Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Zifahamu aina mbalimbali za uzazi wa mpango

Uzazi wa mpango ni nini?

Uzazi wa mpango ni maamuzi ya hiari ya mtu au wenza juu ya ni wakati gani waanze kuzaa, watoto wangapi wazae, wapishane kwa umri gani na lini waache kuzaa.

Uzazi wa mpango una faida gani?

Pamoja na kumuwezesha mama na mtoto kuwa na afya njema, uzazi wa mpango una faida nyingi kwa wanawake, wanaume, watoto, familia na jamii kwa ujumla: • Unamsaidia mama kurudi katika hali yake ya zamani ambayo ilisumbuliwa na hali ya ujauzito, uchungu na kujifungua, mama atakuwa mwenye nguvu, afya nzuri na mchangamfu. Na pia atakuwa na muda mzuri wa kurudisha afya yake kabla ya kupata ujauzito mwingine. • Unamuwezesha kuhudumia familia yake vizuri na kuwa na maisha bora. Utakuwa na muda, fedha na mahitaji muhimu kwa familia yako kama chakula, mavazi, elimu, mapenzi na huduma zote muhimu. • Mama anapata muda wa kutosha wakujishughulisha na mambo mengine ya kiuchumi na kimaendeleo kwa ajili ya familia na jamii kwa ujumla. • Mama na baba wanapata muda mzuri wa kujishughulisha zaidi na mambo na mahitaji yao binafsi. • Unasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Nani anapaswa kutumia uzazi wa mpango?

Yoyote mwenye umri wa kuzaa au anatarajia kufikia umri huo anapaswa kufikiria kuhusu uzazi wa mpango. Uzazi wa mpango ni muhimu kwa: • Wanawake na wanaume • Watu walioa na kuolewa au ambao hawajaoa wala kuolewa • Watu wenye watoto au bado hawajapata watoto.

Ni wakati gani mtu atumie uzazi wa mpango?

Umri sahihi wa kuanza kutumia uzazi wa mpango ni kuanzia miaka ishirini (20) na thelathini na tano(35). Ujauzito ni hatari kwa mama na mtoto endapo mama atajifungua chini ya umri wa miaka ishirini (20) au zaidi ya miaka thelathini na tano (35) vilevile ni hatari kwa mama atakaejifungua zaidi ya watoto wane au hasipowapishanisha watoto. Wenza wanatakiwa kusubiri angalau miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine pia wafikirie kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango wakati wote ambao hawajapanga kupata mtoto.

Njia za uzazi wa mpango ni zipi?

Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kutumiwa na mtu au wenza waweze kusubiri, kuchelewesha, au kupunguza idadi ya watoto watakaowazaa. Zipo njia za mda mfupi, mda mrefu na za kudumu.

• Njia za muda mfupi:

Hizi ni njia za kisasa za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuzibadilisha. Unaweza kupata ujauzito pindi utakapoacha kuzitumia. Njia hizi ni nzuri kwa mama anayetaka kupata ujauzito baada ya miaka miwili baada ya kujifungua. Nazo ni: –
Njia ya vichecheo
Njia hizi zina vichocheo ni sawa na vichocheo vya kawaida vilivyomo kwenye mwili wa mwanamke. Njia ya vidonge
Vidonge hivi hutumiwa na wanawake kila siku.

Njia ya sindano
Mama huchoma sindano kila baada ya miezi mitatu (3).
Njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango
Humezwa na mama ili kuzuwia kupata mimba kwa mama aliyetenda ngono bila kutumia kinga yeyote. Hivi vinaweza kuzuwia mimba hadi siku tano baada ya kujamiana.

Njia za Kizuizi
Kondom za kike na kiume. Ni muhimu kutumia ipasavyo kila unapofanya ngono. Hii ni njia ya pekee ambayo pia inazuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa.

Njia za asili
Kukosa hedhi kwa kunyonyesha mfululizo
Hii ni njia ya asili ambayo inatokea kwa mwanamke anayenyonyesha na ni ya kuaminika zaidi wakati mama huyo bado hajaanza kuona siku zake za hedhi na ili hayo yote yatokee ni lazima mama awe anamnyonyesha mwanae mara kwa mara usiku na mchana na Mtoto awe na umri chini ya miezi sita (6).
Elimu ya kujua siku za hatari uzazi
Hii inawezekana ikiwa mama anaufahamu mzunguko wake mzima wa siku zake za hedhi na kujua ni zipi siku za hatari za kushika mimba. Yeye na mwenza wanatakiwa kuacha kabisa kufanya ngono siku hizo za hatari.
Kukojoa nje
Hii inafanywa na mwanamume wakati wa tendo la ndoa ambapo humwaga shahawa zake nje ya uke.

• Njia za muda mrefu:

Hizi ni njia ambazo pia zinaweza kurudiwa. Unaweza kupata ujauzito mara utakapoacha kuzitumia. Hizi ni nzuri ikiwa unataka kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine.

Njia ya vipandikizi
Hiki ni kijiti cha plastik anachowekewa mwanamke chini ya ngozi kwenye mkono wake kinaweza kuwa kimoja au viwili. Hivi huzuia mwanamke asipate ujauzito kwa muda kati ya miaka 3 hadi 5 kutegemea na aina ya vipandikizi alivyotumia.

Njia ya kitanzi
Ni kifaa kidogo chenye shaba na plastiki ambacho huwekwa kwenye mji wa mimba. Hichi hukuzuia usipate mimba mpaka miaka kumi na mbili (12), unaweza kukitoa wakati wowote utakapoamua au kuhitajia kupata mtoto.

• Njia ya kudumu:

Hizi ni njia huwezi kuzirudia na ukitumia huwezi kupata mtoto tena. Na hutumiwa na watu ambao hawataki kupata mtoto tena. Nazo ni: –

Kufunga kizazi kwa mwanaume
Njia hii inahusisha upasuaji mdogo ambapo mirija ya uzazi ya mwanaume ukatwa au kufungwa hivyo kuzuia yai kusafiri na kukutana na shahawa. Mwanaume anaendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kutoa mbegu lakini mbegu zake hazitaweza kutunga mimba

Kufunga kizazi kwa mwanamke
Njia hii inahusisha upasuaji mdogo inafanyika kwa kuziba au kukata mirija ya kizazi kuzuia yai kukutana na mbegu. Mwanaumke ataendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kuona siku zake za hedhi.

Utafahamu vipi kuwa njia gani ya uzazi wa mpango ni sahihi kwako?

Inategemea na mtu mwenyewe au wenza kuamua njia gani ni sahihi kwao. Tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe uonane na wahudumu wa afya wataweza kukufahamisha njia sahihi kwako.

Imepitiwa: July 2017

Leave a Comment

(17 Comments)

shares