Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Maambukizi ya Njia ya Mkojo (UTI) Wakati wa Ujauzito

UTI ni kifupi cha urinary tract infection au kwa lugha rahisi maambukizi katika njia ya mkojo, ambayo inajumuisha figo, ureta (mirija ya figo inayobeba mkojo kutoka kwenye figo mpaka kwenye kibofu), kibofu cha mkojo na urethra (mrija mfupi unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu mpaka nje ya mwili). Ogani zote hufanya kazi pamoja ili kuondoa uchafu kutoka kwenye damu. Kwanza figo husafisha damu na kugeuza uchafu kuwa mkojo. Halafu mkojo huteremka kwenda kwenye kibofu kwa msaada wa mirija ya figo-ureta ambapo hapo hutunzwa na baadaye kutolewa nje ya mwili kupitia mrija wa urethra.

Maambukizi haya yanasababishwa na bakteria. Mtu yeyote anaweza kuyapata. Mwanamke anaweza kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo wakati wa ujauzito kuliko nyakati zingine zote. Ikiwa utahisi una UTI,ongea na daktari wako mapema. Kwa huduma na matibabu mazuri wewe na mtoto wako mtakuwa salama.

Mara nyingi maambukizi haya ushambulia zaidi kibofu cha mkojo na urethra. Lakini wakati mwingine yanaweza kupelekea maambukizi ya figo, maambukizi haya kwenye figo yanaweza pelekea mama kujifungua kabla ya muda au kujifungua mtoto mwenye uzito duni. Ndio maana ni muhimu kuchunguza dalili na ishara za maambukizi katika kila miadi ya kliniki kwa mjamzito.

Aina za Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI)

Cystitis or Bladder infection: Aina hii hutokea pale bakteria wanakusanyika kwenye kibofu cha mkojo na kusababisha uvimbe.

Maambukizi ya figo: bakteria wanaweza kupita kutoka kwenye kibofu cha mkojo kupitia mirija ya mkojo (ureter) na kuathiri figo moja au zote mbili, ugonjwa unaojulikana kama ‘pyelonephritis’. Ugonjwa huu unawaathiri sana wajawazito na huweza kusambaa kwenye damu. Madhara huwa makubwa kwa mama mjamzito na huweza kusababisha mtoto kuzaliwa njiti.

Asymptomatic bacteriuria: Mara nyingine bakteria katika njia ya mkojo hawaonyeshi dalili zozote.

Dalili za Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI)

Ikiwa una UTI, unaweza kuwa na dalili kama:

 • Kubanwa na mkojo haraka au kwenda kujisaidia haja ndogo kila mara
 • Shida wakati wa kukojoa
 • Kujisikia hali ya kuungua au maumivu sehemu ya chini ya misuli ya mgongo au tumbo la chini
 • Kujisikia hali ya kuungua kila unapojisaidia haja ndogo.
 • Mkojo kubadilika rangi au kuwa na harufu kali.
 • Maumivu wakati wa tendo la ndoa.
 • Damu kwenye mkojo, ambayo itaubadikisha rangi na kuwa pinki inayong’aa au rangi ya cocacola

Ikiwa una maambukizi ya figo unaweza ukawa na dalili kama:

 • Homa kali
 • Kichefuchefu
 • Kutapika
 • Maumivu ya sehemu ya juu ya mgongo, mara nyingi upande mmoja.

Kama una dalili za maambukizi ya figo, muone daktarin haraka katika kituo cha afya kilicho karibu na wewe. Bila matibabu sahihi, maambukizi haya yanaweza kuenea ndani ya mfumo wako wa damu na kusababisha hali za kutishia maisha.

Kwanini UTI Inatokea Mara kwa Mara Wakati wa Ujauzito

Homoni ni moja ya sababu. Kipindi cha ujauzito, homoni zinasababisha mabadiliko katika njia ya mkojo na kumfanya mwanamke awe katika hatari ya kupata maambukizi. Mabadiliko ya homoni yanapelekea hali ambayo mkojo unarudi kwenye kibofu cha mkojo kisha kwenye figo (vesicoureteral reflux), hali hii inaweza kusababisha UTI.

Ukiwa na ujauzito, mkojo wako una sukari zaidi, protini na homoni ndani yake. Mabadiliko haya pia yana kuweka katika hatari kubwa ya kupata UTI.

Kwasababu ya ujauzito, ukuaji wa uterasi unaoendelea kadiri ujauzito unavyokua hugandamiza kibofu cha mkojo. Hali hii inazuia mkojo wote ulio kwenye kibofu kutoka, mkojo unaobaki unaweza kuwa chanzo cha maambukizi.

Sababu/Chanzo cha UTI ni pamoja na:

“Escherichia coli” ni bakteria wanaotoka kwenye kinyesi chako: E.Coli ni chanzo kikubwa cha UTI na anaweza kuhama kutoka kwenye sehemu ya haja kubwa (mkundu) mpaka kwenye urethra ikiwa baada ya kujisaidia unajisafisha kuanzia nyuma kwenda mbele.

Shughuli zinazohusiana na tendo la ndoa. Vidole, uume wa mwenza wako, au vifaa vinavyotumika wakati wa tendo la ndoa vinaweza kusogeza bakteria karibu na urethra yako ku

“Group B streptococcus” baktari huyu anapatikana katika uke na utumbo mkubwa wa chakula, anaweza kusababisha UTI. Maambukizi haya yanaweza kupatiwa kwa watoto wachanga pia kutoka kwa mama zao. Katika wiki kati ya 36 mpaka 37 ya ujauzito daktarin atafanya kipimo kwa mama mjamzito kuchunguza aina hii ya bakteria. Ikiwa utapatikana na bakteria huyu, daktarin wako atakupatia dawa wakati wa kujifungua.

Jinsi Gani Maambukizi Katika Njia ya Mkojo Yanachunguzwa?

 • Kipimo cha mkojo kitachukuliwa. Inapendekezwa kupima mkojo wa kwanza wa asubuhi, ikiwa mkojo una chembechembe nyeupe za damu nyingi huashiria maambukizi.
 • Kipimo cha damu
 • Kipimo cha “urine culture” ni kipimo cha kugundua vijidudu vinavyoleta maambukizi kama vile bakteri kwenye mkojo. Sampuli ya mkojo huongezwa kwenye dutu ambayo inasababisa vijidudu kukua. Ikiwa hakuna vijidudu vinavyokua, basi kipimo ni (-ve), ikimaanisha hakuna bateria ndani ya mkojo. Uchunguzi huu ndio bora zaidi na unafaa kufanywa kabla ya kutumia dawa za antibayotiki.
 • Wakati mwingine kipimo cha Ultrasound hutumika kwa mgonjwa anayepata ugonjwa huu mara kwa mara.

Matibabu ya UTI Wakati wa Ujauzito

Utatumia dawa alizokuandika daktari kwa siku 3 mpaka 7. Ikiwa maambukizi yako yatakufanya ujisikie vibaya daktari wako anaweza kukuanzishia matibabu hata kabla majibu ya mkojo kutoka.

Dalili za UTI zinazokusumbua zitaanza kupotea siku ya tatu baada ya kuanza dozi. Tumia dawa zote ulizoandikiwa kwa wakati. Usiache kutumia dawa mapema hata kama dalili zimepotea.

Baadhi ya antibiotiki zinazotumika kutibu maambukizi ya njia mkojo ni pamoja na: amoxicillin, erythromycin na penicillin, dawa hizi ni salama kwa wanawake wajawazito. Daktari ataepuka kukuandikia dawa ambazo zinaweza kuathiri ukuaji wa mtoto ambazo ni pamoja na ciprofloxacin (Cipro), sulfamethoxazole, na tetracycline.

Matatizo Yanayoweza Kusababishwa na UTI Wakati wa Ujauzito

Maambukiz ya njia ya mkojo yanayoathiri figo yanajulikana kama “pyelonephritis”. Ikiwa wewe ni mjamzito aina hii ya maambukizi inaweza sababisha mambo yafuatayo:

 • Kujifungua kabla ya muda
 • Maambukizi makali
 • Anemia
 • Maambukizi ya mda mrefu ya njia ya mkojo (UTI sugu)

Nitajikingaje Dhidi ya Maambukizi Katika Njia ya Mkojo Wakati wa Ujauzito?

Ili kujaribu kuepuka UTI mambo yafuatayo hayana budi kufuatwa:

 • Kunywa maji ya kutosha angalau glasi 8 kwa siku. Maji huzimua mkojo na kusaidia kutoa bakteria kwenye kibofu cha mkojo kwa njia ya mkojo.
 • Ukimaliza kujisaidia jifute kuanzia mbele kurudi nyuma
 • Jisaidie haja ndogo kabla na baada ya kufanya tendo la ndoa na usisahau kujifuta sehemu za siri baada ya tendo la ndoa, ukianzia mbele kurudi nyuma. Pia inashauriwa kunywa glasi moja ya maji.
 • Epuka sabuni zenye marashi makali zinazoweza sababisha muwasho katika kusafisha sehemu zako za siri.
 • Kula vyakula vyenye vitamini C kama vile matunda(ubuyu, machungwa, machenza,nk)mkojo wenye asidi hupunguza bakteria
 • Vaa nguo za ndani zilizotengenezwa na pamba ili kuruhusu mzunguko wa hewa.
 • Usivae nguo za ndani zinazokubana
 • Jisaidie haja ndogo kila mara, angalau baada ya saa mbili au tatu. Usibane mkojo kwa muda mrefu, hali hii huwapa bakteria nafasi ya kukua
 • Epuka pombe, vyakula vyenye pilipili, kahawa na vyakula vyote vinavyoweza sababisa muwasho katika kibofu chako.

IMEPITIWA: APRIL 2021