Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Wanawake wengi hupendelea kujifungua bila ya upasuaji, lakini kwa wakati mwingine ni vigumu kukwepa upasuaji. Inawezekana wakati mwingine ukajua kuwa utajifungua kwa upasuaji kutokana na matatizo mbali mbali yanayohusiana na ujauzito wako yanayohitaji upasuaji. Inaweza pia ikahitajika kufanyiwa upasuaji ukiwa katika hatua za kujifungua kawaida ila ikaonekana kuna hali hatarishi kwako au kwa mtoto wako.

Sababu za kufanyiwa upasuaji ni kama, uchungu ambao hauendi vizuri kama inavyotarajiwa, dalili za uchungu uliowahi kabla ya muda, kusogea kwa kondo la uzazi karibu na mlango wa uzazi (Placenta Praevia), mtoto aliyegeuka, au kuwepo kwa maambukizi ambayo yanaweza kumuambukiza mtoto kama Hepatitis C au HIV)

Wakati wa upasuaji, mkato mmoja hufanywa kwenye tumbo lako na tumbo la uzazi kumuwezesha daktari kumtoa mtoto wako.

Kama utajua mapema kuwa utajifungua kwa upasuaji, utapata muda kwa kutosha kujitayarisha, lakini kama ni upasuaji wa dharura inaweza kukushtua. Kwa kawaida utachomwa sindano ya ganzi ya uti wa mgongo, itakayokufanya usisikie maumivu kuanzia kwenye nyonga kwenda chini. Hii ni njia salama zaidi kuliko nusu kaputi. Faida nyingine ni kwamba utaweza kumuona mtoto wako mara tuu anapotolewa tumboni.

Kama utakuwa umejifungua kwa upasuaji utahitaji kuendelea kukaa hospitali kwa siku kadhaa uanze kupona.

Kupona baada ya upasuaji ni sawa tu na kupona kwa upasuaji mwingine wa eneo la tumbo. Tofauti kubwa ni kwamba badala ya kupoteza kiungo kimoja kama figo au “appendix” unapata mtoto.

Mojawapo ya matatizo unayoweza kuyaona baada ya kujifungua ambayo ni ya kawaida ni kama hali ya kusikia maumivu kwenye uke, kutokwa na damu nzito nyeusi, matiti kuvimba, nywele kudondoka, uchovu na kutokwa jasho jingi.

Tegemea yafuatayo baada ya kutoka chumba cha upasuaji

Daktari wako atakuchunguza kwa karibu mpaka pale dalili zote za dawa za kuondoa maumivu zimeisha. Kumbukumbu zako zinaweza zikawa zinasumbua kama ulitumia dawa ya usingizi au nusu kaputi. Madhara ya dawa ya kuondoa maumivu ya uti wa mgongo huchukua muda mrefu zaidi kuliko madhara ya dawa za usingizi kabisa.

Baada ya dawa ya kuondoa maumivu kuisha utaanza kusikia kidonda kinauma. Ukali wa maumivu unategemea sababu tofauti, ikiwemo uwezo wako wa kusikia maumivu na kama una historia ya kujifungua kwa upasuaji toka awali, kwani maumivu ya upasuaji wa pili na kuendelea huwa yanaonekana sio makubwa sana kama yale uliyoyasikia kwenye upasuaji wa kwanza. Utapewa dawa za maumivu kupambana na hali hii.

Unaweza ukasikia kichefuchefu, ambapo daktari atakupatia dawa itakayokuzuia kupata kichefuchefu au kutapika.

Nesi atakuwa anakuchunguza mara kwa mara. Atakuwa anachukua vipimo vyako muhimu (joto, shinikizo la damu (BP), na upumuaji). Atakuwa pia anaupima mkojo wako na chochote kinachotoka ukeni. Pia atakuwa anaangalia mfungo wa kidonga chako cha upasuaji, sehemu mfuko wako wa uzazi ulipo na ugumu wake na wakati huo huo akihakikisha mirija ya dripu na mpira wa mkojo ipo sehemu yake.

Kama hali yako itaendelea vizuri, utapelekwa kwenye wodi ndani ya masaa kadhaa baada ya upasuaji kufanyika. Uchunguzi wa vipimo vyako muhimu utafanyika kwa mara nyingine. Kama una uwezo wa kukojoa mwenyewe basi mpira wa mkojo utatolewa masaa 24 baada ya upasuaji.

Unaweza ukawa unasikia maumivu kwenye uke kama mwanamke aliyejifungua kwa njia ya kawaida. Hii isikupe wasiwasi maumivu haya ni kutokana na kukaza kwa misuli ya mfuko wako wa uzazi ukiwa unajirudia kwenye hali yake kabla ya ujauzito.

Dripu za maji zitatolewa na utaruhusuwa kuanza kutumia vinywaji kwa kunywa mwenyewe masaa 24 baada ya upasuaji (Huu ndio muda ambao utumbo wako utakuwa umeshaanza kusogeza chakula kawaida na kufanikiwa kujamba). Taratibu utaruhusiwa kurudia mlo wako wa kawaida kadiri siku zinavyosogea. Mama wanaonyonyesha inabidi wapate maji ya kutosha mwilini.

Utategemea kutolewa nyuzi zako (Kama sio zile zinazoyeyuka zenyewe) ndani ya siku 4 hadi 6 baada ya upasuaji.

Mwishoni kabisa kama kila kitu kitakuwa kimeenda sawa kwako na mtoto, utaruhusiwa kurudi nyumbani ndani ya siku 3 hadi 7 baada ya upasuaji.

shares