Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Zifahamu Aina Mbalimbali za Uzazi wa Mpango

Uzazi wa Mpango ni Nini?

Uzazi wa mpango ni maamuzi ya hiari ya mtu au wenza juu ya ni wakati gani waanze kuzaa, watoto wangapi wazae, wapishane kwa umri gani na lini waache kuzaa. Uzazi wa mpango unawahusu wenza wote wawili, kwahiyo ni vizuri kuliongelea hili pamoja. Hata hivyo chaguzi nyingi za uzazi wa mpango huanzia kwa mwanamke, kwahiyo ni muhimu kwa mwanamke kuamua kutumia njia ile itakayo kubaliana na mwili wake.

Uzazi wa Mpango una Faida Gani?

  • Pamoja na kumuwezesha mama na mtoto kuwa na afya njema, uzazi wa mpango una faida nyingi kwa wanawake, wanaume, watoto, familia na jamii kwa ujumla:
  • Unamsaidia mama kurudi katika hali yake ya zamani ambayo ilisumbuliwa na hali ya ujauzito, uchungu na kujifungua, mama atakuwa mwenye nguvu, afya nzuri na mchangamfu. Na pia atakuwa na muda mzuri wa kurudisha afya yake kabla ya kupata ujauzito mwingine.
  • Unamuwezesha kuhudumia familia yake vizuri na kuwa na maisha bora. Utakuwa na muda, fedha na mahitaji muhimu kwa familia yako kama chakula, mavazi, elimu, mapenzi na huduma zote muhimu. Mama anapata muda wa kutosha wakujishughulisha na mambo mengine ya kiuchumi na kimaendeleo kwa ajili ya familia na jamii kwa ujumla.
  • Mama na baba wanapata muda mzuri wa kujishughulisha zaidi na mambo na mahitaji yao binafsi.
  • Unasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Nani Anapaswa Kutumia Uzazi wa Mpango?

Yoyote mwenye umri wa kuzaa au anatarajia kufikia umri huo anapaswa kufikiria kuhusu uzazi wa mpango. Uzazi wa mpango ni muhimu kwa:

  • Wanawake na wanaume
  • Watu walioa na kuolewa au ambao hawajaoa wala kuolewa
  • Watu wenye watoto au bado hawajapata watoto.

Ni Wakati Gani Mtu Atumie Uzazi wa Mpango?

Umri sahihi wa kuanza kutumia uzazi wa mpango ni kuanzia miaka ishirini (20) na thelathini na tano (35). Ujauzito ni hatari kwa mama na mtoto endapo mama atajifungua chini ya umri wa miaka ishirini (20) au zaidi ya miaka thelathini na tano (35) vilevile ni hatari kwa mama atakaejifungua zaidi ya watoto wanne au watoto wasipopishana. Wenza wanatakiwa kusubiri angalau miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine pia wafikirie kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango wakati wote ambao hawajapanga kupata mtoto.

Njia za Uzazi wa Mpango ni Zipi?

Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kutumiwa na mtu au wenza waweze kusubiri, kuchelewesha, au kupunguza idadi ya watoto watakaowazaa. Zipo njia za mda mfupi, mda mrefu na za kudumu.

Njia za muda mfupi

Hizi ni njia za kisasa za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuzibadilisha. Unaweza kupata ujauzito pindi utakapoacha kuzitumia. Njia hizi ni nzuri kwa mama anayetaka kupata ujauzito baada ya miaka miwili baada ya kujifungua. Nazo ni:

Njia ya vichecheo-njia hizi zina vichocheo ni sawa na vichocheo vya kawaida vilivyomo kwenye mwili wa mwanamke.

Njia ya vidonge-vidonge hivi hutumiwa na wanawake kila siku. Vidonge vya uzazi wa mpango ambavyo hutumiwa na mwanamke huwa na homoni ambazo huepusha mwanamke kupata mimba kwa kuzuia yai la mwanamke kutokupevuka. Vidonge vya uzazi wa mpango havizuii maambukizi ya magonjwa ya ngono.

Njia ya sindano-mama huchoma sindano kila baada ya miezi mitatu (3). Sindano ni kama vidonge na kipandikizi huzuia yai la mwanamke kupevuka kwa kutoa homoni itakayo kukinga usipate mimba. Njia hizi hazitakuzuia kupata/ kuambukizwa magonjwa ya ngono.

Njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango-humezwa na mama ili kuzuia kupata mimba kwa mama aliyejamiana bila kutumia kinga yeyote. Hivi vinaweza kuzuia mimba hadi siku tano baada ya kujamiana.

Njia za Kizuizi

Kondom za kike na kiume-ni muhimu kutumia ipasavyo kila unapofanya ngono. Hii ni njia pekee ya uzazi wa mpango ambayo inazuia vyote, mimba, magonjwa ya ngono ukiwemo virusi vya ukimwi. Zinazuia shahawa za mwanaume kuingia kwenye uke wa mwanamke.

Njia za asili

Kukosa hedhi kwa kunyonyesha mfululizo

Hii ni njia ya asili ambayo inatokea kwa mwanamke anayenyonyesha na ni ya kuaminika zaidi wakati mama huyo bado hajaanza kuona siku zake za hedhi na ili hayo yote yatokee ni lazima mama awe anamnyonyesha mwanae mara kwa mara usiku na mchana na mtoto awe na umri chini ya miezi sita (6).

Elimu ya kujua siku hatari katika uzazi

Hii inawezekana ikiwa mama anaufahamu mzunguko wake mzima wa siku zake za hedhi na kujua ni zipi siku za hatari za kushika mimba. Yeye na mwenza wanatakiwa kuacha kabisa kufanya ngono siku hizo za hatari.

Kukojoa nje

Hii inafanywa na mwanamume wakati wa tendo la ndoa ambapo humwaga shahawa zake nje ya uke.

Njia za muda mrefu

Hizi ni njia ambazo pia zinaweza kurudiwa. Unaweza kupata ujauzito mara utakapoacha kuzitumia. Hizi ni nzuri ikiwa unataka kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine.

Njia ya vipandikizi

Hiki ni kijiti cha plastiki (chenye urefu wa milimita nne) anachowekewa mwanamke chini ya ngozi kwenye mkono wake kinaweza kuwa kimoja au viwili. Hivi huzuia mwanamke asipate ujauzito kwa muda kati ya miaka 3 hadi 5 kutegemea na aina ya vipandikizi alivyotumia. Hutoa homoni ambazo hulizuia yai la mwanamke kupevuka na kukuepusha kupata mimba. Kipandikizi hiki kinauwezo wa kukaa kwa miaka mitatu hadi mitano lakini hakitakuzuia kupata/kuambukizwa magonjwa ya ngono.

Njia ya kitanzi

Ni kifaa kidogo chenye shaba na plastiki ambacho huwekwa kwenye mji wa mimba. Hichi hukuzuia usipate mimba mpaka miaka kumi na mbili (12), unaweza kukitoa wakati wowote utakapoamua au kuhitajia kupata mtoto.

Njia ya kudumu

Hizi ni njia huwezi kuzirudia na ukitumia huwezi kupata mtoto tena. Na hutumiwa na watu ambao hawataki kupata mtoto tena. Nazo ni;

Kufunga kizazi kwa mwanaume

Njia hii inahusisha upasuaji mdogo ambapo mirija ya uzazi ya mwanaume ukatwa au kufungwa hivyo kuzuia yai kusafiri na kukutana na shahawa. Mwanaume anaendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kutoa mbegu lakini mbegu zake hazitaweza kutunga mimba

Kufunga kizazi kwa mwanamke

Njia hii inahusisha upasuaji mdogo inafanyika kwa kuziba au kukata mirija ya kizazi kuzuia yai kukutana na mbegu. Mwanamke ataendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kuona siku zake za hedhi.

Utafahamu Vipi Kuwa Njia Gani ya Uzazi wa Mpango ni Sahihi Kwako?

Inategemea na mtu mwenyewe au wenza kuamua njia gani ni sahihi kwao. Tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe uonane na wahudumu wa afya wataweza kukufahamisha njia sahihi kwako.

Kumbuka sio njia hizi zote zinaweza kupatikana kila mahali, kwahiyo zungumza kuhusu njia hizi za uzazi wa mpango na muhudumu wa afya unaemwamini mahali ulipo

IMEPITIWA: OKTOBA, 2021.

Dalili hatari kipindi cha ujauzito ambazo si za kupuuzia

Hata kama umesoma sana na kuongea na wazazi mbalimbali kuhusu dalili mbali mbali kipindi cha ujauzito, bado itatokea baadhi ya wakati ambapo utakuwa huna uhakika kama unavyojisikia ni kawaida au la.
Dalili zifuatazo ni muhimu kuzipa uzito wake na kuzifuatilia kwa makini. Kama ukizipata dalili hizi ni vyema kuwasiliana na mkunga, daktari wako au kituo cha kliniki ya wajawazito haraka iwezekanavyo.

Nina maumivu tumbo la kati

Maumivu makali au vichomi katikati au juu kidogo ya tumbo, ikiambatana na kchefuchefu na kutapika, inaweza kumaanisha kitu kimoja kati ya vifuatavyo. Unaweza ukawa na:

  • Kuvimbiwa kulikopitiliza
  • Kiungulia
  • Tumbo kuchafuka

Kama upo kwenye miezi mitatu hadi sita ya ujauzitowako, hii inawezza kumaanisha presha mimba ya awali. Hii ni dalili hatari na itahitaji matibabu ya haraka.

Nina maumivu ya tumbo ka chini

Maumivu makali upande mmoja au pande zote kwenye tumbo lako la chini yanahitaji uchunguzi kugundua kama sio kitu cha kushtua.

Kwa kiwango cha chini kabisa inaweza pia ikawa ni dalili za:

  • Mimba nje ya mji wa mimba
  • Mimba kutoka
  • Uchungu uliowahi
  • Uvimbe kwenye kizazi – uliovunjika na kuanza kuvuja damu kwa ndani yake.
  • Kuachia kwa kondo la nyuma (placenta)

Nina homa

Kama una homa na una jotoridi zaidi ya digrii 37.5c, na bila dalili za mafua, ni vyema kumuona daktari ndani ya siku hiyo hiyo.

Kama jotoridi ni zaidi ya nyuzi joto 39c wasiliana au fika kwa daktari wakati huo huo bila kusubiri. Inawezekana umepata maambukizi. Daktari wako atakuandikia dawa za kupambana na bakteria na kushauri upate mapumziko. Kama nyuzi joto za mwili wako zitapanda zaidi ya nyuzi joto 39 kwa muda mrefu itamuathiri mtoto wako tumboni.

Ninaona maruerue (mbili mbili) na nyota nyota

Muone daktari haraka kama, katika miiezi mitatu hadi sita ya ujauzito wako, kuona kwako kunapata shida ya:

  • Kuona mbili mbili
  • Kuona ukungu
  • Kuona giza
  •  Kuona nyota nyota

Matatizo haya kwenye mfumo wa kuona yanaweza yakawa ni dalili za presha mimba ya awali (Pre-eclampsia)

Mikono na miguu yangu imevimba

Kuvimba au kuumuka (oedema) kwenye mikono, uso, macho ni kawaida mwishoni mwa ujauzito. Mara nyingi sio kitu cha kuleta wasiwasi. Lakini kama kuvimba huku ni kukubwa na kumetokea ghafla, kukiambatana na kichwa kuuma na matatizo ya kuona kwako, inawezekana ukawa na presha mimba ya awali (pre-eclampsia). Kama utaona dalili yoyote kati ya hizi wasiliana na daktari bila kuchelewa.

Nina maumivu makali ya kichwa yasiyopungua

Kama maumivu makali ya kichwa yanaendelea kwa masaa mawili hadi matatu, na pia una matatizo ya kuona kwako na kuvimba sana kwa mwili wako, inawezekana ukawa na presha mimba ya awali (pre-eclampsia). Kama presha mimba ya awali ikitokea, mara nyingi huwa ni katika nusu ya mwisho ya ujauzito wako au punde tu baada ya kujifungua.

Ninavuja damu ukeni

Matone au kutokwa na damu kidogo bila maumivu ni kawaida kipindi cha mwanzo cha ujauzito. Inawezekana ni kuvuja kwa damu kunakosababishwa na zile homoni zinazouongoza mzunguko wako wa hedhi ziliendelea kutolewa kwa nguvu ya ziada na kusababisha kuvuja kwa damu kidogo.
Usiwe na wasiwasi kuhusu aina hii ya kutokwa damu, kwani hali hii huondoka yenyewe na si rahisi kumdhuru mtoto wako.
Pamoja na hilo, ni vyema kuwasiliana na mkunga au daktari wako kama utapata kutokwa na damu ukeni katika hatua yoyote ya ujauzito wako. Inaweza ikawa inamaanisha kuna tatizo kubwa kwenye ujauzito wako kama:

  • Kutoka damu tofauti na ilivyo kawaida kwa hedhi yako, inaweza ikawa nyepesi zaidi na nyeusi zaidi kuliko kawaida. Hili pamoja na maumivu makali ya muda mrefu upande mmoja wat umbo lako inaweza ikawa ni dalili ya mimba nje ya mji wa mimba.
  • Kutokwa kwa damu kwingi, ikiungana na maumivu ya muda mrefu ya mgongo au tumbo la chini inaweza kuwa ni dalili ya kutoka kwa mimba.
  • Kutoka kwa damu kwa ghafla kusiko ambatana na maumivu yoyote.

Imepitiwa: April 2017