Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Ujauzito Wiki ya 27

Jinsi mtoto wako anavyokua katika ujauzito wiki ya 27
Sasa unapokaribia miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito wako, mtoto wako ameshajaza nafasi ya kutosha katika mji wako wa mimba.

Mtoto wako sasa anaweza kufungua na kufunga macho yake, kulala na kuamka katika vipindi vya kawaida, na anaweza kuwa anaanza kunyonya vidole vyake, sanasana kidole gumba. Mapafu yake pia yanaweza kufanya kazi kwa msaada wa mashine kama itatokea bahati mbaya akazaliwa mapema (njiti).

Dalili za ujauzito katika wiki ya 27
Mwili wako ni unabadilika kwa kasi sana sasa. Mji wa mimba upo juu karibu na ngome ya mbavu zako na unaweza kuanza kuona misuli ya miguu inabana na unapata choo cha kubana mara kwa mara. Matatizo haya yote ya ujauzito yatatoweka baada ya kupata mtoto wako.

Katika hudhurio lako lifuatalo kliniki unaweza kupewa kipimo cha damu kuangalia kama una upungufu wa damu. Unaweza kuwa na upungufu wa damu kama huna madini chuma ya kutosha katika mlo wako, na kusababisha upungufu wa chembechembe nyekundu za damu. Wanawake wengi wajawazito hupata upungufu kidogo wa damu kipindi cha ujauzito kutokana na mabadiliko ya kawaida katika mwili.

Kama kundi lako la damu ni “Rhesus-Negative” ni lazima kupewa sindano ya “anti-D” ndani ya wiki ya 28.

Uchungu unakaribia sasa hivyo kama bado haujapanga vyema utajifungulia wapi na namna ya kufika kwenye kituo cha afya husika ni vyema kuweka mipango yako sawa sasa.

Amini usiamini, mafanikio ya mama kunyonyeshainategemeana na mtazamo wa mpenzi wake. Kama wewe ni baba-mtarajiwa, ni wakati wa kujifunzavitu vya msingi kuhusu kunyonyesha ili uweze kutoa msaada baada ya mtoto wako kuzaliwa.

Kama unataka kusafiri kwa njia ya ndege, utahitajika kutoa kielelezo kutoka kwa daktari wako kikisema kuwa upo sawa kusafiri kwa ndege. Sheria za baadhi ya ndege na nchi mbalimbali haziruhusu mjamzito aliyefikia miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito kusafiri kwa ndege.