Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Hatua za Uchungu Wakati wa Kujifungua

Hatua ya kwanza ya uchungu ni ile ambayo wanawake wengi wanasema “kuwa kwenye uchungu”. Katika hatua hii mlango wako wa uzazi hutanuka na kupungua unene. Hatua hii ya uchungu ndio yenye maumivu makali kwani kubana kwa misuli “contractions” huongezeka na kuwa karibu zaidi mpaka mlango wa uzazi utakapokuwa umefunguka vizuri. Katika hatua hii utakuwa unatumia mbinu zote za kupambana na uchungu ulizojifunza ukisaidiwa na mkunga au mwenza wako.

Kama utachagua kutumia dawa mbalimbali za kupunguza maumivu, utapatiwa dawa hizi katika hatua hii ya kwanza ya uchungu. Dawa zingine haziwezi kutolewa ukiwa umekaribia kabisa kujifungua. Pale upana wa mlango wako wa uzazi utakapofikia sentimeta 10, utakuwa tayari kuanza kusukuma.

Hatua ya pili ya uchungu ni pale utakapokuwa unamsukuma mtoto wako apite katika njia ya kujifungulia na kuja duniani. Utasikia aina tofauti ya kubana kwa misuli katika hatua hii, itakuwa ni aina fulani ya kubana inayokufanya utamani kusukuma. Katika hatua hii kubana na kuachia kwa misuli yako kutakuwa ni kati ya dakika 2 hadi 4 kutoka mbano mmoja kwenda mbano mwingine na huchukua hadi sekunde 90 kwa mbano mmoja. Urefu wa hatua hii unaweza kuwa mfupi sana au ukachukua hadi lisaa limoja. Ila haitakiwi hatua hii ichukue zaidi ya masaa mawili.

Hatua ya tatu ya uchungu, utajifungua kondo la nyuma (placenta). Wakati mwingine utachomwa sindano ila kuweza kuharakisha hatua hii. Hatua hii haina maumivu ila utashauriwa kusukuma kidogo kusaidia kutoka kwa kondo hili.

Dalili za Uchungu Wakati wa Kujifungua

Kuzijua dalili sahihi za uchungu itakusaidia kuweza kuzitofautisha dalili sahihi za uchungu na zile ambazo si za uchungu.

Katika hatua za mwisho za uchungu mtoto wako atashuka chini kwenye nyonga tayari kwa kutoka.

Wanawake wengine huanza kuhisi uchungu kukaribia siku chache kabla. Unaweza ukahisi ni vyema ukaanza kufanya usafi ili mtoto akizaliwa nyumba iwe safi kwani bado utakuwa mwenye nguvu, ila umbuka kuwa umekaribia kupata uchungu hivyo ni vyema kuhifadhi nguvu zako kwa ajili ya siku kubwa ijayo.

Kabla uchungu haujaanza wanawake wengi hushuhudia kutokwa kwa maji mengi ukeni (kuvunja chupa). Hii ni sababu ya kutoka kwa ule ute ute mgumu uliokuwa umefunika mlango wako wa uzazi. Unaweza ukashuhudia pia kiwango kidogo cha damu. Lakini kutokwa kwa damu nyingi sana sio dalili nzuri na ni vyema ukawahi kumuona daktari haraka.

Kupasuka chupa ni ishara ya kuanza kwa uchungu. Si lazima uone maji mengi sana yanayomwagika nje, yanaweza yakawa maji kiasi lakini mara nyingi utagundua kama chupa imepasuka.

Unaweza ukawa ulianza kusikia maummivu kidogo kwa mbali ya uchungu wiki chache kabla ya uchungu kuanza. Maumivu haya mara nyingi huwa yanakuja na kuondoka lakini yapo kwa mbele ya tumbo lako tofauti kabisa na maumivu sahihi ya uchungu ambayo yanakuwa yanasikika mgongoni na tumboni. Pia maumivu ya uchungu huwa yanazidi kuwa karibu na yenye nguvu zaidi. Tofauti na yale maumivu ambayo sio ya uchungu yanaweza yakawa yanakuja na kuondoka lakini hayaongezeki nguvu au kupungua muda kati ya maumivu yanayofuatana.

Ikiwa hauna matatizo yoyote kwenye ujauzito wako, daktari wako atakushauri kukaa nyumbani mpaka pale uchungu utakapokuwa umeongezeka. Itakapofikia maumivu yapo kati ya dakika 5 kati ya maumivu, au chupa imevunjika, au unatokwa damu, utahitaji kwenda hospitali.

Kuanzishiwa uchungu, sababu na faida zake

Kuanzishiwa uchungu

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kusababisha kuanzishiwa uchungu kuwa lazima. Uchungu utatakiwa kuanzishwa iwapo:

1. Umepitiliza siku yako ya kujifungua, mara nyingi utaanzishiwa uchungu kati ya wiki ya 41 na 42
2. Chupa imevunjika lakini uchungu haujaanza
3. Una kisukari; mara nyingi huanzishiwa uchungu mara tu baada ya wiki 38
4. Umepata shinikizo la damu la mimba (pre-eclampsia)
5. Una utokaji wa damu usio wa kawaida
6. Mtoto wako ametambulika kuwa amechoka tayari
7. Mrija wa chakula wa uzazi (placenta) kushindwa kupeleka chakula na oksigeni kwa mtoto
8. Unategemea kujifungua mapacha na daktari wako ameshauri uanzishiwe uchungu

Kama unafikiria ni kwa namna gani utafanikiwa kujifungua kwa kawaida, basi kuna vidokezo kadhaa vya kuzingatia:

1. Achana kabisa na sigara, pombe na madawa yoyote kipindi chote cha ujauzito wako
2. Mara zote wasiliana na daktari wako kabla ya kutumia dawa ya aina yoyote
3. Hudhuria kliniki mara kwa mara
4. Kula mlo bora na kamili
5. Fanya mazoezi mara kwa mara
6. Muone daktari mara moja pale unapopata dalili hatarishi au usiyoielewa

Kumbuka msaada wa kitaalamu wa kukupa uchungu ukihitajika haimaanishi kwamba kuna kitu ulikosea katika ujauzito wako. Wanawake wengi wanakuwa na ujauzito wenye afya kabisa lakini wanakuja kuhitaji kuanzishiwa uchungu wakati wa kujifungua. Kwa makadirio mwanamke mmoja kati ya watatu atahitaji msaada wa kitaalamu wakati wa kujifungua.

Kuanzishiwa uchungu kunaweza kufanyika kwa njia mbali mbali, ikiwemo:

1. Kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep): Moja ya njia maarufu za kuanzishiwa uchungu. Wakati wa tukio hili daktari au mkunga wako atatenganisha nyavunyavu nyembamba zilizozunguka kichwa cha mtoto wako kutoka kwenye mlango wa uzazi. Ni kawaida kwa kitendo hiki kurudiwa mara kwa mara.
2. Prostaglandini: Homoni hii ya kutengeneza maabara inayopatikana kama kimiminika laini au kidonge huingizwa ukeni. Homoni hii husaidia kuivisha mlango wako wa uzazi ili uweze kufunguka na kutanuka kiurahisi. Inaweza ikahitajika kuwekewa dozi kadhaa mpaka ianze kufanya kazi sawasawa.
3. AROM (Artificial rupture of membranes) – Kupasua chupa: Njia hii inahusisha kupasua chupa yako kwa kukusudia. Njia hii ilikuwa ndio njia maarufu zamani lakini kwa sasa inatumika zaidi kuharakisha uchungu kuliko kuanzisha uchungu.
4. Syntocinon: Hii ni kama homoni ya oksitosini iliyotengenezwa maabara. Husaidia kukuharakishia kupata uchungu. Hutumiwa zaidi pale njia ya kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep) pamoja na kutumia homoni ya Prostaglandini zote zimeshindwa kufanya kazi. Dawa hii hutolewa kwa dripu.
5. Kuanzishiwa uchungu kwa njia ya kawaida: Oksitosini ni homoni ambayo inahusishwa moja kwa moja na uchungu. Homoni hii pia huwa inatolewa pale matiti yanapoguswa guswa, kunyonywa n.k. Hivyo basi kwa miaka mingi inafahamika kwamba kufanya mapenzi pia ni njia ya kawaida kabisa inayoweza kukuanzishia uchungu.

Kama taratibu za kukuanzishia uchungu zote hazitafanikiwa, basi itabidi ujifungue kwa upasuaji kadiri itakavyoonekana ni muhimu kiafya. Lakini, wanawake wengi wameanzishiwa uchungu na wakaweza kupata uchungu na kujifungua kawaida.

Imepitiwa: Dec 2017

Mazoezi Mepesi Kipindi cha Ujauzito

Mazoezi kipindi cha ujauzito.
Je ni salama?

Kufanya mazoezi ni jambo ambalo binadamu wengi hulifanya mara kwa mara ikiwa ni mpango wa kimaisha au hulifanya mara moja moja. Mazoezi ni kitendo cha kuushughulisha mwili kwa njia mbalimbali. Mazoezi yaliyojipatia umaarufu ni kama kutembea, kukimbia, kushiriki michezo mbalimbali na hata watu hutumia vifaa maalumu vya mazoezi kuishughulisha miili yao. Hivi karibuni vituo vingi vya mazoezi ambavyo vilikuwa maarufu kwenye nchi zilizoendelea vinaanza pia kuonekana barani Afrika.

Mazoezi ni mazuri kwa afya ya mwili na akili. Pia mazoezi ni njia nzuri kupata afya bora. Ikiwa ni kawaida kabisa watu wa umri wowote ule kushiriki katika mazoezi, huwa inazua mjadala mara kwa mara ni kwa namna gani wajawazito wafanye mazoezi. Kwanza kabisa je wanaruhusiwa kisayansi kufanya mazoezi?
Waandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya DW waliwahi kuyasema haya kuhusu mabadiliko ya mtazamo wa kisayansi kuhusu kufanya mazoezi wakati wa ujauzito

Nukuu

Miaka 20 iliyopita, madaktari wangemuambia mama mjamzito kupumzika kadiri awezavyo, kwa kuhofia kuathiri ukuaji wa kiumbe aliye tumboni, na kusababisha uchungu wa mapema au hata mimba kutoka. Hata hivyo chuo cha wakunga na madaktari wa wanawake cha nchini Marekani ACOG, kinasema kujishughulisha kimwili kuna hatari ndogo sana na kunawasaidia wanawake wengi zaidi.
Miongozo ya hivi karibuni ya chuo cha ACOG, kuanzia mwishoni mwa mwaka 2015, ambayo inatazamwa kama alama teule duniani kote, inabainisha kuwa wasiwasi kuhusu uzazi wa njiti, kutoka kwa mimba au kudumaa kwa kijusi kutokana na mazoezi haujathibitishwa. Kwa mujibu wa ACOG, wanawake wanatakiwa kuhimizwa kushiriki katika mazoezi ya viungo na kuimarisha misuli kabla na baada ya ujauzito.

Nicole Goebel/Iddi Ssessanga – DW

Aina za Mazoezi Kipindi cha Ujauzito

Mazoezi ya dakika kati ya 20 hadi 30 yanapendekezwa kwa siku nyingi za wiki kwa mwenye ujauzito usio na matatizo yoyote – wakiwemo wale walio na uzito uliopitiliza au wasio na shughuli za kutosha. Haijalishi pia wewe ni mtu wa umri gani. Inapendekeza baadhi ya michezo, kama vile kuogelea au kutembea, ambayo ni rahisi kwa viungo.

Faida za Mazoezi

Mazoezi yanaweza kukusaidia kuwa mwenye afya na kukuepushia kisukari cha ujauzito, ambacho kinaweza kukidhuru kiumbe tumboni na kinachohitaji mlo makhsusi, na katika wakati mwingine sindano za insulini hata kama kwa kawaida hauna ugonjwa wa kisukari. Kulingana na ACOG, mazoezi yanaweza pia kupunguza hatari ya tatizo linalosababishwa na kupanda kwa shinikizo la damu na vilevile kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Wakati watafiti wakiendelea kutafuta njia za kuzuia uzito uliopitiliza hasa miongoni mwa watoto wadogo, faida za mazoezi wakati wa ujauzito zimevutia usikivu wa wanasayansi. Wakati hakuna ushahidi kuonyesha kuwa mtoto wako atakuwa na umbo la kimichezo kwa sababu umekuwa ukifanya mazoezi wakati wa ujauzito, mazoezi yanaweza kuathiri ukuaji wa viungo vya mtoto huyo, na hivyo kuwa na faida katika utoto wake na kuendelea.
Ikiwa mazoezi laini ni jambo usilotegemea kufanya, mazoezi yalioboreshwa ya yoga yanaweza kukusaidia kubakia mnyumbufu na kukusaidia pia dhidi ya maumivu ya mgongo – ambayo ni tatizo la kawaida wakati wa ujauzito, kwa sababu kina mama wanakuwa na kawaida ya kuumwa mgongo kutokana na uzito ulioongezeka.

Hivyo hakuna kisingizio cha kutokufanya mazoezi- lakini unapaswa kuchagua mazoezi yako kwa umakini. Michezo ya kugusana kama vile soka, ndondi, mpira wa kikapu/pete haishauriwi. Pia jiepushe na michezo ya kujitupa majini, kupanda, kupanda juu ya zaidi ya mita 2,000, na jambo lolote linaloweza kukuweka katika hatari ya kuanguka. Pia jihadhari sana wakati wa joto kali, vilevile pumzike ukiwa na dalili zozote za mafua, maumivu ya kichwa au kizunguzungu.

IMEPITIWA: OKTOBA,2021.