Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Vifahamu vyakula bora na vile vinavyokatazwa kipindi cha ujauzito

Ni vyakula gani vya kuepuka kutumiwa na wajawazito?

Ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema pamoja na akili timamu, akiwa tumboni lazima alishwe lishe bora na mlo sahihi. Mwenye jukumu la kutoa lishe bora na sahihi kwa kiumbe kilichomo tumboni ni mama. Anatakiwa kujua aina ya vyakula anavyopaswa kula. Vivyo hivyo, anatakiwa kujua aina ya vyakula vya kuviepuka.

Katika makala ya leo, tunaangalia orodha ya vyakula vilivyokatazwa. Mama mja mzito haruhusiwi kuvila vyakula vifuatavyo kwa faida ya kiumbe kilichomo tumboni na kwa faida yake mwenyewe:

Nyama mbichi

Epuka kula samaki au nyama mbichi au iliyopikwa lakini haikuiva vizuri. Utajiepusha na uwezekano wa kula bakteria na vijidudu vingine hatari kwa afya ya mtoto tumboni. Mjamzito anapokula nyama, anatakiwa kuhakikisha imeiva sawasawa.

‘Soseji” na “Sandwich”
Mjamzito haruhusiwi kula ‘soseji’, ‘sandwichi’ za nyama na vyakula vingine vilivyotengenezwa kwa nyama. Inaaminika kuwa nyama zinazoandaliwa kwa ajili ya kutengenezea vyakula kama hivyo, huwa vimewekewa vihifadhi vyakula (preservatives) ambavyo vinaweza visiwe vizuri kwa afya ya mtoto.

Samaki wenye zebaki (Mercury)
Wajawazito wamekatazwa kula samaki wenye kiasi kingi cha madini ya zebaki. Ulaji wa zebaji kwa wajawazito umehusishwa na uzaaji wa watoto taahira. Mfano wa samaki hao ni pamoja na Papa, Chuchunge na dagaa wakubwa.

Mayai Mabichi
Ulaji wa mayai mabichi au vyakula vilivyochanganywa na mayai mabichi, mjamzito haruhusiwi kuvila. Kuna baadhi ya ‘Ice Cream’ na ‘mayonaizi’ hutengenezwa kwa kuchanganywa na mayai mabichi. Mjamzito amekatazwa kuvila vyakula hivyo.

Maini
Maini yana kiwango kikubwa cha madini aina ya chuma. Hata hivyo, yana kiasi kikubwa cha Vitamin A ambacho huweza kuwa na madhara kwa mtoto kikizidi.

Maziwa mabichi
Maziwa mabichi huweza kuwa na bakteria ajulikanae kama ‘Listeria’, ambaye huweza kusababisha kuharibika kwa mimba. Unapokunywa maziwa, hakikisha yamechemshwa au kama ni ya paketi hakikisha ni yale yaliyoandikwa‘Pasteurized’ na siyo ‘Unpasteurized’.

Kafeini (Caffeine)
Ingawa baadhi ya utafiti unaonesha kuwa unywaji wa kiasi kidogo cha kafeini hauna madhara, lakini kuna utafiti mwingine unaonesha kuwa unywaji wa kafeini una uhusiano na kuharibika kwa mimba. Kafeini ni aina ya kirutubisho kinachopatikana ndani ya kahawa.

Iwapo mjamzito atakunywa kahawa, basi anywe kiasi kidogo sana kisichozidi kikombe kimoja kwa siku. Kwa kawaida kahawa hukausha maji mwilini, hivyo unywaji wake husaidia kukauka maji mwilini ambayo ni muhimu sana kwa mjamzito.

Utafiti mwingine unaonesha kuwa kafeini inahusishwa pia na uharibikaji wa mimba, uzaaji wa watoto ‘njiti’ na watoto wenye uzito mdogo. Ni vizuri kunywa maji ya kutosha, maziwa na juisi na kuepuka kunywa vinywaji vyenye kahawa.

Pombe
Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa unywaji wa pombe kiasi kidogo wakati wa ujauzito hauna madhara, kwa maana hiyo matumizi ya pombe hayaruhusiwi kabisa wakati wa ujauzito, hata kama ni kidogo.
Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito huweza kuathiri ukuaji mzuri wa mtoto. Kutegemeana na kiasi atakachokunywa mjamzito, pombe inaweza kumsababishia mtoto ugonjwa hatari utokanao na pombe (Fetal Alcohol Syndrome).

Vyakula gani ni muhimu sana kutumiwa na wajawazito?

Lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana, kwani lishe hii hutumika kwa mama na mtoto anaendelea kukua tumboni. kwa kawaida mahitaji ya chakula na virutubisho mwilini mwa mwanamke huongezeka wakati wa ujauzito na kadri ujauzito unavyoendelea kukua, virutubisho hivyo hutumika kujenga mwili wa mama na mtoto. hivyo maamuzi ya lishe au lishe mama anayopata huathiri pia maendeleo ya mtoto anayekua mwilini mwake. tutaona vyakula muhimu vya kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baadhi ya vitu vya kukwepa.

Mlo kamili (balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini:

Nafaka na vyakula vya wanga
Vyakula hivi huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni. Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali(mahindi,mtama,ulezi n.k), viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili(whole grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa; cereals n.k.

Nyama, samaki na vyakula vya protini
Hivi ni muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha miwezi wa 4 mpaka wa 9 ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi, senene, panzi na wanyama wengine ; vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere, karanga,korosho n.k . Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya protini muhimu

Vyakula vya mafuta
Hutumika kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti,senene, panzi, samaki na matunnda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu(cholesterol) nyingi.

Mboga za majani na matunda
Matunda na mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na ufanyaji kazi wa mwili. Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini joto(Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni mwa mama.Vitamini B9 (Foliki asidi) na madini ya chuma hutolewa kama virutubisho ziada kliniki wakati wa ujauzito ili kutosheleza mahitaji ya mwili na kuzuia hatari ya upungufu wa damu kutokea.

Maji
Maji ni muhimu kwenye mmenyenyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI). Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.3 kwa siku, yanaweza kuwa katika chai, juisi, soda, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda.

Mfano wa mpangilio wa mlo

Ili kuhakikisha mlo kamili mjamzito anaweza kufuata mfano wa mpangilio wa mlo ufuatao. Katika mpangilio huu inashauriwa kuchagua aina moja ya chakula kutoka katika kila herufi A mpaka E ili kuweza kuupata mlo kamili.

Mfano:

Mlo wa Asubuhi:
A – Chungwa/ Embe/ Ndizi mbivu/ Parachichi
B – Mkate/ Maandazi/ Chapati/ Vitumbua/ Uji
C – Karoti
D – Mayai
E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya

Mlo wa Mchana:
A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na chungwa
B – Ugali/ Wali/ Ndizi/ Makande/ Tambi
C – Mchicha/ matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji
D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa
E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya.

Mlo wa Usiku:
A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na Chungwa
B – Wali/ Ndizi/ Viazi/ Tambi/ Chapati
C – Mchicha/ Matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji,
D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa
E – Maziwa/Mtindi/Siagi/Maziwa ya Soya.

Imepitiwa: July 2017

Ugonjwa wa Malaria

Ufahamu ugonjwa wa Malaria

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyojulikana kama Plasmodium.Vimelea hivi huenezwa na mbu jike aina ya anofelesi (anopheles). Lakini watu wengi huelewa kwamba malaria husababishwa na mbu. Mbu huyu husaidia katika usambazaji tuu wa vimelea husika.

Aina ya vimelea ambavyo humdhuru binadamu kati ya vimelea vingi vya Plasmodium ni:
• Plasmodium Vivax
• Plasmodium Falciparum
• Plasmodium Malariae
• Plasmodium Oval

Plasmodium Vivax: Vimelea hivi havina madhara makubwa ingawa vimesambaa sana kuliko vile vya Plasmodium Falciparum.
Plasmodium Falciparum: husababisha vifo vingi na kwa haraka zaidi.
Vimelea vingine kama Plasmodium Malariae na Plasmodium Oval husababisha pia malaria lakini sio kwa ukali na yenye uharibifu kama vile vya Plasmodium Falciparum. Ukurasa huu umejizatiti zaidi kuzungumzia malaria inayosababishwa na Plasmodium Falciparum, kwani ndio inayotushambulia zaidi ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Jinsi mtu anavyopata maambukizi ya malaria

Vimelea (parasites) huingia kwenye mwili wa binadamu baada ya mbu jike aliyeathirika na vimelea hivyo vya malaria wakati akinyonya damu ya binadamu kama mlo wake, atamng`ata na kunyonya damu binadamu mwingine. Ni katika kipindi hiki ambapo mbu huweza kuviacha vimelea alivyovitoa kwa mtu mwingine na kumuathiri mtu huyu. Mbu huyu ana kawaida ya kumdhuru binadamu kwa kumng`ata kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.
Vimelea huzaliana ndani ya utumbo wa mbu na baadae husafiri hadi kwenye tezi za mate yake. Wakati mbu anamng’ata binadamu hutoa mate kama ganzi ili binadamu asigundue kama anang’atwa na hapo ndipo vimelea vya malaria humuingia binadamu.
Baada ya kuingia kwenye mwili wa binadamu vimelea hivi husafiri hadi kwenye ini ambapo huzaliana kwa wingi na hatimaye kuingia kwenye mzunguko wa damu na kusababisha uharibifu wa seli nyekundu za damu. Hapa ndipo mtu huanza kujihisi homa, kutetemeka na dalili nyinginezo za malaria.

Dalili za malaria

Dalili za malaria zinategemea mtu na mtu kutokana na nguvu ya kinga yake. Hata hivyo dalili zinazowapata wagonjwa wa malaria zinatokana na hatua ya ugonjwa aliyonayo mtu aliyeambukizwa.

Kuna aina mbili za malaria:
1. Malaria ya kawaida, isiyokuwa kali au sugu kitaalamu inaitwa “Uncomplicated Malaria”. Hii inakuwa haijasababisha madhara makuwa katika mwili.
2. Malaria sugu, kitaalamu “Complicated Malaria”. Hii imeishasababisha madhara kama kuharibu viungo muhimu mwilini kama, ubongo (kupoteza fahamu – cerebral coma), figo (figo kufeli-renal failure), ini (ini kufeli -liver failure), moyo (moyo kufeli – heart failure), mapafu (mapafu kufeli – pulmonary failure), upungufu wa sukari mwilini (hypoglycaemia). Na pia kuwa na vimelea vingi (hyperparasitaemia).

Dalili za malaria isiyo kali

1. Homa ikiambatana na maumivu ya kichwa
2. Maumivu ya mwili
3. Tumbo kuuma na kuharisha
4. Kichefuchefu na kutapika
5. Kizunguzungu
6. Kutokwa jasho
7. Kutetemeka
8. Kifua kuuma
9. Kukosa hamu ya kula

Dalili za malaria kali

1. Mabadiliko katika mwenendo na tabia (kuchanganyikiwa)
2. Uchovu mkubwa kupita kiasi (mgonjwa hawezi kukaa au kusimama)
3. Upungufu mkubwa wa damu (mgonjwa husikia kizunguzungu sana)
4. Kupoteza fahamu
5. Kupumua kwa shida
6. Degedege/mtukutiko mwili (Kwa watoto wadogo)
7. Kutapika kila kitu, kushindwa kunywa au kunyonya kwa watoto
8. Mzunguko hafifu wa damu, kutokwa damu isiyo ganda kwa urahisi
9. Figo kushindwa kufanya kazi na kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi/kahawia.

Kumbuka:

Malaria hushambulia zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5), wanawake wajawazito na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Hii ni kutokana na kinga zao za mwili huwa chini.

Hizi dalili pia hutokea katika magonjwa yanayoambukizwa na bakteria, kwa mfano:
Homa inaweza kuwa dalili ya UTI, Pneumonia, Typhoid, n.k
Kukohoa kunaweza kuwa sababu ya maambukizi katika mapafu mfano pneumonia, kifua kikuu n.k
Kutapika na kuharisha inaweza kuwa dalili za magonjwa ya maambukizi ya tumbo pia.

Hivyo ni vema ukipata dalili hizi usichukue dawa bila kupata uchunguzi wa kitaalamu na pia ushauri kutoka kwa madaktari. Unapopata dalili hizi wahi hospitali ili wataalamu wakuchunguze na kujua ni ugonjwa gani ulionao.

Matibabu ya Malaria

Kwa malaria isiyosugu/isiyokali, dawa inayopendekezwa kwa sasa kama tiba ya kwanza ni dawa ya Mseto (ALU), pia gonjwa anatumia dawa akiwa nyumbani kwake. Kutokana na dalili za mgonjwa huyu, inawezekana anaweza kula na kunywa vizuri na dalili nyingine pia sio za kushtua sana ndio maana mgonjwa hupewa vidonge na ushauri wa mlo na vitu vya kuepuka akiwa anatumia dawa za malaria, hususani bidhaa za pombe.

Kwa malaria sugu, matibabu yanayopendekezwa kama tiba kwa mgonjwa ni dawa ya Quinine kwa njia ya dripu. Pia mgonjwa anapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Mgonjwa analazwa hospitalini hadi anapopata nafuu na kuweza kula mwenyewe. Wagonjwa wengi wenye malaria kali au sugu, kutokana na hali yao ya kupoteza fahamu, kutapika kila kitu na kushindwa kula, pamoja na dalili zingine kama zilivyoorodheshwa hapo juu, ni vyema walazwe ili wapewe huduma stahiki.

Jinsi ya kujikinga na Malaria

Malaria ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa vifo nchini Tanzania. Ila ni ugonjwa ambao vilevile kwa maamuzi na bidii za binadamu ugonjwa huu unaweza kukwepeka. Hivyo basi, zifuatazo ni namna mbalimbali za kujikinga na malaria:

1. Kutumia chandarua kilicho wekwa dawa ya kuua mbu. Kutumia tu chandarua haitoshi. Ni muhimu kulala kwenye chandarua kilicho na dawa. Chandarua nyingi zinazouzwa madukani kwa muda huu zimeshawekwa dawa tayari, lakini unashauriwa kuuliza na kuwa na uhakika kuwa chandarua unachonunua kimewekwa dawa.

2. Kuweka mazingira safi kwa kufukia madimbwi na mashimo yasababishayo maji kutuama. Maji yanayotuwama huzalisha sana mbu. Mayai ya mbu hupendelea maeneo yenye majimaji lakini yasiyokuwa na kusogea (yaliyotuama), mfano madimbwi ya maji ya mvua yaliyokaa muda mrefu bila kukauka, unyevunyevu vichakani na kwenye nyasi ndefu, makopo yenye uwazi yaliyotelekezwa na kujaa maji ndani yake, magari mabovu yaliyonyeshewa mvua na kukusanya maji ndani, mabwawa madogomadogo kama ya kufugia samaki n.k. Hivyo ni vyema kufukia madimbwi, kufyeka nyasi, kuchoma au kusafisha makopokopo na magaloni na pia kuondoa magari mabovu na chochote kinachoweza kukusanya maji kwa muda mrefu kwa eneo lote linalozunguka nyumba yako. Ukifanya hivi utakuwa umesababisha hatua muhimu ya kisababishi cha malaria (mbu) asizaliwe.

3. Kuteketeza mazalia ya mbu kwa kunyunyuzia dawa ya DDT. Baada ya kufanikisha namba mbili hapo juu, na kuna sehemu ambazo mazalia ya mbu yanaweza kutokea na hakuna jinsi ya kuepuka maji haya yaliyotuama inashauriwa kunyunyuzia dawa ya DDT. Dawa hii ni sumu ambayo pia inaweza ikamdhuru binadamu. Hivyo shughuli ya kunyunyizia dawa hii hufanywa na wataalamu wa afya na mazingira.

4. Kufukuza na kuzuia kung`atwa na mbu. Ni ukweli kwamba pamoja na juhudi zote hapo juu bado kuna uwezekano wa kung`atwa nambu kwani tupo kwenye eneo la tropiki ambalo ndio makazi yao. Hivyo basi njia nyingine za ziada zinahitajika kujikinga using`atwe na mbu waliofanikiwa kuzaliwa.

Kuua mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba. Kuna baadhi ya kampuni wanafanya kazi ya kuua vimelea (fumigation) maeneo mbalimbali.
Kufukuza mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba (Ifahamike kuwa kuna dawa ambazo zina uwezo wa kufukuza pekee na kuna ambazo zinaua kabisa hivyo unavyonunua dawa dukani elewa unanunua dawa ya aina gani ili uitumie kama inavyoelekezwa)
Kuzuia mbu – Dawa za kupaka. Kwa wakati ambao haupo nyumbani inawezekana ukawepo kwenye sehemu yenye mbu, mfano baa, mpirani au hata kazini katika ule muda ambao mbu hung`ata, ni vyema ukajikinga nao kwa kujipaka dawa mbalimbali za kuwafukuza au kuwaua mbu pale wanapokukaribia au kuanza kukung`ata. Dawa hizi zinatoa harufu ambayosio rafiki kwa mbu hawa au zina uwezo wa kuwaua pindi wanapoanza kukuchoma.

5. Kujikinga na ugonjwa wa malaria kwa kina mama wajawazito ni muhimu. Wajawazito wana hatari kubwa zaidi ya kung`atwa na mbu kutokana na mabadiliko yao ya kimwili, mfano joto la mwili kuongezeka, hivyo mbu huweza kuwafikia kwa urahisi zaidi. Inapendekezwa na wizara ya afya kwamba wanawake wajawazito watumie dawa ya malaria aina ya “SP” kabla ya kujifungua. Hii itawasaidia kama kinga dhidi ya malaria kwao na kwa watoto wao tumboni. Dozi ya dawa hizi hutolewa katika vituo vya afya vinavyo toa huduma kwa mama na mtoto.

6. Ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za malaria kwa wagonjwa. Kuzingatia dozi sahihi inaweza ikawa kinga kwa maambukizi mengine yanayokuja. Vilevile kutokumaliza dozi kunamaanisha kuviacha baadhi ya vimelea mwilini ambavyo havikufa tayari mpaka kipindi ulipoacha dozi.

7. Usitumie dawa bila kumuona daktari kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaongeza usugu wa dawa mwilini mwako bila sababu ya msingi na pia unahatarisha maisha yako. Usugu wa dawa za malaria ni hatari na inamaanisha ukipata malaria na vimelea ulivyonavyo vimeshakuwa sugu kwa dawa zilizopo za malaria, maisha yako yanakuwa hatarini kwani madaktari watashindwa kukutibu.

Wito

Malaria ni ugonjwa hatari unaoua kwa haraka hivyo pindi unapohisi una dalili za malaria kama zilivyoorodheshwa hapo awali, wahi katika kituo cha kutoa huduma za afya kilichokaribu na wewe ili upatiwe uchunguzi na kupata tiba sahihi.

Imepitiwa: July 2017