Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Matumizi ya Nepi na Usafi Wake kwa Watoto

Ndani ya siku chache utakuwa umebobea katika swala la kubadilisha nepi mwanao. Unaweza ukawa unambadilisha mtoto wako karibia mara 10 ndani ya saa 24. Kama utagundua mtoto wao amepata vipele vidogo vidogo au kuchubuka kwa ngozi kulikosababishwa na uvaaji wa nepi, zifuatazo ni mbinu mbalimbali za kumsaidia:

  • Hakikisha ngozi ya mtoto ni kavu na ngozi haikutani na choo chake au mkojo.
  • Badilisha nepi kila mtoto anapokojoa au kupata choo. Wakati wa mchana iangalie nepi ya mwanao kila baada ya masaa matatu. Utahitajika kumbadilisha mtoto wako usiku pia ili kuepuka michubuko ya nepi au kusaidia kupona kwake. Ni kawaida kabisa kumbadilisha mtoto nepi hadi mara 8 kwa saa 24.
  • Tumia nepi yenye uwezo mkubwa wa kunyonya majimaji ili kumuacha mtoto wako mkavu muda wote.
  • Taratibu osha eneo lenye vipele au mchubuko kwa maji vuguvugu na kitambaa laini. Suuza vizuri na kausha vizuri.
  • Usitumie sabuni kama eneo hili limechafuliwa na choo cha mtoto wako, hapa unaweza kutumia sabuni kidogo kadiri itakavyohitajika.
  • Usitumie “wipes” za watoto ambazo zina “spirit” au “propylene glycol” kusafishia ngozi iliyochubuka kwani ngozi itazidi kuungua na kusababisha kusambaa kwa bakteria kwenye ngozi.
  • Unaweza ukaacha kumvalisha nepi kwa muda kadiri itakavyowezekana mpaka atakapopona.
  • Weka maziwa ya mama kidogo kwenye mchubuko. Maziwa ya mama yana vimelea vyenye tiba na uwezo wa kupambana na bakteria.

 

Jinsi ya kumbadilisha mtoto nepi (Za kutumia mara moja na kutupa)

Hatua 1: Mlaze mtoto wako kwenye sehemu ya kumbadilishia na hakikisha hataweza kudondoka. Usikae ukamuacha mtoto wako peke yake hata kwa sekunde kadhaa.

Hatua 2: Endelea kumuangalia mtoto wako machoni na endelea kuongea nae atambue kila kitu kiko sawa.

Hatua 3: Ifungue nepi iliyochafu, lakini usiiondoe kwanza.

Hatua 4: Vifunge vifungio vya nepi pamoja ili visijibane kwenye ngozi laini ya mtoto wako.

Hatua 5: Vuta chini mbele ya nepi ya mtoto wako. Kama nepi ya mtoto wako ni chafu unaweza ukaanza kuitumia hiyo hiyo kufutia kiasi kikubwa cha choo cha mtoto wako.

Hatua 6: Nyanyua matako ya mtoto wako juu kwa kuvishika visigino vya miguu yake kwa mkono wako mmoja na kuinyanyua miguu juu.

Hatua 7: Ifunge nepi chafu mara mbili, sehemu safi ikiwa juu.

Hatua 8: Tumia pamba laini na maji vuguvugu kumsafisha mtoto wako.

Hatua 9: Watoto wa kiume inabidi waoshwe kuzunguka korodani zake na uume wake. Ni vyema kuwa makini wakati wa kubadilisha nepi, na hakikisha unaosha kwa uangalifu sehemu zote zenye mikunjo.

Hatua 10: Subiri kwa dakika kadhaa mpaka mtoto wako akauke kwa hewa au umfute kwa kitambaa kikavu na laini. Unaweza ukampaka mafuta ya kinga ya kuchubuka kama daktari wako alishauri.

Hatua 11: Iondoe nepi chafu na fungua nepi safi.

Hatua 12: Taratibu mnyanyue mtoto wako tena juu kidogo kwa kutumia mkono wako mmoja. Ipitishe nepi safi chini ya matako yake.

Hatua 13: Vuta mbele ya nepi hii kuja mbele katikati ya miguu ya mtoto wako. Nusu ya nepi hii itakuja kwa mbele na kuilaza juu ya tumbo la mtoto wako. Lakini hakikisha haifuniki kitovu.

Hatua 14: Tumia mkono mmoja kuishikilia vizuri juu ya tumbo la mwanao. Kwa kutumia mkono mwingine fungua sehemu yenye gundi ya upande mmoja na kuinatisha mbele ya nepi iliyo juu ya tumbo. Fanya hivi kwa upande mwingine pia.

Hatua 15: Kuhakikisha nepi haijakaza sana au kulegea sana hakikisha unaweza kuingiza vidole viwili kwenye sehemu ya mbele ya nepi iliyo juu ya tumbo.