Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Matumizi ya Dawa Kipindi cha Ujauzito

Mara kwa mara wanawake wengi hugundua kuwa ni wajawazito baada ya kukosa hedhi. Hivyo ni vyema kutambua madhara ya madawa mbali mbali hata kabla hujafikiria kuwa mjamzito ili ujue nini cha kuepuka.

Dawa nyingi hazijafanyiwa majaribio kama ni salama kwa ujauzito. Unachoweza kufanya kuepuka matatizo ni kuamua kutotumia dawa yoyote katika ujauzito wako labda tu uwe umeshauriwa na daktari.

Dawa mbali mbali zinaweza zikaathiri ukuaji wa mtoto wako kwa njia nyingi, ikiwemo:

  1. Kubadilisha mazingira ya mji wa mimba hivyo kusababisa uhaba wa mahitaji muhimu kwa mtoto
  2. Kubadilika kwa uwiano wa ukuaji sahihi wa mtoto hivyo kusababisha mtoto kuzaliwa njiti
  3. Kusababisha kuzaliwa na matatizo au mimba kutoka
  4. Kusababisha matatizo ya kupumua baada ya mtoto kuzaliwa

Kama unatumia dawa za aina yoyote ile na umegundua kuwa ni mjamzito ni vyema kuwasiliana na daktari wako mara moja kabla hujaacha kuzitumia kwani maisha yako yanaweza yakawa yanategemea dawa hizi. Daktari wako ataweza kukushauri kuhusu dawa unazotumia kama ni salama au la kwenye ujauzuto na kukubadilishia kadiri itakavyoonekana ni sawa.

Ni vyema pia kuwa makini na dawa zinazoitwa za asili. Kwa sababu tu zimeandikwa ni dawa za asili haimaanishi hazina uwezo wa kuleta shida kwenye ujauzito wako. Dawa nyingi za asili pia zina uwezo wa kuleta matatizo kipindi cha ujauzito hivyo ni vyema kutokutumia dawa za asili ukiwa mjamzito.

Dawa yoyote ile ambayo utaitumia mwilini kwako kipindi cha ujauzito ni vyema iwe imetolewa na daktari wako anaetambua kwamba wewe ni mjamzito. Baadhi ya wanawake hununua dawa kwenye maduka ya dawa baridi kama Paracetamol pale wanapohisi maumivu. Ni vyema pia kupata ushauri wa daktari kwani kuna baadhi ya dawa za maumivu unaweza ukawa unahisi ni salama (kwani si za maumivu tuu), kumbe zinaweza kuleta shida kwako au kwa mtoto wako tumboni.

Kuweza kuepuka mahitaji ya kutumia dawa kipindi cha ujauzito, kula mlo bora, kunywamaji ya kutosha, fanya mazoezi na pia jifunze kupumzika. Msongo wa mawazo unaweza kusababisha kila maumivu kuwa makali zaidi. Maswali yoyote kuhusu dawa ni vyema ukashirikiana na daktari wako kwani yeye ndiye mwenye uwezo na taarifa sahihi kuhusu usalama wa dawa husika na usalama wako na mtoto wako.