kabla haujaanza wenyewe. Kitendo hichi kitapendekezwa ikiwa daktari ana wasiwasi na afya yako au mtoto wako.

Kujifungua kwa upasuaji mkubwa (Cesarean Section)

Kujifungua kwa njia ya upasuaji hutokea kwa sababu kadhaa. Kama mtoto ni mkubwa au mdogo sana, kama unajifungua mapema au baada ya muda wa kujifungua kupita, una umri mkubwa au ni mwoga sana, kuchoka sana kwa sababu ya ujauzito au kuchoka sana kwa sababu ya uchungu, kama una mapacha, kama mtoto alitanguliza makalio, au kama wakati uliopita alijifungua kwa upasuaji.

Kiwango cha watu wanaojifungua kwa njia ya upasuaji mkubwa kimeongezeka sana kwa kipindi cha miaka thelathini iliyopita. Kujifungua kwa upasuaji huhusisha upasuaji mkubwa wa tumbo. Lazima ufanyike hospitalini, mahali ambapo dawa ya nusu kaputi, dawa za kuua bakteria (antibiotiki), na damu ya akiba pia inapatikana. Kujifungua kwa upasuaji ni operesheni zinazookoa maisha wanapofanyiwa wanawake wenye matatizo fulani wakati wa kujifungua, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kitovu (kamba ya kitovu kutangulia kichwa cha mtoto), kondo la nyuma linapoziba mlango wa uzazi (placenta previa), kondo la nyuma kushindwa kufanya kazi yake vizuri na kusababisha mtoto kushindwa kushuka kupitia kwenye fupa nyonga.

Kama unataka kujifungua kwa upasuaji mkubwa, utapelekwa kwenye chumba cha upasuaji, mahali ambapo utachomwa sindano ya dawa ya usingizi au utachomwa sindano ya ganzi kwenye uti wa mgongo (epidural) ili tumbo na miguu yako ife ganzi kabisa. Utaingiziwa Mpira wa kutolea mkojo ili kuhakikisha kibofu chako kinakuwa kitupu. Utaendelea kubaki macho. Kwa nadra sana wakati ambapo upasuaji unatakiwa ufanywe haraka sana, utachomwa sindano ya dawa ya nusu kaputi ili usinzie kwa sababu hufanya kazi kwa haraka zaidi kuliko ya uti wa mgongo (epidural).

Dawa ya nusu kaputi inapoanza kufanya kazi, daktari atakupasua kwa mlalo chini ya tumbo karibia kwenye kinena (Upasuaji wa wima hufanywa kwenye matukio ya dharura), upasuaji mwingine hufanyika tena kwenye misuli ya mlango wa kizazi ili kurahisisha mtoto kutoka. Halafu atamfyonza pua na mdomo mtoto wako, atakibana kitovu na kukikata na kuangalia upumuaji wa mtoto kama ni wa kawaida. Mambo yote yakienda vizuri, wewe na mwenzi wako mnaweza kumshikilia mtoto wenu wakati daktari akiendela kutoa kondo la nyuma na kushona kidonda. Utaratibu mzima huchukua muda wa saa moja. Kujifungua kwa upasuaji mkubwa kunaweza kuokoa maisha na kuboresha afya katika mazingira ya dharura, lakini sio kwamba ni njia ya kawaida tu ya kukimbilia kuchagua.

KUMBUKA

Vifaa vya kujifungua ambavyo mwanamke mjamzito na familia yake wanapaswa kushauriwa watayarishe kabla ya siku ya kujifungua ni:

  • Nguo safi kabisa za mama kulalia na za kumpangusa mtoto mzawa na kumfunika
  • Wembe mpya wa kukata kamba kitovu
  • Uzi safi mpya wa kufungia kitovu au kibana kitovu maalumu
  • Sabuni, kitambaa safi cha kusafishia na ikiwezekana, pombe tiba tiba ili kuepuka maambukizi
  • Maji safi ya kunywa, kumwosha mama mikono na mikono yako.
  • Ndoo tatu kubwa au bakuli.
  • Vifaa vya kutengenezea vinywaji vya kuongeza maji mwilini au chai.
  • Tochi ikiwa hakuna umeme katika eneo husika.

Kumbuka kuwa, matatizo yanayohusiana na ujauzito kama vile shinikizo la juu la damu na kuvuja damu yanaweza kutokea wakati wowote katika ujauzito, na ugonjwa wowote unaweza kutokea wakati wa ujauzito. Hali hizi zinapohisiwa katika awamu yoyote ya ujauzito, unapaswa kupatiwa rufaa mara moja na mkunga atakushauri kumuona  au kutafuta huduma ya kitabibu haraka iwapo dalili za hatari zitaonekana.

Katika hali ya dharura

Hakikisha kuwa wewe na mwenza wako pamoja na watu wengine katika familia wanajua mahali pa kutafuta usaidizi.

  • Fanya utaratibu wa usafiri
  • Akiba ya pesa za usafiri, dawa na matibabu mengine.
  • Nani ataandamana na wewe hadi kwenye kituo cha afya?
  • Nani ataangalia familia wakati mama hayupo.

Mwanamke mjamzito anaweza kuvuja damu kwa wingi wakati wa kujifungua au baada ya kuzaa hivyo anaweza kuhitaji kuongezewa damu. Hakikisha kuwa wewe au mume wako mmewatambua watu wazima wawili wenye afya watakaokubali kukutolea damu ikiwa mama atahitaji.  Na wasiliana na mtaalamu wa afya ili ahakikishe watu waliojitolea kutoa damu kuwa hawataathirika kwa kutoa damu, na kwamba afya yao kwa ujumla itakaguliwa kabla ya kutoa damu.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Kujifungua kwa njia ya upasuaji, kwa lugha ya kigeni “C-section” ni njia ya kujifungua mtoto kwa kuchana kuta za sehemu ya chini ya tumbo na mji wa mimba (uterasi) ili kutoa mtoto aliye kwenye mji wa mimba.

Katika kipindi fulani kabla uchungu kutokea mama anajua kwa uhakika atajifungua kwa njia fulani, lakini hali tofauti za kiafya zinaweza kubadilisha mpango huo.

Daktari au mkunga anaweza kuamua utajifungua kwa njia ya upasuaji mara moja ukiwa katika uchungu au ukiwa katika chumba cha kujifungua. Mabadiliko haya ya haraka yanaweza kutokea ikiwa afya yako au mtoto aliyeko tumboni imebadilika ghafla na kuwa mbaya, hivyo kufanya kujifungua kwa njia ya kawaida kuwe hatari kwa afya ya mama.

Ni busara kujifunza anachopitia mama wakati wa kujifungua kwa njia ya upasuaji hata kama sio mpango wako wa kujifungua, itakusaidia ikiwa mabadiliko yatatokea katika chumba cha kujifungulia na kuhitajika upasuaji ili kuokoa maisha yako na mtoto wako.

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni salama kwa mama na mtoto. Lakini ni upasuaji mkubwa, inashauriwa isichukuliwe kimzaha.

Aina za Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Upasuaji Uliopangwa

Ikiwa unajua mapema utajifungua kwa njia ya upasuaji, unapata nafasi ya kujua tarehe ya kujifungua na kutopitia uchungu wa kuzaa. Kabla ya utaratibu huu kufanyika utapata dripu ili mwili wako uwe na dawa na majimaji. Utawekewa pia mpira wa mkojo kusaidia kukusanya mkojo katika kibofu chako kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini.

Kama utajua mapema kuwa utajifungua kwa upasuaji, utapata muda kwa kutosha kujitayarisha, lakini kama ni upasuaji wa dharura inaweza kukushtua. Utachomwa sindano ya kaputi kisha kulazwa kwenye kitanda cha upasuaji. Wakati mwingine inaweza ikahitajika kuchomwa sindano ya kaputi ambapo utakuwa hutambui kinachoendelea mpaka utakapoamka. Faida nyingine ni kwamba utaweza kumuona mtoto wako mara tu anapotolewa tumboni. Daktari atakuruhusu umbebe mara baada ya upasuaji kumalizika. Kama una mpango wa kumnyonyesha mtoto wako, unaweza kujaribu kumlisha mtoto. Lakini sio kila mama anapata nafasi ya kumbeba mtoto wake mara baada ya upasuaji.

Wakati mwingine watoto waliozaliwa kwa njia ya upasuaji wanapata shida ya upumuaji, hali hii inawafanya kuhitaji msaada kutoka kwa madaktari. Usiwe na wasiwasi utaweza kumbeba mtoto wako mara baada ya daktari kuamua kuwa ana afya nzuri na hali yake iko salama.

Baada ya mtoto kuzaliwa, daktari atatoa plasenta yako na kukushona. Utaratibu wote huu utachukua dakika 45 mpaka lisaa limoja tu.

Sababu za Upasuaji Uliopangwa

Daktari au mkunga wako anaweza kukupangia kujifungua kwa upasuaji siku ya kujifungua ikiwa una:

  • Aina fulani ya matatizo ya kiafya. Magonjwa makubwa kama magonjwa ya moyo, kusukari, shinikizo kubwa la damu au tatizo la kibofu cha mkojo ni baadhi ya matatizo yatakayofanya kujifungua kwa kawaida kuwe hatari kwa mwili wa mjamzito.
  • Maambukizi. Ikiwa wewe ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi au una ugonjwa wa zinaa ambao haujapona, upasuaji wakati wa kujifungua ni jambo lisilo epukika. Hii ni kwasababu virusi vinavyosababisha magonjwa haya vinaweza ambukizwa kwa mtoto kipindi cha kujifungua.
  • Afya ya mtoto. Ugonjwa kurithi unaweza fanya safari ya mtoto kupita ukeni kuwa changamoto kwa mtoto wako.
  • Mtoto mkubwa.
  • Uzito wa mjamzito. Kuwa na uzito mkubwa au uzito uliopitiliza kunaongeza nafasi ya mjamzito kujifungua kwa njia ya upasuaji kwa sababu ya shida mbalimbali zinazoambatana na uzito mkubwa kama vile kisukari wakati wa ujauzito, lakini pia kwasababu wanawake wenye uzito mkubwa wa mwili wanapitia uchungu wa kuzaa unaochukua muda mrefu.
  • Mtoto akikaa mkao wa tofauti tumboni (breech position). Mtoto anapotanguliza miguu kwanza na ikashindikana kumgeuza, mkunga wako ataamua upasuaji ni lazima.
  • Ujauzito wa mapacha au zaidi.
  • Tatizo ya kondo la nyuma kujishikiza karibu na mlango wa kizazi. Pale kondo la nyuma limejishikiza karibu na shingo ya uzazi, sio rahisi kujifungua kwa njia ya kawaida kwasababu mtoto hatapita vizuri. Kawaida plasenta ina kazi ya kuingiza virutubisho kwa mtoto, kumpa hewa safi na kuondoa hewa chafu. Ikiwa plasenta imezuia kidogo au sana mlango wa uzazi (placenta previa) upasuaji ni njia pekee salama kwako na mtoto wako.
  • Kondo la nyuma kuachia kabla ya muda wa kujifungua (placenta abruption). Endapo kondo la nyuma limenyofoka au sehemu ndogo kuachana na ukuta wa kizazi, upasuaji wa haraka hauna budi kufanyika ili kuokoa maisha ya mtoto. Upasuaji ukichelewa kufanyika mtoto atazaliwa amechoka au wakati mwingine kufia tumboni kwasababu ya ukosefu wa virutubisho na hewa safi.
  • Matatizo mengine hatari ya kiafya. Matatizo kama ujauzito unaosababisha shinikizo kubwa la damu au shinikizo la damu linalokua taratibu na kuathiri mfumo wa kati wa fahamu na kusababisha mama kupoteza fahamu na wakati huohuo hakuna tiba inayofanya kazi. Mkunga wako atashauri upasuaji ili kulinda afya za wote.
  • Ombi la mama. Mjamzito anaweza kuomba kufanyiwa upasuaji kwasababu za kibinafsi. Mkunga anaweza kumzikiliza mama na kumshauri njia salama kulingana na ombi la mama.
  • Ikiwa ulijifungua kwa upasuaji ujauzito wa awali. Mama aliyejifungua kwa upasuaji ujauzito wake wa awali anaweza kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida endapo kovu limepona vizuri, afya yako iko salama na sababu iliyokufanya ukafanyiwa upasuaji katika ujauzito wako wa awali hazipo.
  • Upasuaji unafanyika ikiwa mtoto ni wa kipekee. Kwa wanandoa ambao wamepata shida katika kutafuta mtoto kwa muda mrefu, wanaweza kuamua upasuaji ufanyike wakati wa kujifungua ili kuhakikisha mama na mtoto hawapati madhara wakati wa kujifungua. Wanawake waliopata mimba ya kwanza kwenye umri mkubwa sana kwa mfano miaka zaidi ya 35, wanawake waliopata shida ya mimba kuharibika sana au mtoto kufariki wakati wa kujifungua huchagua upasuaji wakati wa kujifungua.

Upasuaji wa Dharura

Wakati wa upasuaji wa dharura, mambo machache yatabadilika ikiwa ni pamoja na kasi na uharaka wa operesheni. Daktari anaweza kumzalisha mtoto wako kwa dakika mbili baada ya kuchana uterasi yako (inachuka dakika 10 mpaka 15 kwa upasuaji uliopangwa).

Ikiwa mtoto wako anashida katika upumuaji au mapigo ya moyo hayako sawa, madaktari watahitaji kumtoa haraka ndani ya mji wa mimba na kumuwahisha hosspitali kwaajili ya huduma za kitabibu haraka ili aweze kuwa salama.

Katika upasuaji wa dharura kwa kawaida utachomwa sindano ya uti wa mgongo, itakayokufanya usisikie maumivu kuanzia kwenye nyonga kwenda chini. Au ukapigwa kaputi na kulala upasuaji mzima. Kwa bahati mbaya hutasikia au kumuona mtoto wako akiwa anazaliwa, ila hautasikia maumivu au mkandamizo wowote katika tumbo lako la uzazi. Habari njema ni kwamba, baada ya kuzinduka utaweza kumbeba, kumuona na kumlisha kichanga wako.

Upasuaji wa dharura unafanyika pale:

  • Ikiwa kitovu kitatoka nje kabla mtoto, hali hii itasababisha usambazaji wa hewa ya oksijeni kukatishwa.
  • Uterasi ikichanika.
  • Uchungu umechelewa kuanza au hauendi kama inavyotakiwa. Kutoendelea au kusimama kwa uchungu ni moja ya sababu kubwa inayopelekea wajawazito wengi kujifungua kwa upasuaji. Hali hii inapelekea shingo ya uzazi kutofunguka na kupelekea mtoto kushindwa kutoka. Kwa kawaida mkunga au daktari huangalia hali ya shingo ya kizazi mara kwa mara kwa kuingiza vidole viwili kupitia uke, kwa kufanya hivi atagundua kwa kiasi gani (sentimita) ngapi shingo ya uzazi imetanuka. Hii ni njia mojawapo ya kuangalia maendeleo ya uchungu.
  • Mjamzito kuchoka au mtoto kuchoka. Ikiwa daktari atakuona umechoka au kipimo maalum kinachowekwa kwenye tumbo kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto kuonyesha dalili za mtoto kuchoka daktari ataamua upasuaji wa haraka ufanyike.

 Upasuaji wakati wa kujifungua unachukua muda gani?

Upasuaji ni haraka, procedure yenyewe inachukua dakika 10 au pungufu, ikifuatiwa na dakika nyingine 30 za kushona.

Nini hutokea wakati wa upasuaji?

Iwe ni upasuaji uliopangwa tangu awali au wa dharura, upasuaji wa kawaida unafuata mpango maalum.

Maandalizi na sindano ya nusu kaputi

Utafanyiwa vipimo vya damu ili kuangalia wingi wa dam una kundi la damu ili pale itakapotokea shida baada ya upasuaji damu iongozwe kiurahisi. Upasuaji unaanza kwa utaratibu wa dripu na sindano ya kaputi ili sehemu ya chini ya mwili ili usiweze kusikia maumivu na mgandamizo wowote lakini utakua macho na utafanikiwa kushuhudia pale mwanao anapotolewa ndani ya mji wa mimba. Kisha sehemu cha chini ya tumbo la uzazi litanyolewa (kama inahitajika) na kusafishwa kwa dawa maalum ya kuua vijidudu. Utawekwa mpira wa kukusanya mkojo kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini.

Ikiwa unahitajika kufanyiwa upasuaji wa dharura, utachomwa dawa ya kukufanya ulale kipindi kizima cha upasuaji ambayo mara nyingi huchukua dakika chache. Ukiamka utasikia kusinzia kwasababu ya dawa ya usingizi, utajisikia kichefuchefu na kuchoka sana. Unaweza pia kuwa na koo kavu iliyosababishwa na mrija wa kupeleka hewa kwenye mapafu unaowekwa wakati wa upasuaji.

Kuchanwa na kuzaa

Mara baada ya sehemu ya chini ya mwili kufa ganzi au kulala, daktari atachana kidogo kwenye sehemu ya chini ya tumbo-juu kidogo ya uke. Kovu la mchano huu hupotea kadiri mda unavyoenda ikiwa kazi ilifanyika kwa umakini. Daktari atachana tena ndani sehemu ya chini ya uterasi. Zipo aina mbili za michano:

Mchano mlalo. Unatumika kwa asilimia 95 wakati wa upasuaji, kwasababu misuli chini ya uterasi ni mwembamba hivyo damu kutoka kidogo. Pia sio rahisi kuachia wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida hapo baadae.

Mchano wima. Aina hii ya mchano inafanyika pale mtoto amekaa sehemu ya chini ya uterasi au amekaa katika mkao usio kawaida.

Baada ya hapo maji yanayopatikana tumboni mwa mama mjamzito yanayomzunguka mtoto kwenye hatua zake zote za ukuaji hufyonzwa nje, kisha mtoto wako atatolewa nje. Kwasababu uteute wa ziada haukutolewa vizuri nje ya njia ya hewa ya mtoto wako, ufyonzwaji wa ziada utahitajika ili kuhakikisha mapafu ya mwanao ni safi kabla ya kumsikia mtoto wako akilia kwa mara ya kwanza.

Kumbeba mtoto wako kwa mara ya kwanza

Baada ya kitovu kukatwa, daktari ataondoa placenta, kisha kukagua haraka ogani zako za uzazi kabla ya kuanza kukushona. Kisha ushonaji wa sehemu uliochanwa utafanyika, ambao unachukua dakika 30 au zaidi.

Utapokea dawa ya kupunguza nafasi ya kidonda kupata maambukizi na “oxytocin” ya kudhibiti damu kutoka na kusaidia uterasi kubana na kurudi katika hali yake ya awali katika dripu. Shinikizo lako la damu, mapigo ya moyo na kasi yako ya upumuaji na wingi wa damu inayotoka utaangaliwa mara kwa mara.

Kama utakuwa umejifungua kwa upasuaji utahitaji kuendelea kukaa hospitali kwa siku kadhaa uanze kupona. Kupona baada ya upasuaji ni sawa tu na kupona kwa upasuaji mwingine wa eneo la tumbo. Tofauti kubwa ni kwamba badala ya kupoteza kiungo kimoja kama figo au “appendix” unapata mtoto.

Mojawapo ya matatizo unayoweza kuyaona baada ya kujifungua ambayo ni ya kawaida ni kama hali ya kusikia maumivu kwenye uke, kutokwa na damu nzito nyeusi, matiti kuvimba, nywele kudondoka, uchovu na kutokwa jasho jingi.

Tegemea Yafuatayo Baada ya Kutoka Chumba cha Upasuaji.

Daktari wako atakuchunguza kwa karibu mpaka pale dalili zote za dawa za kuondoa maumivu zimeisha. Kumbukumbu zako zinaweza zikawa zinasumbua kama ulitumia dawa ya usingizi au nusu kaputi. Madhara ya sindano ya nusu kaputi inayochomwa kwenye uti wa mgongo huchukua muda mrefu zaidi kuliko madhara ya dawa za usingizi.

Baada ya dawa ya kuondoa maumivu kuisha utaanza kusikia kidonda kinauma. Ukali wa maumivu unategemea sababu tofauti, ikiwemo uwezo wako wa kusikia maumivu na kama una historia ya kujifungua kwa upasuaji hapo awali, kwani maumivu ya upasuaji wa pili na kuendelea huwa yanaonekana sio makubwa sana kama yale uliyoyasikia kwenye upasuaji wa kwanza. Utapewa dawa za maumivu kupambana na hali hii.

Unaweza ukasikia kichefuchefu, ambapo daktari atakupatia dawa itakayokuzuia kupata kichefuchefu au kutapika.

Nesi atakuwa anakuchunguza mara kwa mara. Atakuwa anachukua vipimo vyako muhimu (joto, shinikizo la damu (BP), na upumuaji). Atakuwa pia anaupima mkojo wako na chochote kinachotoka ukeni. Pia atakuwa anaangalia mfungo wa kidonga chako cha upasuaji, sehemu mfuko wako wa uzazi ulipo na ugumu wake na wakati huo huo akihakikisha mirija ya dripu na mpira wa mkojo ipo sehemu yake.

Kama hali yako itaendelea vizuri, utapelekwa kwenye wodi ndani ya masaa kadhaa baada ya upasuaji kufanyika. Uchunguzi wa vipimo vyako muhimu utafanyika kwa mara nyingine. Kama una uwezo wa kukojoa mwenyewe basi mpira wa mkojo utatolewa masaa 24 baada ya upasuaji.

Unaweza ukawa unasikia maumivu kwenye uke kama mwanamke aliyejifungua kwa njia ya kawaida. Hii isikupe wasiwasi maumivu haya ni kutokana na kukaza kwa misuli ya mfuko wako wa uzazi ukiwa unajirudia kwenye hali yake kabla ya ujauzito.

Dripu za maji zitatolewa na utaruhusuwa kuanza kutumia vinywaji kwa kunywa mwenyewe masaa 24 baada ya upasuaji (Huu ndio muda ambao utumbo wako utakuwa umeshaanza kusogeza chakula kawaida na kufanikiwa kutoa hewa chafu nje kwa njia ya kujamba). Taratibu utaruhusiwa kurudia mlo wako wa kawaida kadiri siku zinavyosogea. Mama wanaonyonyesha inabidi wapate maji ya kutosha mwilini.

Utategemea kutolewa nyuzi zako (Kama sio zile zinazoyeyuka zenyewe) ndani ya siku 4 hadi 6 baada ya upasuaji.

Mwishoni kabisa kama kila kitu kitakuwa kimeenda sawa kwako na mtoto, utaruhusiwa kurudi nyumbani ndani ya siku 3 hadi 7 baada ya upasuaji.

Hali gani hatari za kiafya zinazoweza kutokea baada ya kujifungua kwa upasuaji?

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni salama kabisa, lakini mara chache matatizo ya kiafya yanatokea kwa mama na mtoto baada ya upasuaji kufanyika.

Kwa mama, matatizo haya ni pamoja:

  • Kupoteza damu,
  • Mama kupata maambukizi eneo la mshono.
  • Muitikio mbaya wa dawa zinazotumika kipindi cha upasuaji (dawa za nusu kaputi, dawa za kupunguza maumivu n.k).
  • Kujeruhiwa wakati wa upasuaji,
  • Damu kuganda kwenye mishipa ya damu haswa miguuni,viungo ndani ya nyonga na mapafu. Huku madaktari wakifanya kila namna kuhakikisha hali hii haitokei, ni vizuri ukatembea baada ya upasuaji kama unaweza.
  • Mara chache sana, uterasi inaweza kuvimba au kuwasha.
  • Maambukizi katika kuta za kizazi
  • Mama kupata hatari ya kujifungua kwa upasuaji upasuaji unaofuata.

Hatari za kiafya za muda mrefu ni pamoja na: kupata kovu baya kwenye eneo la mshono na kuchanika kizazi kwenye ujauzito unaofuata.

Mtoto aliyezaliwa kwa njia ya upasuaji anaweza:

  • Kupitia kipindi cha mpito cha kupumua haraka haraka, kitakachodumu kwa siku chache baada ya kujifungua, hali hii inasababishwa na mabaki ya maji (yanayopatikana ndani ya mji wa mimba kumzunguka mtoto kipindi chote cha ujauzito) ndani ya mapafu ya mtoto.
  • Kama upasuaji umefanyika kabala ya wiki ya 39 ya ujauzito, mtoto atakuwa katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kupumua ikiwa mapafu yake hayajakua vizuri-lakini kumbuka daktari atakua karibu nawe kumuangalia kwa ukaribu zaidi na kutibu aina yoyote ya tatizo litakalozuka ukiwa bado hospitalini.

Kumbuka

Ukishuhudia ongezeko la maumivu ya nyonga, kutokwa uchafu usio wa kawaida au homa baada ya mtoto kuzaliwa, wasiliana na daktari wako mara moja.

IMEPITIWA: AGUSTI, 2021.

Umuhimu wa Lishe Bora kwa Mjamzito Kabla ya Kujifungua.

Vitamini unazotumia kabla ya kujifungua zina virutubisho vingi mtoto wako anavyohitaji, hivyo basi kuna umuhimu gani waa mama mjamzito kuangalia kwa makini lishe yake?

Inaathiri afya ya mtoto wako maishani: Kila unachokula ukiwa mjamzito kinamuathiri mtoto na maisha yake kwa ujumla, hivyo ni muhimu kula vizui kwa manufaa ya mtoto hapo baadae. Kuna baadhi ya tafiti zinazoshauri ulaji wa vyakula vyenye chumvi, mafuta na sukari vinaathiri mapendekezo ya ladha ya mtoto hapo baadae. Hii inaweza kumsababisha mtoto kupata changamoto katika ulaji, afya na uzito kutokana na aina ya lishe uliyomtambulisha ukiwa mjamzito.

Chakula kinasaidia mwili kufyonza virutubisho vyenye afya: Ikiwa unakula mlo kamili mwili wako una nafasi kubwa ya kupata na kufyonza virutubisho na madini yanayohitajika katika mwili.

Chakula bora kinasaidia mwili kufanya kazi vizuri: Ukiwa unakula vizuri mwili wako utakushukuru. Utakuwa na nguvu ya kutosha, utajisikia vizuri na pengine kuepuka kero, usumbufu na maumivu ya kawaida ya ujauzito.

Aina za Matunda Mazuri Wakati wa Ujauzito

Ndizi

Ndizi ni chakula kizuri sana wakati wa ujauzito. Zinashibisha na zina viwango vikubwa vya madini ya kalishiamu na potasiamu ambayo yanasaidia matatizo ya misuli ya miguu kukaza. Ikiwa una hamu ya kitu chenye sukari kilicho salama kwako na mtoto tumboni, ndizi za kuiva ni chaguo sahihi. Lakini kama una kisukari kilichosababishwa na ubebaji mimba, chagua kula ndizi za kupikwa (mbichi).

Tufaha (apple)

Matunda haya yana vitamini A na C, maji ya kutosha na nyuzinyuzi (fiber) zitakazokusaidia kulainisha choo.

Tikiti Maji

Tunda hili lina kiwango kikubwa cha maji kuliko tunda linguine lolote-92%. Ikiwa unapambana na tatizo la kukosa maji mwili wakati wa ujauzito, unashauriwa kula tunda hili. Tikiti maji lina madini ya potasiamu, zinki na foliki asidi kwaajili ya kupambana na misuli ya miguu kukaza wakati wa usiku na kusaidia ukuaji wa uti wa mgongo wa mtoto tumboni.

Machungwa

Chungwa linaweza kuwa tamu au chachu, ladha hizi zina pendwa na wanawake wengi ambao wanasubuliwa na kichefuchefu wakati wa ujauzito. Yana kiwango kikubwa cha maji, ni chanzo kizuri sana cha vitamini C. Vitamini hii inachangia kukuza kinga yako na mtoto tumboni, na pia inasaidia kujenga tishu muhimu kwa ajili ya ukuaji wa kimwili wa mtoto.

Parachichi

Parachichi lina madini chuma,magnesiamu, potasiamu na nyuzinyuzi (fiber). Madini chuma yanayotumika kuzuia anemia, magnesiamu na potasiamu yanasaidia tatizo la misuli ya miguu kukaza na kichefuchefu. Parachichi ni chanzo cha fati unayotakiwa kupata ukiwa mjamzito.

Peasi

Ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi zinazosaidia kupambana na tatizo la kukosa choo. Ni chanzo kizuri pia cha vitamini C, pamoja na madini chuma, magnesiamu na foliki asidi.

Embe

Ni chanzo kizuri cha vitamini C na A, inayosaidia kukuza kinga ya mtoto.

Faida za Matunda Wakati wa Ujauzito

Je, unataka ujauzito salama na wenye afya?

Kuna sababu nyingi za kula matunda ukiwa mjamzito, nazo ni pamoja na:

Yanatoa virutubisho muhimu: Mtoto wako anahitaji virutubisho fulani ili kukua vizuri. Virutubisho vinavyotolewa na matunda ni pamoja na vitamini C na foliki. Vitamini C ni muhimu kujenga tishu, inasaidia kukuza kinga ya mwili ya mtoto na kuruhusu uhifadhi wa madini chuma yanayotumika kuzuia anemia. Foliki inasaidia kujenga uti wa mgongo na pia kumkinga mtoto anayekua dhidi ya kasoro katika neva za fahamu na hivyo kuepusha dosari katika ubongo, mgongo na uti wa mgongo (neural tube defects).

Yanasaidia kukidhi hamu ya vyakula vitamu: Utofauti mmojawapo wa matunda ni kuwa matamu au machachu, ladha zote hizi ni pendwa kwa wajawazito. Kuchagua tunda badala ya peremende au biskuti itakusaidia kumaliza hamu katika njia ya kuridhisha na salama kwa afya.

Ni chaguo zuri ukisikia kichefuchefu: Ikiwa unapata changamoto ya kichefuchefu wakati wa ujauzito, ni ngumu kuweka chakula tumboni kwa muda mrefu. Vyakula vitamu na baridi ni vizuri ikiwa una pambana na magonjwa ya asubuhi, hakikisha unatunza matunda ya kutosha kwenye friji kwaajili ya kifungua kinywa.

Yanasaidia kudhibiti sukari katika damu: Matunda yana nyuzinyuzi (fiber) zinazosaidia kuratibu ufyonzaji wa sukari katika mfumo wa damu.

Matunda yanakufanya uwe na maji ya kutosha mwilini: Unahitaji kunywa maji ya kutosha ukiwa mjamzito. Tunda lina zaidi ya asilimia 80 ya maji, hivyo ikiwa umechoka kunywa maji kila saa unaweza kuchagua kula matunda kuhakikisha mwili wako unakaa na maji.

Yanasaidia kukabiliana na tatizo la kukosa choo: Ukiwa mjamzito, umeng’enyaji wa chakula unakua polepole, hali hii inaweza sababisha kukosa choo- lalamiko la kawaida kipindi cha ujauzito. Ikiwa unatumia virutubisho vyenye madini ya chuma yanaweza kusababisha kukosa choo. Tatizo kubwa la kukosa choo linaweza kusababisha “hemorrhoids”. Njia nzuri ya kuondokana na tatizo la kukosa choo ni ulaji wa vyakula ambavyo ni vyanzo vizuri vya nyuzi nyuzi na kunywa maji (matunda yana vyote viwili-maji na nyuzi nyuzi).

Kiasi Gani cha Matunda Nile Nikiwa Mjamzito?

Ingawa ulaji wa matunda ni afya, lakini ikumbukwe matunda ni chanzo cha sukari, ambayo inatakiwa kuwekwa kikomo ukiwa mjamzito. Inashauriwa mjamzito kula matunda mara 2-4 kwa siku.

Je, Kuna Matunda Natakiwa Nisile Wakati wa Ujauzito?

Hakuna kikomo cha kula matunda ikiwa limeiva na safi. Ni muhimu kuhakikisha unasafisha vizuri matunda kabla ya kula ili kuepuka uchafu utakaosababisha ugonjwa. Mchanganyiko wa maji na vinegar ni mzuri na salama kusafishia matunda hasa yaliyokuzwa kwa kemikali za kiwandani (nyanya, tufaha, zabibu, peasi, strawberi n.k)

Kumbuka

  • Nanasi limepata sifa ya kusababisha mimba kutoka na kusadikika kuchochea uchungu kabla ya mda wa kujifungua. Ijapokuwa hakuna ushahidi wa kisayansi kuunga mkono madai haya, nanasi linajulikana kama tunda salama kutumia katika viwango sahihi wakati wa ujauzito.
  • Tunda pekee linalotakiwa kuepukwa ni papai bichi, papai ambalo halijaiva lina dutu ambayo inachochea mikazo ya mfuko wa mimba.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Kutoka Kwa Mimba Changa (Miscarriage)

Kutoka kwa mimba changa ni nini?

Miscarriage au kutoka kwa mimba changa ni kupoteza ujauzito kabla haujafikia wiki ya 20. Jina la kitaalamu kwa upotevu huu wa ujamzito mchanga ni “Spontaneous abortion” ikimaanisha “upotevu mimba wa ghafla”.

Zaidi ya asilimia 80 ya upotevu mimba changa hutokea katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito. Upotevu wa mimba ni vigumu kutokea baada ya wiki 20 za mwanzo za ujauzito kupita. Na kama ikitokea madaktari huita hali hii kama upotevu mimba uliochelewa “Late miscarriage”.

Dalili za upotevu mimba changa

Dalili za “miscarriage” ni pamoja na:

  • Kutoka kwa damu inayoanza kutoka kidogo kidogo na kuendelea mpaka kuanza kutoka kwa wingi
  • Maumivu makali ya tumbo la kukata (cramps)
  • Maumivu ya tumbo
  • Uchovu
  • Maumivu ya mgongo yanayoongezeka
  • Homa inayoambatana na dalili zozote kati ya hizo hapo juu
  • Kupungua uzito
  • Kutoka uchafu mweupe wenye upinki ukeni
  • Kukaza kwa misuli ya nyonga (contractions)
  • Kutoka kwa vinyama nyama kama damu iliyoganda kutoka ukeni
  • Dalili dhoofu za ujauzito

Kama una dalili kati ya hizo hapo juu ni vyema kuhudhuria kituo cha afya kwa ushauri Zaidi. Watakuambia kama ni dalili za dharura au kufanyiwa vipimo kuchunguza ujauzito wako kwa ujumla.

Nini husababisha upotevu wa mimba changa kutokea?

Mara kwa mara kutoka kwa mimba changa hutokea pale mtoto anaekua tumboni akiwa na matatizo ya kigenetiki. Matatizo haya hayana uhusiano na mama.

Matatizo mengine yanayoweza kusababisha uwezekano wa kutoka kwa mimba changa ni kama:

  • Maambukizi
  • Matatizo ya kiafya kwa mama kama ugonjwa wa kisukari au matatizo ya thairoidi
  • Matatizo ya mfumo wa homoni
  • Matatizo katika uitikiaji kinga mwili (Immune response)
  • Matatizo ya kimaumbile kwa mama
  • Matatizo katika umbo la mfuko wa kizazi
  • Uvutaji wa sigara
  • Unywaji wa pombe
  • Matumizi ya madawa ya kulevya
  • Kuwa kwenye uwepo wa ukaribu na mionzi au viambata sumu

Mwanamke anakuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupoteza mimba ikiwa changa kama:

  1. Ana umri zaidi ya miaka 35
  2. Ana matatito mengine ya kiafya kama kisukari na matatizo ya kithairoidi
  3. Ameshawahi kupata kupoteza mimba changa mara tatu au zaidi

Udhoofu au kulegea kwa mlango wa mfuko wa uzazi (Cervical Insufficiency)

Kutoka kwa mimba ikiwa changa mara nyingine hutokea pale mama mjamzito anapokuwa na udhoofu au ulegevu wa mlango wa kizazi. Hii inamaanisha mlango wa kizazi hauwezi kuhimili ujauzito kikamilifu na hivyo kufunguka na ujauzito kutoka kabla ya muda wake. Mara nyingi aina hii ya upotevu wa ujauzito mchanga hutokea katika hatua ya pili ya ujauzito. Huwa kuna dalili chache sana kabla ya upotevu wa aina hii kutokea. Unaweza ukahisi mkandamizo wa ghafla, unaweza ukavunja chupa (maji mengi kutoka ukeni), na nyama nyama pamoja na kondo la nyuma la ujauzito kutoka ukeni bila ya kupata maumivu makali.

Madaktari kwenye nchi zilizoendelea hutibu aina hii ya upotevu mimba changa kwa kushona nyuzi kwenye mlango wa kizazi kwenye ujauzito wako utakaofuata. Hufanya hivi kwenye walau wiki ya 12 ya ujauzito. Nyuzi hizi zitasaidia kuufanya mlango wa kizazi uendelee kufungwa mpaka utakapokaribia kujifungua ndipo nyuzi hizi hutolewa na utajifungua kawaida.

Aina za kutoka kwa mimba changa

Kuna aina mbalimbali za upotevu mimba changa, kama:

Upotevu mimba changa hatarishi. Hii hutokea pale unapokuwa unatokwa na damu na kuna hali ya hatari kwa mama kupoteza ujauzito wake lakini mlango wa kizazi haujafunguka. Katika hali hii kama sababu za kutokwa kwa damu zitatatuliwa basi ujauzito huendelea bila matatizo.

Upotevu mimba changa usioepukika. Hapa mama mjamzito hutokwa na damu na pia anakuwa na maumivu ya tumbo mkazo (crampings), na pia mfuko wa kizazi umefunguka. Uwezekano wa kutoka kwa mimba changa kwenye hali hii ni wa hali ya juu sana.

Upotevu mimba changa usiokamilika. Baadhi ya nyama nyama kutoka kwa mtoto wako na sehemu ya kondo la nyuma na mfuko wa mimba vinatoka nje ya uke na baadhi vinabaki ndani ya uke.

Upotevu mimba changa uliokamilika. Ujauzito wote unatoka nje ya mwili wako. Kila kitu kinatoka, yaani, mtoto, mfuko wa mimba na kondo la nyuma. Aina hii mara nyingi hutokea kabla ya wiki ya 12 ya ujauzito kufika.

Upotevu mimba ulionusurika. Aina hii inahusisha kifo cha kiini cha mimba lakini nyama nyama za ujauzito husika zinabaki kwenye mfuko wa uzazi bila kutoka nje.

Upotevu mimba changa unaojirudia rudia. Aina hii inatambulika pale unapopoteza mimba zaidi ya tatu mfululizo ambazo hazikufikia umri wa zaidi ya wiki 12. Aina hii ya upotevu mimba changa hutokea kwa asilimia moja tu (1%) ya wenza wanaojaribu kupata mtoto.

Daktari atatambuaje kwamba una tatizo la upotevu mimba changa?

Kuhakikisha kwamba umepata upotevu mimba changa, daktari wako atafanya yafuatayo:

  • Uchunguzi wa mlango wako wa kizazi kuangalia kama umefunguka
  • Kipimo cha “ultrasound” Hapa atajaribu kuangalia maendeleo ya mtoto tumboni na kutafuta mapigo ya moyo ya mtoto. Kama itashindikana kupata jibu la moja kwa moja kipimo hiki kinaweza kurudiwa baada ya wiki moja.
  • Vipimo vya damu. Hapa daktari ataangalia uwepo wa homoni za ujauzito kwenye damu yako na kulinganisha kiwango cha homoni hizi na vipimo vilivyofanywa hapo awali. Pia ataangalia wingi wa damu kama umekuwa ukitokwa na damu nyingi ukeni.
  • Vipimo vya vinyama vinyama vilivyotoka ukeni pia huweza kufanyika kama vilikuwa vinatoka. Hii husaidia kuwa na uhakika kwamba umepata upotevu mimba changa na pia kuweza kutambua kama kuna matatizo mengine yanayosababisha kupatwa na tatizo hili.
  • Kipimo cha kromosomu (chromosome test). Kipimo hiki kinaweza kufanyika kama wewe na mwenza wako mmepoteza zaidi ya mimba changa mbili mfululizo. Daktari atachunguza kama mfumo wenu wa genetiki ndio unaosababisha upotevu huu.

Matibabu ya upotevu mimba changa

Asilimia 85% ya wanawake wanaopata upotevu mimba changa hufanikiwa kupata ujauzito salama na kujifungua salama baadae. Kupata upotevu mimba changa haimaanishi una tatizo la uwezo wa kupata watoto. Kwa upande mwingine, karibia asilimia 1 mpaka 2 ya wanawake hupata upotevu mimba changa unaojirudia rudia. Yani mara tatu au zaidi. Baadhi ya watafiti wanaihusisha hali hii na magonjwa ya ukinzani wa kinga mwili binafsi (autoimmune diseases)

Kama umepata upotevu mimba changa mara mbili mfululizo, ni vyema kuacha kujaribu kupata ujauzito, tumia uzazi wa mpango na wasiliana na mtaalamu wa afya ili waweze kutambua sababu ya upotevu wako wa mimba changa mfululizo.

Kama upotevu wako wa mimba changa ni uliokamilika na mfuko wa uzazi ni mtupu, inawezekana hautahitaji matibabu zaidi.

Wakati mwingine sio tishu zote na nyama nyama hutoka nje ya mfuko wa uzazi. Kama hili litatokea, daktari wako atafanya “Dilation and Curretage”. Haya ni matibabu ambayo itambidi daktari aupanue mlango wa uzazi na kutoa kila kitu kilichabaki kwenye mfuko wa uzazi kwa umakini. Pia kuna madawa ambayo ukitumia husaidia kutoa tishu zilizobaki kwenye mwili ziweze kutoka nje.

Baada ya utokaji wa damu kuisha unaweza ukaendelea na shughuli zako za kila siku. Kama mlango wako wa uzazi umefunguka lakini ujauzito bado upo salama daktari wako ataweza kufunga mlango wa kizazi kwa kuushona ili kuepusha ujauzito kutoka mpaka pale wakati wa kujifungua utakapofika.

Kama kundi la damu yako ni lile lenye Rh hasi (Rh-), daktari wako anaweza akakupa chembechembe tiba za damu ziitwazo (Rh Immune Globulin). Hizi husaidia kuepusha wewe kutengeneza kinga mwili (antibodies) ambazo zinaweza zikamdhuru mwanao au mimba zijazo.

Unaweza ukafanyiwa vipimo vya damu, vipimo vya genetiki au madawa kama umeshapata upotevu mimba changa mara mbili mfululizo. Kuweza kuhakikisha kwamba una upotevu mimba changa mfululizo (recurrent miscarriages) daktari wako atafanya vipimo vifuatavyo:

  • “Ultrasound” ya nyonga
  • Hysterosalpingogram (Hii ni X-ray ya mfuko wa uzazi na mirija ya uzazi kwa pamoja)
  • Hysteroscopy (Daktari wako atatumia mrija mrefu mwembaba wenye mwanga na kamera kuingia kwenye mfuko wako wa uzazi kuweza kuona kama una matatizo yoyote)

Dalili mbalimbali baada ya kupata upotevu mimba changa

Kutoka kwa damu na hali ya kujisikia vibaya ni dalili mojawapo baada ya kupata upotevu mimba changa. Kama utakuwa na kutoka kwa damu nyingi ikiambatana na homa, mwili kutetemeka na maumivu makali, hudhuria kituo cha afya haraka kwani hizi ni dalili za maambukizi.

Pamoja na dalili za kimwili unaweza pia ukawa unajihisi kuwa na hisia za huzuni, kujilaumu na pia kuwa na wasiwasi kuhusu mimba zitakazofuata. Unachojisikia ni kawaida na ni vyema kupitia hatua hii ya huzuni kuliko kuipotezea mbali na kuiacha ikusononeshe ndani kwa ndani.

Kama unaweza na hautajali, ni vyema kuliongelea swala hili na watu wako wa karibu kama mwenza wako, rafiki au mwanafamilia uliyemzoea. Vikundi vya wamama waliopoteza mimba kwenye jamii vinaweza kuwa na manufaa makubwa kwako na kwa mwenza wako. Pia muulize daktari wako kama kuna taarifa au ushauri wa ziada ambao anaweza kukupatia. Kumbuka kila mtu anapona na kuhuzunika na kurudia hali yake ya kawaida tofauti. Hivyo usikate tamaa.

Kupata mimba tena baada ya upotevu wa mimba changa

Unaweza ukapata ujauzito tena baada ya upotevu wa mimba changa. Zaidi ya 85% ya wanawake waliojaribu mara moja baada ya kupoteza mimba changa walipata ujauzito na kuendelea na kuja kujifungua salama. Kuwa na upotevu wa mimba changa haimaanishi kwamba una tatizo kwenye uwezo wako wa kupata mtoto. Hivyo hivyo asilimia 1 mpaka 2 ya wanawake wanaweza wakapata upotevu mimba changa unaojirudia rudia (mara tatu au zaidi).

Kama umepata upotevu mimba changa mara mbili mfululizo, ni vyema kuacha kujaribu kupata ujauzito, tumia uzazi wa mpango na wasiliana na mtaalamu wa afya ili waweze kutambua sababu ya upotevu wako wa mimba changa mfululizo.

Ni wakati gani ujaribu kupata ujauzito tena baada ya kupoteza mimba changa

Ni vyema kufanya mazungumzo haya na daktari wako. Wataalamu wengine wa afya wanasema ni vyema kusubiria kwa muda fulani kabla ya kupata ujauzito mwingine. Muda kati ya mzungumko mmoja wa hedhi mpaka miezi mitatu kabla ya kufikiri kujaribu tena kupata ujauzito. Kuzuia upotevu mwingine wa mimba changa daktari wako anaweza kukupa matibabu kutumia “Progesterone”, homoni inayosaidia kiini mimba kujishika kwenye mfuko wa uzazi na kusaidia maendeleo yake kwenye hatua za mwanzo za ujauzito.

Kuchukua muda kupona kimwili na kiakili ni muhimu pia baada ya kupoteza mimba changa. Ni vyema kutokujilaumu na kujiona mwenye makosa. Hakikisha unapata msaada wa kimawazo na ushauri kujitayarisha na kuwa tayari pale utakapoweza kujaribu tena.

Je, utazuiaje kutokea kwa upotevu mimba changa?

Upotevu mimba changa mara nyingi hutokea kwa sababu kuna tatizo kwenye ujauzito husika. Huwezi kuzuia hili. Kama daktari wako atakupima na kuona tatizo, aina mbalimbali za matibabu zinapatikana.

Kama una ugonjwa, kuutibu ugonjwa husika kutaongeza uwezekano wa kupata ujauzito ulio salama na kujifungua bila matatizo. Njia bora unayoweza kuchukua mwenyewe ni kuhakikisha unakuwa mwenye afya kadiri uwezavyo kabla ya kujaribu kupata ujauzito:

  • Fanya mazoezi ya mara kwa mara
  • Kula mlo kamili na wenye afya
  • Zingatia kuwa kwenye uzito wako kiafya
  • Epuka maambukizi
  • Usivute, kunywa pombe au kutumia madawa ya kulevya
  • Punguza utumiaji mkubwa wa “caffeine” kama kahawa.

IMEPITIWA: MARCH 2021

Vidokezo vya Urembo Kipindi cha Ujauzito

Ni vipi nitaonekana mrembo kipindi cha ujauzito ni swali wanalokuja nalo wakina mama wengi. Kuna njia kumi sahihi za kukusaidia kufurahia urembo wako hasa katika kipindi maalumu maishani mwako.

  1. Kunywa maji

Kipindi cha ujauzito unahitajika kupata maji mengi kwa siku. Yatakusaidia kusafisha na kutoa taka na sumu mwilini mwako. Zaidi maji yanasaidia kutunza kiasi cha kimiminika kinachotakiwa mwilini mwako. Maji ni muhimu zaidi kwa afya yako na mwanao. Kunywa angalau lita 2 za maji kwa siku.

  1. Mlo sahihi

Unahitaji uangalizi na umakini wa ziada katika chakula unachokula wakati wa ujauzito na afya yako. Inashauriwa kumuhusisha daktari wako kukuandalia ratiba ya aina ya chakula unachotakiwa kula. Fuatilia ratiba hii kwa umakini, kula kwa afya, ikiwa pia ni muhimu kwa ajili ya mtoto wako.

  1. Pata muda wa kulala

Uchovu ni dalili moja wapo anazopata mama mjamzito hasa katika kipindi cha mwanzo. Kupumzika vizuri ni muhimu kwa ajili ya mwili na akili yako mwenyewe. Hakikisha unapata muda mzuri na wa kutosha kupumzika kiasi kwamba mwili wako uwe unahisi uchovu kidogo. Jiweke huru wakati wa kulala. Pumzika kwa usahihi, unaweza kutaka kutumia mito au kitu kingine cha kukuweka huru unapolala.

  1. Uzito sahihi

Unahitajika kuangalia uzito wako kipindi cha ujauzito. Baadhi ya wakina mama wanakula chochote na kila kitu pasipo kuhofia kuhusu uzito. Ikiwa ni kawaida kuongezeka uzito wakati wa ujauzito, si vema kiafya kuongezeka katika njia tofauti. Uzito unaongezeka kwa kula vyakula ambavyo havina msaada mwilini, mara kwa mara kula mlo sahihi, unaweza kumuhusisha daktari wako kwa machaguo bora.

  1. Mazoezi

Ndio, ni muhimu! Kuna mazoezi maalumu kwa ajili ya wajawazito. Hudhuria darasa la mazoezi ya yoga yaliyoandaliwa kwa ajili ya wajawazito, pata muda wa kukutana na wajawazito wengine na kujifunza na kupata uzoefu. Unaweza pia kumuomba ushauri daktari ni michezo gani unaweza kushiriki.

  1. Epuka michirizi

Wakina mama wengi wanalalamika kupata michirizi baada ya kujifungua. Unahitaji kuchukulia uangalizi hili wakati wa ujauzito.  Tumia cream uliyoshauriwa au zinazouzwa kwa ajili ya kuondoa michirizi. Tumia kila siku kuukanda mwili wako. Unaweza pia kutaka kuepuka kukimbia, kuruka au kugonga kama njia ya kuepuka michirizi.

  1. Thamini umbo lako

Pindi unatoka katika matembezi vaa nguo ya kuonyesha umbo lako, umbo la mwanamke ni zuri wakati wa ujauzito, ujauzito unamuongezea hipsi mwanamke. Tumia nafasi hii kuvaa nguo za kushika mwili wako vizuri ili kuonyesha vema hipsi zako.

  1. Uangalizi wa ngozi

Pamoja na yote wakati wa ujauzito, usisahau ngozi yako. Urembo katika kipindi cha ujauzito ikiwemo urembo wa ngozi, kwa kupendelea mimea tiba katika kipindi sahihi. Kutokana na mabadiliko ya homoni kunaweza kuwa na athari kidogo katika ngozi yako. Unaeza kutumia bidhaa za kulinda ngozi kwa kuzingatia aina ya ngozi yako lakini hakikisha hutumii kemikali hatarishi.

  1. Make-Up

Mwanamke hachukizwi na make up! kutokana na mabadiliko ya homoni unaweza kupata madoa usoni hivyo poda ni mkombozi. Make up ndio mkombozi, tena angalia zile ambazo hazitumii kemikali kali.

  1. Pumzika

Mwisho na muhimu zaidi ni kukumbuka kupumzika, weka mapumziko katika ratiba yako. Lala chini kwa muda unapopata nafasi. Pumzisha mwili wako. Ujauzito unaweza kuja na stress sana lakini hakikisha hazikushindi, jinsi unavozidi kupumzika ndivo jinsi unaonekana mrembo.

IMEPITIWA: JUNI 2020

Ratiba za Kliniki kwa Mama Mjamzito

Wiki ya 8-12

 Miadi yako ya kwanza ya kliniki inatakiwa kuchukua nafasi wiki ya 10 ya ujauzito ili mkunga wako akufanyie vipimo na uchunguzi mapema kama anahisi ni lazima. Ila inaweza fanyika kati ya wiki ya 8 na 12.

Katika miadi hii, mkunga atakuuliza:

  • Historia yako ya matibabu
  • Unajisikiaje
  • Mlo na maisha yako
  • Kazi yako
  • Wapi ungependa ujifungulie
  • Kama utaendelea kumnyonyesha mwanao

Mkunga wako atakupatia taarifa nyingi. Na atakueleza:

  • Virutubisho gani unapaswa kutumia
  • Faida za uzazi ambazo utakuwa nazo
  • Uchunguzi wa magonjwa ya akili
  • Lini utarajie kipimo cha “ultrasound”
  • Faida na hatari ya baadhi ya vipimo, uchunguzi na vitendo-tiba.

Utapata nafasi nyingi za kuuliza maswali na kuongelea tatizo lolote linalokupa wasiwasi. Ingependeza zaidi kama ukitengeneza orodha ya mambo unayotaka kuuliza kabla ya miadi yako.

Mkunga wako atakuuliza kama anaweza kuchukua damu yako, ambayo itatumika kuangalia kundi la damu yako, viwango vya madini ya chuma na pia kuangalia kama kundi lako la damu ni resusi chanya au hasi (rhesus status), na kama una antibodi au la.

Watahitaji sampuli ya mkojo wako katika miadi hii na kila miadi na mkunga wako. Atapima kama mkojo wako una protini ikiwa ni dalili ya kifafa cha mimba, na atapima maambukizi ya mkojo. Atakupima shinikizo la damu, uzito na urefu.

Mwisho wa miadi utapewa taarifa za uzazi kuenda nazo nyumbani mpaka miadi yako ijayo. Wakati huu pia unaweza ukafunguliwa kadi yako ya kliniki ya mama mjamzito.

Wiki 10-14

Picha yako ya “ultrasound” itakua tayari. Mtaalamu wa ultrasound atachunguza ukuaji wa mwanao na kuhakikisha siku ya kujifungua kwako. Atakuambia pia kama una mtoto zaidi ya mmoja.

Wiki 15-20

Utapatiwa kipimo cha damu kuangalia viwango vya protini na homoni katika damu yako ili kuangalia kama mwanao ana magonjwa ya kurithi ya akili. Kama majibu yataonyesha mtoto wako anaweza akawa na magonjwa ya akili, matibabu ya haraka yataanza kufanyika kwa mtoto aliye ndani ya tumbo.

Wiki ya 16

Mkunga wako atajadiliana na wewe matokeo ya kipimo cha damu na mkojo vilivyofanyika katika miadi yako ya kwanza (wiki ya 10). Kama kiwango cha chuma ni kidogo, anaweza kukushauri kutumia virutubisho vya chuma.  Na kama ana wasiwasi wowote, atakupeleka kwa mtaalamu wa mambo ya uzazi kwa huduma ya ziada.

Mkunga wako ataangalia shinikizo lako la damu na kuchukua sampuli mpya ya mkojo wako kuangalia kama kuna uwepo wa protini,na atafanya hivi kila mara ukienda kumwona.

Na kwa kila miadi, ni muda mzuri wa kuuliza maswali na kuongea tatizo lolote linalokupa wasiwasi.

Wiki ya 18-21

Uchunguzi (scan) ya kasoro za ukuaji utafanyika. Uchunguzi utaangalia jinsi mtoto anavyokua na kwa baadhi ya hospitali zitakuambia jinsia ya mtoto wako kama ungependa kujua.

Wakati mwingine kondo la nyuma (plasenta) huziba mlango wa uzazi, na kufanya ugumu kupata vipimo sahihi wakati wa kipimo cha skani. Kama hii imetokea kwako utapangiwa muda mwingine wa kipimo.

Wiki ya 25 (kwa mimba za kwanza tu)
Kama kawaida mkunga wako ataangalia shinikizo la damu na kupima mkojo wako kama kuna protini. Pia atapima umbali kutoka mfupa wa sehemu za siri mpaka juu ya tumbo lako na tepu kuangalia kama mtoto wako anakua vizuri.

Wiki ya 28

Mkunga wako watachukua sampuli ya damu katika miadi hii. Hii itatumika kuhakikisha viwango vya chuma ni vya kawaida na kuandalia kingamwili. Iwapo una kiwango kidogo cha chuma, atashauri uchukue virutubisho vya chuma atakayokuandikia.

Kwa kila miadi kuanzia sasa, mkunga atakupima tumbo lako kuangalia kama mtoto anakua vizuri. Ataangalia pia shinikizo la damu na kupima mkojo wako kama kuna protini.

Wiki ya 31 (wenye ujauzito wa mara ya kwanza)

Mkunga atakupima tumbo lako kuangalia kama mtoto anakua vizuri. Ataangalia pia shinikizo la damu na kuima mkojo wako kama kuna protini. Atakupatia majibu ya vipimo vya damu vilivyochukuliwa wiki ya 28.

Upate pia mda wa kuuliza maswali, kama unayo na kujadiliana masuala yanayohusiana na afya yako.

Wiki ya 32

Uchunguzi wa kasoro (anomaly scan) uliofanyika wiki ya 18 lakini majibu hayakuonekana vizuri kwasababu wakati mwingine kondo la nyuma au kirutubisho mimba (plasenta) ilikuwa inaziba mlango wa uzazi, na kufanya ugumu kupata vipimo sahihi wakati wa kipimo cha skani unaweza ukarudiwa tena kipindi hiki. Sasa ni wakati mwingine wa kufanya kipimo hichi.

Wiki ya 34

Mkunga atakupima tumbo lako kuangalia kama mtoto anakua vizuri. Ataangalia pia shinikizo la damu na kupima mkojo wako kama kuna protini na kupima ukubwa wa tumbo lako kuangalia kama mtoto anakua vizuri ndani ya tumbo lako.

Kama huu ni ujauzito wako wa pili, mkunga wako atakupa majibu ya vipimo vilivyochukuliwa wiki ya 28. Kama atakua na wasiwasi atajadiliana na wewe. Pata nafasi ya kuongea na mkunga wako kuhusu matayarisho ya uchungu na kuzaa. Mkunga atakuelezea hatua za kujifungua na lini utapata uchungu.

Wiki ya 36

Mkunga wako atafanya vipimo na uchunguzi wa kawaida. Atashika tumbo lako kwa mkono kuangalia mlalo wa mtoto wako.

Baadhi ya watoto wengi watakua wamegeuka kichwa chini katika wiki ya 36, tayari kwa kuzaliwa. Kama mtoto wako bado hajageuka, mlalo wa kutanguliza matako. Mkunga wako atakupa miadi mingine ili huduma ya kumgeuza mtoto huku mimba ikiwa inaendelea kukua ifanyike.

Sasa umekaribia miezi tisa, mkunga wako ataanza kuzungumzia nini kitatokea baada ya mtoto kuzaliwa. Ataelezea vipimo na uchunguzi vitakavyofanywa kwa mtoto wakati ukiwa hospitali na wakati ukienda nyumbani.

Wiki ya 38

Mkunga atakupima tumbo lako kuangalia kama mtoto anakua vizuri. Ataangalia pia shinikizo la damu na kupima mkojo wako kama kuna protini na kupima ukubwa wa tumbo lako kuangalia kama mtoto anakua vizuri ndani ya tumbo lako. Mkunga wako ataanza kukuelezea kwa undani kama mimba yako itachukua mpaka wiki 41.

Utaanza kupata hofu na wasiwasi ukifikiria siku ya kwenda kujifungua. Ondoa shaka kwasababu mkunga wako atafurahi sana kuongea na wewe kuhusu wasiwasi wako na kujibu maswali yote.

Wiki ya 40 (wajawazito wa mara ya kwanza)

Mkunga wako atakupima ukubwa wa tumbo lako na kupima shinikizo la damu na kipimo cha mkojo kama kawaida. Ni wakati mzuri kuongelea wakati gani ni wa kwenda hospitali kujifungua na nini kitatokea baada ya mtoto kuzaliwa.

Kama uchungu wako haujaanza ni wakati mzuri wa mkunga kukufanyia huduma itakayosaidia kuanzisha uchungu kwa kuingiza vidole vyake ukeni taratibu na kuvizungusha kwa ukakamavu (membrane sweep)

Wiki ya 41

Kama hakuna dalili yeyote ya uchungu mpaka wiki ya 41, mkunga wako atakupatia huduma ya “membrane sweep” (kuingiza vidole taratibu ndani ya uke wako na kuvizungusha kwa ukakamavu) ili kuuanzisha uchungu. Kama ulifanyiwa huduma hii wiki ya 40 unaweza kuchagua kama unataka kufanyiwa mara ya pili au la. Mkunga wako atakupima shinikizo la damu na vipimo vya mkojo kama kawaida, pia atapima ukubwa wa tumbo.

Kufikia wakati huu mkunga wako atakuandalia huduma nyingine ya kuanzisha na kuchochea uchungu iitwayo “induction” (hii inasaidia kuchochea mikazo ya ukuta wa kizazi wakati wa kujifungua badala ya kusubiria uchungu kuja, mkunga atakupatia dawa au huduma ya kimatibabu) huduma hii itafanyika pale “membrane sweep” imeshindikana. Ikiwa umechagua kuendela kusubiri na ujauzito wako ukafika wiki ya 42 au zaidi,utaangaliwa kwa karibu zaidi, ikiwemo kufanyiwa kipimo cha “ultrasound” na kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto.

Fahamu Mambo Muhimu ya Kufanya Katika Kila Hatua ya Ujauzito

Hatua ya kwanza: Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

1. Panga kuonana na mkunga wako

Mara baada ya kujua una ujauzito, mjuliswhe daktari wako ili uweze kupanga kuonana naye. Kwenda na wakati ni jambo la msingi pindi unaonana na daktari, inategemea unaishi wapi na lazima uwe umepanga kuonana na daktari wakati una ujauzito wa wiki 10, lakini inaweza kutokea wiki ya 8 au 12.

Kuonana na daktari inaweza ikachukua masaa 2 ikiwa ni nyumbani, kliniki au chumba cha upasuaji. Wakati umeonana na daktari unaweza kufanya yafuatayo;

  • Akakuuliza kuhusiana na historia ya matibabu yako, ikiwemo ujauzito uliopita na jinsi ya maisha yako.
  • Akakupa taarifa kuhusu namna ya kujihudumia wakati wa ujauzito kama vile kula vizuri na kufanya mazoezi.
  • Akakupima shinikizo la damu (presha)
  • Akakupima uzito na urefu, atachukua vipimo hivi ili kuweza kujua hali ya uzito wako kiafya (BMI)
  • Akachukua vipimo vingine vya mwili.

2. Tumia vidonge vya virutubisho-lishe kwa siku mara moja

Anza kula kidonge lishe cha asidi ya foliki mara moja. Asidi ya foliki ina virutubisho vya muhimu ambavyo vinamlinda mtoto asipate matatizo ya mgongo wala ubongo kama vile mgongo wazi “spina bifida”. Unahitaji mikrogramu 400 (400mcg) ya kidonge lishe cha foliki ya asidi (vitamin ya b9). Unaweza kununua vidonge hivi kwenye duka la dawa au maduka makubwa. Vivyohivyo unatakiwa kutumia vidonge vya vitamin B kila siku pia unaweza ukatumia vidonge vya vitamini za ujauzito kama unapenda, lakini kula mlo kamili utakusaidia kupata vitamini zote unazohitaji.

3. Pima kabla hujatumia madawa

Unahitaji kuwa muangalifu wakati wa kutumia dawa hasa za kununua madukani kwani zinaweza zikawa siyo nzuri kwa mtoto wako. Ongea na daktari wako kuhusiana na madawa yoyote utakayotumia au pia unaweza ukamuuliza muuza madawa kuhusiana na dawa husika.

4. Kama unavuta sigara ni muda wa kuacha

Kuvuta sigara wakati wa ujauzito siyo nzuri kwa mtoto wako unaweza kusababisha mimba kuharibika au kupata matatizo wakati wa kujifungua na pia inaweza kumletea mtoto matatizo wakati wa ukuaji. Hujachelewa sana kuacha sigara kama unahitaji msaada ongea na daktari wako anaweza kukupa msaada kwa namna ya kuacha kuvuta sigara, sigara zote huwa na nikotini, hivyo kama unatumia ongea na daktari wako namna ya kuacha.

5. Acha pombe

Hakuna njia ya uhakika kujua kama pombe ni salama wakati wa ujauzito ndio maana wataalamu wengi hushauri kuacha pombe kabisa wakati wa ujauzito.

6. Acha kunywa vinywaji vyenye kafeini

Wakati wa ujauzito unaweza kuendelea kunywa kahawa lakini punguza hadi 200mg kwa siku ambayo ni sawa na kikombe kimoja au viwili. Ikiwa unaweza kutumia zaidi ya 200gm za kafeini kwa siku wakati wa ujauzito inaweza kuongeza uwezekano wa mimba kuharibika. Kiwango cha 200mg kinajumuisha vyanzo vyte vya kafeini ikiwemo chai, cocacola, vinywaji vya kuongeza nguvu na chokoleti.

7. Jifunze nini cha kula na nini siyo cha kula

Mlo kamili utahakikisha unapata mahitaji yote yanayotakiwa kwa ajili ya ukuaji wa mtoto. Inaweza ikakushangaza kujua kwamba unahitaji nguvu nyingi miezi mitatu ya kwanza au miezi mitatu ya pili. Lakini utatakiwa uache baadhi ya vyakula wakati wa ujauzito kwani inaweza ikawa na vijidudu au sumu ambayo inaweza kumdhuru mtoto, hii inaweza ikajumuisha vyakula vya maziwa, nyama ambayo haijaiva kama maini na samaki wabichi.

8. Pata ahueni katika magonjwa (magonjwa ya asubuhi) yanayoambatana na ujauzito

Wamama wengi wanapata magonjwa miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito. Kula kidogo lakini mara nyingi, jaribu kutambua vyakula gani vinakufaa na vipi havikufai. Kula vyakula kama biskuti, karanga, mkate vinaweza kusaidia. Kuumwa kwako kutaanza kupungua kuanzia wiki ya 16 mpaka 20. Kama unatapika mara nyingi kwa siku wasiliana na daktari wako mapema iwezekanavyo, unaweza ukawa na ugonjwa unajulikana kama “hyperemesis gravidarum” unaohusisha kupata kichefichefu kilichopitiliza na kutapika sana.

9. Tambua ishara hatarishi

Kuna baadhi ya ishara wakati wa ujauzito ambazo ni hatari kwako na sio za kupuuza. Wakati tumbo la uzazi linakua utaanza kuhisi vichomi na nyonga kuuuma, kila mara jaribu kuwasiliana na daktari wako.Kama utakuwa na vichomi vinavyoambatana na damu wasiliana na daktari wako mapema iwezakanavyo.

10. Pata Mapumziko yakutosha iwezekanavyo

Ni kawaida kuhisi uchovu wakati wa miezi mitatu ya kwanza. Hii ni kwasababu mwili wako unapata mabadiliko mengi ya haraka ya homoni na viwango vyake. Weka miguu juu ukiwa na nafasi ingawa hii huweza kuwa ngumu kama unafanya kazi. Jaribu kupanda kitandani mapema japo mara moja katika wiki. Hatakama hutaweza kulala mpaka baadae kupumzika na kitabu au mziki laini itasaidia kukutuliza. Zima simu na sahau kuhusu kazi. Mtoto akija usingizi utakua mgumu kupata kwahiyo jaribu kuupata vyema kwa kipindi hiki. Ni vyema ukaanza kujizoesha kulala na ubavu kwani jinsi tumbo lako linavyokua utashindwa kulala kwa tumbo au mgongo. Kwani ukilala na mgongo utaathiri mzunguko wa damu katika mwili wako hatahivyo mpaka miez mitatu ya mwisho kulala kwa ubavu husaidia kupunguza hatari ya mtoto mfu, ukilinganisha na kulala na mgongo. Kwahiyo ni vyema ukaanza sasa.

11. Jiandae kumwona mwanao

Kama hauna tatizo lolote katika kipimo cha ultrasound cha kwanza, kipimo hiki hufanyika wiki 10 au 14 za kwanza.Daktari wako atamwangalia mtoto mapigo ya moyo na kukwambia lini utampata mtoto wako kwani kipimo hiki huchukua dakika 20 tu au huweza kuchukua zaidi hivyo ni vyema kumsubiri mtoto ageuke.

12. Amua lini uwajulishe watu kuwa wewe ni mjamzito

Baadhi ya wanawake hupenda kuwaambia ndugu zao na marafiki kuwa ni wajawazito papo hapo wengine husubiri mpaka miezi mitatu ya pili kwani tumbo halifichiki. Kama umepata matatizo au kazi yako ni hatarishi na inachosha ni vema ukawaambia mapema.

13. Mazoezi

Mazoezi ya mara kwa mara huweza kusaidia mahitaji ya kimwili na kiakili. Hakuna sababu ya kukuzuia kufanya mazoezi ikiwa wewe ni mjamzito, kufanya mazoezi kutakusaidia kupata wepesi na kuwa mchangamfu.

14. Fanya kazi zako kiusalama

Kuwa muangalifu na kemikali za kusafishia nyumba, vaa kinga muhimu kuzuia hatari wakati unatumia kemikali hizi hatarishi na wakati unafanya usafi fungua madirisha yako na milango. Kumbuka ujauzito unaweza ukaathiri utendaji kazi wako, hasa kama unafanya kazi na x-ray au kemikali.

15. Anza kufanya mazoezi ya nyonga

Mazoezi ya nyonga yanaweza kusaidia kuzuia kuvuja kwa mkojo wakati wewe ni mjamzito na baada ya mtoto kuzaliwa. Kama hujaonyeshwa namna ya kufanya mazoezi ya nyonga wakati umeonana na daktari basi muulize unapoenda kuonana naye tena.

16. Muhusishe mwenza wako

Wamama wengi watarajiwa kupata uzoefu mapema wakati wa ujauzito, mazoezi wakati wa ujauzito yanasaidia kuunganika na mtoto tangu akiwa tumboni.

17. Nunua sidiria ya uzazi

Maziwa yaliyojaa yanaweza yakawa ishara mojawapo ya kuwa wewe ni mjamzito na kama sidiria zinakuumiza fikiria njia mbadala.

18. Fanya mapenzi kama una hamu

Kama miezi mitatu ya kwanza unajihisi umechoka basi usifanye mapenzi lakini kama hujapata matatizo yoyote hakuna sababu ya kuacha kufanya kipindi chote cha ujauzito.

19. Fanya “massage”

Kuna unapata matatizo ya kuumwa kichwa mgongo au unataka tuu upumzike basi nenda kafanye “massage” ya wajawazito au muombe mwenza wako akukandekande mabega, mgongo na kichwa kupunguza maumivu.

20. Fanya bajeti kwa ajili ya mtoto

Anza kufikiria kuhusu namna gani utamuhudumia mtoto kama vile nguo,chakula, nepi(diapers) nk.

Hatua ya pili: Miezi mitatu ya pili ya ujauzito

1. Jifunze kuhusu kipindi hiki na ratiba ya kumuona daktari

Katika wiki ya 16 daktari wako na mkunga wako watakuambia kuhusu vipimo vitakavofanyika ukiwa wiki ya 18 au 21 na kipimo hichi kitaangalia namna mtoto anavyokua. Utaenda kumuona daktari wiki ya 25 na 28 kujua ukubwa wa mfuko wa uzazi na kupima shinikizo la damu (pressure) na kuangalia kama umeathirika na ugonjwa wowote ikiwemo UTI.Lakini miezi mitatu ya pili utapata vipimo hivi kila mara uendapo hospitali.

2. Amua kama unataka kujua jinsia ya mtoto

Je ni wa kike au wa kiume? Wakati wa kipimo ni rahisi kujua jinsia ya mtoto kama hajifichi kwa mpimaji.

3. Mwanao akisogea kwa mara ya kwanza

Katika wiki ya 18 na ya 20 ya ujauzito utaanza kumsikia mwanao akisogea ndani ya mfuko wa uzazi. Kama ni ujauzito wako wa kwanza inaweza ikakuchukua muda kuweza kutambua mtoto akisogea.

4. Chagua mzazi mwenzako

Katika kipindi cha miezi mitatu ya pili ni wakati mzuri wa kujua unataka nani awepo wakati wa kujifungua, kuwa na mtu anayekusaidia anaweza akafanya mabadiliko makubwa hasa wakati unakaribia kupata mtoto.Mzazi mwenzako siyo lazima awe baba mtarajiwa, anaweza akawa rafiki, mama yako au mama mkwe.Unaweza ukawa na wazazi wasaidizi zaidi ya mmoja.

5. Angalia kuongezeka kwa uzito wako

Ni kawaida kuongezeka uzito kidogo wakati wa ujauzito. Kula mlo kamili kutahakikisha unaongezeka uzito kidogo, kadiri mtoto anavyokua . Angalia namna uzito wako unavoongezeka. Pumzisha mwili na akili yako wakati wa ujauzito kwa kufanya mazoezi malaini kama yoga.

6. Kunywa maji ya kutosha

Wakati wa ujauzito ni muhimu kunywa maji, ni vizuri kunywa japo glasi 8 ambayo ni sawa na lita 1.5 kila siku, jaribu kutembea na chupa ya maji kila uendapo.Maji husaidia kubeba mahitaji ya muhimu kwenye damu kwenda kwa mtoto. Kunywa maji pia husaidia kuzuia magonjwa kama maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI), kuvimbiwa nk. Yote ni kawaida wakati wa ujauzito.Kama una tatizo la mwili la kutunza maji (oedema) kunywa maji ya kutosha kwani husaidia kutunza maji mwilini.

7. Panga muda wa mapumziko

Muda wa mapumziko unaweza ukapunguza matumizi ya hela na muda. Miezi mitatu ya pili ni kipindi muhimu cha kupumzika, kwa kawaida kichefuchefu kinakua kimeisha na uchovu utakua umeisha. Ni salama kusafiri kwa ndege wakati wa ujauzito mpaka wiki ya 36.

8. Chagua jina la mtoto

Kwa sasa tayari utakua na majina machache unayodhani yanaweza kumpendeza mwanao na pia ni vema umshirikishe mwenzi wako. Chagua idadi ya majina kumi unayoyapenda wewe na mwenzi wako, alafu futa yale usioyapendelea, endelea mpaka mtakaporidhia majina machache.

9. Anza manunuzi ya nguo za uzazi

Kama tumbo bado halijaanza onekana, ni vizuri kuanza kununua nguo za uzazi, nunua kidogo sasa na nyingine baadae tumbo linavozidi kukua.

10. Anza kutafuta huduma kwa mtoto

Ni vema kuanza fikiria kuhusu huduma kwa mtoto hata kama unadhani bado muda ni mrefu, tafuta vipeperushi vya watoa huduma kwa watoto. Anza kufanya utafiti wa mtu wa kumuangalia mtoto na kukusaidia mara baada ya kujifungua na ulizia watoa huduma wazuri mtaani kwako.

11. Muandae dada mtu au kaka mtu kwa ndugu anayekuja

Kama una mtoto tayari ni vema ukamuandaa kwa ujio wa mdogo wake, mwambie kwamba kuna mtoto anayekuja na ikiwezekana nenda naye kwa daktari wako.

12. Tembelea daktari wa meno

Ni vema kufanya hivi kwani muongezeko wa homoni mwilini unaweza kuathiri meno yako na fizi zinaweza kuvimba na kutoa damu hivyo kuna nafasi kubwa ya kupata maambukizi wakati huu.

13. Sherehekea nusu ya kipindi cha ujauzito

Katika wiki ya 20 ni nusu ya kipindi cha ujauzito hivyo ni vema ukajipongeza na kufurahia kipindi hicho.

14. Lala kwa ubavu

Tumbo lako linavyozidi kukua linaongeza msukumo wa damu katika mishipa mikuu kwa hiyo haishauriwi kulala na mgongo kwani utaathiri ufikaji wa oksijeni kwa mtoto, hata hivyo miezi mitatu ya mwisho hupunguza hatari ya kujifungua mtoto mfu, ukichangia kulala kwa mgongo. Kwahiyo kama hujaanza kulalia ubavu ni vema uanze mapema.

15. Andika ndoto zako kipindi cha ujauzito

Utaanza kugundua unakumbuka ndoto nyingi kipindi hichi ni vema kuandika ndoto hizo wewe pamoja na mwezi wako.

16. Andaa mahala salama kwa mtoto

Mahali salama kwa mtoto wako ndani ya miezi sita ya kwanza ni chumba unacholala wewe, haina haja ya kuhangaika awali, unaweza omba msaada mtu mwingine akusaidie kuandaa mahitaji hayo.

17. Omba vitu vya mtoto visivotumika kutoka kwa rafiki au mwanafamilia

Kununua vitu vya mtoto inaweza ikawa gharama kubwa kwahivyo ni bora kuomba kutoka kwa rafiki au mwanafamilia (mama yako, dada yako, wifi au mama mkwe) vitu visivotumika kwa ajili ya mtoto.

18. Fikiria kuhusu likizo ya uzazi

Kama unafanya kazi ni vizuri ujue unastahili mda gani na toa taarifa kwa muajiri wako kwamba wewe ni mjamzito japo wiki 15 kabla mtoto hajazaliwa na umuombe akuandikie likizo ya uzazi.

19. Tuliza akili

Kama unahisi unachanganyikiwa, kuvaa nguo zilizotengenezwa kwa pamba inaweza kusaidia kukutuliza au kama kuna baridi vaa nguo ambazo ni rahisi kutoa pindi ukisikia joto.

20. Chagua mazoezi au mchezo salama

Kufanya mazoezi wakati wa ujauzito ni vizuri kwako na kwa mtoto hivyo mazoezi ya kuogelea hufanya uwe mchangamfu kipindi tumbo lako linakua, maji yanabeba uzito wako na kunyoosha misuli. Tumbo lako linavyokua mchezo wowote hatarishi hauruhusiwi.

21. Ungana na mwanao

Mwanao anaanza kusikia sauti wiki ya 23 ya ujauzito ambapo inasemekana mfumo wa kusikia unafanya kazi vizuri ili kukusaidia uungane na mwanao. Kuongea na kumuimbia mwanao ni jambo la msingi la kuwaunganisha pamoja mpaka utakapozoea.

22. Pata muda na mwenzi wako

Katikati ya maandalizi za mtoto wako unahitaji kupata muda na mwenzi wako, mnaweza  kutoka kuangalia sinema au kwenda kula au kupumzika popote, kama una watoto tayari ni vema utafute msaidizi wa kazi ili uwe na muda wa peke yako.

Hatua ya tatu: Miezi mitatu ya tatu ya ujauzito

1. Tambua kusogea kwa mtoto wako

Mtoto wako anakua kila muda na kumbuka kusogea kwake kunaongezeka kila mara. Kila mtoto ana utaratibu wake wa kutembea na kulala na wewe utatambua wa mwanao utahisi mtoto anavyosogea mpaka kipindi cha kujifungua, kama utahisi mabadiliko yoyote mtaarifu daktari au mkunga wako haraka iwezekanavyo.

2. Jifunze kuhusu miezi mitatu ya mwisho

Katika kipindi hiki mkunga wako atakuambia ujiandae kwa ajili ya kujifungua na mengine ikiwemo dalili za uchungu na namna ya kukabiliana nazo. Mkunga wako atapima ukubwa wa tumbo lako na namna mtoto anavyokua kila mtakapoonana kama kuna haja ya kipimo zaidi atakuambia.

Kama  ni mtoto wako wa kwanza na umekaribia  tarehe ya kujifungu na hakuna dalili zozote za uchungu, mkunga wako atakufanyia  huduma yenye kusaidia uchungu kuanza(membrane sweeping) .

3. Tambua dalili za ujauzito ambazo sio za kupuuzia

Kifafa cha mimba ni tatizo linalopatikana kipindi cha ujauzito wakat plasenta haifanyi kazi vizur inaweza kutokea wiki ya 20 lakini hasahasa miezi mitatu ya mwisho.Mkunga wako ataangalia dalili za tatizo hilo pindi unapoenda kumuona. Vipimo mkunga wako atakavyochukua ni vya muhimu kuweza kutumia. Ni vizuri kuweza kutambua dalili zake. Angalia sana maumivu ya kichwa, kutokuona vizuri, kutapika, kuvimba mikono na miguu wasiliana na mkunga au daktari wako haraka iwezekanavyo.

4. Kula vizuri

Katika kipindi hichi ni vizuri kula vyakula vyenye afya na vyenye kuongeza madini ya chuma, kwahiyo kula vyakula vinavyosaidia kutengeneza chembechembe nyekundu za damu ambazo zitamsaidia mwanao. Kula vyakula kama vile nyama, mboga za majani, juisi zitakazosaidia kuongeza madini hayo.

5. Nyoosha mwili

Sasa ni wakati muhimu wa kunyoosha mwili kujiandaa kujifungua, miezi mitatu ya mwisho mazoezi hayo yatakusaidia kupunguza maumivu wakati wa kujifungua.

6. Massage tumbo lako

Tumbo lako linavozidi kukua ni vema ukaanza kumjua mwanao kabla hajazaliwa, ni salama kabisa wewe au mwezi wako kulikandakanda tumbo lako kwa ustaarabu.Ni jambo la upendo kwenu kuwa karibu na mtoto wenu, na utahisi akipiga mateke au kusogea kama kukujibu kutokana na “massage” unayomfanyia.

7. Weka sawa mahitaji ya mwanao, zikiwemo nguo na vifaa

Hii ni kazi mahususi kwa mwenza wako kupanga na kuweka vizuri mahitaji ya mwanao, ni vizuri ukiwa na marafiki waliotayari kukusaidia, ukikosa usingizi ni wakati mzuri wa kuandaa mahitaji ya mwanao.

8. Ongea na mwanao

Mtoto wako anasikia sauti yako, kuongea nae ni sehemu ya kuwa karibu na mwanao, kama kuongea na mwanao unaona ni jambo la ajabu, unaweza ukasikiliza mziki, ukaimba, ukasoma kitabu kwa sauti akusikie.

9. Jifunze kuhusu hatua za uchungu

Ni vigumu kutabiri nini kitatokea lakini jambo la busara kujifunza hatua za uchungu kabla wakati huo haujafika, kitu ambacho kitakusaidia kuwa tayari kwa kipindi hicho.

10. Andaa mpango wa kujifungua

Mpango wa kujifungua ni namna ya kuwasilisha mahitaji yako kwa wakunga na daktari wako ambao wanakusaidia wakati wa uzazi. Kitu ambacho kitafanya utaratibu mzima wa kujifungua kuwa sawia, unachotaka kutokea na kitakachotokea. Unaweza pia ukaandika mambo unayohitaji ili yakusaidie wakati wa kujifungua.

11. Jua uchungu wako

Baada ya kupita nusu ya kipindi chako cha uzazi, utaanza kusikia misuli ya tumbo lako kuanza kukaza mara kwa mara kukaza inajulikana kama “Braxton hicks contractions”. Sio kila mtu anayo, ukipata misuli kukaza huku andika namna inavyotokea na kwa kipindi gani ili uweze kujua jinsi gani inatofautiana na uchungu wa kujifungua.

12. Nunua nguo kwa ajili ya mtoto wako

Anza kufikiria kuhusu nguo na kitanda cha mtoto wako kama nepi, ambazo mtoto atahitaji, nunua mahitaji muhimu kabla mtoto hajazaliwa na uweke akiba ili ununue nyingine baadae. Kumbuka kwamba utapata nguo nyingi kwa marafiki na ndugu, safisha kila kitu kabla ya kutumia ili kuepuka muwasho kwa mtoto wako.

13. Andaa begii la hospitali

Ni jambo la muhimu kuwa na begi lako la hospitali tayari limeandaliwa kabla ya siku yako ya kujifungua,hata kama huendi kujifungulia hospitali.Kama unapendelea unaweza kuwa na mabegi mawili moja kwa ajili ya siku ya uzazi na nyingine kwa ajili ya siku baaada ya uzazi.

14. Pata usingizi wa kutosha

Kama unapata wakati mgumu kupata usingizi, jaribu kuwa na mito mipya na ilio bora kukusaidia. Kuweka mmoja katikati ya mapaja na mwingine mgongoni na mwingine chini ya tumbo itakusaidia sana kuweza kupata usingizi wa kutosha. Kumbuka kulala kwa ubavu ili uendelee kupunguza nafasi ya kuzaa mtoto mfu.

15. Andaa mahitaji ya ndani ya familia

Fanya maisha yawe rahisi, kwa kuandaa   mahitaji ya muhimu kama mboga mboga, dawa za kufanyia usafi nk.

16. Andaa kiti cha mtoto kwenye gari

Kama unapata mtoto wako hospitali utahitaji siti kwa ajili ya mtoto wako.

17. Kuwa mbunifu katika mapenzi ndani ya miezi mitatu ya ujauzito

Kama una ujauzito ambao hauna shida, unaweza kuendelea kujamiana mpaka pale kufikia kipindi mfuko wa uzazi kupasuka, au wewe kwenda kujifungua, na pia utahitaji kujua ni mikao gani itakua nzuri kwa mwenza wako kuweza kuwa huru wakati wa kufanya mapenzi.

18. Waite wasaidizi

Usijiskie vibaya marafiki wakija kukusaidia, au wanafamilia. Watapendelea kusikia na kuona wanafanya jambo la msingi kwa ajili yako. Kuwa na mtu wa kufanya usafi ndani kuosha vyombo, kukupikia ambaye atakuwa msaada mkubwa kabla  ya mtoto wako kuzaliwa na kuja nyumbani.

19. Ijue hospitali

Kama unatarajia kujifungua hospitali, fahamu utaratibu wa wodi za uzazi.

20. Epuka maumivu ya mgongo

Je,tumbo lako linakupa maumivu ya mgongo? Usiinue kitu chochote kizito, kitakuumiza misuli yako, jaribu kutafuta mkanda wa uzazi utakaokusaidia kuweza kuepuka maaumivu ya mgongo.

21. Jiandae kujifungua

Hakikisha wewe na mwenzi wako mna namba zote za muhimu, namba ya mkungwa wako, namba ya daktari na namba ya hospitali, kama una watoto au mifugo itakua bora kumtafuta mtu wa kuweza kuwatunza ndani ya kipindi hichi.

22. Jifunze kutunza kichanga chako

Kama bado hujajifunza, wakati huu ni mzuri sana kuweza kujifunza kuhusu kichanga chako kutoka kipindi cha ujauzito mpaka kuwa na mtoto jifunze kuhusu wiki ya kwanza ya mtoto wako kuzaliwa.

23. Jiandae kunyonyesha

Unavyojua zaidi kuhusu kunyonyesha, ndivyo itakavyokua rahisi kwa wewe kunyonyesha. Uliza mkunga wako kuhusu unyonyeshaji, mkunga wako atakujuza zaidi na itakusaidia sana.

24. Saidia kuleta uzazi kwa njia ya kawaida

Madaktari bado hawajajua nini kinasababisha uchungu wa uzazi, lakini wamama wengi wanasema kwamba ukitembea, ukifanya mapenzi au kula vyakula vyenye pilipili itasaidia kuleta uchungu mapema.