Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Ninawezaje Kuongeza Nafasi ya Kupata Mtoto wa Kike au Kiume?

Je, moyo wako unafarijika kila uonapo nguo ya mtoto wa kike au kiume dukani au sokoni?

Hakika unapata furaha ndani ya moyo wako ndio maana upo kusoma makala yetu hii. Makala hii itakujuza vidokezo mbalimbali vinavyoweza kuongeza nafasi ya kupata ujauzito wa mtoto wa kike au kiume. Jambo la kwanza unalotakiwa kujua ni kwamba njia hizi za kujaribu kupata mtoto wa kike au kiume hazihakikishi kufanikiwa na pia hazithibitishwi na ushaidi wa kisayansi.  Njia pekee ya kukuhakikishia kupata mtoto wa jinsia unayotaka ni kutumia utaratibu maalumu unaohusisha kupandikiza kiinitete (kike au kiume) ndani ya uterasi ya mama, njia hii inajulikana kama “IVF- in vitro fertilization”. Njia hii ni gharama sana na sio halali kwa baadhi ya nchi.  Hivyo basi sio mbaya kujaribu baadhi ya mbinu hizi hata kama hazikupati uhakika asilimia 100 wa kupata mtoto wa jinsia unayotaka.

Ni muhimu kujua kuwa mbegu ya mwanaume ndiyo inayotoa uamuzi wa jinsia ya mtoto. Ijapokuwa mbinu mbalimbali zinashauri vitu ambavyo wanandoa wanaweza kufanya ili kupata mtoto wa kike au kiume,mwisho wa siku uteuzi wa jinsia ya mtoto una amuliwa na mbegu ya kiume itakayolifikia yai la mwanamke. Mara baada ya urutubishaji kutokea, jinsia ya mtoto huamuliwa.

Vifuatavyo ni vidokezo vitakavyokusaidia kuongeza nafasi ya kupata mtoto wa kike au kiume:

Matumizi ya njia ya “Shettles”

Ingawa hakuna data zinazoweza kuthibitisha ufanisi wa njia hii inayoitwa “the shettles” baadhi ya wanandoa wamekiri imewasaidia na wengine wameamua kujaribu njia hii. Nadharia inayotumika hapa ni kwamba mbegu ya kiume inayobeba jinsia ya kike (X) inasafiri taratibu lakini pia ina nguvu na inaishi mda mrefu ukilinganisha na mbegu ya kiume iliyobeba jinsia ya kiume (Y) ambazo zinasafiri haraka sana lakini zinaishi kwa muda mfupi. Hii inamaanisha kwa wanandoa wanaofanya tendo la ndoa siku mbili mpaka tatu kabla ya siku yai linapevuka ndani ya mwili wa mwanamke, wanaweza kuongeza nafasi ya kupata mtoto wa kike. Hii ni kwasababu mbegu za kiume zenye jinsia ya kike zinaweza kuishi mda mrefu hadi kipindi yai linapevuka, siku chache baadae zitakuwa bado zinaishi ndani ya mirija ya uzazi.

Lakini kama unataka kupata ujauzito wa mtoto wa kiume, wanandoa wanashuriwa kufanya tendo la ndoa siku moja kabla ya “ovulation” au siku yai linapevuka kujishindia nafasi ya mwanamke kubeba ujauzito wa mtoto wa kiume, kwasababu mbegu hizi zina kasi zaidi hivyo ni rahisi kulifikia yai haraka zaidi. Utafiti unaonyesha njia hii inaweza kuongeza nafasi ya kupata mtoto wa kike kwa asilimia 75, ijapokuwa hakuna utafiti wa kisayansi unaothi itisha iwapo njia hii inafanya au haifanyi kazi.

Matumizi ya njia ya “Whelan”

Njia hii ilianzishwa na Elizabeth Whelan. Njia hii inafanana na “shettles” kwani zote mbili zinaamini muda ni kitu muhimu katika kutafuta mtoto wa jinsia fulani. Nadharia inayotumika hapa inashauri ikiwa unataka kupata mtoto wa kike fanya tendo la ndoa siku 2 au tatu kabla ya yai kupevuka au siku ya ovulation kabisa. Wazo linatumika hapa kuunga mkono nadharia hii ni kwamba mbegu zenye kubeba jinsia ya kike na kiume zinafanya kazi tofauti katika kipindi tofauti ndani ya mzunguko wa hedhi wa mwanamke. Mbegu za kiume zenye kromosomu X zinaweza kurutubisha yai zaidi katika kipindi hichi cha mzunguko. Hivyo basi ikiwa utakutana kimwili na mwenza wako siku chache kabla ya “ovulation” au siku ya “ovulation” mbegu hizi zina nafasi kubwa ya kuishi. Kulingana na mvumbuzi wa nadharia hii- Elizabeth, kiwango cha kufanikiwa kupata mtoto wa kike kwa kutumia njia hii ni asilimia 57.

Njia hii ya Whelan inategemea wazo la kwamba mabadiliko ya dutu za kemikali ndani ya mwili wa mwanamke katika kipindi fulani ndani ya mzunguko wake yanafanya mbegu zilizobeba jinsia ya kiume “Y”kurutubisha yai, na wakati mwingine dutu za kikemikali kuruhusu mbegu zilizobeba jinsia ya kike “X” kurutubisha yai. Hivyo basi, ikiwa unatamani kupata mtoto wa kiume, dhana inasema, wanandoa wajitahidi kukutana kimwili siku nne mpaka sita kabla ya ovulation. Mbali na kuwa na rekodi za kuonyesha njia hii inafanya kazi, wakosoaji wanasema kufanya tendo la ndoa siku nne mpaka sita kabla ya yai kupevuka ni mbali sana na mara nyingi mbegu zilizobeba jinsia ya kiume haziishi mda mrefu.

Mikao wakati wa kujamiana

Zipo dhana nyingi kuhusu aina fulani ya mikao itakusaidia kupata mtoto wa kike au kiume, lakini ijulikane kwamba hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha hivyo, lakini pia hakuna madhara ikiwa wewe na mwenza wako mkajaribu. Mikao inayoruhusu uume kupenya kwa kina ndani ya uke (deep penetration),itasaidia kupata mtoto wa kiume wakati mikao ile isiyoruhusu upenyo wa kina inasaidia kupata ujauzito wa mtoto wa kike (shallow penetration). Kukusaidia kujua zaidi kuhusu mikao hii, soma makala yetu ya “mikao mizuri ya kujamiana ili kupata ujauzito haraka”.

Kufika kileleni “Orgasm”

Wataalamu wa mambo ya uchaguzi wa jinsia wanashauri ili kupata ujauzito wa mtoto wa kike mwanamke anatakiwa asifike kileleni. Mwanamke akifika kileleni anatoa alkali ambayo inasaidia mbegu zilizbeba jinsia ya kiume kuishi zaidi kwa kutengeneza mazingira yasiyohatarishi. Bila alkali hii inayotolewa pindi mwanamke amefika kileleni, mbegu zilizobeba jinsia ya kiume hushindwa kuishi na zina nafasi ndogo ya kufika kwenye yai lililotolewa na ovari tayari kwa kurutubishwa. Mwanamke akifika kileleni inaongeza nafasi ya kupata mtoto wa kiume.

Vidokezo vinginevyo ikiwa unajaribu kupata mtoto wa kike ni pamoja na:

 • Kutana na mwenza wako kimwili mara kwa mara
 • Punguza chumvi katika milo yako
 • Kula vyakula vyenye asidi nyingi (machungwa, machenza,n.k)na epuka vyakula vyenye alkali kama vile tango, tofaa, parachichi na almond. Mbegu za kiume zilizobeba jinsia ya kiume haziwezi kuishi katika mazingira yenye aside, hivyo kuongeza wingi wa aside mwili kupitia chakula kunasaidia kubadilisha kiwango cha Ph ya uke wako. Vilevile ikiwa mnatafuta mtoto wa kiume ulaji wa vyakula vyenye alkali ya kutosha utasaidia kuishi vizuri kwa mbegu zilizobeba jinsia ya kiiume.

Je, Vyakula Gani Vitaongeza Nafasi ya Kupata Mtoto wa Kike?

Vyakula vinavyofikiriwa kuongeza nafasi ya kupata mtoto wa kike ni pamoja na:

 • Maharagwe
 • Mboga za majani zenye kijani kilichokolea
 • Almond
 • Vyakula vya baharini hasa dagaa
 • Bidhaa za maziwa kama vile jibini, maziwa na mtindi
 • Bamia
 • Matunda jamii ya machungwa
 • Mayai
 • Karanga ya kusaga
 • Korosho
 • Mbegu kama mbegu za maboga na chia
 • Spinachi
 • Shayiri
 • Apple
 • Matunda kama strawberi,zabibu

Je, Vyakula Gani Vitaongeza Nafasi ya Kupata mtoto wa Kiume?

Vyakula vinavyofikiriwa kuongeza nafasi ya kupata mtoto wa kiume ni pamoja na:

 • Vyakula vyenye potasiamu ya kutosha kama vile ndizi, parachichi,uyoga,apple,almond, samaki aina ya salmon
 • Vyakula vyenye alkali ya kutosha kama vile machungwa, machenza,
 • Matunda freshi na mbogamboga
 • Nafaka ambazo hazijakobolewa
 • Epuka bidhaa za maziwa

Kumbuka

Kwa kadri unavyotamani kupata mtoto wa kike au kiume, ukweli ni kwamba hakuna njia inayoweza kuahidi matokeo unayotaka. Na ukweli ni kwamba, hakuna madhara katika kujaribu njia hizi – lakini utafiti zaidi unahitajika ili kujua ufanisi wa mapendekezo haya. Bila kujali kama utapata mtoto wa kike au kiume, jambo muhimu ni kuwa na ujauzito salama na kujifungua mtoto mwenye afya.

IMEPITIWA: APRILI 2021