Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Ujauzito Wiki ya 1

Jinsi mtoto wako anavyokua katika ujauzito wiki ya kwanza
Japokuwa wewe sio mjamzito bado, siku yako ya kwanza ya hedhi ndio mwanzo wa wiki ya kwanza ya ujauzito wako. Hii itakuwa ndio hedhi ya mwisho utakayoiona mpaka mtoto wako atakapozaliwa. Lile yai ambalo litakuja kuwa mtoto wako ndio linategemea kuanza safari kutoka kwenye mfuko wako wa mayai “ovary” na kuelekea kwenye mirija ya uzazi “fallopian tubes” ambapo litaungana na mbegu.
Kutungwa kwa mimba hakutatokea mpaka siku 14 zijazo, lakini mwanzo wa ujauzito huhesabiwa kuanzia siku ya kwanza kuona hedhi yako ya sasa. Katika wiki mbili za mwanzo tumbo lako la uzazi huanza kujitayarisha kuweza kubeba na kurutubisha mtoto wako kuanzia pale mimba itakapotungwa.

Dalili za ujauzito katika wiki ya kwanza
Japokuwa hedhi hii inaweza kuonekana kama hedhi nyingine yoyote, ni vyema kutambua kuwa hedhi hii ni ya kipekee. Mwili wako unafanya kazi ya ziada kutengeneza homoni inayoitwa “Follicle Stimulating Hormone (FSH)” inayoipa mifuko yako ya mayai uwezo wa kuyarutubisha mayai. Kila yai lililokomaa kwenye mifuko yako ya mayai linahifadhiwa kwenye mfuko “follicle”, ambayo hutoa homoni ya estrogeni kwa wakati huu. Kadiri mzunguko wako wa hedhi unavyoendelea, mayai yaliyokomaa huanza safari kuelekea kwenye mdomo wa mfuko wako wa mayai. Hapa mfuko wenye yai lililokomaa zaidi husubiri mpaka ni karibia muda wa wewe kuwa na uwezo wa kutunga mimba “ovulation” ndipo utaliachia yai. Kazi ya estrogeni ni kuongeza msukumo wa damu kwenye mji wako wa uzazi “uterus” na kurutubisha ukuta wake tayari kusubiria kujitunga kwa yai lililochavushwa tayari.

Unachotakiwa kufahamu katika ujauzito wiki ya kwanza
Huu ndio wakati wa kuacha kunywa pombe na kuvuta sigara kama ulikuwa bado hujafanya hivyo. Pia ni vyema ukaanza kutumia virutubisho vya vitamini za kipindi cha ujauzito kuanzia sasa. Virutubisho unavyotumia sasa vitasaidia kupunguza matatizo mbali mbali kwenye ujauzito wako na kwa mtoto wako. Pia kuna baadhi ya dawa zinazoweza kumdhuru mtoto wako hivyo ni vyema kumuona daktari wako na kufanya uchunguzi kama kuna chochote unachotumia kitakachoweza kumdhuru mtoto wako wakati huu. Kupata usingizi wa kutosha na kuhudumia afya yako kadiri uwezavyo itasaidia ujauzito wako kuanza vizuri na kuendelea vizuri.