Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Ujauzito Wiki ya 19

Jinsi mtoto wako anavyokuwa katika ujauzito wiki ya kumi na tisa
Huu ni wakati muhimu sana ambao akili na fahamu ya mtoto wako inajitengeneza. Seli za neva fahamu ambazo zitamsaidia mtoto wako kuelewa na kuguswa na dunia ambayo inayomzunguka zinaendelea kuongezeka katika maeneo fulani ya ubongo wake.

Miguu na mikono ya mtoto wako kwa sasa ipo kwenye uwiano sawa na mwili wake. Anajitahidi sana kwa sasa kupiga mateke na kukunja na kukunjua miguu na mikono yake kipindi hiki. Hii inamaanisha unaweza ukamuona ukienda kituo cha afya kwa ajili ya kipimo cha “ultrasound” kijacho.

Dalili za ujauzito katika wiki ya kumi na tisa
Unaweza kugundua maumivu chini ya tumbo lako la chini. Ni kitu cha kawaida usiwe na wasiwasi juu ya hilo. Hii inatokana na kukaza kwa misuli yako na mishipa inayosaidia kuubeba mfuko wako wa uzazi “uterus”. Kadiri ujauzito wako unavyokua, misuli na mishipa hii hujikaza na kujivuta kuweza kukishikilia kizazi vizuri. Kujikaza na kujivuta huku ndio kunakosababisha kusikia maumivu kwenye nyonga.

Ni kawaida kwa misuli hii kuwa inauma upande mmoja zaidi kuliko upande mwingine. Hii inatokana na kwamba mfuko wa uzazi huzunguka kuelekea kulia kadiri ujauzito unavyozidi kukua. Hivyo, mara kwa mara maumivu huwa yanatokea upande wa kulia.

Unachotakiwa kufahamu katika ujauzito wiki ya kumi na tisa
Unahitaji madini chuma kwa wingi zaidi kipindi cha ujauzito. Mwili wako unatumia madini chuma kutengeneza hemoglobini, inayosaidia damu yako kuweza kubeba hewa ya oksigeni kuzunguka mwili wako. Kama hauna kiwango cha kutosha cha madini chuma, kiwango cha hemoglobini pia kitashuka na kusababisha kupata upungufu wa damu utokanao na upungufu wa madini chuma “Iron-Deficiency Anaemia”. Hali hii inaweza ikawa ya hatari sana kwa ujauzito na mtoto wako kama haitapatiwa matibabu mapema.

Kula vyakula vyeme madini chuma kwa wingi kama nyama nyekundu, kuku, samaki, mbogamboga za majani, nk itasaidia kuhakikisha kiwango cha madini chuma hakishuki. Pia unahitaji kupata Vitamini C, kwani husaidia pia kwenye umeng`enyaji wa chakula kupata madini chuma. Matunda kama machungwa, maembe yana vitamini C ya kutosha.

Hauhitaji kutumia dawa za kuongeza madini chuma ila pale tu daktari anaposhauri. Dawa hizi zinaweza zikakupa hali ya kujisikia vibaya kama kichefuchefu, maumivu ya tumbo au choo kikavu. Inashauriwa uzitumie dawa hizi kama kweli una umuhimu wa hali ya juu wa kuzitumia.