Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Ujauzito Wiki ya 23

Jinsi mtoto wako anavyokua katika ujauzito wiki ya 23
Moyo wa mtoto wako unapiga kwa nguvu zaidi na unasambaza damu nyingi zaidi mwilini mwake. Ndani ya muda huu mtoto wako ameanza kusikia sauti za karibu kwa usahihi zaidi. Anaweza pia kusikia sauti za mbali kidogo kama mlango kufungwa kwa nguvu.

Dalili za ujauzito katika wiki ya 23
Kama unasumbuliwa na kutopata choo au choo kigumu au kujisikia mzembe mzembe, inaweza kuwa inasababishwa na homoni ya progesteroni. Wakati wa ujauzito chakula kinasafiri taratibu zaidi kwenye utumbo wako, hali inayopelekea wewe kupata shida ya kupata choo. Kadiri mtoto wako anavyokuwa atasukuma zaidi chini eneo la haja kubwa hivyo kufanya hali ya choo kigumu kuwa mbaya zaidi. Utaona ya kuwa kukosa choo au choo kigumu inakera, lakini karibia nusu ya wanawake wajawazito wanasumbuliwa na tatizo hili wakati fulani katika ujauzito wao. Hivyo haupo peke yako.

Ulaji wa mbogamboga na matunda itasaidia chakula kusafiri vizuri na kupunguza kuvimbiwa na tumbo kujaa gesi. Kuongeza kiwango cha maji unayokunywa pia itasaidia choo chako kuwa kilaini.

Kujikamua wakati wa haja kubwa kunaweza kusababisha kupata mipasuko midogo midogo inayoweza kusababisha kutoka damu. Hali hii ikitokea ni vyema ukapata kumuona daktari kwa matibabu zaidi.

Unachotakiwa kufahamu katika ujauzito wiki 23
Mtoto wako ameanza kusikia sauti mbalimbali na kuweza kuzitofautisha. Ana uwezo wa kuitambua sauti yako pia. Ni wakati mzuri sasa kuanza kuwasiliana na mtoto wenu kwa kuimba nyimbo mbalimbali za watoto na kuongea nae mara kwa mara akiwa bado tumboni. Utakuja kugundua kwamba kuziimba nyimbo hizi hizi baada ya mtoto kuzaliwa zitakuwa zinambembeleza haraka zaidi.