Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kunyonyesha

Hongera kwa kujifungua mtoto wako! Tunajua umechoka na unaweza ukawa unamuangalia mtoto wako kwa furaha sana. Unaweza ukawa unataka kuanza kumnyonyesha, kitu ambaho ni bora kwa afya ya mtoto wako. Shirika la afya duniani na shirika la umoja wa mataifa kwa watoto wanasisitiza kumnyonyesha mtoto wako kwa muda usiopungua miezi sita bila kumpa kitu kingine chochote. Na vile vile uendelee kumyonyesha na kumpa vyakula vingine mpaka atakapofikisha miaka miwili au zaidi. Kama umeamua kumnyonyesha mtoto wako anza mara moja na usikatishwe tamaa na namna mambo yanavyokuwa magumu, kwani kunyonyesha huwa na tabu kidogo mwanzoni.

Masaa 48 ya kwanza na mtoto wako

Muweke mtoto wako kifuani kwako kwa masaa ya mwanzo baada ya kujifungua. Hakikisha ngozi yako nay a mtoto wako zinagusana ili muweze kuanza kujuana mapema lakini pia atapata joto zaidi kutoka kwako. Kwa kawaida baada ya masaa machache mtoto wako ataanza kuhangaika kutafuta chuchu zako. Usiogope kuomba msaada kutoka kwa mkunga au nesi aliyepo karibu kukusaidia kumsogeza kwenye chuchu. Mwanzoni kichanga chako kinaweza kisijaribu kunyonya kabisa na kuweka midomo yake tu kwenye chuchu. Kuwa mvumilivu, pale mtoto wako atakapokuwa amepata nafasi nzuri utasikia kitu kama kinavuta.

Kumbeba mtoto wakati wa kunyonya

Ni vyema kama utamuweka mtoto wako kwenye mkao wa kunyonya masaa mawili baada ya kujifungua. Watoto wanaoanza kunyonya masaa mawili baada ya kujifungua huwa na uwezo wa kunyonya maziwa mengi zaidi siku ya nne ukilinganisha na wale ambao hawakufanikiwa kunyonya masaa mawili baada ya kujifungua. Baada ya hapo wewe na mtoto wako mtakuwa mmechoka sana, pata kumpumzika lakini uamke kila baada ya masaa matatu hivi ujaribu kumnyonyesha. Jaribu kumnyonyesha hadi mara 8 katika masaa 24 ya kwanza baada ya kujifungua. Kwa kawaida ni vyema kumnyonyesha mtoto kila baada ya masaa matatu ndani ya mwezi wa kwanza ili kuweza kuhakikisha kiasi cha maziwa hakipungui na mtoto anaongezeka uzito inavyotakiwa.