Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Zifahamu Aina Mbalimbali za Uzazi wa Mpango

Uzazi wa Mpango ni Nini?

Uzazi wa mpango ni maamuzi ya hiari ya mtu au wenza juu ya ni wakati gani waanze kuzaa, watoto wangapi wazae, wapishane kwa umri gani na lini waache kuzaa. Uzazi wa mpango unawahusu wenza wote wawili, kwahiyo ni vizuri kuliongelea hili pamoja. Hata hivyo chaguzi nyingi za uzazi wa mpango huanzia kwa mwanamke, kwahiyo ni muhimu kwa mwanamke kuamua kutumia njia ile itakayo kubaliana na mwili wake.

Uzazi wa Mpango una Faida Gani?

  • Pamoja na kumuwezesha mama na mtoto kuwa na afya njema, uzazi wa mpango una faida nyingi kwa wanawake, wanaume, watoto, familia na jamii kwa ujumla:
  • Unamsaidia mama kurudi katika hali yake ya zamani ambayo ilisumbuliwa na hali ya ujauzito, uchungu na kujifungua, mama atakuwa mwenye nguvu, afya nzuri na mchangamfu. Na pia atakuwa na muda mzuri wa kurudisha afya yake kabla ya kupata ujauzito mwingine.
  • Unamuwezesha kuhudumia familia yake vizuri na kuwa na maisha bora. Utakuwa na muda, fedha na mahitaji muhimu kwa familia yako kama chakula, mavazi, elimu, mapenzi na huduma zote muhimu. Mama anapata muda wa kutosha wakujishughulisha na mambo mengine ya kiuchumi na kimaendeleo kwa ajili ya familia na jamii kwa ujumla.
  • Mama na baba wanapata muda mzuri wa kujishughulisha zaidi na mambo na mahitaji yao binafsi.
  • Unasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Nani Anapaswa Kutumia Uzazi wa Mpango?

Yoyote mwenye umri wa kuzaa au anatarajia kufikia umri huo anapaswa kufikiria kuhusu uzazi wa mpango. Uzazi wa mpango ni muhimu kwa:

  • Wanawake na wanaume
  • Watu walioa na kuolewa au ambao hawajaoa wala kuolewa
  • Watu wenye watoto au bado hawajapata watoto.

Ni Wakati Gani Mtu Atumie Uzazi wa Mpango?

Umri sahihi wa kuanza kutumia uzazi wa mpango ni kuanzia miaka ishirini (20) na thelathini na tano (35). Ujauzito ni hatari kwa mama na mtoto endapo mama atajifungua chini ya umri wa miaka ishirini (20) au zaidi ya miaka thelathini na tano (35) vilevile ni hatari kwa mama atakaejifungua zaidi ya watoto wanne au watoto wasipopishana. Wenza wanatakiwa kusubiri angalau miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine pia wafikirie kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango wakati wote ambao hawajapanga kupata mtoto.

Njia za Uzazi wa Mpango ni Zipi?

Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kutumiwa na mtu au wenza waweze kusubiri, kuchelewesha, au kupunguza idadi ya watoto watakaowazaa. Zipo njia za mda mfupi, mda mrefu na za kudumu.

Njia za muda mfupi

Hizi ni njia za kisasa za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuzibadilisha. Unaweza kupata ujauzito pindi utakapoacha kuzitumia. Njia hizi ni nzuri kwa mama anayetaka kupata ujauzito baada ya miaka miwili baada ya kujifungua. Nazo ni:

Njia ya vichecheo-njia hizi zina vichocheo ni sawa na vichocheo vya kawaida vilivyomo kwenye mwili wa mwanamke.

Njia ya vidonge-vidonge hivi hutumiwa na wanawake kila siku. Vidonge vya uzazi wa mpango ambavyo hutumiwa na mwanamke huwa na homoni ambazo huepusha mwanamke kupata mimba kwa kuzuia yai la mwanamke kutokupevuka. Vidonge vya uzazi wa mpango havizuii maambukizi ya magonjwa ya ngono.

Njia ya sindano-mama huchoma sindano kila baada ya miezi mitatu (3). Sindano ni kama vidonge na kipandikizi huzuia yai la mwanamke kupevuka kwa kutoa homoni itakayo kukinga usipate mimba. Njia hizi hazitakuzuia kupata/ kuambukizwa magonjwa ya ngono.

Njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango-humezwa na mama ili kuzuia kupata mimba kwa mama aliyejamiana bila kutumia kinga yeyote. Hivi vinaweza kuzuia mimba hadi siku tano baada ya kujamiana.

Njia za Kizuizi

Kondom za kike na kiume-ni muhimu kutumia ipasavyo kila unapofanya ngono. Hii ni njia pekee ya uzazi wa mpango ambayo inazuia vyote, mimba, magonjwa ya ngono ukiwemo virusi vya ukimwi. Zinazuia shahawa za mwanaume kuingia kwenye uke wa mwanamke.

Njia za asili

Kukosa hedhi kwa kunyonyesha mfululizo

Hii ni njia ya asili ambayo inatokea kwa mwanamke anayenyonyesha na ni ya kuaminika zaidi wakati mama huyo bado hajaanza kuona siku zake za hedhi na ili hayo yote yatokee ni lazima mama awe anamnyonyesha mwanae mara kwa mara usiku na mchana na mtoto awe na umri chini ya miezi sita (6).

Elimu ya kujua siku hatari katika uzazi

Hii inawezekana ikiwa mama anaufahamu mzunguko wake mzima wa siku zake za hedhi na kujua ni zipi siku za hatari za kushika mimba. Yeye na mwenza wanatakiwa kuacha kabisa kufanya ngono siku hizo za hatari.

Kukojoa nje

Hii inafanywa na mwanamume wakati wa tendo la ndoa ambapo humwaga shahawa zake nje ya uke.

Njia za muda mrefu

Hizi ni njia ambazo pia zinaweza kurudiwa. Unaweza kupata ujauzito mara utakapoacha kuzitumia. Hizi ni nzuri ikiwa unataka kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine.

Njia ya vipandikizi

Hiki ni kijiti cha plastiki (chenye urefu wa milimita nne) anachowekewa mwanamke chini ya ngozi kwenye mkono wake kinaweza kuwa kimoja au viwili. Hivi huzuia mwanamke asipate ujauzito kwa muda kati ya miaka 3 hadi 5 kutegemea na aina ya vipandikizi alivyotumia. Hutoa homoni ambazo hulizuia yai la mwanamke kupevuka na kukuepusha kupata mimba. Kipandikizi hiki kinauwezo wa kukaa kwa miaka mitatu hadi mitano lakini hakitakuzuia kupata/kuambukizwa magonjwa ya ngono.

Njia ya kitanzi

Ni kifaa kidogo chenye shaba na plastiki ambacho huwekwa kwenye mji wa mimba. Hichi hukuzuia usipate mimba mpaka miaka kumi na mbili (12), unaweza kukitoa wakati wowote utakapoamua au kuhitajia kupata mtoto.

Njia ya kudumu

Hizi ni njia huwezi kuzirudia na ukitumia huwezi kupata mtoto tena. Na hutumiwa na watu ambao hawataki kupata mtoto tena. Nazo ni;

Kufunga kizazi kwa mwanaume

Njia hii inahusisha upasuaji mdogo ambapo mirija ya uzazi ya mwanaume ukatwa au kufungwa hivyo kuzuia yai kusafiri na kukutana na shahawa. Mwanaume anaendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kutoa mbegu lakini mbegu zake hazitaweza kutunga mimba

Kufunga kizazi kwa mwanamke

Njia hii inahusisha upasuaji mdogo inafanyika kwa kuziba au kukata mirija ya kizazi kuzuia yai kukutana na mbegu. Mwanamke ataendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kuona siku zake za hedhi.

Utafahamu Vipi Kuwa Njia Gani ya Uzazi wa Mpango ni Sahihi Kwako?

Inategemea na mtu mwenyewe au wenza kuamua njia gani ni sahihi kwao. Tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe uonane na wahudumu wa afya wataweza kukufahamisha njia sahihi kwako.

Kumbuka sio njia hizi zote zinaweza kupatikana kila mahali, kwahiyo zungumza kuhusu njia hizi za uzazi wa mpango na muhudumu wa afya unaemwamini mahali ulipo

IMEPITIWA: OKTOBA, 2021.

Umuhimu wa Asidi ya Foliki Kipindi cha Ujauzito.

Asidi ya foliki ni shujaa katika mimba! Kumeza vitamini kabla ya kupata ujauzito kwa kiwango kinachokubalika cha mikrogramu 400mcg kabla na wakati wa ujauzito huweza kusaidia matatizo ya kuzaliwa nayo kwenye ubongo, mgongo na uti wa mgongo wa mtoto wako. Ni vyema kumeza kidonge cha asidi ya foliki kila siku kama unategemea au wewe ni mjamzito tayari.

Asidi ya foliki (Folic acid) ni nini?

Asidi ya foliki ni aina ya vitamini B inayoitwa “folate” inayotengenezwa na mwanadamu maabara (inajulikana kama vitamini B9). “Folate” inafanya kazi muhimu kwenye utengenezaji wa chembe damu nyekundu na pia husaidia katika kukinga dhidi ya kasoro katika neva za fahamu na hivyo kuepusha dosari za kimaumbile katika ubongo, mgongo na uti wa mgongo. Chakula bora chenye wingi wa asidi ya foliki ni “fortified cereals”. Folati hupatikana zaidi kwenye mbogamboga zenye rangi kijani iliyokolea na matunda jamii ya chungwa.

Ni lini uanze kutumia asidi ya foliki?

Matatizo ya kuzaliwa nayo (dosari katika neva za fahamu) huanza kutokea ndani ya wiki ya 3-4 ya ujauzito (siku 28) baada ya mimba kutungwa, kabla hata mama kujua kuwa ni mjamzito. Hivyo ni muhimu kuwa na “folate” tayari kwenye mzunguko wa mwili wako kwenye kipindi hiki muhimu cha mwanzoni ambapo ndio ubongo na uti wa mgongo wa mtoto wako unajijenga.

Kama ulizungumza na daktari wako kipindi ulichokuwa unataka kupata ujauzito, inawezekana alishakushauri tayari kuanza kutumia vitamini na asidi ya foliki. Tafiti moja ilionesha wanawake waliotumia asidi ya foliki kwa kuanzia mwaka kabla ya kupata ujauzito walipunguza uwezekano wa kujifungua mapema kabla ya muda (kabla ya wiki 37) kwa asilimia 50 au zaidi.

Tafiti zinaonesha nusu ya mimba zote hazikuwa zimepangwa hivyo inapendekezwa kuwa mwanamke yeyote anayetarajia kupata ujauzito atumie mickrogramu 400 za vidonge vya foliki asidi kila siku, akianza kabla ya kupata ujauzito na kuendelea namna hiyo kwa wiki 12 za ujauzito. Muda huu wa wiki 12 za mwanzo wa ujauzito ndiyo muda ambao ubongo na mfumo wa neva unajengwa na kukua

Shirika la kuzuia magonjwa la Marekani (CDC) linashauri Vilevile shirika wanawake wote walio kwenye umri wa kuweza kuwa wajawazito kutumia asidi ya foliki kila siku. Hivyo hata ukiamua kuanza kutumia asidi ya foliki mapema zaidi ni vyema zaidi.

Kama utaamua kununua nyongeza ya vitamini wewe mwenyewe, ni vyema ukazungumza pia na daktari wako baada ya kupata ujauzito ili kuwa na uhakika kuwa nyongeza hiyo ya vitamini ina mjumuisho wa kila kitu unachotakiwa ukipate kwa ujauzito wako ikiwemo asidi ya foliki.

Kiasi gani cha asidi ya foliki nitumie?

Dozi inayoelekezwa kwa wanawake wote waliopo kwenye umri wa kuweza kupata ujauzito ni mikrogramu 400 au 400mcg za folati kila siku. Ikiwa wewe ni mjamzito au unajaribu kupata ujauzito unashauriwa kutumia foliki asidi mapema kadiri uwezavyo na ndani ya wiki 12 za kwanza za ujauzito. Kufanya hivi kutamsaidia mtoto kukua vizuri na kawaida.

Daktari anaweza kukushauri kutumia dozi kubwa zaidi ya foliki asidi ikiwa uko katika hatari kubwa ya kupata dosari katika neva za fahamu (neural tube defects) wakati wa ujauzito.

Huu ndio mchanganuo wa kiasi cha asidi ya foliki kinachoelekezwa kwa wanawake wajawazito kwa siku

  • Ukiwa unataka kupata ujauzito – 400mcg
  • Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito – 400mcg
  • Kuanzia mwezi wa 4 hadi wa 9 wa ujauzito – 600mcg
  • Ukiwa unanyonyesha – 500mcg.

Mama ambaye tayari amepata mtoto mwenye dosari katika neva za nyuroni (mfumo wa fahamu) anahitaji ajadiliane na daktari wake kama atahitaji vidonge vya foliki na dozi yake itakuwa ni ipi. Tafiti zinaonesha kwamba matumizi ya mikrogramu 4,000 kwa mwezi mmoja kabla na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito zinaweza kusaidia kutatua tatizo hili. Tafadhali usitumie dawa hizi mwenyewe bila kujadiliana na daktari kwanza.

Asidi ya foliki ina faida gani?

Bila kuwa na asidi ya foliki ya kutosha, dosari katika neva za fahamu na hivyo kuepusha kasoro za kimaumbile katika ubongo, mgongo na uti wa (neural tube defects). Magonjwa haya ni kama:

  • Spina bifida: Kutokukamilika ukuaji wa uti wa mgongo au pingili za uti wa mgongo.
  • Anencephaly: Kutokukamilika kwa ukuaji wa sehemu kubwa ya ubongo.

Watoto wenye “Anencephaly” mara nyingi hawaishi muda mrefu na wale wenye “spina bifida” huwa na ulemavu maisha yao yote. Habari njema ni kwamba kutumia nyongeza ya asidi ya foliki kipindi cha ujauzito inaweza kumuepusha mtoto wako kupata magonjwa haya kwa zaidi ya asilimia 50.

Kama utatumua kabla na wakati wa ujauzito, asidi ya foliki inaweza kumkinga mtoto wako dhidi ya:

  • Mdomo sungura
  • Kuzaliwa kabla ya muda (Njiti)
  • Kuzaliwa na uzito mdogo
  • Mimba kutoka
  • Ukuaji dhaifu tumboni

Asidi ya foliki pia inahusishwa na kupunguza hatari ya kupata:

  • Matatizo kwenye ujauzito
  • Magonjwa ya moyo
  • Kiharusi
  • Aina baadhi ya saratani
  • Ugonjwa wa “Alzheimer”

Je, kuna vyanzo vingine vya folati?

Vyakula vilivyo na foliki asidi katika kiwango kiubwa ni kama:

  • Mboga za majani kama spinachi, kabichi, loshu, broccoli
  • Mimea jamii ya kunde kama maharage, mbaazi, njegere, njugu
  • Karanga, njugumawe, nazi na korosho
  • Matunda jamii ya sitrusi kama machungwa, machenza, limao n.k
  • Nafaka zisizokobolewa
  • Maini na samaki
  • Vyakula vilivyoongezwa foliki asidi.

Kumbuka

  • Kichefuchefu, kupoteza hamu ya kulan a kuvimbiwa ni madhara yanayoweza kutokea kwa mjamzito kama matokeo ya kutumia vidonge hivi. Ulaji wa chakula kidogo kidogo badala ya kula milo mikubwa mitatu kwa siku, kula na kunywa taratibu na kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara yanaweza kusaidia dalili hizi unazoweza kupata kama matokeo ya kutumia asidi ya foliki. Ikiwa dalili hizi zinaendelea kuwa mbaya, wasiliana na daktari/mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako mara moja.
  • Mtoto tumboni yuko katika hatari ya kupata dosari katika mfumo wa fahamu ikiwa: mama mjamzito aliwahi kupata ujauzito ulipata dosari katika mfumo wa neva za fahamu, wewe au mwezi wako ana kasoro katika neva za fahamu aliyozaliwa nayo,katika familia yako au mwezi wako kuna historia ya watu kuzaliwa na dosari katika neva za fahamu, mjamzito ana kisukari,mjamzito ana uzito mkubwa uliopitiliza na mjamzito ana ugonjwa wa siko seli.
  • Mama ambaye hakutumia foliki asidi kabla au miezi ya awali ya ujauzito ajadiliane na daktari/mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wake, wataweza kukushauri nini kifanyike na dozi kiasi gani itumike kuokoa maisha ya mtoto tumboni. Tafadhali usitumie dawa hizi mwenyewe bila kujadiliana na daktari kwanza.

IMEPITIWA: JUNI,2021.