Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kupevuka mayai ya uzazi wa mwanamke (ovulation)

Kupevuka kwa yai ni nini?

Ovulation (kupevuka kwa mayai ya uzazi wa mwanamke) ni pale yai moja au zaidi yanaachiwa kutoka kwenye moja ya ovari (mifuko ya mayai) ya mwanamke. Kila mwezi, kati ya mayai 15 hadi 20 yanakua ndani ya mfuko wa mayai ya mwanamke. Yai lililokomaa zaidi hutolewa na kusukumwa kwenye mirija yako ya uzazi (fallopian tubes) inayounganisha mfuko wa mayai na uterasi. Mifuko ya mayai haipokezani kutoa yai lililokomaa kila mwezi,hali hii inatokea bila mpangilio maalumu.

Haijalishi kama yai limerutubishwa au halijarutubishwa, litasafirishwa kwenye mirija ya uzazi kisha kwenye uterasi. Kama yai limerutubishwa na mbegu linapandikizwa ndani ya ukuta wa uterasi ambao umeandaliwa na homoni husika kwaajili yake, huu ndio mwanzo wa ujauzito. Ikiwa yai halijarutubishwa basi ukuta ulioandaliwa ndani ya uterasi hutolewa nje ya mwili pamoja na yai lisilorutubishwa wakati wa hedhi.

Chanzo cha kupevuka kwa mayai ya uzazi (ovulation) wa mwanamke ni nini?

Homoni ya LH (luteinizing hormone) inayotolewa na tezi ya pituitari inaanza kuongezeka ndani ya mwili wa mwanamke pindi anapokaribia “ovulation”. Homoni ya FSH (follicle-stimulating hormone) inahusika katika kuhakikisha yai linakomaa haraka na kutolewa na ovari. Homoni ya LH inasababisha estrogeni kuongezeka taratibu. Kadiri siku zinavyoendelea homoni ya LH inajenga tena kiwambo laini ndani ya ukuta wa uterasi, kiwambo hiki kinaongezeka unene uliojaa damu na virutubisho kama maandalizi ya upandikizaji wa yai (egg implantation)

Utaratibu huu unafanyika kila mwezi mpaka yai litakapopandikizwa kwenye ukuta wa uterasi au hedhi yako itakapoaanza. Ongezeko la homoni ya estrogeni inafanya uteute unaopatikana katika mlango wa kizazi kuwa katika hali ya kuruhusu mbegu za kiume kusafiri kuelekea kwenye yai. Viwango vya homoni hii vinaendelea kuongezeka mpaka kufikia hatua ya kuhamasisha kuongezeka kwa homoni ya LH inayosukuma utoaji wa yai lililokomaa kwenye mirija ya uzazi, kitendo hiki kinaitwa “ovulation”

Ni wakati gani kupevuka kwa yai kunatokea?

Muda haswa wa lini “ovulation” inatokea sio maalum. Kwa kawaida hutokea kati ya siku 11 na 21 baada ya siku ya kwanza ya hedhi yako ya mwisho. Kwa mfano, tuseme una mzunguko wa kawaida wa hedhi wa siku 28, hesabu siku ya kwanza ya kuona hedhi yako kama siku ya kwanza. Siku za wewe kuweza kupata ujauzito ni kati ya siku ya 10 hadi ya 15.

Baadhi ya wanawake inaweza kuwahi kutokea, na wengine kuchelewa. Kila mwanamke ni tofauti na vilevile kila mzunguko wa hedhi unaweza kuwa tofauti kwa mwanamke huyo huyo mmoja. Hata hivyo, makadirio mazuri yaliyofikiwa ni kwamba “ovulation hutokea katikati ya mzunguko wako wa hedhi, yaani karibu na siku ya 14.

Ovulation hudumu kwa muda gani?

 Yai linaweza kuchavushwa kati ya masaa 12 na 24 baada ya kupevushwa. Kiasi cha muda ambao yai huchukua kutolewa na ovari na kupokelewa na mirija ya falopiani hubadilika lakini mara nyingi huchukua masaa 12 hadi 24 baada ya homoni inayotolewa na tezi ya pituiatari kuongezeka (LH).

Ovulation inatokea sehemu gani?

Kila mwanamke anazaliwa na mayai ambayo yatadumu milele (mwili wa mwanamkee hautengenezi mayai). Yapo takribani mayai milioni moja hadi mbili wakati wa kuzaliwa, namba hii inaopungua hadi laki tatu muda kubale unapowadia. Kipindi ambapo mwanamke anaweza kubeba ujauzito, idadi ya mayai 500 yatolewa wakati wa “ovulation”. Yanayobakia yatakufa taratibu kadiri mwanamke anapoelekea uzeeni. Mara baada ya yai kutolewa linapokelewa na mirija ya falopia, “cilia” ndani ya mirija hiyo husaidia yai kusafiri kwa usalama kutoka mirija ya falopia kuelekea kwenye uterasi.

Lini naweza kupata ujauzito?

“Fertile window” ni kipindi katika mzunguko wa hedhi wa mwanamke ambacho mwanamke anaweza kupata ujauzito. Kipindi hichi kinadumu kwa siku tano au sita kila mwezi kwa wanawake wengi. Ili kupata ujauzito kwa njia ya kawaida, moja ya yai na mbegu kutoka kwa mwenza wako lazima vikutane kwenye mirija yako ya uzazi. Yai lako haliwezi kuwa hai kwa zaidi ya saa 24 baada ya kuwa kupevushwa. Kwa hiyo kukutana kwa yai na mbegu lazima kufanyike ndani ya muda huu. Kwa upande mwingine, mbegu za mwanaume huweza kuwa hai hadi kufikia siku saba. Zitaishi kwa raha kwenye uke, mfuko wa mimba, au kwenye mirija ya uzazi kwa muda wote huu. Kiuhalisia una jumla ya siku sita kwenye mzunguko wako ambazo unaweza ukapata ujauzito. Kwa hiyo ukifanya ngono katika kipindi hiki, yai lako lililopevuka tayari linaweza likakutana na mbegu yenye afya na kuchavushwa(fertilized).

Hivyo basi, ikiwa ulifanya tendo la ndoa bila kinga siku chache kabla ya “ovulation” unaweza kupata ujauzito. Hii inamaanisha sio lazima kufanya tendo la ndoa siku halisi ya ‘ovulation” ili utungisho wa mimba kutokea.

Jambo hili linaweza kuelezewa zaidi kwa mtazamo huu, kama yai linapevuka siku ya 14 katika mzunguko wako wa mwezi, basi yai linaweza ishi mpaka siku ya 15. Mda wako wa kupata ujauzito “fertile window” utaanza tangu siku ya 9 ya mzunguko wako, vilevile ikumbukwe mbegu za kiume zinaishi ndani ya mwili wa mwanamke kwa siku 5-7. Hii itakupa uwazi wa kupata ujauzito wa siku sita kila mwezi.

Uwazi wa kupata ujauzito “fertilite window” unadumu kwa siku 6 kuanzia siku 5 kabla yai kupevuka mpaka siku halisi ya kupevuka kwa yai. Hivyo basi siku ulizo katika nafasi kubwa ya kupata ujauzito ni siku ya 4-5 kabla na siku ya “ovulation”

Utafiti unaonyesha kupevuka kwa yai hakutokei siku ile ile kila mwezi hata kwa wanawake walio na mtiririko mzuri wa hedhi. Kwa kawaida kipindi cha uwazi cha kupata ujauzito “fertile window” ni siku sita, lakini idadi ya siku ambazo mwanamke anakuwa katika nafasi ya kupata ujauzito “fertile days” ni nyingi zaidi kwasababu siku hizi zinajumuisha siku zote katika mzunguko wa hedhi ambapo mwanamke anapokuwa na uwezo wa kupata ujauzito. Hivyo basi kukokotoa na kujua siku hizi itawasaidia wanandoa wanatafuta ujauzito kuongeza nafasi ya utungisho wa mimba.

Nitajuaje mayai yanapevuka ndani ya mwili wangu?

Ili kuongeza nafasi ya kupata ujauzito, fahamu ishara zinazotokea katika mwili wako siku mayai yanapevuka “ovulation” ili kujua siku zipi uko katika hali nzuri ya kubeba ujauzito. Baadhi ya ishara na dalili ni pamoja na:

Mabadiliko ya uteute kwenye mlango wa uzazi
Huu ni ule uteute unaona kwenye chupi au kwenye “toilet paper” unapokwenda kukojoa. Mabadiliko ya uteute wa mlango wa uzazi ni ishara kuwa upo kwenye siku nzuri za kupata ujauzito. Baada ya hedhi kumalizika uteute kwenye via vya uzazi unaongezeka kwa ujazo na hubadilika pia hali yake. Mabadiliko haya yanaendana na kuongezeka kwa kiwango cha homoni ya estrojeni kwenye mwili wako. Pia inaonesha umekaribia muda wa mayai kupevuka.

Uwezo wa kupata ujauzito unaongezeka ikiwa uteute unakuwa kama hauna rangi (clear), unateleza sana na unavutika. Utafanana kama sehemu nyeupe ya yai ukilivunja. Huu uteute huzisaidia mbegu za kiume kuwa na kasi zaidi wakati zinaogelea kuelekea kwenye mfuko wako wa uzazi (uterasi). Uteute huu unazilinda mbegu za kiume zinapokuwa zinasafiri kuelekea kwenye mirija yako ya uzazi (fallopian tubes) kukutana na yai lako.

Maumivu ya tumbo la chini
Mwanamke mmoja kati ya watano huwa anasikia kitu kinaendelea kwenye mifuko yao ya mayai (ovaries) wakati wa kipindi cha kupevushwa mayai. Hii inaweza ikatokea kama maumivu madogo madogo au maumivu yanayovuta na kuachia endapo maumivu ni makali sana pata ushauri zaidi hospitali. Maumivu haya yanatokea upande mmoja wa tumbo la chini (tumbo la uzazi) kwasababu kila mwezi yai moja linatolewa na ovari moja kila mwezi. Maumivu haya yanaweza hamia upande mmoja kwenda mwingine kila mzunguko, au kubaki upande mmoja kwa mizunguko kadhaa. Kama ukihisi dalili hizi katika kipindi hiki kila mwezi, angalia uteute wa mlango wako wa uzazi pia. Maumivu kipindi hichi cha mwezi yanaweza yakawa ni njia ya kukuwezesha kutambua kuwa una uwezo wa kupata ujauzito.

Mabadiliko ya hisia za mapenzi
Mabadiliko ya homoni kipindi hiki cha “ovulation” yanachangia kuongeza ashiki(hamu ya kufanya tendo la ndoa) kisha kushuka tena baada ya kipindi hiki kumalizika. Tafiti zinaonyesha kuongezeka kwa homoni ya estrojeni na homoni inayotolewa na tezi ya pituitary (lutenising hormone- inayoratibu kazi zinazofanyika katika ovari za mwanamke) zinachangia kumfanya mwanamke kutamani kufanya tendo la ndoa zaidi wakati huu. Lakini kama una msongo wa mawazo, huzuni au wasiwasi ni ngumu kupata ongezeko hili la kutaka kufanya tendo hili. Baadhi ya dalili zifuatazo zinaonyesha uko katika kipindi hiki lakini si rahisi kugundua:

  • Kuonekana na kujisikia vizuri: kujihisi una mvuto zaidi kimuonekano kadiri unavyokaribia “ovulation”. Kwa mfano unaweza ukajikuta unachagua nguo zinazokuvutia na kuvutia wengine zaidi kimapenzi kwenye kipindi hiki.
  • Manukato ya mwanamke: unanukia vizuri katika kipindi hiki. Harufu ya mwili wako ni nzuri na inawavutia wanaume kimapenzi katika kipindi hiki. Harufu hizi zinaweza kuwajulisha watu upo katika kipindi cha“ovulation”.

Matiti kujaa na chuchu kuuma

Viwango vya juu vya homoni ya estrojeni siku chache kabla ya “ovulation” zinayafanya matiti ya mwanamke kuwa malaini, kuvimba kidogo na kuwa na uwezo wa kuhisi haraka kuliko siku za kawaida.

Matone ya damu katika nguo zako za ndani

Unaweza kuona matone ya damu au kuvuja damu kidogo wakati mayai yanapevushwa ndani ya mwili wa mwanamke. Hii ni kwasababu kushuka kwa viwango vya homoni ya estrojeni huathiri ukuta wa uterasi.

Mabadiliko katika mkao wa seviksi

Seviksi hubadilisha mkao kutokana na homoni zinazosababisha uteute ukeni kutolewa na kukauka. Wakati mwanamke yuko katika kipindi ambacho hawezi kupata ujauzito, seviksi hushuka chini katika mfereji wa uke, ikiguswa huwa ngumu, na mlango wa seviksi unakuwa mdogo au kufunga ukilinganishwa na wakati mwingine. Kadiri mwanamke anavyozidi kufikia kipindi cha “ovulation” ndivyo seviksi inavyopanda juu katika mfereji wa uke, inakuwa laini ikiguswa, na upenyu (mlango wa seviksi) unakuwa wazi zaidi kuruhusu mbegu za kiume kusafiri kwa urahisi kuelekea kwenye mfuko wa uzazi na mirija ya falopiani. Baada ya yai kupevushwa seviksi itarejea mkao wake wa siku za kawaida.

 

 

 

 

 

 

Mabadiliko ya joto la mwili

Joto la msingi la mwili ni joto la mwili wa mtu linalopimwa mara anapoamka asubuhi (au baada ya usingizi wa muda mrefu zaidi katika siku). Wakati yai linapevushwa joto la mwanamke hupanda kwa kwa 0.3°C hadi 0.9° C (0.5°F hadi 1.6°F) na kubakia hivyo kipindi chote hadi wakati wa hedhi ijayo. Mabadiliko hayo ya joto yanaweza kutumika kubaini siku mwanamke anazoweza kupata ujauzito (fertile days), hivyo basi mwanamke na mwenza wake wajitahidi kufuatilia joto la mwili kwa kutumia kipima joto maalumu.

Mabadiliko ya hisia

Kupanda na kushuka kwa viwango vya honi zinazoratibu kupevuka kwa mayai ya uzazi wa mwanamke yanaweza kumfanya mwanamke awe mwenye hasira, wasiwasi au huzuni. Kwa baadhi ya wanawake hali hupita na kurudi tena wiki moja kabla ya hedhi yake. Kwa wengine hali hii inaweza kuchukua mda mrefu na kuleta madhara makubwa.

Uwezo wa kutambua harufu unaongezeka

Wakati unakaribia “ovulation” utagundua uwezo wako wa kunusa unaimarika, utazigundua harufu mbalimbali na chaguo lako linaweza badilika pia.

Dalili nyingine za kimwili ni pamoja na:

  • Tumbo kujaa gesi. Pia mabadiliko ya homoni yanasababisha uhifadhi wa maji ndani ya tishu za mwili ambao utadumu kwa siku kadhaa.
  • Uchovu na maumivu ya kichwa
  • Fizi kuwa nyekundu au kuvimba kipindi unakaribia “ovulation” nayo ni moja ya dalili.

Nitawezaje kuongeza uwezo wangu wa kupata ujauzito?

Unaweza kuongeza nafasi ya kupata ujauzito ikiwa utafanya tendo la ndoa na mpendwa wako mara moja ndani ya siku 4-5 ambazo mwili wa mwanamke uko katika hali nzuri ya utungisho wa mimba kutokea “fertile days” na siku ya ovulation

Jaribu kufanya tendo la ndoa kila baada ya siku mbili au tatu kabla yai kupevuka. Mbegu zinazoogelea vizuri ndani ya mwili wako zitakuwa tayari siku yoyote ukiwa kwenye “ovulation”. Pia kufanya tendo la ndoa mara kwa mara siku nyingine katika mzunguko wako itaongeza nafasi ya kupata ujauzito.

Kufanya ngono wakati via vya uzazi wako vina uteute unaoteleza, unaongeza hali ya kuzipokea mbegu utaongeza uwezo wako wa kupata ujauzito. Kwa wapenzi wenye uzazi salama, wana uwezo kati ya asilimia 20 hadi 25 ya kupata ujauzito kwa kila mzunguko wa hedhi. Zaidi ya asilimia 80 ya wanawake chini ya miaka 40 ambao hufanya ngono kwa kawaida bila kutumia uzazi wa mpango hupata mimba kila mwaka. Zaidi ya asilimia 90 ya wenza wapya hupata ujauzito ndani ya miaka miwili.

IMEPITIWA: MACHI 2O2I