Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kipimo cha Ultrasound Kipindi cha Ujauzito

Kipimo cha Ultrasound ni Nini?

Kipimo cha ultrasound ni uchunguzi unaotolewa kwa wajawazito wengi kabla ya kujifungua. Kinatumia mawimbi ya sauti kuonyesha picha ya mtoto aliyeko tumboni. Kipimo hichi kinamsaidia mtoa huduma kuangalia afya na ukuaji wa mtoto aliye tumboni.

Kipimo cha ultrasound kinamsaidia daktari kuona kama kuna tatizo katika ogani, mishipa na tishu bila kufanya upasuaji. Tofauti na tekinolojia nyingine, ultrasound haitumi mionzi, ndio maana ni njia inayopendekezwa kwaajili ya kuangalia ukuaji wa kijusi kipindi cha ujauzito. Wakati wa kufanya kipimo cha ultrasound ni muhimu sana kwa wajawazito wengi- ni mara ya kwanza unapoweza kumuona mtoto wako. Unaweza kuona mikono, miguu na sehemu nyingine za mwili kulingana na lini kipimo kitachukuliwa na mkao wa mtoto wako tumboni. Utaweza pia kujua jinsia ya mtoto wako.

Wanawake wemgi wanafanya kipimo cha ultrasound katika kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito (second trimester) wiki 18-20 ya ujauzito. Baadhi wanafanya katika kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya ujauzito (kabla ya wiki ya 14 ya ujauzito). Idadi ya vipimo vya utrasound na muda unaweza tofautiana kwa wanawake wenye aina fulani ya matatizo ya kiafya kama asthma na kisukari.

Kuna Tofauti Gani Kati ya Kipimo cha Ultrasound na X-ray?

Ultrasound inatumia mawimbi ya sauti na mwangwi kutoa picha hai, kama video.

X-rays ni njia rahisi na haraka kwa mtaalamu wa afya kutumia kuona viungo vya ndani ya mwili na hali ya mifupa. X-rays zinatumia mionzi kupiga picha ya ogani za ndani ya mwili, na mionzi hiyo ina madhara makubwa kwa afya ya binadamu. Picha zinazopigwa zinafanana na kivuli cha mwili wa ndani wa binadamu.

Kwanini kipimo cha Ultrsound Kinafanyika?

Vipimo hivi vitampatia mama mtarajiwa nafasi ya kumuona mtoto wake ambaye hajazaliwa. Lakini pia kipimo hichi kina kazi nyingine.

Daktari wako atakutaka ufanye kipimo hich kama utakua na maumivu, kuvimba au dalili nyingine itakayo hitaji uchunguzi wa ogani za ndani ya mwili. Ultrasound inaweza kuangalia sehemu za mwili kama vile: kibofu cha mkojo, ubongo (wa mtoto), macho, figo, ini, ovari, bandama, uterasi, korodani, na mishipa ya damu.

Je, Kuna Aina Tofauti za Vipimo vya Ultrasound?

Ndio. Aina ya kipimo inategemea na uchunguzi anaoufanya daktari na ujauzito wako una umri gani. Ultrasound zote zinatumia kifaa kinachoitwa ‘transducer’ kinachotumia mawimbi ya sauti kutengeneza picha ya mtoto wako kwenye kompyuta. Aina kuu mbili za ultrasound ni:

‘Transabdominal ultrasound’: aina hii inafanyika sana kipindi cha ujauzito, mama mjamzito hulala juu ya kitanda kwa mgongo kisha mhudumu wa afya atapaka kimiminika maalumu ‘gel’ juu ya tumbo lako kusaidia mawimbi ya sauti kutembea kwa urahisi na kupata picha nzuri. Baada ya kukupa ‘gel’ atatumia ‘transducer’ kupapasa juu ya tumbo lako. Masaa mawili kabla ya kufanya kipimo hichi ni vizuri kunywa maji glasi kadhaa ili kibofu kiwe kimejaa wakati wa zoezi hili. Kibofu kilichojaa kinasaidia mawimbi ya sauti kutembea kwa urahisi zaidi na kupata picha nzuri. Aina hii ya ultrasound itachukua dakika 20.

‘Trasvaginal ultrasound’: aina hii inafanyika kupitia ukeni (njia ya uzazi). Utalala juu ya kitanda kwa mgongo na kupanua miguu yako. Mtoa huduma ataingiza kwenye uke wako ‘transduce’ nyembemba yenye muonekano kama kijifimbo cha kiongozi wa muziki. Utasikia msuguano kutoka kwenye ‘transducer’ bila maumivu. Katika aina hii ya ultrasound kibofu chako si lazima kijae, itachukua dakika 20.

Mtoa huduma anaweza kutumia aina nyingine za ultrasound kupata taarifa zaidi lakini mara nyingi ni kwa jambo muhimu:

‘Doppler ultrasound’: aina hii inatumika kuangalia usambazaji wa damu kwa mtoto wako ikiwa sio mzuri. ‘Transducer’ itatumika kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto wako na kupima usambaaji wa damu kwenye kitovu cha kichanga na baadhi ya mishipa ya damu ya mtoto wako. Matumizi ya aina hii ya ultrasound yanatumika kuangalia kama una aina fulani ya ugonjwa wa damu (Rh disease) ambao unaleta matatizo makubwa kwa mtoto kama hautatibiwa. Kipimo hichi kinaweza kufanyika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, lakini kinaweza kufanyika mapema zaidi.

‘3-D ultrasound’: kinachukua picha elfu moja kwa wakati mmoja, inaweza chukua picha ya kuonekana vizuri kama picha za kawaida. Kipimo hichi kinatumika kuhakikisha ogani za mtoto zinakua na kuendelea vizuri. Kinaangalia kasoro katika uso wa mtoto na matatizo katika mfuko wa uzazi.

‘4-D ultasound’: ni sawa na 3-D, ila hiki kinaonyesha mwondoko wa mtoto wako katika video.

Maandalizi ya Kufanya Kipimo cha Ultrasound Kipindi cha Ujauzito

Kabla ya kufanya kipimo hichi, utaambiwa unywe maji mengi na kubana mkojo wako kwa kipindi fulani ili kibofu chako kiwe kimejaa mda wa uchunguzi. Hii ni muhimu kwa vipimo vya ujauzito mchanga, kibofu kilichojaa kinasukuma mfuko wa uzazi juu ili picha za mtoto zipatikane kwa urahisi zaidi.

Mtoa huduma au daktari atakayeshughulikia suala zima la kufanya kipimo cha ultrasound atakupa maelekezo ya mda gani kabla ya kipimo unywe maji na kiasi gani cha maji unywe.

Kwa kawaida ultrasound hazina maumivu. Unaweza kuona usumbufu wakati kibofu chako kimejaa au wakati wanafanya ‘transvaginal ultrasound’.

Nini Kinatokea Wakati wa Ultrasound?

Wakati wa ultrasound utapakwa kimiminika maalumu ‘gel’ kwenye tumbo lako na kifaa maalumu kinachotoa na kupokea mawimbi ya sauti ‘transducer’ kitapitishwa juu ya Ngozi yako. Mawimbi ya sauti yanatua juu yam too na maeneo mengine ndani ya mwili, kutengeneza picha kwenye skrini ya TV.

Ultrasound zinazofanyika mimba ikiwa change zinatakiwa kufanyika kwa njia ya uke ‘transvaginally’. Hii ina maanisha badala ya kutumia ‘transducer’ juu ya ngozi ya tumbo la chini, kifaa chembamba kitaingizwa taratibu ukeni na kuchuka picha za mtoto.

Mtaalamu wa huduma hii anaweza kukuonyesha baadhi ya picha za mtoto wako kwenye skrini na kutoa kopi baadhi kwaajili yako. Picha hizi zitaangaliwa pia na mkunga wako.

Je, Unahitaji Kufanya Kipimo cha Ultrasound Mara Ngapi Kipindi cha Ujauzito?

Ikumbukwe kuwa itakuwa ngumu kuona chochote katika wiki chache za kwanza za ujauzito, ila kijusi kitaanza kuonekana zaidi wiki ya 13.

Wanawake wengi wanajiuliza mara ngapi anatakiwa kufanya kipimo cha ultrasound? Inatofautiana kulingana na mama na ujauzito wake, zifuatazo ni baadhi ya vipimo vya ultrasound unavyoweza kutarajia:

Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

Kipimo cha kwanza kinaweza kufanyika kati ya wiki ya 6 mpaka ya 8. Lakini baadhi ya madaktari wanafanya kipimo hichi kama uko katika hali hatari ya ujauzito. Hali hizi ni pamoja na maumivu ya tumbo la chini, kutoka damu na historia yoyote ya kasoro baada ya kuzaliwa mtoto au mimba kuharibika.

Kipimo kingine (dating scan) kinashauriwa kufanyika kwa wanawake wajawazito wasio na uhakika wa umri wa ujauzito wao na lini wanatarajiwa kujifungua, hii inasababishwa na uwepo wa mzunguko wa hedhi usio wa kawaida. Majibu ya kipimo cha ultrasound yatasaidia kuthibitisha umri wa ujauzito na kumpatia mama rekodi za uhakika. Vilevile matokeo ya kipimo hichi yanaweza kumuonyesha kama mama ana ujauzito wa mtoto mmoja au mapacha. Kipimo hichi kinaweza kufanyika kuanzia wiki ya 10-13 ya ujauzito.

Ndani ya kipindi hichi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito kipimo kingine cha ultrasound (nuchal translucency scan) kinafanyika kwa wajawazito kati ya wiki 14-20 ya ujauzito. Kipimo hiki kinafanyika pamoja na kipimo cha damu kwa nia ya kutambua kama mtoto yuko na hatari ya kuwa kasoro za maumbile (down syndrome). Kama majibu yataonyesha kuna hatari zaidi vipimo vingine vitafanyika zaidi.

Miezi mitatu ya pili ya ujauzito

Wiki ya 18 mpaka 20 kipimo cha ultrasound kinashauriwa kufanyika ili kuangalia ukuaji wa mtoto. Vipimo tofauti vitafanyika kuangalia ukuaji na maendeleo yam toto. Kijusi kitatathminiwa kama kina aina yeyote ya kasoro katika kichwa, miguu, moyo na ogani nyingine ndani ya mwili.

Katika hatua hii ya ujauzito jinsia ya mtoto inaweza kugunduliwa. Inaweza kuwa vigumu kuona sehemu za siri za mtoto ikiwa mtoto amekaa vibaya tumboni.

Uchunguzi wa mlango wa uzazi, kiasi cha uoevu wa amnion (amniotic fluid) na nafasi ya placenta katika mfuko wa uzazi utafanyika .

Miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito

Kipimo cha ultrasound baada ya wiki ya 35 ni salama zaidi na cha uhakika zaidi kukuhakikishia kuwa mtoto wako anakua kawaida.

Lakini pia, ikiwa ujauzito wako uko katika hatari kubwa kwa mfano kama una shinikizo kubwa la damu, kisukari, unatoka damu, kiasi kidogo cha uoevu wa amnion, una dalili za kujifungua kabla ya wakati, umri zaidi ya miaka 35, daktari anaweza kufanya kipimo cha ultrasound ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto ni nzuri. Kipimo cha ultrasound wakati huu kitasaidia kutathmini kama mtoto amekaa mkao unaotakiwa tumboni au amegeuka. Na njia gani ya kujifungua itumike kama mtoto amegeuka.

Licha ya hayo, kipimo cha ultrasound katika kipindi hiki hakiwezi onyesha siku ya uhakika ya kujifungua na uzito wa mtoto.

Kumbuka:

Inapendekezwa kwa wanawake wenye ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja au wanapatwa na kutoka damu ukeni mara kadhaa kufanya kipimo cha ultrasound mara kwa mara.

Sababu / Faida za Kufanya vipimo vya Ultrasound Kipindi cha Ujauzito

 • Kuthibitisha ujauzito.
 • Kuangalia kama una mtoto zaidi ya mmoja.
 • Kuweka tarehe ya kujifungua kwa kuangalia umri na ukuaji wa mtoto.
 • Kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto, hali ya misuli, mwondoko na ukuaji kwa ujumla.
 • Kupima ovari na mfuko wa ujauzito.
 • Kufuatilia ujauzito uliotungika nje ya mfuko wa uzazi.
 • Kutathmini hatari za mtoto aliyepatikana na kasoro za maumbile kama ugonjwa wa ‘down sydrome’
 • Kuangalia ukuaji wa kimwili wa mtoto na kuangalia kama anakua ipasavyo.
 • Kuangalia kiasi cha uoevu wa amioni (amniotic fluid) kinachomzunguka mtoto katika mfuko wa uzazi.
 • Kutambua nafasi ya plasenta.
 • Kuangalia mkao wa mtoto kabla ya kujifungua.

Hasara za kufanya kipimo cha ultrasound

Ultrasound ni salama kwako na kwa mtoto ikiwa itafanywa vizuri na mtoa huduma mwenye ujuzi nayo. Ultrasound ni kipimo salama zaidi kuliko X-rays kwasababu kinatumia mawimbi ya sauti badala ya mionzi.

Kama ilivyo kama vipimo vingine, kipimo cha ultrasound hakiwezi kuona kila tatizo. Wakati mwingine kinakosea kugundua baadhi ya kasoro.

IMEPITIWA: 28 APRILI 2020.