Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Umuhimu wa Kunywa Maji Wakati wa Ujauzito.

Ninywe Maji Kiasi Gani Kila Siku Wakati wa Ujauzito?

Uhitaji wa maji wakati wa ujauzito ni mkubwa zaidi ili kuhakikisha mfumo wa mwili unaosimamia maisha ya viumbe wawili unafanya kazi vizuri. Ijapokuwa utofauti upo wa kiasi gani cha maji unywe kwa siku kutokana na sababu mbalimbali kama aina na ukubwa wa mwili wako na kwa kiasi gani unaushughulisha mwili wako, kwa ujumla angalau glasi 8 mpaka 12 za maji kwa siku.

Inashauriwa ukiwa unakunywa maji, kunywa kidogo kidogo badala ya kugugumia maji mengi kwa wakati mmoja hali ambayo inaweza kukufanya kujisikia vibaya. Unaweza kujaza chupa mbili za maji asubuhi na kuhakikisha uko karibu nazo kila wakati itakusaidia kukumbusha kunywa maji kila utakapoiona.

Hakikisha unakunywa maji kabla, wakati na baada ya mazoezi. Kumbuka kiu ni ishara mwili wako unaelekea kupata upungufu wa maji.

Faida za Kunywa Maji Wakati wa Ujauzito

Maji yanasaidia kuzuia kukosa choo

Sasa wewe ni mjamzito, kumbuka unakula na kutoa taka za watu wawili. Hii ina maanisha utoaji taka mwilini ni mkubwa kuliko hapo awali. Maji ya kutosha mwili yatasaidia kuyeyusha takamwili na mabaki, kisha kuzisafirisha nje ya mwili. Unywaji wa maji ya kutosha unasaidia kutoa haraka nje ya mwili mabaki ya chakula baada ya kumeng’enywa kupitia njia ya mfumo wa umeng’enyaji. Ikumbukwe tatizo la kukosa choo linawapata wajawazito wengi bila kusahau athari zake ambazo zinahusisha kuota nyama sehemu ya haja kubwa (hemorrhoids).

Maji yanasaidia kuzuia maambukizi katika njia ya mkojo (UTI)

Unywaji wa maji ya kutosha unazimua mkojo, hali ambayo inasaidia mkojo kutolewa nje haraka na kuzuia bakteria zinazosababisha maambukizi katika kibofu kuzaliana (bakteria hizi zinazaliana mkojo unapobanwa kwa muda mrefu kwenye kibofu). Pia mama anayekunywa maji ya kutosha hana hatari ya kupata maambukizi katika kibofu na figo.

Maji yanapunguza joto la mwili.

Ni kweli ukiwa mjamzito joto la mwili ni kubwa. Lakini ukinywa maji ya kutosha wakati wa ujauzito unasaidia kupooza mwili na kufanya mwili kufanya kazi vizuri.

Maji yanapambana dhidi ya uchovu.

Moja ya ishara za awali za upungufu wa maji mwilini ni uchovu. Unywaji wa maji ya kutosha unasaidi kuhakikisha tatizo la uchovu wakati wa ujauzito linadhibitiwa, vilevile maumivu ya kichwa (ishara nyingine ya upungufu wa maji mwilini). Pia maji yanasiadia mwili kutoa sodiamu iliyozidi mwilini- hali ambayo itapunguza miguu kuvimba “edema”.

Je, Vinywaji Gani Vingine Mjamzito Anaweza Kutumia?

Maji ndio kinywaji cha kwanza kizuri na salama kwa mjamzito, lakini vipo vimiminika vingine vinavyoweza kutumiwa na mjamzito kusaidia mwili wake uwe na maji ya kutosha:

 • Maziwa
 • Maji yaliyotiwa ladha (ladha ya limao)
 • Juisi safi na salama ya matunda na mbogamboga (kuwa makini na sukari inayoongezwa katika juisi ya matunda)
 • Chai zisizo na kafeini.

Kwa hali yeyote, weka kikomo cha unywaji wa soda na vinywaji vingine vilivyo na kafeini kwasababu vina dutu inayosababisha kasi na kiwango cha kukojoa kuongezeka.

Kumbuka pia, karibia asilimia 20 za maji yanayoingia mwilini yanatoka kwenye vyakula. Matunda yana maji ya kutosha.

Ishara Mwili Wako Una Upungufu wa Maji.

Mwili wako utakuonyesha hauna maji ya kutosha kwa kuangalia ishara zifuatazo:

 • Kiu na njaa
 • Midomo kukauka na kuchanika.
 • Mabadiliko ya rangi ya mkojo. Mwili ukiwa na maji ya kutosha mkojo wako utakuwa na rangi ya njano ya kupauka (yaani “pale-yellow color”). Wakati mkojo wenye rangi ya njano iliyokolea ni ishara ya kukosa maji ya kutosha mwilini.
 • Kupungua kwa safari za kwenda uwani
 • Kutotoka jasho hata wakati wa joto
 • Tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu
 • Uchovu, kizunguzungu na maumivu ya kichwa. Upungufu wa maji mwilini unasababisha uchovu na maumivu ya kichwa, hakikisha unakunywa maji ya kutosha kutunza nguvu uliyo nayo kwasababu ujauzito ni kazi kubwa inayohitaji nishati ya kutosha haswa miezi ya kwanza.
 • Kusahau, kuchanganyikiwa kushindwa kuelewa na kukosa mwelekeo ni baadhi ya dalili za mtu mwenye hali inayoitwa “brain fog”.
 • Ngozi mwili kukauka.
 • Baadhi ya wajawazito wanapitia leba ya uongo (Braxton Hicks contractions)

Dalili kama kizunguzungu na kuchanganyikiwa, mapigo kasi ya moyo, mabadiliko ya kucheza kwa mtoto tumboni,shinikizo dogo la damu, mshtuko na ogani kushindwa kufanya kazi zinawapata wajawazito walio na tatizo kubwa la ukosefu wa maji.

Vidokezo Vitakavyokusaidia Kuhakikisha mwili una Maji ya Kutosha Muda Wote

Zipo baadhi ya siku unaweza kuhitaji msaada kuhakikisha unafikia dozi yako ya kila siku ya maji. Vifuatavyo ni vidokezo vitakavyokusaidia kuendelea kunywa maji:

 • Ongeza ladha, unaweza kuongeza kipande cha tango, limao majani ya mnanaa (mint) katika maji.
 • Jaribu chai zenye majani ya mitishamba, hakikisha daktari au mkunga wako anakupa kibali cha kutumia kiungo hicho.
 • Hakikisha una chupa ya maji mkononi mwako. Ni rahisi kufuatilia unywaji wako wa maji ukiwa na chupa yako ya maji mkononi nyakati zote.
 • Anza siku kwa kunywa glasi moja ya maji. Kunywa maji mara baada ya kuamka ni njia nzuri ya kujijengea tabia ya kunywa maji.
 • Kula vyakula vyenye maji kwa wingi kama vile supu, tikitimaji, nanasi n.k.

Kumbuka

Ukosefu wa maji ya kutosha mwilini wakati wa ujauzito unaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto tumboni.Inaweza kusababisha matatizo makubwa na hatari kwa afya kama vile:

 • Kupungua viwango vya maji yanayomzunguka mtoto ndani ya uterasi “amniotic fluid” ambayo ni muhimu katika maendeleo na ukuaji wa mtoto.
 • Mama kujifungua kabla ya wiki 37 za ujauzito kwasababu ya kupungua kwa “amniotic fluid”.
 • Mtoto kuzaliwa na kasoro za mirija ya neva za fahamu
 • Kiasi kidogo cha uzalishaji wa maziwa
 • Mtoto kuzaliwa na kasoro kwasababu ya ukosefu wa maji na virutubisho muhimu vya kumsaidia mtoto.
 • Mara chache,kukosa maji ya kutosha kunaweza hatarisha uhai au kusababisha mama kulazwa chumba cha wagonjwa mahutihuti.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.

Umuhimu wa Lishe Bora kwa Mjamzito Kabla ya Kujifungua.

Vitamini unazotumia kabla ya kujifungua zina virutubisho vingi mtoto wako anavyohitaji, hivyo basi kuna umuhimu gani waa mama mjamzito kuangalia kwa makini lishe yake?

Inaathiri afya ya mtoto wako maishani: Kila unachokula ukiwa mjamzito kinamuathiri mtoto na maisha yake kwa ujumla, hivyo ni muhimu kula vizui kwa manufaa ya mtoto hapo baadae. Kuna baadhi ya tafiti zinazoshauri ulaji wa vyakula vyenye chumvi, mafuta na sukari vinaathiri mapendekezo ya ladha ya mtoto hapo baadae. Hii inaweza kumsababisha mtoto kupata changamoto katika ulaji, afya na uzito kutokana na aina ya lishe uliyomtambulisha ukiwa mjamzito.

Chakula kinasaidia mwili kufyonza virutubisho vyenye afya: Ikiwa unakula mlo kamili mwili wako una nafasi kubwa ya kupata na kufyonza virutubisho na madini yanayohitajika katika mwili.

Chakula bora kinasaidia mwili kufanya kazi vizuri: Ukiwa unakula vizuri mwili wako utakushukuru. Utakuwa na nguvu ya kutosha, utajisikia vizuri na pengine kuepuka kero, usumbufu na maumivu ya kawaida ya ujauzito.

Aina za Matunda Mazuri Wakati wa Ujauzito

Ndizi

Ndizi ni chakula kizuri sana wakati wa ujauzito. Zinashibisha na zina viwango vikubwa vya madini ya kalishiamu na potasiamu ambayo yanasaidia matatizo ya misuli ya miguu kukaza. Ikiwa una hamu ya kitu chenye sukari kilicho salama kwako na mtoto tumboni, ndizi za kuiva ni chaguo sahihi. Lakini kama una kisukari kilichosababishwa na ubebaji mimba, chagua kula ndizi za kupikwa (mbichi).

Tufaha (apple)

Matunda haya yana vitamini A na C, maji ya kutosha na nyuzinyuzi (fiber) zitakazokusaidia kulainisha choo.

Tikiti Maji

Tunda hili lina kiwango kikubwa cha maji kuliko tunda linguine lolote-92%. Ikiwa unapambana na tatizo la kukosa maji mwili wakati wa ujauzito, unashauriwa kula tunda hili. Tikiti maji lina madini ya potasiamu, zinki na foliki asidi kwaajili ya kupambana na misuli ya miguu kukaza wakati wa usiku na kusaidia ukuaji wa uti wa mgongo wa mtoto tumboni.

Machungwa

Chungwa linaweza kuwa tamu au chachu, ladha hizi zina pendwa na wanawake wengi ambao wanasubuliwa na kichefuchefu wakati wa ujauzito. Yana kiwango kikubwa cha maji, ni chanzo kizuri sana cha vitamini C. Vitamini hii inachangia kukuza kinga yako na mtoto tumboni, na pia inasaidia kujenga tishu muhimu kwa ajili ya ukuaji wa kimwili wa mtoto.

Parachichi

Parachichi lina madini chuma,magnesiamu, potasiamu na nyuzinyuzi (fiber). Madini chuma yanayotumika kuzuia anemia, magnesiamu na potasiamu yanasaidia tatizo la misuli ya miguu kukaza na kichefuchefu. Parachichi ni chanzo cha fati unayotakiwa kupata ukiwa mjamzito.

Peasi

Ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi zinazosaidia kupambana na tatizo la kukosa choo. Ni chanzo kizuri pia cha vitamini C, pamoja na madini chuma, magnesiamu na foliki asidi.

Embe

Ni chanzo kizuri cha vitamini C na A, inayosaidia kukuza kinga ya mtoto.

Faida za Matunda Wakati wa Ujauzito

Je, unataka ujauzito salama na wenye afya?

Kuna sababu nyingi za kula matunda ukiwa mjamzito, nazo ni pamoja na:

Yanatoa virutubisho muhimu: Mtoto wako anahitaji virutubisho fulani ili kukua vizuri. Virutubisho vinavyotolewa na matunda ni pamoja na vitamini C na foliki. Vitamini C ni muhimu kujenga tishu, inasaidia kukuza kinga ya mwili ya mtoto na kuruhusu uhifadhi wa madini chuma yanayotumika kuzuia anemia. Foliki inasaidia kujenga uti wa mgongo na pia kumkinga mtoto anayekua dhidi ya kasoro katika neva za fahamu na hivyo kuepusha dosari katika ubongo, mgongo na uti wa mgongo (neural tube defects).

Yanasaidia kukidhi hamu ya vyakula vitamu: Utofauti mmojawapo wa matunda ni kuwa matamu au machachu, ladha zote hizi ni pendwa kwa wajawazito. Kuchagua tunda badala ya peremende au biskuti itakusaidia kumaliza hamu katika njia ya kuridhisha na salama kwa afya.

Ni chaguo zuri ukisikia kichefuchefu: Ikiwa unapata changamoto ya kichefuchefu wakati wa ujauzito, ni ngumu kuweka chakula tumboni kwa muda mrefu. Vyakula vitamu na baridi ni vizuri ikiwa una pambana na magonjwa ya asubuhi, hakikisha unatunza matunda ya kutosha kwenye friji kwaajili ya kifungua kinywa.

Yanasaidia kudhibiti sukari katika damu: Matunda yana nyuzinyuzi (fiber) zinazosaidia kuratibu ufyonzaji wa sukari katika mfumo wa damu.

Matunda yanakufanya uwe na maji ya kutosha mwilini: Unahitaji kunywa maji ya kutosha ukiwa mjamzito. Tunda lina zaidi ya asilimia 80 ya maji, hivyo ikiwa umechoka kunywa maji kila saa unaweza kuchagua kula matunda kuhakikisha mwili wako unakaa na maji.

Yanasaidia kukabiliana na tatizo la kukosa choo: Ukiwa mjamzito, umeng’enyaji wa chakula unakua polepole, hali hii inaweza sababisha kukosa choo- lalamiko la kawaida kipindi cha ujauzito. Ikiwa unatumia virutubisho vyenye madini ya chuma yanaweza kusababisha kukosa choo. Tatizo kubwa la kukosa choo linaweza kusababisha “hemorrhoids”. Njia nzuri ya kuondokana na tatizo la kukosa choo ni ulaji wa vyakula ambavyo ni vyanzo vizuri vya nyuzi nyuzi na kunywa maji (matunda yana vyote viwili-maji na nyuzi nyuzi).

Kiasi Gani cha Matunda Nile Nikiwa Mjamzito?

Ingawa ulaji wa matunda ni afya, lakini ikumbukwe matunda ni chanzo cha sukari, ambayo inatakiwa kuwekwa kikomo ukiwa mjamzito. Inashauriwa mjamzito kula matunda mara 2-4 kwa siku.

Je, Kuna Matunda Natakiwa Nisile Wakati wa Ujauzito?

Hakuna kikomo cha kula matunda ikiwa limeiva na safi. Ni muhimu kuhakikisha unasafisha vizuri matunda kabla ya kula ili kuepuka uchafu utakaosababisha ugonjwa. Mchanganyiko wa maji na vinegar ni mzuri na salama kusafishia matunda hasa yaliyokuzwa kwa kemikali za kiwandani (nyanya, tufaha, zabibu, peasi, strawberi n.k)

Kumbuka

 • Nanasi limepata sifa ya kusababisha mimba kutoka na kusadikika kuchochea uchungu kabla ya mda wa kujifungua. Ijapokuwa hakuna ushahidi wa kisayansi kuunga mkono madai haya, nanasi linajulikana kama tunda salama kutumia katika viwango sahihi wakati wa ujauzito.
 • Tunda pekee linalotakiwa kuepukwa ni papai bichi, papai ambalo halijaiva lina dutu ambayo inachochea mikazo ya mfuko wa mimba.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Vyakula vya Kuepuka Kipindi cha Ujauzito

Wakati ni muhimu kujua ni vyakula gani vya kula wakati wa ujauzito, ni muhimu vile vile kujua ni vyakula gani vya kuepuka.

Epuka kula fati zisizo na afya, ambazo hujumlisha vyakula vilivyojaa mafuta. Epuka aina hiyo ya vyakula kwani vinaongeza viwango vya mafuta mwilini na kuongeza magonjwa hatari. Pia vinahusika kukuongezea uzito usiohitajika na kukufanya uwe mvivu. Aina hii ya fati inapatikana kwenye vyakula vilivyotiwa kwenye makopo, vyakula vya kukaanga. Soma maelezo ya vyakula unavyonunua ili kuepuka vyakula vilivyo na fati isiyo na afya.

Watu wengine wanaamini vyakula vya wanga ni vibaya kwa afya yako, lakini sio katika kipindi hiki. Vyakula vya wanga vinavyochukua muda mrefu kumeng`enywa ni vizuri kwa afya yako. Vyakula vya wanga vinavyomeng`enywa kwa urahisi na ndani ya muda mfupi sio vizuri kwani vinaweza kuongeza kiwango cha sukari mwilini. Vyakula vya wanga rahisi ni kama mikate, pasta, sukari, keki, vyakula vyote vilivyotengenezwa na unga wa ngano, pipi, soda na juisi mbalimbali.

Vyakula vyenye vitamini A lazima viepukwe wakati wa ujauzito. Vitamini nyingi inaweza kuwa hatari katika ukuaji wa mtoto wako, na kusababisha mimba kutoka au mtoto kuzaliwa na kasoro. Chakula kibaya kabisa katika hili kundi ni maini.

Mayai mabichi na nyama mbichi sio sahihi kwa mjamzito, kwani yanaweza msababishia mtoto matatizo katika utumbo wake wa chakula yanayoletwa na salmonella na toxoplasma.

Kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya samaki na kiwango cha mekyuri. Njia rahisi ya kuepuka kula mekyuri wakati wa kula samaki ni kuhakikisha unafahamu aina ya samaki unayokula na kuepuka aina za samaki zilizojaa kiwango kikubwa cha mekyuri.

Pamoja na aina ya vyakula vya kuepuka, pia kuna vinywaji ambavyo pia inabidi kuviepuka au kutumiwa katika kiwango kidogo sana. Vinywaji hivi ni kama vinywaji vyenye kafeini, mfano kahawa na pia kuna baadhi ya aina za chai za kuepuka. Wanawake wote wanafahamu pia ni muhimu kuepuka pombe moja kwa moja kipindi cha ujauzito.

Vyakula Vizuri Kipindi Cha Ujauzito

Kipindi cha ujauzito, unahitaji kuangalia kwa umakini mlo wako. Vyakula unavyokula lazima viwe na virutubisho ili kumpatia mtoto wako mafuta ya kutosha kwa ajili ya ukuaji mzuri. Chakula hicho pia kinahitajika kugawa virutubisho kwa ajili ya ukuaji wa mwili wako uliobeba mtoto.

Ili kuupatia mwili wako mlo mzuri kwa ajili ya wewe na mtoto wako katika hii miezi tisa, unatakiwa kuelewa vyakula vipi ni vizuri na muhimu, na pia njia za kutengeneza mlo kamili. Ili kutimiza mahitaji ya kula mlo kamili ni vyema kujitahidi kula chakula kutoka katika kila kundi la chakula kila siku. Hii inajumuisha mayai, maziwa, matunda na mboga mboga, nyama, vyakula vya wanga na mafuta.

Nafaka nzuri kwa matumizi ni zile nafaka ngumu ambazo huchukua muda mrefu kumeng’enywa na kutoa nguvu ya kutosha, lakini pia huongeza sukari mwilini. Nafaka hizo ni kama nafaka ambazo hazijakobolewa, mikate, tambi, mchele pori, tango, maziwa mgando na alizeti. Protini nyembamba ni muhimu kwa mlo wa ujazito,mfano wa hivi vyakula ni pamoja na nyama, samaki, maharagwe na bidhaa za soya.

Wakati wa kuchagua chakula, ni muhimu kuwa makini juu ya aina ya fati iliyopo. Fati zenye afya inajumuisha mafuta ya mizeituni, karanga, samaki, maparachichi.

Kuna uhitaji wa kula kwa sana matunda na mboga mboga kila siku. Ni muhimu kujumuisha vyakula vyenye nyuzinyuzi zinazotokana na mimea na kunywa maji mengi ili kupambana na hali ya kukosa choo au kuwa na choo kikavu.

Vitamini Madini na Virutubisho Kipindi cha Ujauzito

Wakati wa ujauzito wanawake wengi wamekua wakitumia virutubisho vya vitamini kwani wamekua wakikosa virutubisho hivi kupitia vyakula wanavyokula, hasa wanapotapika na kuwa na magonjwa ya asubuhi ambayo yanaingilia ulaji wao.

Kwa sababu mwili wako utakua unatengeneza damu ya kutosha, nyongeza ya nusu mpaka lita mbili za damu, ni muhimu kuhakikisha unapata madini ya kutosha ya chuma kwenye mlo wako. Madini ya chuma yanapunguzwa kwa kunywa kahawa au chai, ila yanaongezwa kwa vitamin C. Ni vyema kunywa juisi safi ya machungwa.

Kalsiamu ni madini mengine muhimu kwa mimba yako. Haihitajiki kudumisha uzito wa mifupa yako tuu, ila husaidia ukuaji wa mifupa na meno ya mtoto wako pia. Sababu nyingine ya kuhitaji kalsiamu katika mwili ni kukuepusha na msukumo mkubwa wa damu, ni muhimu katika kugandisha damu, kwa kukaza misuli na pia kusafirisha taarifa za neva. Vyanzo vikuu vya kalsiamu ni maziwa na bidhaa nyingine za maziwa, mboga za majani na samaki kama sangara na samaki wenye minofu.

Zinki ni muhimu sana pia kwenye lishe yako kipindi cha ujauzito, kwani inasaidia kwenye mgawanyiko wa seli na husaidia kuhakikisha mtoto anazaliwa akiwa na uzito unaotakiwa. Milo mingi iliyo kamili ina ina zinki ya kutosha, inayopatikana kwenye mayai, kunde, nyama na samaki wa baharini.

Vitamini nyingine muhimu kwenye mlo wako kipindi cha ujauzito ni pamoja na Vitamin A (itakayotoka kwenye mlo wako lakini usile maini). Vitamini B, C, D na E (ambazo utazipatata kwenye mlo wako kamili na pia kwenye vidonge vya vitamini ulivyoanza kutumia hata kabla ya ujauzito).

Magnesiamu, madini yanayohitajika kuleta uwiano wa homoni mwilini na pia kusaidia kwenye ufyonzwaji wa baadhi ya vitamini mwilini ni madini muhimu sana, vile vile madini ya seleniamu na fosiforasi.

Ulaji Bora Kipindi cha Ujauzito

Kuna msemo wa zamani wa ujauzito usemao, “ukiwa mjamzito, unakula chakula cha watu wawili”. Wanawake wengi wanaamini wanaweza kuongeza chakula wanachokula na uzito wa ziada wanaopata utapungua baada ya ujauzito. Hata hivyo, hii sio kweli. Kabla ya ujauzito unatakiwa kula takribani kalori 2000 kwa siku kutegemea na uzito na aina ya kazi yako. Kipindi cha ujauzito kalori unayochukua ndani ya mwili lazima iongezeke kwa karibu kalori 200 kwa siku kuanzia kipindi cha tatu cha miezi mitatu ya ujauzito (Third trimester).

Kalori za ziada zinampatia mtoto nguvu na virutubisho. Zinahitajika pia kwa ukuaji wa plasenta, kuongeza ujazo wa damu, na kujenga maji maji ya ukuta wa uzazi. Pia zinahitajika kusambaza nguvu ya ziada kwenye mwili wako inayohitajika kufanya mambo yote ya ziada ya ujauzito katika mwili wako.

Mwanamke aliye na uzito wa kuzidi mwanzoni mwa mimba yake aendelee kula kalori ya ziada isipokuwa daktari akimshauri vinginevyo. Ujauzito sio mda wa kupunguza uzito au kama moja ya njia ya kuyeyusha mafuta, hii ni hatari kwa mtoto wako. Hata hivyo wanawake walioanza na uzito mkubwa mwanzoni mwa ujauzito, hupungua wakiaanza kufuata maisha yenye afya, ikiwemo vyakula vyenye nyuzinyuzi zitokanazo na mbogamboga, matunda na mbogamboga na protini pungufu na punguzo la fati mbaya. Hawa wanawake watajikuta wanapungua uzito baada ya mtoto kuzaliwa kiurahisi kama wametumia miezi tisa kuwa wenye afya na kuwa katika umbo zuri.

Mwanamke aliye na uzito pungufu inawezekana kuhamasishwa kuongeza uzito wa ziada, ambapo atashauriwa kula zaidi ya kalori 200 zilizopendekezwa, na atashauriwa kuongeza kalori zake anazochukua kwenye vyakula kabla ya kipindi cha tatu cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito. Hii itakua lazima kumruhusu kuwa na ujauzito wa afya na kuwa na uwezo wa kuunga mkono ukuaji mzuri wa mtoto.

Ukiwa umezoea kula milo mitatu kwa siku kabla ya ujauzito, utajikuta ukila milo sita midogo ndani ya siku. Hii haimaanishi kuwa unakula milo mingi, ila ni milo midogo mitatu na vitafunwa vitatu vyenye afya. Hii haisaidi tu kudhibiti kiwango cha sukari ndani ya mwili, lakini pia hurahisisha mmeng’enyo wa chakula.

Milo midogo pia inamsaidia mwanamke anayesumbuliwa na magonjwa ya asubuhi yanayosababisha matatizo machache katika mfumo wa chakula. Wanawake wanosumbuliwa na kukosa choo wanaweza kupata faida na milo midogo midogo kila baada ya masaa machache badala ya kula milo miwili au mitatu mikubwa.

Kama magonjwa ya asubuhi ni makali (kichefuchefu cha asubuhi na kutapika), na hauna chakula cha kutosha mwilini ni hatari kwa afya ya mtoto wako, ni muhimu kuongea na daktari wako kuepuka matatizo wakati wa ujauzito. Kutapika kwa kupitiliza ni vema kuripotiwa kwa daktari mara moja.

Kuongezeka Uzito Kipindi cha Ujauzito

Kiwango cha uzito ambacho unatakiwa kuongezeka kipindi cha ujauzito, hutegemea na uzito ulioanza nao mwanzoni mwa ujauzito wako. Sababu zinazoweza kukusaidia kugundua uzito wako wa kawaida ulioongezeka kipindi cha ujauzito wako inategemea na idadi ya watoto ulio nao tumboni, ikiwa una mtoto mmoja au wawili au wengi tumboni hili ni jambo la kuzungumza na daktari wako kipindi cha mwanzo cha ujauzito wako.

Mjamzito mwenye uzito wa chini atahitajika kuongezeka uzito ili kusaidia mahitaji ya ujauzito na mtoto wake, lakini mjamzito mwenye uzito mkubwa hahitajiki kuongezeka uzito tena. Mwanamke atakayebeba mimba katika uzito wa kawaida, atahitajika kuongezeka uzito maalumu na mzuri wa kuisaidia mimba yake.

Kawaida uzito kuongezeka ni kilo 1-2 kila mwezi katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito wako, hii ni kama nusu kilo kwa wiki. Ujauzito wa mapacha utapelekea kuongezeka uzito wa wastani wa kilo 1.3 -1.5 kila wiki baada ya kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito wako.

Mtoto wako atakua na kilo kati ya 3.5 – 4 wakati wa kuzaliwa. Kondo la nyuma (placenta) na majimaji ya ukuta wa mimba vyote vina uzito wa kilo 1 – 1.5 kila moja. Kukua kwa tishu za matiti yako kunachangia kilo 1 – 1.5 na damu ya ziada ndani ya mwili wako ina uzito wa kilo 2. Kilo 2.5 – 4.5 zilizobaki ni hifadhi ya mafuta na kilo 1 – 2.5 ni za mfuko wako wa mimba.

Kama una mapacha uzito wa watoto wako wakizaliwa ni takribani kilo 6-7 na kutakua na ongezeko kidogo la uzito.