Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Umuhimu wa Kunywa Maji Wakati wa Ujauzito.

Ninywe Maji Kiasi Gani Kila Siku Wakati wa Ujauzito?

Uhitaji wa maji wakati wa ujauzito ni mkubwa zaidi ili kuhakikisha mfumo wa mwili unaosimamia maisha ya viumbe wawili unafanya kazi vizuri. Ijapokuwa utofauti upo wa kiasi gani cha maji unywe kwa siku kutokana na sababu mbalimbali kama aina na ukubwa wa mwili wako na kwa kiasi gani unaushughulisha mwili wako, kwa ujumla angalau glasi 8 mpaka 12 za maji kwa siku.

Inashauriwa ukiwa unakunywa maji, kunywa kidogo kidogo badala ya kugugumia maji mengi kwa wakati mmoja hali ambayo inaweza kukufanya kujisikia vibaya. Unaweza kujaza chupa mbili za maji asubuhi na kuhakikisha uko karibu nazo kila wakati itakusaidia kukumbusha kunywa maji kila utakapoiona.

Hakikisha unakunywa maji kabla, wakati na baada ya mazoezi. Kumbuka kiu ni ishara mwili wako unaelekea kupata upungufu wa maji.

Faida za Kunywa Maji Wakati wa Ujauzito

Maji yanasaidia kuzuia kukosa choo

Sasa wewe ni mjamzito, kumbuka unakula na kutoa taka za watu wawili. Hii ina maanisha utoaji taka mwilini ni mkubwa kuliko hapo awali. Maji ya kutosha mwili yatasaidia kuyeyusha takamwili na mabaki, kisha kuzisafirisha nje ya mwili. Unywaji wa maji ya kutosha unasaidia kutoa haraka nje ya mwili mabaki ya chakula baada ya kumeng’enywa kupitia njia ya mfumo wa umeng’enyaji. Ikumbukwe tatizo la kukosa choo linawapata wajawazito wengi bila kusahau athari zake ambazo zinahusisha kuota nyama sehemu ya haja kubwa (hemorrhoids).

Maji yanasaidia kuzuia maambukizi katika njia ya mkojo (UTI)

Unywaji wa maji ya kutosha unazimua mkojo, hali ambayo inasaidia mkojo kutolewa nje haraka na kuzuia bakteria zinazosababisha maambukizi katika kibofu kuzaliana (bakteria hizi zinazaliana mkojo unapobanwa kwa muda mrefu kwenye kibofu). Pia mama anayekunywa maji ya kutosha hana hatari ya kupata maambukizi katika kibofu na figo.

Maji yanapunguza joto la mwili.

Ni kweli ukiwa mjamzito joto la mwili ni kubwa. Lakini ukinywa maji ya kutosha wakati wa ujauzito unasaidia kupooza mwili na kufanya mwili kufanya kazi vizuri.

Maji yanapambana dhidi ya uchovu.

Moja ya ishara za awali za upungufu wa maji mwilini ni uchovu. Unywaji wa maji ya kutosha unasaidi kuhakikisha tatizo la uchovu wakati wa ujauzito linadhibitiwa, vilevile maumivu ya kichwa (ishara nyingine ya upungufu wa maji mwilini). Pia maji yanasiadia mwili kutoa sodiamu iliyozidi mwilini- hali ambayo itapunguza miguu kuvimba “edema”.

Je, Vinywaji Gani Vingine Mjamzito Anaweza Kutumia?

Maji ndio kinywaji cha kwanza kizuri na salama kwa mjamzito, lakini vipo vimiminika vingine vinavyoweza kutumiwa na mjamzito kusaidia mwili wake uwe na maji ya kutosha:

 • Maziwa
 • Maji yaliyotiwa ladha (ladha ya limao)
 • Juisi safi na salama ya matunda na mbogamboga (kuwa makini na sukari inayoongezwa katika juisi ya matunda)
 • Chai zisizo na kafeini.

Kwa hali yeyote, weka kikomo cha unywaji wa soda na vinywaji vingine vilivyo na kafeini kwasababu vina dutu inayosababisha kasi na kiwango cha kukojoa kuongezeka.

Kumbuka pia, karibia asilimia 20 za maji yanayoingia mwilini yanatoka kwenye vyakula. Matunda yana maji ya kutosha.

Ishara Mwili Wako Una Upungufu wa Maji.

Mwili wako utakuonyesha hauna maji ya kutosha kwa kuangalia ishara zifuatazo:

 • Kiu na njaa
 • Midomo kukauka na kuchanika.
 • Mabadiliko ya rangi ya mkojo. Mwili ukiwa na maji ya kutosha mkojo wako utakuwa na rangi ya njano ya kupauka (yaani “pale-yellow color”). Wakati mkojo wenye rangi ya njano iliyokolea ni ishara ya kukosa maji ya kutosha mwilini.
 • Kupungua kwa safari za kwenda uwani
 • Kutotoka jasho hata wakati wa joto
 • Tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu
 • Uchovu, kizunguzungu na maumivu ya kichwa. Upungufu wa maji mwilini unasababisha uchovu na maumivu ya kichwa, hakikisha unakunywa maji ya kutosha kutunza nguvu uliyo nayo kwasababu ujauzito ni kazi kubwa inayohitaji nishati ya kutosha haswa miezi ya kwanza.
 • Kusahau, kuchanganyikiwa kushindwa kuelewa na kukosa mwelekeo ni baadhi ya dalili za mtu mwenye hali inayoitwa “brain fog”.
 • Ngozi mwili kukauka.
 • Baadhi ya wajawazito wanapitia leba ya uongo (Braxton Hicks contractions)

Dalili kama kizunguzungu na kuchanganyikiwa, mapigo kasi ya moyo, mabadiliko ya kucheza kwa mtoto tumboni,shinikizo dogo la damu, mshtuko na ogani kushindwa kufanya kazi zinawapata wajawazito walio na tatizo kubwa la ukosefu wa maji.

Vidokezo Vitakavyokusaidia Kuhakikisha mwili una Maji ya Kutosha Muda Wote

Zipo baadhi ya siku unaweza kuhitaji msaada kuhakikisha unafikia dozi yako ya kila siku ya maji. Vifuatavyo ni vidokezo vitakavyokusaidia kuendelea kunywa maji:

 • Ongeza ladha, unaweza kuongeza kipande cha tango, limao majani ya mnanaa (mint) katika maji.
 • Jaribu chai zenye majani ya mitishamba, hakikisha daktari au mkunga wako anakupa kibali cha kutumia kiungo hicho.
 • Hakikisha una chupa ya maji mkononi mwako. Ni rahisi kufuatilia unywaji wako wa maji ukiwa na chupa yako ya maji mkononi nyakati zote.
 • Anza siku kwa kunywa glasi moja ya maji. Kunywa maji mara baada ya kuamka ni njia nzuri ya kujijengea tabia ya kunywa maji.
 • Kula vyakula vyenye maji kwa wingi kama vile supu, tikitimaji, nanasi n.k.

Kumbuka

Ukosefu wa maji ya kutosha mwilini wakati wa ujauzito unaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto tumboni.Inaweza kusababisha matatizo makubwa na hatari kwa afya kama vile:

 • Kupungua viwango vya maji yanayomzunguka mtoto ndani ya uterasi “amniotic fluid” ambayo ni muhimu katika maendeleo na ukuaji wa mtoto.
 • Mama kujifungua kabla ya wiki 37 za ujauzito kwasababu ya kupungua kwa “amniotic fluid”.
 • Mtoto kuzaliwa na kasoro za mirija ya neva za fahamu
 • Kiasi kidogo cha uzalishaji wa maziwa
 • Mtoto kuzaliwa na kasoro kwasababu ya ukosefu wa maji na virutubisho muhimu vya kumsaidia mtoto.
 • Mara chache,kukosa maji ya kutosha kunaweza hatarisha uhai au kusababisha mama kulazwa chumba cha wagonjwa mahutihuti.

IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.