Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kujifungua Watoto Mapacha au Zaidi

Kama una ujauzito wa mapacha au zaidi, inawezekana hautapita zaidi ya wiki 38. Kujifungua kwako kunaweza kukahitazi zaidi ya mtaalamu mmoja wa afya, akiwemo daktari wako, mkunga na mara kwa mara daktari bingwa kwa kila mtoto mmoja atakayezaliwa.

Kujifungua zaidi ya mtoto mmoja ni sawasawa na kujifungua mtoto mmoja, lakini watoto wako watahitaji uangalizi wa ziada, Kama utajifungua kwa njia ya kawaida, pale mtoto wa kwanza atakapozaliwa, wa pili atachukua muda mfupi zaidi kutoka.

Kama unajifungua zaidi ya watoto wawili, uwezekano mkubwa ni kwamba utajifungua kwa upasuaji. Kama ulipata matatizo yoyote katika ujauzito wako, kujifungua kwako huwa kunapangiwa siku maalumu na utaambiwa mapema kabla ya muda. Kutokana na mkao wa watoto wako tumboni pia unaweza kuhitaji kufanyiwa upasuaji. Mara chache huwa pacha wa kwanza anatoka na anayefuata kuhitaji upasuaji wa dharura ili kumuokoa. Lakini hili hutokea mara chache sana.

Madaktari watapendelea ujifungulie kwenye chumba cha upasuaji kama kujitayarisha kwa dharura yoyote itakayohitaji upasuaji. Kwa kawaida kujifungua mapacha huenda vizuri bila matatizo na punde utakuwa unamshika mtoto wako. Kama mapacha wako watakuja mapema kabla ya muda, watahitaji kuwepo hospitali kwa muda. Kwa sababu wamewahi baadhi ya viungo vyao havijakomaa vya kutosha kufanya kazi vyenyewe bila msaada. Mapacha huwa na uzito mdogo kuliko watoto wa kawaida wakati wanazaliwa hivyo ni vyema kuwa kwenye uangalizi mpaka watakapokuwa na afya njema kuruhusiwa kwenda nao nyumbani.

Kupona baada ya upasuaji au baada ya kujifungua kawaida mapacha ni sawa sawa tu na aliyejifungua mtoto mmoja.

Kujifungua Mtoto Ambae Hajageuka (Breech)

Mtoto asiyegeuka (breech) inamaanisha mtoto wako yupo kichwa juu matako chini ndani ya mfuko wako wa uzazi. Hata kama umefikisha wiki 37 tayari na mtoto wako bado hajageuka inavyotakiwa, bado kuna nafasi ya kujifungua kawaida. Mtoto ambae hajageuka huweza kugundulika unapokwenda kliniki, lakini bado asilimia 15 ya watoto ambao hawajageuka hutambulika wakati wa kujifungua.

Watoto ambao hawajageuka mara nyingi huhitaji upasuaji wakati wa kujifungua badala ya kumuanzishia mama uchungu.

Kama mtoto wako atagundulika kuwa hajageuka (breech), kuna aina mbali mbali za kujifungua unaweza ukachagua, ikiwemo:

Kujifungua hivyo hivyo mtoto ambae hajageuka (breech delivery)

Majaribio ya kumgeuza mtoto yatafanyika, ambapo ikishindikana daaktari ataweza kukusaidia kujifungua mtoto akiwa bado hajageuka (breech delivery).

Kama utakuwa umeamua kujifungua mtoto ambae hajageuka kwa njia ya kawaida, kuna mambo kadhaa ambayo lazima yawe sawa:

  1. Mtoto hatakiwi awe mkubwa sana au mdogo sana
  2. Nyonga yako haitakiwi iwe ndogo
  3. Lazima uwe na uchungu ulioanza wenyewe

Unaweza kuchagua kuchomwa sindano ya uti wa mgongo kwa ajili ya maumivu. Pia daktari wako anaweza akatumia vifaa maalumu au mikono yake kuweza kuvuta kichwa cha mtoto. Kuna uwezekano pia njia ikahitajika kuongezwa.

Mtoto wako atakapozaliwa utapata wasaa wa kumbeba baada ya daktari bingwa wa watoto kumfanyia uchunguzi.

Upasuaji uliopangwa

Njia nyingine ni maamuzi ya kufanyiwa upasuaji uliopangwa. Hii itasaidia kama imegundulika kuwa mtoto wako bado hajageuka na pia siku zako za kujifungua zimefika tayari au zimekaribia. Matayarisho na kufanyika kwa upasuaji kwa mtoto ambae hajageuka ni sawasawa tuu nay ale ya mtoto aliyegeuka ila kuna uhitaji wa kufanyika upasuaji.

Daktari wako atakuchoma sindano ya ganzi ya mgongo, ili usisikie maumivu kuanzia kwenye nyonga kuelekea chini. Atapasua tumbo lako kwa chini ya kitovu na kupasua tumbo la uzazi vilevile kuweza kumtoa mtoto. Utaweza kupewa mtoto wako papo hapo baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari uweze kumbeba wakati wakiendelea kutoa kondo la nyuma na kukushona eneo la upasuaji. Mara nyingi utabaki hospitali kwa uangalizi zaidi kati ya siku 3 hadi 7.

Hatua za Uchungu Wakati wa Kujifungua

Hatua ya kwanza ya uchungu ni ile ambayo wanawake wengi wanasema “kuwa kwenye uchungu”. Katika hatua hii mlango wako wa uzazi hutanuka na kupungua unene. Hatua hii ya uchungu ndio yenye maumivu makali kwani kubana kwa misuli “contractions” huongezeka na kuwa karibu zaidi mpaka mlango wa uzazi utakapokuwa umefunguka vizuri. Katika hatua hii utakuwa unatumia mbinu zote za kupambana na uchungu ulizojifunza ukisaidiwa na mkunga au mwenza wako.

Kama utachagua kutumia dawa mbalimbali za kupunguza maumivu, utapatiwa dawa hizi katika hatua hii ya kwanza ya uchungu. Dawa zingine haziwezi kutolewa ukiwa umekaribia kabisa kujifungua. Pale upana wa mlango wako wa uzazi utakapofikia sentimeta 10, utakuwa tayari kuanza kusukuma.

Hatua ya pili ya uchungu ni pale utakapokuwa unamsukuma mtoto wako apite katika njia ya kujifungulia na kuja duniani. Utasikia aina tofauti ya kubana kwa misuli katika hatua hii, itakuwa ni aina fulani ya kubana inayokufanya utamani kusukuma. Katika hatua hii kubana na kuachia kwa misuli yako kutakuwa ni kati ya dakika 2 hadi 4 kutoka mbano mmoja kwenda mbano mwingine na huchukua hadi sekunde 90 kwa mbano mmoja. Urefu wa hatua hii unaweza kuwa mfupi sana au ukachukua hadi lisaa limoja. Ila haitakiwi hatua hii ichukue zaidi ya masaa mawili.

Hatua ya tatu ya uchungu, utajifungua kondo la nyuma (placenta). Wakati mwingine utachomwa sindano ila kuweza kuharakisha hatua hii. Hatua hii haina maumivu ila utashauriwa kusukuma kidogo kusaidia kutoka kwa kondo hili.

Dalili za Uchungu Wakati wa Kujifungua

Kuzijua dalili sahihi za uchungu itakusaidia kuweza kuzitofautisha dalili sahihi za uchungu na zile ambazo si za uchungu.

Katika hatua za mwisho za uchungu mtoto wako atashuka chini kwenye nyonga tayari kwa kutoka.

Wanawake wengine huanza kuhisi uchungu kukaribia siku chache kabla. Unaweza ukahisi ni vyema ukaanza kufanya usafi ili mtoto akizaliwa nyumba iwe safi kwani bado utakuwa mwenye nguvu, ila umbuka kuwa umekaribia kupata uchungu hivyo ni vyema kuhifadhi nguvu zako kwa ajili ya siku kubwa ijayo.

Kabla uchungu haujaanza wanawake wengi hushuhudia kutokwa kwa maji mengi ukeni (kuvunja chupa). Hii ni sababu ya kutoka kwa ule ute ute mgumu uliokuwa umefunika mlango wako wa uzazi. Unaweza ukashuhudia pia kiwango kidogo cha damu. Lakini kutokwa kwa damu nyingi sana sio dalili nzuri na ni vyema ukawahi kumuona daktari haraka.

Kupasuka chupa ni ishara ya kuanza kwa uchungu. Si lazima uone maji mengi sana yanayomwagika nje, yanaweza yakawa maji kiasi lakini mara nyingi utagundua kama chupa imepasuka.

Unaweza ukawa ulianza kusikia maummivu kidogo kwa mbali ya uchungu wiki chache kabla ya uchungu kuanza. Maumivu haya mara nyingi huwa yanakuja na kuondoka lakini yapo kwa mbele ya tumbo lako tofauti kabisa na maumivu sahihi ya uchungu ambayo yanakuwa yanasikika mgongoni na tumboni. Pia maumivu ya uchungu huwa yanazidi kuwa karibu na yenye nguvu zaidi. Tofauti na yale maumivu ambayo sio ya uchungu yanaweza yakawa yanakuja na kuondoka lakini hayaongezeki nguvu au kupungua muda kati ya maumivu yanayofuatana.

Ikiwa hauna matatizo yoyote kwenye ujauzito wako, daktari wako atakushauri kukaa nyumbani mpaka pale uchungu utakapokuwa umeongezeka. Itakapofikia maumivu yapo kati ya dakika 5 kati ya maumivu, au chupa imevunjika, au unatokwa damu, utahitaji kwenda hospitali.

Kuanzishiwa uchungu, sababu na faida zake

Kuanzishiwa uchungu

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kusababisha kuanzishiwa uchungu kuwa lazima. Uchungu utatakiwa kuanzishwa iwapo:

1. Umepitiliza siku yako ya kujifungua, mara nyingi utaanzishiwa uchungu kati ya wiki ya 41 na 42
2. Chupa imevunjika lakini uchungu haujaanza
3. Una kisukari; mara nyingi huanzishiwa uchungu mara tu baada ya wiki 38
4. Umepata shinikizo la damu la mimba (pre-eclampsia)
5. Una utokaji wa damu usio wa kawaida
6. Mtoto wako ametambulika kuwa amechoka tayari
7. Mrija wa chakula wa uzazi (placenta) kushindwa kupeleka chakula na oksigeni kwa mtoto
8. Unategemea kujifungua mapacha na daktari wako ameshauri uanzishiwe uchungu

Kama unafikiria ni kwa namna gani utafanikiwa kujifungua kwa kawaida, basi kuna vidokezo kadhaa vya kuzingatia:

1. Achana kabisa na sigara, pombe na madawa yoyote kipindi chote cha ujauzito wako
2. Mara zote wasiliana na daktari wako kabla ya kutumia dawa ya aina yoyote
3. Hudhuria kliniki mara kwa mara
4. Kula mlo bora na kamili
5. Fanya mazoezi mara kwa mara
6. Muone daktari mara moja pale unapopata dalili hatarishi au usiyoielewa

Kumbuka msaada wa kitaalamu wa kukupa uchungu ukihitajika haimaanishi kwamba kuna kitu ulikosea katika ujauzito wako. Wanawake wengi wanakuwa na ujauzito wenye afya kabisa lakini wanakuja kuhitaji kuanzishiwa uchungu wakati wa kujifungua. Kwa makadirio mwanamke mmoja kati ya watatu atahitaji msaada wa kitaalamu wakati wa kujifungua.

Kuanzishiwa uchungu kunaweza kufanyika kwa njia mbali mbali, ikiwemo:

1. Kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep): Moja ya njia maarufu za kuanzishiwa uchungu. Wakati wa tukio hili daktari au mkunga wako atatenganisha nyavunyavu nyembamba zilizozunguka kichwa cha mtoto wako kutoka kwenye mlango wa uzazi. Ni kawaida kwa kitendo hiki kurudiwa mara kwa mara.
2. Prostaglandini: Homoni hii ya kutengeneza maabara inayopatikana kama kimiminika laini au kidonge huingizwa ukeni. Homoni hii husaidia kuivisha mlango wako wa uzazi ili uweze kufunguka na kutanuka kiurahisi. Inaweza ikahitajika kuwekewa dozi kadhaa mpaka ianze kufanya kazi sawasawa.
3. AROM (Artificial rupture of membranes) – Kupasua chupa: Njia hii inahusisha kupasua chupa yako kwa kukusudia. Njia hii ilikuwa ndio njia maarufu zamani lakini kwa sasa inatumika zaidi kuharakisha uchungu kuliko kuanzisha uchungu.
4. Syntocinon: Hii ni kama homoni ya oksitosini iliyotengenezwa maabara. Husaidia kukuharakishia kupata uchungu. Hutumiwa zaidi pale njia ya kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep) pamoja na kutumia homoni ya Prostaglandini zote zimeshindwa kufanya kazi. Dawa hii hutolewa kwa dripu.
5. Kuanzishiwa uchungu kwa njia ya kawaida: Oksitosini ni homoni ambayo inahusishwa moja kwa moja na uchungu. Homoni hii pia huwa inatolewa pale matiti yanapoguswa guswa, kunyonywa n.k. Hivyo basi kwa miaka mingi inafahamika kwamba kufanya mapenzi pia ni njia ya kawaida kabisa inayoweza kukuanzishia uchungu.

Kama taratibu za kukuanzishia uchungu zote hazitafanikiwa, basi itabidi ujifungue kwa upasuaji kadiri itakavyoonekana ni muhimu kiafya. Lakini, wanawake wengi wameanzishiwa uchungu na wakaweza kupata uchungu na kujifungua kawaida.

Imepitiwa: Dec 2017